Utumishi yajitosa kujibu hoja za Tucta

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
Tucta%2816%29.jpg

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta).



Malumbano kati ya serikali na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), yamezidi kushika kasi nje ya meza ya majadiliano, baada ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kusema tamko la Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo kuhusu mgomo wa wafanyakazi lilitolewa juzi, limepotosha umma na kwamba, hawajamdanganya Rais.
Kauli hiyo, ambayo ilitolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi, jijini Dar es Salaam jana, inafuatia tamko la Tucta juzi kwamba, wasaidizi wa Rais Jakaya Kikwete walimdanganya na kumpotosha kuhusu ukweli wa majadiliano kati yao na serikali juu ya maslahi ya wafanyakazi.
Yambesi, alisema Tucta wamekanusha kuendelea kwa majadiliano kati yao na serikali kuhusu kima cha chini cha mshahara kwa vile tayari walishakubaliana kutokukubaliana, wakati siyo sahihi.
Alisema hoja ya Tucta si sahihi kwani majadiliano kuhusu suala hilo yanaendelea. “Kwa mujibu wa vifungu vya 18 na 19 vya Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma namba 19 ya mwaka 2003, majadiliano yanaweza yakafikia makubaliano na kwa kwakati mwingine yasifikie makubaliano…Hivyo, ninapenda kusisitiza kuwa majadiliano hayajaisha na bado yanaendelea,” alisema.
Alisema Tucta pia walidai kuwa badala ya kujadili mapendekezo ya wafanyakazi ya kuhuisha mifuko ya hifadhi ya jamii ili itoe mafao yaliyo bora kama yanayotolewa na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), wawakilishi wa serikali waliacha suala la msingi, wakasimamia kufanyika kwa uteuzi wa Mdhibiti na Msimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Yambesi alisema haina usahihi wowote kwa vile kwa kawaida majadiliano na makubaliano yanayofikiwa ndani ya baraza, ni ya wajumbe wote wa Baraza la Majadiliano ya Pamoja. Katika majadiliano, ilibainika kuwa suala la ubora wa mafao linategemea sheria, kanuni na taratibu za mifuko husika, ambapo masuala ya uchangiaji, ukokotoaji na ulipaji wa mafao hufanyika na kwamba, wajumbe wote wa Baraza walikubaliana kuwa uteuzi ukamilike kabla au ifikapo Septemba 30.
Yambesi alisema Tucta pia, ilieleza Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Juma Kapuya, Aprili 19, mwaka huu alitangaza ongezeko la asilimia 100 bila kufuata taratibu za sheria namba 7 ya mwaka 2004 na kushusha baadhi ya vima vya mishahara, kama vile viwanda, ambavyo kima cha chini kimeshuka kutoka Sh. 150,000 hadi 80,000 kwa mwezi.
Alifafanua kuwa taratibu zote zinazoelezwa kisheria kuhusu utangazaji wa vima vya chini vya mishahara zimezingatiwa na kutekeleza vilivyo na kwamba, siyo sahihi kuwa viwango vyote vya mishahara vimepandishwa kwa asilimia 100.
Alisema viwango vipya vya mishahara vimeainishwa katika Tangazo la Serikali Namba 172 lililochapishwa katika Gazeti la Serikali la Aprili 30, mwaka huu na kuwashauri waandishi wa habari, wafanyakazi na wananchi kwa jumla kulisoma.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom