Uvujaji mapato ya madini tishio: Ni Mara Nne ya Misaada inayotolewa na Wafadhili...

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,869
1,225
Ripoti maalumu Uvujaji mapato ya madini tishio

Ni mara nne ya misaada inayotolewa na wafadhili
Wataalamu washauri namna ya kudhibiti uvujaji huo

KATIKA hali ya kawaida kwa jinsi nchi inavyopoteza mapato katika madini ilipaswa Mikataba ya Uchimbaji (MDAs) iliyopo ifutwe, lakini kwa kuwa hilo haliwezakani, basi Tanzania iungane na nchi nyingine kushinikiza kampuni za uchimbaji madini ziweke wazi ripoti za mapato na matumizi.

Mratibu wa taasisi inayojihusisha na masuala ya sera Tanzania, Policy Forum, Semkae Kilonzo, anasema haina maana kuendelea kulalamika kuhusu mikataba mibovu ya uchimbaji madini kwa vile haiwezi kubadilishwa sasa.

" Tuwe wakweli. Mikataba ile hatuwezi kuibadili. Tuliambiwa hapa kwamba wanaipitia mikataba hiyo. Lakini mpaka sasa hatujui walipitia mikataba mingapi? Ipi? Nusu au yote? Na matokeo ni nini?

"Kwa mikataba ile migodi haitatusaidia. Tuliwaita wenyewe, wakaja wakachunguza mifumo yetu ya fedha wakatengeneza ya kwao ili kuweza kuwekeza hapa, tukaingia mikataba wenyewe. Leo huwezi kusema basi tunaivunja mikataba ile. Watasema nini kwa wanahisa wao?," anasema Kilonzo.

Kwa mujibu wa Kilonzo dawa si kung'ang'ania mikataba ibadilishwe bali kuungana na nchi nyingine kuhakikisha kwamba uhamishwaji wa fedha kiasi "kisichopungua trilioni moja kinachotoroshwa kutoka katika nchi zinazoendelea, nusu yake, zaidi ya dola za Marekani bilioni 500 zikitoka Bara la Afrika, unakomeshwa".

Anasema fedha hizo zinazovushwa zinadhihirisha kiwango cha juu cha uhalifu, ufisadi, na ukwepaji kodi na kinawakilisha hali "isiyokubalika ya uyumbishaji wa uchumi wa nchi zinazoendelea, ambacho ni sawa na mara nane ya kiwango cha misaada ya fedha za kigeni".

Katika hali hiyo nini kifanyike? Anasema Kilonzo: " Waafrika wanaweza kunufaika kwa kufanya mabadiliko chanya na kushirikiana na mataifa mengine kwa kubadilishana taarifa za fedha, mauzo, faida, na taarifa za kodi zinazolipwa na kampuni za wawekezaji wa kimataifa katika mfumo uitwao country by country reporting.

"Wananchi wafahamishwe kwa uwazi habari za mapato ya kodi kutoka kwenye mashirika yote. Ili nchi zinazoendelea zinufaike kiuchumi ni vyema kuwapo mfumo mzuri unaotenda haki kwa pande zote, ili kufanikisha ndoto za usawa katika mapato."

Anasema inawezekana kabisa kwamba mikataba ile mibovu iliingiwa kwa woga wa kukosa wawekezaji kwa vile hata katika eneo la Afrika Mashariki nchi za eneo hilo zimekuwa zikishindana zenyewe kuweka viwango vya chini ili kuvutia wawekezaji.

" Tuna uwoga mkubwa. Hata sasa hivi tumeanza kutishiwa kuhusu gesi. Eti kwamba Msumbiji nao wanachimba yao. Lakini ukweli ni kwamba mkisimamia malengo yenu wawekezaji watakuja tu. Gesi iko kibao hapa, wasije kwa nini," anahoji.

Kwa maoni yake tatizo kubwa analoliona ni jinsi ya kuunganisha mfumo ili sekta ya uziduaji iweze kukuza sekta nyingine na hivyo kukuza mapato hasa katika sekta za huduma.

"Itakuwa vigumu kuweza kupata manufaa kama sekta ya uziduaji haitahusiana na sekta nyingine. Haitatusaidia sana kama walinzi, mahitaji kama vyakula na huduma nyingine badala ya kuzalishwa nchini ziwe zinatoka nje," anasema Kilonzo.

Apronius Mbilinyi ni mtafiti wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), kwa maoni yake matatizo ya upotevu wa mapato yatokanayo na uziduaji nchini Tanzania ni ya kujitakia.

"Hakuna utashi wa kisiasa wala wa watu kujitoa. Kuna mifano mingi ya nchi zilizofanikiwa. Huku kwetu iko Botswana. Wao waliweza vipi ambacho sisi tumeshindwa?

"Kwa hiyo ukiniuliza kwamba tunapata mapato stahiki kwenye migodi yetu nitasema ndiyo na hapana. Ndiyo kwa sababu mikataba tuliyoingia na kampuni za kimataifa zinazoendesha migodi inatuingizia hicho kidogo tunachopata. Hapana kwa sababu mikataba hiyo inazipendelea sana kampuni hizo, haina manufaa kwetu. Na tumetoa misamaha mingi ya kodi.

"Mikataba hii ina matatizo makubwa. Kama si uwoga na wanasiasa kukosa utashi ungeweza kusema jamani naivunja kwa sababu wenye mali, yaani wananchi, hawaridhiki, dunia ingekuelewa, lakini jeuri hiyo hatuna. Ndiyo maana nasema wenye matatizo ni sisi. Itabidi siku zijazo tuingie mikataba ya win win (asilimia 50 kwa asilimia 50)," anasema.

Kwa mujibu Mbilinyi, Tanzania ni kati ya nchi tajiri wa maliasili kwa vigezo vya Shirika la Fedha la Kimataifa (IFM) vinavyotaja kwamba nchi yoyote yenye kufikisha mapato ya asilimia 25 yatokanayo na maliasili zake ni tajiri wa maliasili.

"Ukiangalia takwimu za Wizara ya Nishati na Madini, sisi ni tajiri wa maliasili. Lakini, je, tunafaidika na maliasili hizo, jibu ni hapana. Duniani kote wafanyabiashara hupangilia masuala ya kodi. Sisi hapa tumesema kodi ya shirika, kwa mfano, itokane na faida.

"Faida hupatikana baada ya kuondoa gharama za uwekezaji, sisi hatuna namna wala uwezo wa kujua gharama hizo za uwekezaji, maana, pamoja na mambo mengine, jamaa hawa hufanya biashara na kampuni tanzu zao zilizoko nje ya nchi. Huwezi kupata hesabu zao za huko nje, hivyo wanachotaka tujue ndicho tunachokiona, na kila mwaka wanasema wameongeza uwekezaji," anasema.

Mbilinyi anasema ni muhimu kwa Tanzania kujenga uwezo kwa maana ya rasilimali watu, taasisi na sheria ili changamoto za kwenye shughuli za madini zisihamie kwenye gesi na mafuta.

Meneja wa Ukaguzi wa Kodi wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), Venance Bahati Mwase, anasema masuala wanayohusika nayo katika sekta ya madini yanategemea mambo mawili makubwa; suala la sheria zilizopo zinazotawala taratibu za fedha ama fiscal regime na usimamizi.

"Hapa kuna mambo ya sheria na usimamizi wa sheria. Sisi tupo katika usimamizi. Unasimamia sheria zilizopo hata kama ni mbaya kwa kuwa ndizo zilizopo. Kama mgodi unatakiwa kulipa kodi ya shirika baada ya kutengeneza faida kwa mujibu wa sheria, sisi tunahakikisha hiyo inafanyika," anasema Venance Mwase.

Anaongeza: "Kama mgodi unatakiwa kulipa kodi ya zuio kwa mujibu wa sheria, sisi tunahakikisha hilo linafanyika. Kama ni mrabaha kwa mujibu wa sheria hilo tunahakikisha linafanyika.

"Kwa hiyo kwa kuangalia utendaji wa chombo hiki kwa maana ya usimamizi naweza kusema usimamizi umeimarishwa sana. Kila ambacho kinapaswa kulipwa na kampuni kwa mujibu wa sheria sisi tunahakikisha kinalipwa. Zile njia imara za usimamizi kwa mujibu wa sheria zipo."

Mwase anasema ni kweli kuna changamoto katika suala la mapato yatokanayo na madini na matarajio yao ni kwamba mwaka huu wanaweza kuwa na ripoti nzuri zaidi ya hali halisi ya mambo yalivyo.

"Ngoja nikuambie. Chombo hiki kinafanya kazi nzuri. Na ushahidi wa jambo hilo ni kwamba hata wakati kinaanzishwa kampuni za migodi hazikukipenda sana. Na tunashirikiana vizuri na vyombo vingine ambavyo havikuwa vikituelewa vyema wakati TMAA ikianzishwa.

" Sasa hivi kwa mfano tuna makubaliano na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tunakutana kila baada ya miezi minne kuangalia kuna changamoto zipi katika sekta, tunakabiliana nazo vipi na ushirikiano wetu unakwenda vizuri," anasema.

Ukiacha uwezo huo wa usimamizi, TMAA ina maabara ambayo inapima kila aina ya mzigo kwa maana ya thamani na ubora.

"Hapa hakutoki kitu bila kupimwa. Hata huo mchanga mnaosikia huko mitaani kwamba umevushwa si kweli. Mzigo wowote unaopelekwa nje lazima kwanza upimwe hapa. Na hii ni kazi ya kila siku kwa mzigo wowote unaokwenda nje," anasema Meneja wa Maabara, Mhandisi Mvumilwa Mwarabu.

Anasema pia Mwarabu: Hapa zikanuja sampuli za kila mgodi. Kila mgodi una nembo yake. Tunahakikisha kwamba sampuli hizo hazichanganywi ili kuweza kuzichambua vizuri. Ni hapa unapojua kwa hakika kwamba hii ni dhahabu. Ukishakufanya mchujo mwishoni utabakiwa na dhahabu, madini mengine kama fedha yanakuwa yametengwa.

"Waambie wananchi huko nje wajue kwamba wakija hapa, hata kama wanataka kuuza madini yao, tutawapimia na watajua kwamba wanauza dhahabu kiasi gani, au shaba au fedha kiasi gani. Kwa njia hiyo wataweza kujua thamani ya madini yao kabla hata ya kuyauza."

Anasema kwa ubora wa maabara hiyo wamekuwa wakipokea wataalamu wengine wa nchi kama Mali, Sierra Leone na Zambia wanaokuja kujifunza.


Source: Raia Mwema
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom