Utawala ng’ang’anizi na Muungano tata | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Utawala ng’ang’anizi na Muungano tata

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Kakke, Apr 27, 2012.

 1. Kakke

  Kakke JF-Expert Member

  #1
  Apr 27, 2012
  Joined: Dec 4, 2010
  Messages: 1,797
  Likes Received: 389
  Trophy Points: 180
  [h=1][/h]Posted on April 27, 2012 by zanzibaryetu

  [​IMG]wazanzibari wakiwa katika mhadhara unaoandaliwa na taasisi za dini kuzungumzia katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania

  Na Jabir Idrissa
  MUUNGANO wa Tanzania , zao lililopatikana baada ya kuunganishwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika , unazidi kutikiswa. Ukiwa umeasisiwa tarehe 26 Aprili, 1964, hivyo leo 25 Aprili, kuwa siku ya mkesha wa maadhimisho yake ya miaka 48, Wazanzibari wanauombea dua “mbaya.”
  Ni katika mkusanyiko ulioandaliwa na Jumuiya ya Uamsho, moja ya jumuiya za kiraia zilizo mstari wa mbele kuelimisha raia kuhusu haki zao, ambapo wataongoza sala na dua maalum kwenye uwanja wa wazi.
  Waandaaji wanasema dua zilizotajwa zaidi ni dua ya kuombea Zanzibar izidi kuwa nchi ya amani, leo na siku za usoni; na irudi katika kuwa dola inayojitegemea.
  Muungano umekuwa katika mjadala mpana Zanzibar tangu pale Rais Jakaya Kikwete alipotangaza nia ya kuanzisha utaratibu wa kupatikana kwa katiba mpya ya kwanza itakayoshirikisha maoni ya Watanzania.
  Uamsho wanahamasisha watu watoke na kusema hawapo tayari kuchukuliwa mamlaka ya nchi yao Zanzibar na kwa hivyo hata katiba inayoandaliwa, haiwahusu, bali wanachotaka serikali yao, Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kwanza iitishe kura ya maoni ili wananchi watamke kama wanataka au hawataki muungano.
  Jambo hili limekuwa mtihani mkubwa kwa serikali katika kipindi hichi ambacho tayari tume ya kuratibu maoni ya wananchi kuhusu katiba imeundwa, wajumbe wameapishwa na inatarajiwa kuanza rasmi kazi tarehe 2 Mei 2012.
  Kuthibitisha namna serikali ilivyotishwa na hamasa zinazoenezwa na wahadhiri wa Uamsho dhidi ya muungano, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar , Balozi Seif Ali Idi, amekemea mwenendo huo.
  Akifunga mkutano wa Baraza la Wawakilishi Ijumaa iliyopita, Balozi Seif alisema serikali haikusudii kuzuia mihadhara, bali haitakuwa tayari kuvumilia vikundi vinavyoeneza chuki na kutukana viongozi wa serikali.
  Mara zote viongozi wa Uamsho wanajinasibu kuendesha mihadhara kwa mamlaka waliyopewa na Katiba ya Zanzibar yanayowapa haki ya kusema na kushiriki katika shughuli za uendeshaji wa nchi yao .
  Ndani ya mitandao ya kijamii inayoongozwa na vijana wasomi wa Kizanzibari, kuna maoni yanayojengwa kwa lugha kali watoa maoni wakitaka muungano upitiwe upya na sasa wakiibua hoja ya kutaka kuwe na muungano wa mkataba badala ya muungano wa kikatiba uliopo sasa.
  Kumekuwa na hoja hii Zanzibar kwamba muungano uliundwa kwa usiri mkubwa na hivyo kusababisha kumong’onyoa siku hadi siku mamlaka ya Zanzibar , yale yalikuwepo mara baada ya uhuru wa 10 Desemba 1963 ambapo Zanzibar ilipata kiti chake Umoja wa Mataifa na yalipofanyika mapinduzi 12 Januari 1964.
  Wazanzibari walio wengi wamekuwa wakitaka muungano unaojali haki sawa kwa nchi mbili zilizoungana, na Zanzibar iachiwe mamlaka yake ya kufanya mahusiano na nchi za nje pamoja na kupata misaada kule itakako.
  Pia wanasema wamechoshwa na mfumo wa muungano wa serikali mbili kwa msimamo kuwa umeinyonga Zanzibar kiasi cha kulazimika kupata idhini ya serikali ya muungano hata kwa yale mambo ambayo kwa asili hayapo chini ya muungano.
  Hoja kuu kwao ni kwamba haiwezekani muungano ukaendelea kwa miaka yote 48 bila ya wananchi kupewa nafasi ya kuujadili na kuamua kama ungali na manufaa yaliyokusudiwa.
  Kwa hivyo basi, nafasi ya muungano katika katiba mpya inayolengwa kupatikana ifikapo 2014, inachukuliwa kama jambo la msingi sana Zanzibar na wataalamu wa sheria wanaamini hilo ndilo jambo lililozaa katiba ya muungano.
  Maana yake, wanasema, kulikuja kwanza muungano ndipo ukajumuishwa katika mfumo wa katiba ingawa, wanaeleza, utayarishaji wenyewe wa katiba ya jamhuri haukufuata sheria kulingana na makubaliano ya pande mbili.
  Wanasheria, wakiwemo wale waliojumuika pamoja na kuanzisha asasi iitwayo Baraza la Katiba Zanzibar kwa ajili ya kuhamasisha watu Unguja na Pemba kutoa maoni yao mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ndio hasa wanaojenga hoja ya kwamba sasa ni vema kuwe na muungano wa mkataba.
  Awadh Ali Said, wakili maarufu Zanzibar , katika waraka aliowasilisha kwenye moja ya mijadala ya wazi hivi karibuni, amesema mkataba wa muungano ulitayarishwa na wanasheria wa Tanganyika kwa usiri mkubwa na katika zoezi lote hadi uliposainiwa, viongozi waandamizi wa serikali ya Zanzibar hawakushirikishwa.
  Anasema hata mwanasheria mkuu wa serikali wakati ule, Wolfghang Dourado (amefariki dunia Machi mwaka huu), hakushirikishwa katika hatua yoyote ile.
  Awadh ambaye ni mmoja wa wajumbe 15 kutoka Zanzibar walioteuliwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, anasema kulingana na mfumo wa sheria uliofuatwa kuunda muungano, viongozi wakuu wa nchi mbili wana uwezo kisheria kuingia mikataba ya kimataifa.
  Hata hivyo, anasema, mfumo huo unashurutisha kwamba mara baada viongozi hao wakuu kusaini mkataba, lazima mkataba huo uridhiwe na bunge la nchi husika na upitishiwe sheria ya ndani ndipo upate nguvu za kisheria.
  Anasema, “… hata mkataba wenyewe wa muungano uliweka suala la kuridhia (Ratification) kuwa ni sharti moja la awali la mkataba (condition precedent. Wakati Tanganyika iliridhia mkataba na kutunga sheria rasmi ili kuupa nguvu na uhalali (kupitia Sheria Na. 22/1964), Zanzibar hadi leo hii haikuridhia mkataba.”
  Ukweli huu, anasema Awadh, umebainishwa pia na Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, rais wa pili wa Zanzibar , na magwiji wa sheria Dourado na Profesa Issa Shivji katika maandiko yao mbalimbali.
  Hoja ya kutaka muungano wa usawa na maridhiano, ndiyo iliyosababisha Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa rais wa jamhuri, amtake Mzee Jumbe ajiuzulu urais wa Zanzibar mwaka 1984 wakiwa vikaoni, mjini Dodoma .
  Ipo katika kumbukumbu kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ) aliieleza Mahakama Kuu kwamba SMZ haina mkataba halisi wa muungano.
  Alitoa maelezo hayo mbele ya mahakama hiyo katika kesi Na. 20/2005 iliyofunguliwa na Rashid Salum Adi na wenzake tisa (G10) wakitaka serikali ioneshe nakala ya mkataba halisi wa muungano.
  Badala yake, kilichopo tangu muungano ulipoasisiwa, ni sheria iliyoridhia mkataba ya Tanganyika , ndani yake kukiambatanishwa kinachodaiwa kuwa ndio mkataba ambacho ndicho hadi leo kinatumika kama ndio mkataba wa muungano. Hili linaleta maswali mengi yasiyojibiwa.
  Kutojibiwa kwa utata kuhusu uhalali wa muungano, ndiko kulitarajiwa kuzindue viongozi wakuu wa taifa ili wawape Watanzania wa pande zote mbili nafasi ya kujadili na kutoa maamuzi kupitia maoni yao katika katiba inayolengwa kupatikana.
  Hili pengine lisitimie kwa kuwa tayari Rais Kikwete “ameshatoa uamuzi” aliposema wananchi wapo huru kujadili namna ya kuimarisha muungano na siyo kujadili kama muungano uwepo au usiwepo.
  Inawezekana tamko la Rais likachukuliwa kama ung’ang’anizi wa utawala kutaka muungano uendelee kuhojiwa hata sasa unapokaribia kutimiza robo karne ya uhai wake.
   
 2. k

  karafuu Member

  #2
  Apr 27, 2012
  Joined: Apr 1, 2012
  Messages: 63
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  muda sina muungano hatuutaki
   
Loading...