Utawala bora, Utawala wa Sheria na Madaraka ya Wananchi

mwengeso

JF-Expert Member
Nov 27, 2014
9,219
6,650
Napitia Ilani za vyama vya siasa ambavyo nimefanikiwa kupata na kupitia Ilani zao za Uchaguzi Mkuu, 2020.

Moja ya agenda inayongumziwa sana kwenye kampeni, hasa na Mgombea Urais wa CHADEMA, ni Uhuru na Haki, ambavyo kimsingi ni sehemu ya utawala bora.

CCM na CHADEMA, kwenye ilani zake, vyote vinaamini kuwa utawala bora ni pamoja na uwazi na uwajibikaji Serikalini na wananchi kushirikishwa katika kuamua masuala muhimu yanayohusu maisha yao.

Katika Ilani ya CHADEMA inaeleza kuwa kwa kuwa kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa misingi ya kidemokrasia, utawala bora, utawala wa sheria, na uwajibikaji duni wa viongozi na watumishi wa umma katika muhula wa uongozi uliopita; Serikali ya Chadema inakusudia, pamoja na mambo mengi:

√ kupeleka miswada ya Sheria Bungeni kwa madhumuni ya kuzifuta Sheria zote kandamizi na zinazokiuka misingi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora;

√ kudumisha dhana ya mgawanyo wa madaraka katika mihimili ya Dola (Serikali, Bunge na Mahakama) kwa kuondoa vikwazo vya kiutawala na kibajeti vilivyokuwa vinasababisha mwingiliano wa majukumu miongoni mwa mihimili hiyo; na hivyo kuathiri
utendaji wake wa kazi.

√ Hivyo basi, itagatua madaraka kwa kuweka mfumo wa Serikali za majimbo. Tanzania ya Majimbo, nini hatima ya maendeleo ya majimbo ambayo bado yako nyuma na yana uhaba wa rasimali?

Kwa upande wake, CCM inadai kuwa Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015-2020), kilihakikisha kuwa Taifa linakuwa na utawala bora unaozingatia misingi hiyo ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kutokomeza umasikini katika jamii.

Hivyo basi, Katika kipindi cha Miaka mitano ijayo, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuhakikisha viongozi wanaoteuliwa ni waadilifu, wawajibikaji, wanaoleta matokeo chanya na kutumia rasilimali za umma kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Ili kufikia azma hiyo, Chama kitaelekeza Serikali, pamoja na mengineyo:

√ Kuimarisha taasisi za utawala bora, maadili na uwajibikaji kama vile Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi katika Utumishi wa Umma, TAKUKURU, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya ili ziweze kutimiza wajibu ipasavyo;

√ Kuimarisha Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili iweze kuboresha utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi;
√ Kubuni na kutekeleza mikakati ya kukuza, kulinda na kutekeleza misingi ya haki za binadamu na wajibu wao.

Kwa ufupi, vyama vyote viwili vina nia njema ya kujenga nchi ya watu wanaotii sheria bila shurti iwapo tu Serikali itatawala kwa kuheshimu haki za binadamu. Tofauti ni jinsi ya kufikia azima hiyo.

Wakati viongozi wa CHADEMA wakiituhumu Serikali ya CCM kuwa imekuwa ikitawala kidikteta, viongozi wake hawajaonesha kwa vitendo kuwa CHADEMA kinaendeshwa kwa misingi ya kidemokrasia.

Isitoshe, viongozi wa CHADEMA wanaaimini mwarobaini wa utawala bora ni kufumua mfumo wa utawala uliopo wa Serikali kuu na Serikali za mitaa (kuweka madaraka zaidi kwa wananchi) badala ya viongozi watawala kuwa na UTASHI wa KISIASA (political will).

Utashi wa kisiasa ni nia ya kisiasani iliyo imara au ya kujitolea kwa upande wa serikali kutekeleza sera, hata ambayo si mara moja mafanikio yake yanaweza kuonekana. Kiongozi mwenye utashi wa kisiasa ni yule ambaye ana uamuzi binafsi wa kisiasa wa kusema na kutenda mambo ambayo yataleta matokeo chanya.

Tafsiri hiyo ndiyo inawatofautisha sana viongozi wa kisiasa katika kuwajibika kwa jamii na siyo tu kubadili mifumo ya utawala au Katiba.

Kinachotakiwa ni kuweka Sheria, Kanuni na Taratibu zinazo hakikisha kiongozi anawajibika kwa mwananchi (awe na utashi wa kisiasa au la) na mwananchi awe na madaraka ya kumwajibisha. CHEO NI DHAMANA. Rushwa, urasmu, matumizi mabaya ya madaraka, nk ni baadhi ya tabia za kiongozi wasio kuwa na utashi wa kisiasa.

NAWASILISHA
 
Back
Top Bottom