SoC01 Utawala Bora ni nyenzo muhimu katika kukuza Uchumi na Uwekezaji

Stories of Change - 2021 Competition

Haki sawa

JF-Expert Member
Oct 3, 2007
4,780
3,208
UTAWALA BORA NI KICHOCHEO MUHIMU KATIKA KUKUZA UCHUMI NA KUVUTIA UWEKEZAJI

Utangulizi.

Nianze Makala haya Kwa kutoa tafsiri/maana ya utawala Bora ambao naumaanisha katika makala yangu hii ya Leo .

Utawala Bora ni uendeshaji wa Serikali au taasisi unaofuata misingi ya Katiba,Sheria,kanuni,taratibu,maadili na mifumo ambayo Serikali au taasisi husika imejiwekea katika kuhakikisha kuwa maamuzi yote yanazingatia kikamilifu uwepo wa sheria.

Aidha, maamuzi ni lazima yafuate mkondo wa Haki,usawa na uwajibikaji kwa kila mmoja bila kujali ukubwa au udogo wake, rangi,dini au Kabila,jinsi,nafasi katika jamii,utajiri au umaskini wa kipato,matabaka ya kielimu na mengineyo.

Utawala Bora ni mfumo unaofuata misingi ya Sheria zilizopo na zilizokubalika katika kuwezesha kufikia uamuzi ambao kila upande utaridhika kwamba hapa nimetendewa Haki pamoja na kuwa nimekuwa mkosaji au nimeadhibiwa mimi na yule kupewa Haki.

Utawala Bora husikiliza pande zote bila kupokea maagizo ambayo ni Kinyume na utaratibu ambao jamii imejiwekea ,mathalani, Mahakama zinakuwa huru katika kutafsiri Sheria na kutoa Haki,Bunge linakuwa na Uhuru wa kutunga sheria,kuisimamia Serikali na kushauri bila kunyimwa Haki na kwa uwazi bila kuingiliwa na dola.

Jamii na asasi za kiraia wanaendesha Mambo yao kwa mujibu wa Katiba na sheria ambazo wote Kwa pamoja wamekubaliana kuzifuata na kila mmoja akiheshimu Uhuru wa Mwingine bila kumuingilia na inapotokea kuingiliana kila mmoja ana Uhuru wa kwenda Mahakamani na kupata tafsiri sahihi na Haki zake .

Utawala bora, huzuia kwa kiasi kikubwa vitendo vya rushwa na ufisadi.Panapokosekana utawala bora vitendo vya rushwa na ufisadi hukua , kushamiri , kukomaa na kuzaa mbegu za ufisadi. Rushwa na ufisadi ni adui mkubwa katika kukuza uchumi na kuvutia uwekezaji ,hakuna mwekezaji ambaye atakuwa tayari kuwekeza fedha zake kwenye mazingira ya rushwa wani hazitakuwasalama kama haki itakuwa inanunuliwa kwa njia ya Rushwa na kama vyombo vya kutenda haki vinaendeshwa kwa nguvu za rushwa na ufisadi.

Utawala unaotii sheria huzuia rushwa kwa nguvu zote kwani uchumi hautaweza kukua kama rushwa imeshamiri na kutamalaki bali uchumi hushikiliwa na kakikundi kadogo ambako huamua nani ashike na kuongoza serikali na mihimili mingine ya dola jambo ambalo ni la hatari katika ustawi wa kiuchumi , kijamii na kisiasa.

Utawala wa sheria hukuza usawa katika kupata fursa za ajira na ujira ulio sawa kulingana na aina ya kazi bila ubaguzi, hali ambayo hupelekea kukuza uchumi na uwekezaji katika taifa kwani kila mmoja anakuwa na fursa sawa katika kupata ajira na ujira .Panapokosekana utawala wa sheria ni rahisi sana kuwa na upendeleo katika kupata fursa za ajira na mara nyingi mazingira hayo yanaweza kuligawa taifa kwa misingi ya ukabila na ukanda na hivyo kuhatarisha amani na usalama vitu ambavyo ni msingi katika kukuza uchumi na kuvutia uwekezaji.

Utawala wa sheria huweka mazingira wezeshi kwa taasisi za fedha kuweza kujiendesha na kuwa na uhakika kuwa mitaji yao itakuwa salama jambo ambalo litaimarisha na kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya taasisi, mashirika na hata watu binafsi kuweza kupata mikopo kwa ajili ya mitaji ya kuanzisha biashara mpya na ambazo zitasaidia kutoa ajira na kukuza uchumi.Uwepo wa utawala bora husababisha kutabirika kwa soko kitu ambacho ni kichocheo muhimu katika kuvutia wawekezaji na uwekezaji.

Utawala bora husababisha kuwepo kwa utulivu wa kisiasa kitu ambacho ni nyenzo muhimu sana katika kuvutia uwekezaji na mitaji, kama hakuna utulivu wa kisiasa hakuna mwekezaji ambaye atakuwa tayari kuwekeza sehemu ambayo hana uhakika kuwa kesho hali itakuwaje , pasipokuwa na utulivu wa kisiasa ni hatari kwa mitaji na uwekezaji, wananchi na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.Kutabirika kwa utulivu wa hali ya kisiasa ni nyezo muhimu kwa wawekezaji kufanya maamuzi ya kuwekeza ama la!

Utawala bora husababisha kutabirika kwa sera mbalimbali na hasa sera juu ya kodi, kama utawala haufuati sheria ni jambo rahisi sana kwa watawala kubadilisha sera za kibiashara na uwekezaji kwa njia ya matamko na hivyo kuathiri uwekezaji moja kwa moja ,kwa mfano unapokuwa unawekeza mtaji unakuwa umefuatilia aina na viwango vya kodi ambazo utatakiwa kulipa kulingana na mtaji wako , panapokuwa hakuna utawala wa sheria ni rahisi sana kwa sheria za kodi kubadilishwa kiholela bila kuzingatia misingi ya utawala bora, jambo ambalo ni la hatari kwa uwekezaji na ukuaji wa uchumi.

Uhakika wa mikataba ambayo mwekezaji anaweka baina yake na serikali kama hakuna utawala bora na unaofuata sheria ni rahisi sana kwa mikataba hiyo kubadilishwa kwa nguvu au hata kuvunjwa na hata ukienda Mahakamani inakuwa vigumu kuweza kupata haki kwani kama hakuna utawala wa sheria hata mahakama inakuwa haifuati sheria vilevile, jambo ambalo ni hatari kwa ukuaji wa uchumi katika taifa lolote lile.

Nitoe mfano wa nchi ya Zimbabwe ambayo iliwahi kusifika Sana katika Kasi ya kukuza uchumi wake na kuvutia wawekezaji wengi ,lakini utawala wa Rais Robert Mugabe ulipoamua kutokufuata sheria na kuwanyanganya wawekezaji Ardhi kinyume cha mikataba na sheria za Zimbabwe,kila mmoja anajua athari ambazo Zimbabwe walizipata za kiuchumi na mbinyo kutoka katika mataifa makubwa hali ambayo kwa kiasi kikubwa imeuvuruga uchumi wa Zimbabwe kwa kiwango kisichoelezeka kwa sababu ya uamuzi walioufanya wa kubadilisha sera na sheria za uwekezaji bila kufuata misingi ya utawala bora .

Mfano Mwingine ni wa hapa Tanzania,pale ambapo Serikali kupitia Benki Kuu walipoamua kufungia maduka ya kuibadilisha fedha za kigeni , madhara yake yapo mpaka leo kama vile watu kukosa ajira,serikali yenyewe kukosa mapato ya kodi na tozo mbalimbali zilizotokana na uwepowa biashara hiyo,kupotea kwa mitaji na baadhi ya wawekezaji kuhamisha mitaji yaona kwenda kuwekeza katika nchi za jirani na mengine mengi. Kwa sababu uamuzi ule haukufuata misingi ya utawala bora wala sheria na ndio maana Leo wawekezaji wale wanaambiwa wakachukue leseni na waendelee na biashara, tungekuwa tunafuata utawala Bora basi waliosababishiwa hasara wangelipwa fidia kutokana na uamuzi huo wa Serikali na waliosababisha hasara walipaswa kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria!

Utawala wa sheria huwezesha kushamiri kwa demokrasia jambo ambalo ni la muhimu katika kukuza uchumi.Demokrasia ni pamoja na uwepo wa vyombo huru vya kufanya maamuzi,vyombo huru vya habari,uwazi na ushirikishwaji katika kufanya maamuzi, mambo ambayo yanaongeza kujiamini na ujasiri kwa wawekezaji (Investor’s confidence)

Hitimisho.

Nihitimishe kwa kusema kuwa bila utawala bora hakuna uchumi imara utakaoweza kujengeka katika mazingira ambayo hakuna utii wa Katiba na Sheria. Vyombo vya dola vinapashwa kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ili kuweza kuvutia uwekezaji na hivyo kukuza uchumi wa taifa.

Uwekezaji unahitajika katika kilimo,uvuvi,viwanda,nishati na Nyanja zote za kukuza uchumi, na ili iwezekane kufika hapo ni lazima utawala bora na utii wa sheria uheshimiwe kwa viwango vinavyokubalika .
 
Back
Top Bottom