Utembelee nyota ya Magufuli kama taifa?

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
MWAKA wa 2015 ni mwaka ambao watanzania tunapaswa kuukumbuka sana. Ni mwaka ambao taifa letu lingeweza kuangamia. Kama ni treni basi treni iliyokwishatoka kwenye reli ingepinduka kabisaa! Bahati mbaya sana haielekei watanzania wanatambua kuwa 2015 taifa lao lilichungulia kaburi! Walioshinda wanashereheka walioshindwa wanasononeka! Hakuna anayeona tulikaribia angamio (an abyss).

We were almost there! The nation came back from the grave! Kama Mwalimu angefufuka leo akaja akakuta Mzee Kingunge na Mngeja waliasi CCM yake atajua kama ni mtetemeko wa ardhi huu ulikuwa ritcher scale 10.2! Si jambo dogo hata kidogo!

Hakika kwa wenye kuitambua 2015 kulikuwa na uwezekano wa wenye pesa kutumia hali ya treni yetu kuwa imetoka relini kutuchagulia viongozi wawatakao na kwa kawaida wenye pesa huchagua watakoalinda na kuendeleza maslahi yao na si ya taifa.Kama ambavyo imefanyika nchi mbalimbali za kiafrika wenye pesa walitumia mbinu zilezile maarufu: - kuvuruga vyama hasa chama tawala, kuhadaa vijana, kumwaga pesa kushoto, kati na kulia na mbinu kadha wa kadha za kimamboleo.

Kwa kawaida nchi zetu hizi zikianza kuvuna utajiri wa maliasili haya hutokea; si siri tena japo geological survey ya nchi yetu ilishafanywa na mjerumani hivyo kila kilichopo ardhini mwetu kinafahamika vyema ni miaka hii ya karibuni tai wa kimataifa (international vultures) wameanza kwa nguvu kubwa kuinyemelea Tanzania. Kwa nini? Kwa kuwa tumeanza kuvuna kwa wingi vilivyopo ardhini. Kuna watu wanadai kwa kuwa tumevumbua! Si kweli, kila kitu kinajulikana.

Ni Rais wa Kwanza aliamua tu kuhifadhi mpaka tutakapokuwa na uwezo. Tumeamua kuvuna bila uwezo sasa matai yenye uwezo yametua! Kama si mapenzi ya mungu na huenda wachache wenye busara tusingempata John Pombe Magufuli! Tai wa kimataifa wangetuchagulia mtu wao! Na ni rahisi kuona hili la hii bahati.

Hakuna kwa mfano mwezi April mwaka jana aliyedhani JPM atakuja kuwa raisi wa nchi hii. Hata mie ungeniuliza singemtaja yeye! Hata alipochukua form ilikuwa utaonekana mchawi kama ungesema yeye ndie atateuliwa! Alionekana ni miongoni mwa wasindikizaji kama walivyokuwa wengine isipokuwa labda Membe, Lowasa na Jaji Ramadhani.

Hata alipopita baadhi ya wajumbe wazito wa Kamati Kuu wa chama chake walitoka nje na kupinga majina yaliyojadiliwa kwa kuwa waliyemtegemea hakupita. Na hata wao walidhani kwa kuwa mtu wao hakupita basi njia ni nyeupe kwa Membe na si JPM! Huu ndio ukweli kila nafsi ya mtu mkweli itamuongoza hivyo. Hata pale JPM alipopitishwa na wanawake wawili wengi walianza kubashiri rais wa awamu ya 5 atakuwa mwanamke! Bado ilikuwa haijaingia akilini JPM atakuwa raisi!

Ndio maana nasema kama si muujiza wa Mungu kwa upendo kwa nchi hii basi ni busara ya watu wachache ndio iliokoa taifa kutoka makucha ya international vultures!
Sasa hata waliochonga funguo kudhihaki kofuli wanamshangilia JPM! Mapenzi ya mungu kwa Taifa la Tanzania yametia!

Lakini ndio tubweteke?Tutembelee nyota ya Magufuli? Jibu ni hapana. Kama ambavyo ametokea Nyerere mmoja ndivyo itakavyokuwa kwa Magufuli; baada yake hatatokea Magufuli mwingine. Jamii ya watu wenye busara hawabweteki na kushinda wakishangilia utumbuaji majipu. Hivi baada ya JPM atakuja nani? Mungu atatusimamia tena? Wenye busara watakuwepo na wasiwe na woga? Kama yote haya yatakosekana si majipu yatarudi tena kwa kasi ya ajabu? Tuliyaona kwa Nyerere! Mzee wa watu alipoondoka na makupe yakarudi midomo juu!

International vultures hawakubali kushindwa kirahisi hivi. Wamerudi kwenye meza kuchora mchoro mpya !Tusidhani wamesalimu amri hata kidogo.Wanajiuliza ‘tulijikwaa wapi’? Kama taifa ni lazima sasa tuweke mazingira yasiyoruhusu matai haya si tu kututeulia bali hata kuingilia mchakato wa uteuzi. Katika kuweka mazingira hayo tusimuonee mtu, tusimhurumie mtu wala tusimpendelee mtu! Tuweke maslahi mapana ya taifa mbele.

Tusiweke mazingira haya huku tumetanguliza uchama au upenzi wetu kwa mtu yeyote. Wenzetu wameweka namna ya kuchuja (vetting) wagombea ukuu wa nchi. Ukuu wa nchi ni dhamana kubwa kuliko hata ya viongozi wa kiroho. Tukiacha kila mwenye kutaka au kutakiwa augombee ipo siku mchawi atapata kura nyingi! Tuweke chombo na vigezo vya maana! Si kusema kwa urahisi tu eti awe raia wa Tanzania, mwenye akili timamu, hajafungwa, awe na miaka fulani na vigezo vingine ambavyo hata jambazi ambalo halijafungwa linaweza kuwa navyo! Kwanza kwa mfano huwa tunawapima vipi kuwa wana akili timamu? Mbona wengine wanatenda kama hawana akili timamu?

Chombo (taasisi) hiyo iundwe na watu wema, wazee, viongozi wa kiroho wasio na mawaa, waliotumikia nchi kwa uadilifu. Hawa wawachambue waombaji wote wa ukuu wa nchi watakaopendekezwa na vyama na wajiridhishe nchi ikiwa mikononi mwa mhusika itakuwa salama. Haingii akilini kwa hapa tulipofikia mathalani mgombea uraisi awe alihusika na kashfa hadi akaachia nafasi kubwa serikalini! Tuacheni ushabiki! Haingii akilini kwa mfano mgombea nafasi ya ukuu wa nchi awe na historia ya kutoa maamuzi ya mahakama yaliyobinya haki za raia!

Haingii akilini mgombea uraisi awe mfanyabiashara ambaye haijulikani analipa au halipi kodi? Tusifanye mzaha na IKULU! Mwalimu alituasa pale ni mahala PATAKATIFU!
Taarifa ya chombo hiki iwekwe wazi ili kila mtanzania ajue ni kwa nini huyu kapita huyu kakataliwa. Aliyekataliwa apewe nafasi ya kukata rufaa Mahakama Kuu. Nina uhakika kama kutakuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu mawaa ya aliyekatwa hatathubutu kwenda mahakamani. Hajipendi ?

Tukifanya hivi tutadhibiti wagombea waliotangulizwa mbele na mapapa ya kimataifa ! Tutaachana na wagombea uraisi ambao watakuja kutuahidi watageuza kilimo chetu kiwe cha umwagiliaji kwa kutumia helikopta ! Tutaepuka msururu wa wagombea uongozi wa nchi na tutapunguza mno gharama za uchaguzi. Hivi si ujuha kumruhusu mkulima ambae hata pembejeo taabu agombee ukuu wa nchi ? Ndio haki za binadamu zinadai hivyo ? Mbona basi haturuhusu kila mtu kuwa daktari ili atakayeshindwa kutibu watu arudi kupiga tunguri ?

Tusiifanyie nafasi ya ukuu wa nchi mzaha wa Pwagu na Pwaguzi. Hivi nani alijua mkulima yule analima ufuta au bangi ? Iko siku muuza kahawa ya magendo atapita!
Naelewa kuna watakaodai na tume iwe huru au na katiba ibadilike ! Sio kwamba siamini uhuru wa tume au hitilafu zilizopo kwenye katiba ya sasa. Lakini hayo kwangu ni secondary ! Lililo primary kwangu na kwa makala hii ni kupata wagombea swafi awe ni wa chama chochote.

Kwangu mimi hata akipatikana mgombea mchafu na ndiye akapeperusha bendera ya CCM bado ni hatari mno kwa nchi ! Tupate clean candidates wakapambane ! Walau tutakuwa na uhakika atakayepita ni msafi ! Tunaweza kuwa na tume huru na katiba safi kama ya mbinguni lakini tukiruhusu kila atakaye agombee ukuu wa nchi ipo siku tutajuta huku tukiwa tumelalia tume na katiba yetu nzuri!

Kina Magufuli ni bidhaa adimu hawaji mara mbili!
Kwa mteule wetu JPM, tumbua majipu huku ukijua usipoweka njia nzuri ya kumpata mwingine wa aina yako ukitoka tutajaa majipu mapya mpaka kwenye ulimi ! Sitaki ustaafu ukisononeka kama Mwalimu ! Mwalimu katika ustaafu wake aliwahi kusema – viongozi wetu waliondoka wakaenda Zanzibar wakarudi kimya kimya tukaona wanafanya mambo wenye akili tukajua ndio limekwisha hilo !

Akasema yeye bado anatembea na kijitabu cha Azimio la Arusha na Biblia ! Ukiondoka bila kuweka utaratibu huo usije kushangaa katika maisha yako ya kustaafu kila ukipita ukaona majipu makuuubwa ! Utasononeka saana maana naamini utaendelea kutembea na sindano ya kutumbulia na biblia ! -
 
Ahsante sana kwa bandiko lako ...
Kiukweli, sikujua kwamba ndani ya nyinyiem anaweza akatokea mtu mwenye machungu na nchi hii + wananchi wake kama JPM, lakini kwa kasi hii na kwa namna anavyowajibu wanaombeza naendelea kuwa na imani ra kiongozi wetu mahili. Ninachoofia ni kwamba wenye pesa wanaweza kufanya hujuma uongozi wake ukaonekana kuwa na kasoro.
Tangu amekuwa madarakani maisha ya walio wengi yamekuwa magumu, pesa imekuwa ngumu kupatikana ... na hii ni kwa sababu watanzania walio wengi walikuwa wanaishi kwa deal za ajabuajabu bila kufanya kazi .... Namwombea kwa Mungu ampe hekima na busara ya hali ya juu ili aweze kuibua mianya ya kazi kwa Watanzania ili waweze kupata mkate wa kila siku.
MUNGU IBARIKI ISRAEL, MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU NIBARIKI MIMI NA WANA JF KWA UJUMLA WAO
 
Back
Top Bottom