Utulivu wa maji ndani ya mtungi, au tunanyolewa? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Utulivu wa maji ndani ya mtungi, au tunanyolewa?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Oct 17, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Oct 17, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,773
  Likes Received: 83,114
  Trophy Points: 280
  Utulivu wa maji ndani ya mtungi, au tunanyolewa?

  Rai ya Jenerali Ulimwengu Oktoba 15, 2008
  Raia Mwema~Muungwana ni itendo

  HEBU sasa tujaribu kuchora picha ya hali ya nchi yetu, lengo likiwa ni kuainisha ukweli wa maisha yetu kama Taifa, hatua za maendeleo tulizopiga, matatizo yanayotukabili na nini tunahitaji kufanya ili tuweze kwenda mbele zaidi, na katika maeneo kadhaa, tuache kurudi nyuma.

  Kwanza ningependa tutambue kwamba si lazima tuendelee, hakuna sheria ya maumbile inayosema kwamba maendeleo ni lazima na yatakuja tu, tutake tusitake. Maendeleo yanakuja kwa utashi wa jamii na uamuzi wa dhati wa jamii hiyo kujivuta kutoka hali duni na kwenda katika hali ya unafuu wa maisha.

  Utashi wa dhati ninaoutaja hapa ni tofauti na kutamani tu kuwa na maisha bora bila kuchukua hatua za dhati za kuyatafuta. Ni tofauti na kutoa matamko matamu na kuimba nyimbo za kuvutia kuhusu maendeleo na maisha bora. Utashi wa dhati hauna budi kuandamana na matendo yenye murua, na wakati mwingine kuchukua hatua ngumu zinazoumiza.

  Uthibitisho kwamba maendeleo si lazima kwa kila jamii tunaupata katika mifano mingi ambayo sina shaka msomaji ataitambua kirahisi. Hebu tuangalie mfano wa Haiti, nchi ambayo inatambulika kama jamhuri ya kwanza ya Mtu Mweusi duniani, mfano wa ushujaa wa Waafrika waliokuwa watumwa na walioamua kuchukua silaha na kujikomboa dhidi ya mabwana zao zaidi ya miaka 200 iliyopita.

  Simulizi za ushujaa huo zinasisimua kwa kila Mwafrika anayeumizwa na historia ya uonevu waliofanyiwa Waafrika na watu weusi kwa karne kadhaa. Mfano wa kiongozi wa uasi wa Haiti, Toussaint L'Ouverture na wapiganaji wake, na jinsi walivyoweza kupambana na Wafaransa waliokuwa na kila aina ya silaha na kuwashinda ni jambo la kujivunia na ambalo limewekwa katika kumbukumbu ya kudumu katika vitabu, tamthilia na nyimbo.

  Pamoja na hayo, Haiti ya leo ni nchi masikini, iliyovurugika, iliyokata tama, isiyotawalika, isiyo na heshima mbele ya mataifa mengine. Ule moto uliowashwa na Toussaint umezimika kabisa, hata majivu yake hayaonekani tena. Ni historia ya kutia simanzi kwa Waafrika duniani kote, lakini pia ni funzo kwamba maendeleo si lazima kama jamii husika haifanyi juhudi endelevu za kujiendeleza.

  Bila shaka miaka 200 ni muda mrefu, lakini na sisi kama Taifa tumekwisha kuihesabu. Miaka mitatu ijayo tutakuwa tumetimiza miaka 50 tangu tupate Uhuru, nusu karne ya "kujitawala." Hiyo ni robo ya miaka ya "kujitawala" ya Haiti. Hebu tujiangalie tulivyo, halafu tujiulize maswali yafuatayo:

  Iwapo tutaenenda kama tulivyoenenda katika miaka hii 50 ya kwanza kwa kipindi kingine cha nusu karne, tutakuwa tumefikia hatua gani ya maendeleo?

  Je, tunaona dalili kwamba tutakuwa tumekwenda mbele zaidi au tutakuwa tumerudi nyuma?

  Je, hatuoni hatari ya kuja kuwa kama Haiti iwapo tutasafri vipindi vingine vitatu vya nusu karne na kutimiza miaka 200?

  Ni nini tumejifunza kutokana na uzoefu wetu wa juhudi za kuleta maendeleo, na ni mabadiliko gani tunatakiwa kuyafanya ili tuepukane na matatizo yaliyotukwaza huko nyuma ili tusirudie makosa tuliyokwisha kuyafanya?

  Haya ni baadhi ya maswali ambayo hatuna budi kujiuliza, lakini yako mengi zaidi, na kila mmoja wetu anaweza akairefusha orodha ya matatizo hayo kutokana na mtazamo wake na uzoefu wake binafsi. Lakini kwa pamoja hatuna budi kufanya ukaguzi/uchunguzi wa hali yetu kama Taifa na tutathmini matatizo tuliyo mkabala nayo.


  Baada ya nusu karne, taswira niliyo nayo ya nchi yetu ni hii ifuatayo.

  Tanzania imeendelea kuwa nchi ya amani kwa kiasi kikubwa, tukiacha matukio ya hapa na pale ambayo yametutikisa kidogo lakini hayajatuyumbisha. Sifa hii si haba, hasa tukikumbuka kwamba nchi yetu inapakana na nchi zilizokumbana na tufani za kutisha za mifarakano ya kisiasa, vita na hata mauaji ya halaiki ya mara kwa mara.

  Hata hivyo, si busara kuimba siku zote kwamba nchi yetu ni nchi ya "amani na utulivu" na kusahau kwamba amani hiyo inaweza kutoweka iwapo tutazidharau dalili mbaya tunazoziona zikiashiria matatizo makubwa ya hapo baadaye. Ishara hizo ndizo nitakazozijadili leo na katika makala zitakazofuata.

  Kwanza najiruhusu kusaili dhana hii ya "amani na utulivu." Sina tatizo na neno "amani" kwani hiyo ndiyo sala ya kila jamii na kila taifa. Tatizo langu linajitokeza ninapokutana na neno "utulivu". Inawezekana tatizo langu hilo linatokana na nakisi ya kimsamiati ambayo huisumbua sana lugha yetu na kuwakwaza watumiaji wake. Inawezekana neno lililokusudiwa ni "utangamano," au "maridhiano," au "maelewano." Ungeweza hata kuongeza "upendo."

  Tatizo langu na neno "utulivu" ni kwamba haliendani kabisa na hali ya watu masikini waliodhamiria kuboresha maisha yao kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Hii ni nchi ya watu ambao wanatakiwa wawe wanahangaika huko na huko, watu waliochangamka, wanaochakarika kusaka maendeleo yao, wakiwania kugeuza maliasili ya nchi yao kuwa utajiri na furaha.

  Ndiyo maana sikubaliani hata kidogo na mtazamo wa "utulivu," neno linalonipa picha ya watu waliopigwa ganzi, waliozubaa na kubweteka, walioridhika na uduni wa maisha yao na wasio na kitu wanachokitaraji katika maisha yao.

  Najiuliza, katika ile misemo miwili ya Kiswahili sisi tumeteua upi katika kujisifia kuwa watulivu? Je, ni ule utulivu wa maji ndani ya mtungi, au ni ule utulivu "kama unanyolewa"? Kati ya maji mtungini na kunyolewa hakuna hata moja linalonipa faraja. Na wala sipati faraja kwa kujua kwamba makaburini kuna « utulivu » mkubwa kuliko mahali po pote pengine. Kwa kiasi fulani utulivu ni dalili ya ufu.


  Aidha, hatuna budi kukumbushana kwamba « amani » siyo sera ya chama cho chote wala serikali yo yote. Sera haina budi kutokana na uchaguzi wa makusudi kati ya mikondo kadhaa ya kufuata. Amani si mojawapo ya mikondo hiyo, na hivyo haiwezi kuwa sera. Amani ni matokeao ya sera nzuri zilizotekelezwa vizuri.

  Katika makala zijazo nitajadili mambo ambayo naamini kwamba yasipoangaliwa kwa uangalifu yanaweza yakawa ni chanzo cha mwisho wa wimbo wetu wa « amani na utulivu .» Nia kuu katika kuyajadili haya ni kuendeleza kile kile ambacho nimekuwa nikikiandika tangu takriban mwaka mmoja, yaani umuhimu wa kujenga misingi ya uongozi bora ambayo ndiyo nyenzo pekee ya kuleta maendeleo kwa ajili ya watu wetu ambao tumewasababishia ubeuzi wa hatari.

  Naamini kwamba ni jukumu la kila mzalendo kupigana na mshawasha wa ubeuzi, kwa sababu ubeuzi haujengi bali unaua jamii kwa kufisha nyoyo za watu wake.
   
Loading...