SoC01 Uvumilivu: Changamoto kubwa ya vijana kushindwa kujiajiri

Stories of Change - 2021 Competition
May 7, 2021
29
64
Uvumilivu ni ile hali ya kustahimili machungu.Mtu yoyote ni lazima ajenge tabia ya kustahimili machungu,kwenye kuvumilia ndipo uzoefu wa kufanya kazi kwa mafanikio unakopatikana.Uzoefu ni hali ya kukaa na jambo au kitu kwa muda mrefu. Kwenye ujasiriamali uzoefu ni jambo kubwa na la muhimu,ili kuijulia kazi yako ni lazima uwe na uzoefu na uzoefu unapatikana kutokana na kuvumilia kazi unayoifanya.

Septemba 14,2021 nilimtembelea Juma Mshola(34) mkulima wa vitunguu mwenye mafanikio wilayani Simanjiro mkoani Manyara anasema "vijana wengi wanafikiria kuwa na mtaji ndiyo jambo muhimu kwenye kujiajiri lakini uvumilivu na uzoefu ndiyo vitu vya msingi ambavyo kijana anayetaka kufanya biashara au shughuli yoyote ya kijasiriamali anatakiwa avijue,mtaji unaweza kukopa au kupewa lakini uvumilivu hakuna anayeweza kukupa"

Duniani kote kuna tatizo kubwa la ukosefu wa ajira na nchi zinazoendelea ndiyo kuna tatizo kubwa zaidi nchi zilizoendelea zina uchumi mkubwa unaowezesha kuwa na makampuni makubwa,viwanda vingi na vikubwa pamoja,sekta imara ya fedha na shughuli nyingi za kiuchumi zinazosaidia kuajiri watu wengi tofauti na nchi zinazoendelea ambazo zina uchumi mdogo ambao hauwezeshi watu wengi kuajiriwa.

Kwa nchi yetu yenye uchumi mdogo Serikali ndiyo muajiri mkuu lakini inaajiri watu wachache chini ya 700,000,Tanzania kampuni kubwa binafsi inayoajiri watu wengi na iliyoweka taarifa zake wazi ni Mohamed Enterprises Tanzania Limited(MeTl)ambayo imeajiri watu 24,000.

Marekani nchi wenye watu milioni 333,378,983 kuna watumishi wa umma milioni 2 na laki moja,sekta binafsi imeajiri watu 107,800,000,kampuni kubwa inayoajiri watu wengi Marekani ni Walmart ambayo imeajiri watu 2,200,000 na kati ya hao milioni moja na laki tatu wapo Marekani,wengine wapo nje ya Marekani.Kampuni ya Amazon imeajiri watu 1,298,000 na kati ya makampuni makubwa 10 ya Marekani yaliyoajiri watu wengi kila moja imeajiri watu zaidi ya 300,000.

Afrika kusini wapo 59,308,690 watumishi wa umma ni milioni 1 na laki moja.Kenya ina watu milioni 46 na laki sita ina watumishi wa umma 700,000,makampuni makubwa yanayoajiri watu wengi Kenya ni Safari com iliyoajiri watu 5500 na Equity bank iliyoajiri watu 8,959.

Kwahiyo suluhisho la ajira kwa nchi zinazoendelea ni kwa mtu mmoja mmoja kujiajiri kwa sababu serikali inaajiri watu wachache na sekta binafsi inaajiri watu wachache ingawa kila mwaka kuna wahitimu wengi wa vyuo vikuu,vyuo vya kati,vyuo vya ufundi pamoja na wale waliomaliza kidato cha sita na cha nne wanaoingia mtaani kusaka ajira ambazo hazipo.

Kwa nchi yetu pamoja na kuwepo changamoto lukuki zinazokwamisha vijana kujiajiri lakini changamoto ya uvumilivu na uzoefu ndizo za msingi na vijana wengi wanashindwa kuvumilia machungu ya kujiajiri ambayo yanapatikana mwanzoni tu.Mwanzoni kuna changamoto nyingi ambazo zinaumiza kuna kupata hasara,kufirisika na nyinginezo ambazo zinasababishwa na kutokuwa na uzoefu. Hata hivyo haitakiwi kukimbia kwani uzoefu unapatikana kwa kutoikimbia biashara au shughuli nyingine za ujasiliamali,jifunzekwa wenzako waliotangulia na waliofanikiwa.

Juma Mshola baada ya kumaliza kidato cha nne mwaka 2007 alianza kulima vitunguu akiwa hana uzoefu alianza kulima heka moja ambayo yote ilishambuliwa na ukungu alirudi kulima tena mwaka 2010 kwa kuanza na nusu heka ambako alijifunza taratibu kilimo cha vitunguu kwa kufuata kanuni za kilimo bora,kutumia mbegu bora na madawa bora ya kuua wadudu"ili ufanikiwe kwenye kilimo cha vitunguu ni lazima upate shamba zuri,upate mbegu bora lakini kama huna uzoefu unaweza kupata shamba baya,mbegu mbaya na madawa mabaya"anasema Mshola.

Mshola anasema mwaka 2010 alilima vitunguu akiwa na mtaji mdogo"kuanzia 2010 mpaka 2013 mambo yalikuwa magumu,nilikuwa napata hasara".

Lakini uvumilivu na uzoefu ulimfanya afanikiwe kwani sasa hivi analima heka 20,amejenga nyumba mbili,anawasomesha wadogo zake,amenunua fuso moja na pia anamiliki duka la kuuza pembejeo lakini kikubwa na anachojivunia ameweza kuajiri vijana wenzake zaidi ya 10 "vijana wakizingatia kilimo watafanikiwa ila inatakiwa nia hasa, unataka kufanya nini na una lengo gani,mtaji wa kwanza ni wewe mwenyewe ambako ndani yake kuna uvumilivu, uzoefu,afya njema na kujituma"alisema Mshola.

Samuel Moore Walton ambaye wazazi wake walikua mafukara waliokua wanahama kutoka mji mmoja kwenda mji mwingine kwa ajili ya kutafuta unafuu wa maisha alianzisha biashara ya duka lake la kwanza nchini Marekani mwaka 1945 kwenye mazingira magumu mtaji alikopa kwa baba mkwe wake na pia alikua na fedha kidogo alizopata baada ya kuacha jeshi baada ya kupitia changamoto nyingi mwaka 1962 ndiyo aliweza kufungua mtandao wa maduka ya Walmart ambayo yametapakaa sehemu nyingi Duniani na mpaka sasa Walmart ndiye muajiri mkuu Duniani.Kama Walton angekata tamaa na kushindwa kuvumilia machungu leo hii watu 2,200,000 Duniani wasingekuwa waajiriwa wa Walmart.

Kwa hapa Tanzania somo la uvumilivu pia tunalipata kutoka kwa Aristablis Elvis Musiba mwandishi mashuhuri wa Riwaya za upelelezi ambaye ameandika vitabu kama Njama,Kikosi cha kisasi,Kikomo na Hujuma lakini uandishi wa vitabu hivyo haukua rahisi kwani mswada wake wa kwanza wa Riwaya alivyoupeleka kuchapwa meneja wa kizungu kwenye kampuni ya uchapaji alivyoona umeandikwa kwa kiswahili alimrushia usoni lakini Musiba hakukata tamaa aliupeleka kwenye kampuni nyingine na kuchapwa.

Vitabu cha Musiba viliuza sana na fedha hizo alizitumia kuanzisha biashara kama biashara ya duka la kubadilishia fedha za kigeni duka hilo lilimfanya awe Mtanzania wa kwanza mzawa kufungua duka la kubadilishia fedha za kigeni ambalo hata hivyo baada ya muda lilitaifishwa na serikali.Pamoja na changamoto hizo Musiba hakukata tamaa aliendelea kufanya biashara zingine zilizopelekea kutajirika na mafanikio hayo yaliwavutia wafanyabiashara wenzake ambao walimchagua kuwa Mwenyekiti wa sekta binafsi nchini na Mwenyekiti wa baraza la wafanyabiashara wa Afrika mashariki.

Mpaka anafariki Oktoba 31,2010 alikuwa ametajirika vya kutosha.


IMG-20210927-WA0001.jpg


Picha kutoka mtandaoni ikionyesha
makao makuu ya kampuni ya Walmart iliyopo nchini Marekani ambayo muanzilishi wake Samuel Moore Walton alijiajiri kwa kuanza na duka moja dogo lakini sasa hivi kuna utitiri wa maduka hayo na ndiyo kampuni inayoongoza Duniani kwa kuajiri watu wengi.

Kwa kifupi kwa sasa Duniani kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira na suluhisho pekee ni kujiajiri lakini kujiajiri si kitu rahisi inabidi kuvumilia changamoto zinazotokana na kujiajiri.


Naomba mchangie mjadala na naomba kura zenu nyingi.
 
Umenikumbusha mwandishi mahiri kuwahi kutokea Tanzania wa Riwaya Elvis Musiba na character wake Willy Gamba sikujua Kama alipitia changamoto zote hizo.
 
Serikali isiwalipishe kodi na malipo ya leseni kwa watu wanaofungua biashara kwa mara ya kwanza.Ni lazima Serikali itengeneze mazingira mazuri ya watu kujiajiri.
 
Umenikumbusha mwandishi mahiri kuwahi kutokea Tanzania wa Riwaya Elvis Musiba na character wake Willy Gamba sikujua Kama alipitia changamoto zote hizo.
Elvis Musiba alikua mwandishi mahiri aliweza kumchora Gamba utafikiri alikuwa mtu wa ukweli.
 
Serikali isiwalipishe kodi na malipo ya leseni kwa watu wanaofungua biashara kwa mara ya kwanza.Ni lazima Serikali itengeneze mazingira mazuri ya watu kujiajiri.
Serikali ingeondoa kodi kwa wajasiriamali wapya wanaweza kuwapa Grace period kama wanavyofanya kwa wawekezaji wakuja.
 
4 Reactions
Reply
Back
Top Bottom