Uvunjaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na sifa za Tundu Lissu kugombea Urais wa Jamhuri

Matojo Cosatta

JF-Expert Member
Jul 28, 2017
234
390
UVUNJAJI WA SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA NA SIFA ZA TUNDU LISSU KUGOMBEA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.

SEHEMU 1: UTANGULIZI.


Jana tarehe 4 Augosti, 2020 nilisoma waraka ulioandikwa na Kaka yangu Daddy Igogo ambapo kupitia waraka huo alijenga hoja kuwa Mhe. Tundu Lissu hana sifa za kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja ya Ndugu Igogo ilijikita kwenye sababu kuwa Mhe. Lissu hana sifa za kugombea ubunge kutokana na uvunjaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 kwa kushindwa kutangaza na kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma. Ndugu Igogo aliendelea kujenga hoja kuwa mtu ambaye hana sifa za kugombea ubunge pia anapoteza sifa za kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kitu ambacho ni kweli.

Pia, Ndugu Igogo anasema kuwa Baraza la Maadili ndo lililompa adhabu ya kumvua ubunge Tundu Lissu na sio Spika wa bunge. Hii hoja ya Igogo ina mapungufu makubwa ya kisheria na kitaarifa (facts), it is a mistaken and misconceived argument both in law and in fact lakini hoja hii nitaichambua katika makala nyingine inayojitegemea, hivyo, leo tujikite kwenye hoja hii ya uvunjaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na sifa ya kugombea Urais au ubunge kwa upande wa Mhe. Tundu Lissu.

Hata hivyo, katika waraka wake Ndugu Igogo akufanya rejea yoyote ya masharti mahususi ya kifungu cha sheria au masharti mahusi ya Ibara ya Katiba. Siwezi kumlaumu Ndugu Igogo kwa kushindwa kufanya rejea kwenye masharti mahususi ya sheria na katiba kwa kuwa yeye sio mwanasheria kitaaluma.

Kutokana na waraka wa Ndugu Igogo, na mimi ninachukua fursa hii kutoa maoni yangu kuhusu swala hili kama ifuatavyo hapa chini.


SEHEMU 2: MTAZAMO WA JUMLA.

Kila Kiongozi wa Umma ana wajibu wa kutii, kuheshimu na kutekeleza masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 (Sheria Na. 13 ya 1995). Na uvunjaji wa masharti ya Sheria Na. 13 ya 1995 unaweza kumuondolea mtu sifa za kugombea nafasi ya Urais na ubunge. Pia, uvunjaji wa baadhi ya masharti ya sheria hii unaweza kumuondolea mtu moja kwa moja (automatically) sifa za kuwa Waziri Mkuu, Waziri na Naibu Waziri kwa sababu mojawapo ya sifa ya mtu kuwa Waziri Mkuu, Waziri na Naibu Waziri lazima mtu huyo awe ni mbunge kwa mujibu ya Ibara 51 (2) na 55 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

Vipo vitendo vingi ambavyo vinachukuliwa na sheria kuwa uvunjaji wa Maadili ya Viongozi wa Umma na uvunjaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 (the Public Leadership Code of Ethics, Act, Cap. 398) iwapo vitendo havyo vitafanywa na kiongozi wa umma. Hata hivyo, kwa leo nitajikita katika kitendo kimoja tu ambacho kinachukuliwa na sheria kuwa uvunjaji wa Maadili ya Viongozi wa Umma na uvunjaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398. Na kitendo hicho ni kitendo cha kiongozi wa umma kushindwa kutangaza mali na madeni ya Kiongozi wa Umma kwa kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni (ari maarufu kama Fomu ya Maadili) kwa Kamishna wa Maadili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Na kwa upande wa viongozi wa umma nitajikita kwa mbunge ambaye naye pia ni kiongozi wa umma kwa mujibu wa sheria.

Kila Kiongozi wa Umma ana wajibu wa kutangaza mali na madeni yake kwa kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni (Fomu ya Maadili) kwa Kamishna wa Maadili ndani ya siku 30 baada ya kuapishwa kuwa kiongozi wa umma na kila mwisho wa mwaka na mwishoni mwa muhula wake wa uongozi wa Umma (at the end of his term in office) kwa mujibu wa Kifungu cha 9 (1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398.

Mbunge ni kiongozi wa umma kwa mujibu wa Kifungu cha 4 (1) (xi) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398. Hivyo, mbunge ana wajibu wa lazima wa kutangaza mali na madeni yake kwa kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili ndani muda uliotajwa hapo juu.

Kushindwa kutangaza mali na madeni ya Kiongozi wa Umma kwa kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili ni kosa la kimaadili kwa mujibu wa Kifungu cha 15 (a) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398.

Mojawapo ya sifa za mtu kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuwa na sifa za kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Ibara ya 39 (1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

Na mojawapo ya kitu kinachoondoa sifa ya mtu kuwa mbunge ni kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa la kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kipindi cha miaka 5 kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu kwa mujibu wa Ibara ya 67 (2) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 ambayo inasema kama ilivyonukuliwa hapa chini;


"67 (2) Mtu hatakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge-

(a) ........................................
(b) ........................................
(c) ........................................

(d) ikiwa katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu amepata kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;"



Sio kila uvunjaji wa sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na sio kila kosa la Maadili ya Viongozi wa Umma linamuondelea mtu moja kwa moja (automatically) sifa ya kuwa mbunge, la hasha. Kuna masharti kadhaa ambayo yamewekwa na sheria na katiba ambayo lazima yatimizwe kabla ya mtu kupoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na sababu ya kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Ili mtu hakose sifa za kuwa mbunge kutokana na sababu ya kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma lazima masharti 5 yafuatayo yatimizwe;

(1) Lazima mtu huyo ahukumiwe au akutwe na hatia ya kijinai ya kosa la kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398.

(2) Na kosa hilo la kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 lazima liwe ni kosa la jinai.

(3) Adhabu ya hatia ya kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 dhidi ya mtu huyo lazima iwe ni kifungo cha gerezani.

(4) Lazima mtu huyo awe ametiwa hatiani kwa kosa la jinai linaloambatana na uvunjaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na amepata adhabu ya kifungo katika kipindi cha miaka 5 kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu.

(5) Mtu huyo lazima ahukumiwe au akutwe na hatia na apewe adhabu ya kifungo kutokana na kosa la kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na mahakama tu na sio mamlaka nyingine.


SEHEMU YA 3: MAMLAKA YA KUTIA HATIANI NA KUTOA ADHABHU YA KIJINAI.

Ili mtu akose sifa za kuwa mbunge lazima ahukumiwe au akutwe na hatia ya kosa la jinai la kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na mahakama tu na sio Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kama watu wengi wanavyoamini ikiwemo wanasheria na hii ni kwa sababu mbili zifuatazo

(a) Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma lina mamlaka ya kiuchunguzi ( investigatory jurisdiction )
na mamlaka ya kimapendekezo na ( recommendatory jurisdiction ) tu kwa mujibu Kifungu cha 26 (8) na 22 (5) na (6) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 ambapo Baraza la Maadili hufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma za kiongozi wa umma na kutoa mapendekezo kwa mamlaka za kinidhamu ya kiongozi wa umma na mamlaka za mashtaka ya kijinai na mamlaka za uchunguzi wa kijinai kama vile Ofisi ya DPP, PCCB na Ofisi ya DCI.

Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma halina kabisa mamlaka ya kumtia Kiongozi wa Umma hatiani ama hatia ya kimaadili ( ethical conviction ) au hatia ya jinai ( criminal conviction) wakati katiba inataka mtu akutwe na hatia ya kijinai ili kupoteza sifa za kuwa mbunge. Hivyo, mtu hawezi kupoteza sifa za kugombea ubunge chini ya Ibara ya 67 (2) (d) ya Katiba ya Nchi kutokana na ripoti ya uchuguzi na mapendekezo ya Baraza la Maadili kwa sababu uchunguzi na mapendekezo ya Baraza la Maadili hayamtii kiongozi wa umma katika hatia ya kimaadili au hatia ya kijinai.

Ni mahakama pekee ndo ina mamlaka ya kumtia katika hatia ya kijinia kiongozi wa umma kwa kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambapo uvunjaji huo unaambatana na utendaji wa kosa la jinai na mamlaka haya Mahakama inayapata chini ya masharti ya Kifungu cha 235 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura 20 (the Criminal Procedure Act, Cap. 20) yakisomeka pamoja na Kifungu cha 27 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398.


(b) Baraza la Maadili halina mamlaka ya kutoa adhabu za kijinai ( criminal penalties) ikiwemo faini na kifungo na halina mamlaka ya kutoa adhabu za kimaadili ( disciplinary sanctions ).

Ni mahakama pekee ndo ina mamlaka ya kutoa adhabu ya kijinai ya kifungo gerezani kwa kiongozi wa umma kwa kuvunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo yanaambatana na utendaji wa kosa la jinai kwa mujibu wa Kifungu cha 25 na 27 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (the Penal Code, Cap. 16) kikisomeka pamoja na Kifungu cha 27 (1) na (2) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398.


SEHEMU YA 4: KOSA LAZIMA LIWE LA JINAI NA ADHABU YAKE LAZIMA IWE YA KIFUNGO GEREZENI.

Ili mtu hakose sifa za kuwa mbunge kutokana na sababu ya kuvunja sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma lazima kosa ambalo ametiwanalo hatiani liwe ni kosa la jinai na adhabu ya kosa hilo lazima iwe ni ya kifungo gerezani kwa mujibu wa Ibara ya 67 (2) (d) ya Katiba ya Nchi. Hii ni kwa sababu Ibara ya 67 (2) (d) ya Katiba imeunganisha neno "kuhukumiwa" na neno "adhabu" kwa kutumia kiunganishi (conjunction) "na" (and), hii inamaana kwamba "hatia"
na "adhabu ya kifungo" kwa pamoja ndo vinamuondolea mtu sifa ya kuwa mbunge na sio kimojawapo pekee.

Hatia ya jinai pekee bila adhabu ya kifungo cha gerezani haiwezi kumondolea mtu sifa ya kuwa mbunge chini Ibara ya 67 (2) (d) ya Katiba na adhabu ya kifungo cha gerezani pekee bila hatia ya kijinai haiwezi kumondolea mtu sifa ya kuwa mbunge chini Ibara ya 67 (2) (d) ya Katiba. Ili mtu apoteze sifa za kuwa mbunge kutokana na sababu ya kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma lazima kuwepo vyote viwili yaani hatia ya kijinai na kifungo cha gerezani, hili ndo takwa na sharti bayana la Ibara ya 67 (2) (d) ya Katiba.


SEHEMU YA 5: HADHI NA ADHABU YA KOSA LA KUSHINDWA KUTANGAZA NA KUWASILISHA TAARIFA YA MALI NA MADENI.

Kosa la maadili la kushindwa kutangaza na kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamashna wa Maadili sio kosa la jinai chini ya masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398. Kuna makosa ya jinai mawili (2) tu ambayo yanatambuliwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 moja kwa moja.

Na kuna kosa moja lingine ambalo linatambuliwa na sheria hii (Sura 398) kupitia Kanuni zake yaani kupitia Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma ( Kutangaza Maslahi, Mali na Madeni) za 1996 ambazo ni Tangazo la Serikali Na. 108 la 1996 . Kanuni hizi kwa Kiingereza zinajulikana kama the Public Leadership Code of Ethics (Declaration of Interests, Assets and Liabilities) Regulations, 1996.

Makosa hayo 3 yanayotambuliwa moja kwa moja na Kifungu cha 27 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 na Kanuni ya 7 (1) na (2) ya Tangazo la Serikali Na. 108 la 1996 ni haya yafuatayo;

(a) Kutoa tangazo (declaration) la uongo kuhusu Mali na Madeni ya kiongozi wa umma.

(b) kutoa taarifa au tuhuma au ushahidi wa uongo dhidi ya kiongozi wa umma kuwa amevunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

(c) Matumizi mabaya ya taarifa kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma.

Pamajo na ukweli kwamba Kuna makosa ya jinai matatu (3) tu ambayo yanatambuliwa moja kwa moja na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 na Kanuni zake, hatahivyo, kila kitendo cha kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni kosa la jinai chini ya masharti ya Kifungu cha 81 cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura 1. Hii ni kwa sababu kila kitendo cha kuvunja masharti ya sheria iliyoandikwa ( written law ) yoyote ni kosa la jinai chini ya Kifungu cha 81 cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura 1(the Interpretation of Laws Act, Cap. 1) .

Sheria Iliyoandikwa (written law) ni sheria iliyotungwa na bunge (principal legislation) au sheria ndogo ndogo (subsidiary legislation) na sheria zilizopokelewa (received laws) kutoka nchi za nje hususani Uingereza na India na sheria za jumuia ya Afrika Mashariki.

Kosa la maadili la kushindwa kutangaza na kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamashna wa Maadili ni kosa la jinai chini ya masharti ya Kifungu cha 81 (1) (a), (b) na (c) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura 1.

Hata hivyo, adhabu ya kosa hili la kushindwa kutangaza Mali na Madeni sio kifungo bali ni faini ya Tshs 30, 000/= kwa kosa hili chini ya masharti ya Kifungu cha 81 (1) (a), (b) na (c) (iii) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura 1.

Iwapo mtu amepewa adhabu ya faini tu bila kifungo kama adhabu ya kutenda kosa la maadili linaloambatana na kosa la jinai basi mtu huyo hawezi kupoteza sifa za kuwa mbunge kwa sababu ili mtu apoteze sifa za kugombea ubunge lazima awe amepewa adhabu ya kifungo kutokana na kuvunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, 398.

Kwa kuwa kushindwa kutangaza na kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili ni kosa la jinai ambalo adhabu yake ni faini ya Tshs 30, 000/= basi kosa hili la jinai haliwezi kumuondolea mbunge mstaafu au mtu yoyote sifa ya kugombea Urais au ubunge kwa sababu Ibara ya 67 (2) (d) ya Katiba inaelekeza kuwa kosa la uvunjifu wa maadili linalomuondolea mtu sifa ya kuwa mbunge lazime liwe ni kosa la jinai ambalo adhabu yake ni kifungo cha gerezani.


SEHEMU 6: SABABU ZA MSINGI ZA KUSHINDWA KUTANGAZA NA KUWASILISHA TAARIFA YA MALI NA MADENI.

Kushindwa kutangaza na kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili moja kwa moja (automatically) ni kosa la Maadili chini ya masharti ya Kifungu cha 15 (a) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398.

Hata hivyo, sio kila kiongozi wa umma anayeshindwa kutangaza na kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili hutenda kosa la Maadili, la hasha.

Kiongozi wa umma akishindwa kutangaza na kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma uchukuliwa kuwa ametenda kosa la Maadili iwapo ameshindwa kufanya hivyo bila sababu za msingi.

Hata hivyo, Kiongozi wa umma akishindwa kutangaza na kuwasilisha taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili kutokana na sababu za msingi ( reasonable cause ) basi kiongozi wa umma huyo hana hatia yoyote ya kutenda kosa la maadili kwa mujibu wa Kifungu cha 15 (a) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398.

Kama Kiongozi wa umma hana hatia ya kosa la Maadili la kushindwa kutangaza Mali na Madeni kutokana na kuwepo kwa sababu za msingi basi Kiongozi wa umma huyo pia hana hatia ya kutenda kosa la jinai chini ya ya Kifungu cha 81 (1) (a), (b) na (c) (ii) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura 1.

Hivyo, Mhe. Tundu Lissu kwa sababu alishindwa kutangaza na kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili kutokana na sababu ya msingi ya kuwa nchi za nje Kenya na Ubelgiji (Belgium) kwa ajili ya matibabu kwa miaka takriban 3 kutokana na kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mjini Dodoma mwaka 2017, hivyo basi, Mhe. Tundu Lissu hawezi kutiwa hatiani kwa kosa la Maadili chini ya Kifungu cha 15 (a) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 na moja kwa moja (automatically) hawezi kutiwa hatiani kwa kutenda kosa la jinai linaloambatana na uvunjaji wa Sheria Maadili ya Viongozi wa Umma chini ya masharti ya Kifungu cha 81 (1) (a), (b) na (c) (ii) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura 1.

Kwa mazingira haya, Mhe. Tundu Lissu ana sifa ya kugombea Urais au ubunge kwa kuwa hawezi kutiwa hatiani kwa kutenda kosa la jinai linaloambatana na uvunjaji wa Sheria Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuwa alikuwa na sababu za msingi za kushindwa kufanya hivyo.


SEHEMU YA 7: HITIMISHO.

Kutokana na uchambuzi yakinifu hapo juu, ninayo haki itokanayo Mantiki ya Kisheria (Legal Logic) na ninayo nguvu ya maadili (moral authority) kufanya mahatimisho matano (5) yafuatayo;

(1) Mbunge Mstaafu au Kiongozi wa Umma au mtu yoyote atakosa sifa za kugombea Urais au ubunge kutokana na kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma chini ya Ibara ya 67 (2) (d) ya Katiba ya Nchi iwapo mtu huyo ametiwa hatiani na Mahakama kwa kutenda kosa la jinai linaloambatana na uvunjaji wa Sheria Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 na kupewa adhabu ya kifungo gerezani. Mhe. Tundu Lissu haijawai kutiwa hatiani na Mahakama kwa kutenda kosa la jinai linaloambatana na uvunjaji wa Sheria Maadili ya Viongozi wa Umma na haijawai kupewa adhabu ya kifungo gerezani kutokana na kosa hili.

(2) Mbunge kushindwa kutangaza na kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamashna wa Maadili ya Viongozi wa Umma ni kosa la jinai (criminal offence), hata hivyo, kosa hili haliwezi kumuondolea mbunge mstaafu, kiongozi wa Umma au mtu yoyote sifa ya kugombea Urais au ubunge kwa sababu adhabu yake ni faini pekee ya Tshs 30, 0000/= na sio kifungo gerezani. Hivyo basi, kwa ajili ya kujenga hoja tu (for sake of argument only) hata kama Mhe. Tundu Lissu angetiwa hatiani kwa kosa la jinai kutokana na kushindwa kutangaza na kuwasilisha Taarifa ya mali na madeni kwa Kamashna wa Sekretarieti ya Viongozi wa Umma bado angeendelea kuwa na sifa ya kugombea Urais na ubunge kwa sababu adhabu ya kosa hili ni faini tu na sio kifungo cha gerezani.

(3) Kama Kiongozi wa umma ameshindwa kutangaza Mali na Madeni kutokana na sababu za msingi basi Kiongozi wa umma huyo hana kabisa hatia ya kutenda kosa la maadili na hana hatia ya kutenda kosa la jinai. Mhe. Tundu Lissu kwa sababu alishindwa kutangaza na kuwasilisha Taarifa ya Mali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili kutokana na sababu ya msingi ya kuwa nchi za nje Kenya na Ubelgiji (Belgium) kwa ajiri ya matibabu hawezi kutiwa hatiani kwa kosa la Maadili na hawezi kutiwa hatiani kwa kutenda kosa la jinai linaloambatana na uvunjaji wa Sheria Maadili ya Viongozi wa Umma.

(4) Hivyo basi, Mhe. Tundu Lissu ana sifa zote za kuteuliwa na kuchaguliwa kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya masharti ya Ibara ya 67 (1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

(5) Kwa kuwa Mhe. Tundu Lissu ana sifa zote za kuteuliwa na kuchaguliwa kuwa mbunge basi moja kwa moja (automatically), Mhe. Tundu Lissu ana sifa zote za kuteuliwa na kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini masharti ya Ibara ya 39 (1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

Mungu Ibariki Tanzania.
 
Hakuna chochote hapa unapoteza tu nguvu. kesho anapewa fomu, atajaza atarudisha
 
Asante kwa ufafanuzi mzuri. Ukiwa na simu mbovu nitafute nitakutengezea kwa bei poa ama vitu vinavyo tumia umeme
 
Asante sana kiongozi nitakutafuta, huko vizuri sana kwenye marketing
Karibu naandika pia kitabu cha ujasiriamali, ili wale wanao ilaumu serikali kuhusu masoko waache, kiko hatua za mwisho naandika kitabu mama ambacho kitakuwa kwa kimombo chenye lugha rahisi kwaajili ya kada zote .Serikali inatakiwa ilaumiwe kwenye sera mbovu
 
Karibu naandika pia kitabu cha ujasiriamali, ili wale wanao ilaumu serikali kuhusu masoko waache, kiko hatua za mwisho naandika kitabu mama ambacho kitakuwa kwa kimombo chenye lugha rahisi kwaajili ya kada zote .Serikali inatakiwa ilaumiwe kwenye sera mbovu

Ninakutakia kila la kheri katika juhudi zako za kutoa elimu kwa wajasiriamali.
 
Ooh,sawa kabisa lakini hapo kwenye mahakama hujataja in mahakama ipi yenye mamlaka ya kumtia hatiani kiongozi
 
Aisee, asante sana ndugu...

Umetoa elimu maridhawa sana ya sheria...

Na kwa kweli, mjadala huu wa anastahili au hastahili utakuwa umefungwa rasmi sasa...

Ambao hawataelewa, watakuwa wameamua wenyewe kuwa wajinga kwa hasara yao....
 
Ooh,sawa kabisa lakini hapo kwenye mahakama hujataja in mahakama ipi yenye mamlaka ya kumtia hatiani kiongozi

Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa na Mahakama ya Wilaya zote zina uwezo wa kumtia kiongozi wa umma au mtu mwingine kwa kutenda kosa la jinai chini ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398.

Hatahivyo, kuna swala la kitaalamu hapa ambalo nitalieleza kesho.
 
Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa na Mahakama ya Wilaya zote zina uwezo wa kumtia kiongozi wa umma au mtu mwingine kwa kutenda kosa la jinai chini ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398.

Hatahivyo, kuna swala la kitaalamu hapa ambalo nitalieleza kesho.
Hebu tuwekee hizo sheria PDF hapa
 
Back
Top Bottom