Utata uhamishaji mabilioni BoT | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Utata uhamishaji mabilioni BoT

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Jun 7, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Jun 7, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,681
  Likes Received: 82,533
  Trophy Points: 280
  Utata uhamishaji mabilioni BoT

  Mwandishi Wetu Juni 3, 2009
  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  Ni Sh bilioni 137 za Tanesco na IPTL

  Gavana Ndullu asema hajajulishwa

  TAKRIBAN Sh. bilioni 137.8 zilizohifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika akaunti ya pamoja ya Serikali na kampuni ya kufua umeme ya IPTL, zimeandaliwa mpango wa kuhamishwa kwa utaratibu unaoibua maswali mengi zaidi, Raia Mwema imedokezwa.

  Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kwamba kuna mpango wa kuhamisha fedha hizo kutoka BoT kwenda kwenye akaunti tofauti bila maelezo ya kuridhisha.

  Haikuweza kufahamika mara moja fedha hizo zitahamishiwa kwenye akaunti ipi kutokana na nyaraka husika kutobainisha taarifa muhimu kuhusiana na uhamishaji huo.

  Mpango huo umekuwapo kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni fedha hizo ‘kuzubaa' BoT baada ya mali za IPTL kuwekwa chini ya mfilisi, ambaye ni Wakala wa Usajili, Vizazi na Vifo (RITA) bila kujumuisha fedha hizo.

  Ikiwa mpango wa kuhamisha fedha hizo utafanikishwa kabla ya mwaka 2010, itakuwa ni mtikisiko mwingine mkubwa kutokea ndani ya BoT baada ya ule wa fedha zilizoibwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Fedha zilizothibitishwa kuibwa EPA mwaka 2005 ni Sh bilioni 133.


  Fedha hizo ambazo ziliwekwa kwenye akaunti maalumu (Escrow account) ndani ya BoT hadi kufikia Sh 137, 769, 763, 052.84, zilitokana na malipo yaliyokuwa yalipwe kwa kampuni ya IPTL kutokana na kuliuzia umeme Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kabla ya kubainika kuwapo udanganyifu uliofanywa na kampuni hiyo tata kuhusiana na gharama halisi za uwekezaji.

  Raia Mwema imefanikiwa kupata mawasiliano ya awali ambayo yanaonyesha kuwapo kwa barua kutoka RITA kwenda kwa Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu, kwa lengo la kuomba mfilisi huyo, kwa niaba ya IPTL, apatiwe udhibiti wa fedha hizo.


  Barua hiyo, ambayo Raia Mwema imepata nakala yake, ni yenye kumbukumbu namba ADG/OR/IPTL/GEN/009, ya Mei 6, mwaka huu.

  Nakala za barua hiyo pia zimepelekwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mtendaji Mkuu wa Tanesco.

  "…Mfilisi wa IPTL ameamua kutumia mamlaka yake kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa kifungu cha 188 ya sheria za makampuni ili kudhibiti kikamilifu akaunti ya pamoja (Escrow account) ya IPTL Tegeta ambayo ipo BoT," inasema barua hiyo ambayo pia inaweka bayana kuwa wenye mamlaka ya kutoa fedha hizo katika akaunti hiyo ni watu wawili tu.

  Watu hao wawili waliotajwa katika barua hiyo ambayo sahihi zao ndizo zinazoweza kutoa mabilioni hayo ni Theophil Rugonzibwa na Dk. Magesvaran Subramaniam anayetajwa kuwa raia wa kigeni.


  Imeelezwa na barua hiyo kwamba watu hao ndio wenye mamlaka ya kutoa maelekezo kwa BoT na kutoa fedha hizo kutoka katika akaunti hiyo ya pamoja, wakimtaka Gavana Ndullu kutekeleza matakwa ya mkataba huo.

  Gavana wa Benki Kuu, Profesa Ndullu, ameliambia Raia Mwema kwamba hadi jana Jumanne alikuwa hajapokea maelekezo yoyote kuhusiana na kutolewa kwa fedha hizo akikwepa kufahamu lolote kuhusiana na barua ya RITA.

  Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Idrissa Rashidi, hawakuweza kupatikana jana ikielezwa kuwa walikuwa na mikutano muhimu, lakini habari za ndani ya ofisi zao zimethibitisha kufahamu kuwapo kwa mawasiliano ya kutaka kuchukuliwa fedha hizo.

  Habari zaidi zinasema kwamba wakati kukiwa na mkakati wa kuhamisha fedha hizo kumekuwapo Azimio la Bunge linalotaka suala hilo kumalizwa haraka nje ya mahakama ili fedha hizo kutumika katika kumaliza madeni ya Tanesco na kuichukua mitambo ya IPTL ili ibadilishwe na kutumia gesi na hivyo kupunguza makali ya bei na uhaba wa umeme nchini.

  Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, ambaye kamati yake ndiyo iliyowasilisha mapendekezo yaliyotoa azimio hilo, alisema "uamuzi wowote utakaofikiwa kuhusiana na IPTL unapaswa kuzingatia azimio la Bunge."

  Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard) azimio ambalo linahusu IPTL lilitolewa Aprili 29, 2000 likiwa na maelezo ya kuitaka Serikali na wadau wengine wa suala hilo kuzingatia zaidi maslahi ya Taifa katika maamuzi yao.

  "Suala la IPTL limalizwe kwa haraka nje ya Mahakama ili kuharakisha ubadilishaji wa mtambo huo ili utumie gesi na hivyo kuongeza uzalishaji wa umeme wa megawati 100 ambao unatakiwa hivi sasa ambapo kuna nakisi kubwa ya umeme na hivyo kupelekea mgawo unaoumiza uchumi wa nchi," inaeleza sehemu ya azimio hilo la Bunge na kuendelea;

  "Katika kutekeleza hili la IPTL lazima izingatiwe kwamba IPTL iliitapeli nchi na Tanesco wamewalipa wamiliki zaidi ya kiasi cha fedha ambacho walipaswa kulipwa na Tanesco…..Serikali inatakiwa itumie ushahidi wote uliopo kuhakikisha kuwa kiwango cha fedha kilichopo kwenye akaunti maalumu (Escrow account) ndicho kinatumika kumaliza madeni na kufanyia marekebisho mtambo huo ili utumie gesi bila kuhitajika kwa Serikali kutoa fedha nyingine…."

  Suala la utapeli uliofanywa na IPTL liligusiwa pia na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusiana na kashfa ya umeme wa Richmond, akisema kwamba Tanesco wanaidai IPTL fedha walizolipa kwa makosa kama gharama za uzalishaji (Capacity Charge).

  Mgogoro uliopo baina ya Tanesco na IPTL unatokana na kutokubaliana kwa pande zote mbili kuhusu kiwango cha gharama za uzalishaji kinachotozwa na IPTL.

  Pinda alisema kwa mujibu wa mkataba wa kuuziana umeme kati ya IPTL na Tanesco, inapaswa kukokotolewa kwa kuzingatia mtaji kwa asilimia 30 na faida ya asilimia 22.31 uliopaswa kuwekezwa ambao ni dola za Kimarekani 36.54 milioni wakati IPTL ilipoanza kuzalisha umeme na kuanza kuiuzia Tanesco Januari 2002.

  Alisema katika uchunguzi uliofanywa na Tanesco na asasi nyingine, imegundulika kwamba mtaji halisi wakati IPTL inaanza kuzalisha umeme ulikuwa Sh 50,000 tu, hivyo mtaji huo ndio unaostahili kutumika kukokotoa gharama za uzalishaji inayolipwa na IPTL na si vinginevyo.

  Baada ya uchunguzi wa Tanesco iligundulika ya kuwa hadi Mei, 2008, TANESCO ilikwisha kuilipa IPTL jumla ya Sh. bilioni 221 tangu waanze kuzalishaji Januari, mwaka 2002.

  Hivi karibuni, Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) alisema Taifa limewalipa zaidi IPTL na kuongeza:

  "Mahakama Kuu tayari imeamua kuiweka IPTL chini ya mufilisi, Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu, na majadiliano ya kumaliza suala hili kwa haraka yanaendelea ili Benki iliyokopesha IPTL, TRA, wabia wa IPTL (Mechmar na VIP Engineering) na TANESCO kila mmoja apate anachostahili na nchi ipate umeme inaouhitaji sana.


  "Kuichukua IPTL na kuigeuza ili itumie gesi itaokoa Sh. bilioni 9 kila mwezi na kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kununua umeme na kuliwezesha TANESCO kujiendesha kwa faida."

  Mradi wa IPTL umekuwa katika mjadala wa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuhusishwa na rushwa, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya wahusika pamoja na kuwapo hadi hati za viapo kuthibitisha kuwapo kwa rushwa wakati wa mchakato wa mradi huo.

  Hivi karibuni, kuliibuka utata wa uamuzi wa Jaji Thomas Mihayo wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kuhusiana na uteuzi wa Wakili Charles Rwechungura, kuwa mfilisi mpya wa IPTL badala ya RITA, uamuzi uliotenguliwa na jopo la majaji watatu.

  Majaji hao, Edward Rutakangwa, Steven Bwana na Othman Chande, walibaini kuwapo udhaifu mkubwa wa kisheria kabla ya kufikiwa kwa maamuzi ya Jaji Mihayo ikiwa ni pamoja na kutotoa nafasi kwa pande husika kusikilizwa katika uamuzi huo uliotolewa kwa haraka.

  Uamuzi wa Jaji Mihayo ulielezwa kwamba ungewanufaisha zaidi wageni hususan benki ya Standard Chartered Bank ya Hong Kong na kampuni ya Mechmar ya Malaysia, wenye hisa kubwa katika IPTL.

  Tayari Tanesco wana ukata mkubwa na sasa wameomba serikalini kupatiwa kwa haraka Sh bilioni 312 za kununulia mitambo na miradi mingine ya uzalishaji umeme wa dharura.
   
Loading...