Utata waibuka wachimbaji wadogo kupigwa mabomu wakiwa mgodini

Kurzweil

JF-Expert Member
May 25, 2011
6,622
8,410
Utata umeibuka baada ya askari wa Jeshi la Polisi wa Mirerani wilayani Simanjiro (Manyara) kudaiwa kuwafyatulia mabomu ya machozi na kuwajeruhi wachimbaji wadogo saba wakiwa ndani ya mgodi takribani mita 240.

Wachimbaji hao waliokuwa mgodi namba P.M.L 0000049 Kitalu D, unaomilikiwa na Theresia Wapalila walikumbwa na tukio hilo baada ya kutoboza eneo la Delta, Kitalu C linalomilikiwa na kampuni ya Tanzanite One.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Issa Bukuku alikanusha kutumia mabomu kutuliza vurugu licha ya kuthibitisha kutokea kwa tafrani hiyo.

“Polisi bado inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, lakini wachimbaji wadogo hawana budi kufuata maelekezo ya maeneo yao,” alisema.

Wakizungumzia tukio hilo lililotokea juzi, wachimbaji hao walidai kuwa kitendo cha kupigwa mabomu wakiwa chini ya ardhi na kuharibu miundombinu ya umeme na kunyang’anywa vifaa vya kazi kimewaathiri kiafya na kisaikolojia.

Wachimbaji wanaodaiwa kuathiriwa na mabomu hayo ni Boxer Dennis (35), Phillipo Paul (31), Ramadhani Hamza, Hamis Hassan (30), Edmund Mosha, Benjamin Shakoti (47) na Emmanuel Afred (25).

Meneja wa godi huo, Frank Mushi alisema vitendo hivyo vya kupiga mabomu na kutembea na silaha za moto chini ya migodi vimekuwa vikifanywa na askari hao aliodai wanatumiwa na mwekezaji wa Tanzanite One.

Alisema siku ya tukio hilo, polisi wakiwa na maofisa wa Tanzanite One walizama chini ya mgodi wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi na katika purukushani hiyo, vijana wawili walinusurika na kutoa taarifa.

“Hiki ni kilio kwetu pindi tunapotobozana. Wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kinyume na sheria kwa kuwa wanapora vifaa vya kazi. Tangu tumeanza kazi kwenye hii shafti tulifikisha mita 240 na tayari tulikuwa tumeanza kufanya uzalishaji,” alisema.

“Tukarudishwa nyuma na kubakiziwa mita 30 kutoka sehemu tunayoiita kiraka ili tubadili muelekeo. Tuliwauliza sababu za kuturudisha mita zote hizo wakati inatakiwa kurudi mita 10 au 15 nyuma,” alisema Mushi.

Akizungumzia tukio hilo mkurugenzi mwenza wa Tanzanite One inayochimba kwa ubia na Serikali kupitia Shirika la Stamico, Faisal Juma alisema, changamoto kubwa inayojitokeza ni kwa wachimbaji wadogo kushindwa kutambua mipaka na kutoheshimu sheria.

“Mgodi ule si wa kwetu pekee pale tunachimba kwa ubia na Serikali kupitia Stamico. Hivyo ni lazima vyombo vya dola viwepo ili kusimamia masilahi ya umma na kuona yakilindwa,” alisema Juma.

“Sasa kwa eneo la Delta ambalo hawa wanalalamika kuwa lilikuwa halichimbwi hiyo si sababu, sasa hivi limeanza uzalishaji na linamilikiwa kisheria na Tanzanite One. Ni kweli wachimbaji wadogo katika harakati zao za kuchimba wanapitiliza na kuingia eneo hili.

“Sisi na Serikali kwa pamoja tunayo haki ya msingi ya kusimamia maeneo hayo yawe salama. Uamuzi unaochukuliwa mara nyingi ni wa kuwarudisha nyuma, ambao umekuwa ukilenga usalama mgodini na kulinda masilahi ya Serikali na mwekezaji.”

Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema licha ya sheria ya madini kutozungumizia suala mabomu chini ya ardhi, bado wao kama wizara hawaruhusu kufanyika kwa vitendo hivyo.

“Hatuhitaji kutumia nguvu kubwa ya kuwapiga Watanzania mabomu ya machozi chini ya ardhi kwa sababu tu ya mtobozano wa uchimbaji. Suala hili linahitaji mazungumzo zaidi,” alisema kamishna huyo.

“Hata hao Tanzanite One tulishawapa maagizo ya maandishi kwamba hairuhusiwi kutumia risasi za moto chini ya ardhi wala mabomu.

“Sisi tuna ofisi pale Mirerani wanatakiwa kwenda kutoa taarifa muda wowote na tumekuwa tukishawashauri kufanya mazungumzo badala ya kutumia nguvu.”

Chanzo: Mwananchi
 
Jeshi la polisi linahusishwa kuwashambulia harafu polisi wanaendelea na uchungu!!!!..... What do you espect?
 
Hawa wahindi wakiskia mgodi wa jirani mawe yanatoka wanakuja na police,walinzi wao na kuteka njia....hao wizara ya madini mererani ni wala rushwa tu wao kazi ni kusema wewe rudi mita 100 nyuma huyu tanzaniteone ndio mwenye haki.yani wanatia hasara sana umekata njia yote mpka umeweka miundombinu n baruti unapiga wanakua wapi mda huo......kila nkiwakumbuka hao wizara ya madini napata hasira sana waliturudisha nyuma mita 700 gharama yote ya miaka zaidi ya 15 ni hasara kubwa kwetu
 
Kipindi mzungu yupo hapo TANZANITEONE mambo yalikuwa poa sana kila mtu alipata riziki yake bila kele wala migongano. Lakini walipokuja hawa wanaoitwa wawekezaji wazawa au wanyanyasaji wazawa mambo yamekuwa ovyo sana. Mimi nilifanya kazi hapo kwa kipindi kirefu kiasi so najua kila kinachoendelea japo kwa sasa ninafanya kazi sehemu nyingine kabisa
 
Polisi wa bongo huwa siwaelewi kabisa aseeh
Jamaa wanatoboa kwa makusudi ili waingie channel ya mzungu kwa sababu wanajua watakutana na mawe kwa urahisi ,niliwahi kuwa broker arusha kuna mambo mengi sana Kule MTU anawaza jiwe tu kifo baadaye
 
Jamaa wanatoboa kwa makusudi ili waingie channel ya mzungu kwa sababu wanajua watakutana na mawe kwa urahisi ,niliwahi kuwa broker arusha kuna mambo mengi sana Kule MTU anawaza jiwe tu kifo baadaye
kumbe ndio ilivyo mkuu
 
Back
Top Bottom