Utamu wa Tunda la kuiba - Kwanini? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Utamu wa Tunda la kuiba - Kwanini?

Discussion in 'Jukwaa la Lugha' started by Mzee Mwanakijiji, Apr 11, 2008.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Apr 11, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Nabisha hodi watani, mjuao Kiswahili,
  Nimetingwa mawazoni, sasa nauliza swali,
  Jibu niandikieni, moyo wangu ukubali,
  Kula tunda kwa kuiba, kwanini huko kutamu?

  Ni tunda naulizia, lile lililonawiri,
  Si langu nawaambia, la kwake bwana Bushiri,
  Miye nimetamania, njama nikatafakuri,
  Kula tunda kwa kuiba, kwanini huko kutamu?

  Mwenyewe yuko kazini, shamba liliko ni mbali,
  Zamu yake ni jioni, asubuhi yangu mali,
  Nalila kiulani, pasipo ya mushkeli,
  Kula tunda kwa kuiba, kwanini huko kutamu?

  Tunda silili kwa pupa, na silili kibahili,
  Siling'ati kwa kuepa, kama vile mbilikili,
  Mbegu yake sitotupa, namung'unya kimahili,
  Kula tunda kwa kuiba, kwanini huko kutamu?

  Utamu wake adimu, unaizidi asali
  Tunda hili siyo ndimu, na wala siyo figili,
  Ninaling'ata kwa zamu, unasisimka mwili,
  Kula tunda kwa kuiba, kwanini huko kutamu?

  Siogopi kuja bambwa, na yeye bwana Bushiri,
  Ni fumbo lilifumbwa, tunda sitalighairi,
  Hata akileta Mbwa, nalifunguia safari,
  Kula tunda kwa kuiba, kwa nini huko kutamu?

  Beti zangu nazifunga, jibu lenu nasubiri,
  Mlo mabingwa kutunga, mnijibu kishairi,
  Na hata mso malenga, nijibuni bila shari,
  Kula tunda kwa kuiba, kwanini huko kutamu?

  Na. M.M.Mwanakijiji (Sauti ya Shamba)
   
 2. Steve Dii

  Steve Dii JF-Expert Member

  #2
  Apr 11, 2008
  Joined: Jun 25, 2007
  Messages: 6,416
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  Mwakijiji mla matunda, hachambui yapi hayafai,
  Ajivunia bila kuvunga, Leo embe kesho papai,
  Yapo yalo vunda, kutofaa ndani ya kalai,
  Chambua kama mpunga, usikonde kama Mmasai,
  Mboga chungu mchunga, utamu si kuitia asali.

  Wachuma wabinjuka, kiherehere kutojivunga,
  Alfajiri wainuka, kutembelea mti ulio tunda,
  Watikisa nao wapukuta, huupigi teke kama punda,
  Starehe ndani ya shuka, wasahau maganda huvunda,
  Mboga chungu mchunga, utamu kulia na ugali.

  Mti usio panda, yanini tenga kuuchuma,
  Mti ulo' wa Mganda, Mkenya kuchuma ni hujuma,
  Mti ulo' wa mganga, siku yaja tumbo kuuma,
  Mti uso' magamba, huteleza upepo ukivuma,
  Mboga chungu mchunga, utamu kula ilo halali.

  Malenga natoweka, ushauri tele n'shapanda,
  Beti zimeeleweka, wako uroho uweze kuganga,
  Yangu misingi kuweka, kamwe kutojilia maganda,
  Mwanakijiji aliye neemeka, mti wa tunda huupanda,
  Mboga chungu mchunga, utamu kutochuma wa mbali.


  SteveD. (Mwangwi wa Handaki)
   
 3. Nyani Ngabu

  Nyani Ngabu Platinum Member

  #3
  Apr 11, 2008
  Joined: May 15, 2006
  Messages: 73,651
  Likes Received: 35,408
  Trophy Points: 280
  Hahahahaaaaa...Steve weee kiboko!!
   
 4. Steve Dii

  Steve Dii JF-Expert Member

  #4
  Apr 11, 2008
  Joined: Jun 25, 2007
  Messages: 6,416
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  Nyani, ni kutokana na kutaka kubanana humu humu ndani na huyu kaka'ngu Mwanakijiji ndiyo kunanipeleka kuingilia fani za watu.... in a way it's encouraging kuona kumbe binadamu tunaweza kujitahidi na kufanya vitu vingine ukiachilia mbali mambo ya IT na kubishana kwenye technicality na semantics za siasa. At the same time, kufanya hivi kunaleta challenge kwa walio katika fani hii na kuwafanya wajihime zaidi kama si kuboreka. laters dawg!

  SteveD.
   
 5. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #5
  Apr 11, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Steve.. much improvement in a week!! I like that piece.. hasa kibwagizo chako.. "Mboga chungu mchunga"...! I love it!
   
 6. Waridi

  Waridi JF-Expert Member

  #6
  Apr 11, 2008
  Joined: Mar 30, 2008
  Messages: 1,027
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 135
  Siku moja nikaenda, kumsabahi Ngoyai,
  niloona sikupenda,nikadhani hayafai,
  mtoto wake wa kenda,hataki kula mayai,
  kisa cha kutoyapenda,mayai kayazoea .

  moyo wangu ulidunda,kama natokwa uhai,
  kesho gari nikapanda,mapema ya asubui
  tukio nilipoponda,nikijiuliza whai?
  nikagundua kupenda,hakutaki mazoea.

  kitu ulichozoea,thamaniye huioni,
  maana wakichezea,mchana hata jioni,
  na kisichozuiliwa,hadhi ye huwa ya chini,
  ila kilichopelea,hicho utakitamani.

  mate utakimezea,kilichoko kwa jirani,
  ikibidi wamwibia,ni kitamu unadhani,
  kumbe hakijazidia,ulichonacho nyumbani,
  tatizo ni kasheria,usile tunda mtini.

  Bila hako kasheria... EBU ENDELEZENI JAMANI NINA USINGIZI
   
 7. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #7
  Apr 14, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Waridi nimependa hiyo.. nitakujibu...
   
 8. Sanda Matuta

  Sanda Matuta JF-Expert Member

  #8
  Apr 14, 2008
  Joined: May 9, 2007
  Messages: 950
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Du..h!
  Kweli waridi ni Mkali,Steve D ,Mkjj kadhalika wote humu ni wakali..yes i mean nyote kabisa ni wakali.
   
 9. Sanda Matuta

  Sanda Matuta JF-Expert Member

  #9
  Apr 14, 2008
  Joined: May 9, 2007
  Messages: 950
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Salamu na watolea,Nisai na Malijari.
  Kilingeni nimefika,ngaliba lete Mwali.
  Govile nitamtoa,ukubwa aukubari.
  Mti usio upanda wanini,Vinginevyo unashari.

  Steve D kasha sema,Huyu bwana hafai.
  vya mitini avitaka,hata vile vya bahari.
  Kwa jirani avifata,hata vya bwana Bushiri.
  Mti usio upanda wanini,Vinginevyo unashari.

  Wavinadi vimevunda,kumbe unatukebehi.
  Kwa Bushiri unakwenda,umesema huna siri.
  Mti wewe hujapanda,kwanini wataka kivuli.
  Mti usio upanda wanini,Vinginevyo unashari.

  Vyakwao wavivulaga,vyako wewe viko shwari.
  Nakwambia utapigwa,wamesama wenye wali.
  Korofi sasa acha,tena uanza kusali.
  Mti usio upanda wanini,Vinginevyo unashari.

  Kitu ulichozoea,thamanie huioni.
  Waridi unatetea,ngoja wakutoe soni.
  Mtio wakiutwaa,hauta upata sokoni.
  Mti usio upanda wanini,Vinginevyo unashari.
   
 10. Domo Kaya

  Domo Kaya JF-Expert Member

  #10
  Apr 14, 2008
  Joined: May 29, 2007
  Messages: 530
  Likes Received: 7
  Trophy Points: 0
  Nimekupenda sanda, umetulia.
   
 11. Palloma

  Palloma Member

  #11
  Apr 14, 2008
  Joined: Apr 8, 2008
  Messages: 8
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Jamvini najikongoja,
  Cheichei kwa pamoja,
  Heko mlotoa hoja
  'Sauti ya Shamba' kwa kuleta hii hoja,
  Naye 'Mwangwi wa Handaki' kajibu moja kwa moja,
  Kaomba tumalizie Waridi chake kioja,
  Nami nabinya vitufe kujibu hoja kwa hoja,
  Tunda la kuiba tamu!

  Tulia na utulize moyo wako,
  Punguza kilio chako,
  Kwani si wewe peke yako,
  Hata wa pembeni yako,
  Tuna kilema ka'chako,
  Tunda la kuiba tamu!

  Ingawaje nina tunda langu,
  Lindani shambani mwangu,
  Naliona kama nungunungu,
  Linachoma kwa uchungu,
  Nachelea la mwenzangu,
  Nauona ulimwengu,
  Si wangu ni wa wenzangu,
  Nidokoe tunda tamu!

  Tunda limenishangaza,
  Kwa unono lapendeza,
  Kwa deko lanipumbaza,
  Lina ngozi yateleza,
  Na macho yakulegeza,
  Udenda nikachuruza,
  Jino nikatumbukiza,
  Tunda nikalibinyiza,
  Jamani la kuiba tamu!

  La kuiba tamu tunda,
  Hiyo ndiyo yake inda,
  Lau upepo ukipinda,
  Akakufuma mlinda,
  Tendo baya takutenda,
  Kwa machozi utaenda,
  Nenda ewe mwana kwenda,
  Hapo tamu huwa chungu!

  Wahenga wajisemea,
  Yana tabu mazoea,
  Tunda 'kishalizoea,
  Sasa lishakupotea,
  Tena umelikimbia,
  Masikini la kuiba tamu!

  Yana tabu mazoea,
  Mengine 'takodolea,
  Kwani tamu 'mekolea,
  'Talinyemelea pea,
  Kidole talinyoshea,
  Nono tajichagulia,
  Mate tajidondoshea,
  Utamu jamani tamu,
  Tunda la kuiba tamu!
  Litabaki kuwa tamu!!!

  By Palloma (Binti wa Kitanga)
   
 12. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #12
  Apr 14, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  karibu Palloma!
   
 13. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #13
  Apr 14, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Tulia mwana nipange, majibu yangu niseme,
  Tulia bila mawenge, hoja zangu mzisome,
  Tulia miye nilonge, hili tunde nisiteme,
  Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!

  Tulia nikuambie, uzuri wa tunda lile,
  Tulia nisimulie, tunda hilo ni la kale,
  Tulie nihabarie, na wewe hilo ukale,
  Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!

  Tulia mwenye kuhoji, Bwana Bushiri kapanda,
  Tulia la mwenye mji, hakuliacha kuvunda,
  Tulia yeye mpaji, kalitunza hilo tunda,
  Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!

  Tulia mimi nakiri, sikuingia gharama,
  Tulia akisafiri, najinoma huku nyuma,
  Tulia alfajiri, hadi wanapoadhama,
  Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!

  Tulia kama mlevi, ndivyo ninavyosambua,
  Tulia kama mvuvi, tunda ninalichambua,
  Tulia silete gomvi, utamu nimeng'amua,
  Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!

  Tulia hata samadi, wa kijiji sikuweka,
  Tulia si ukaidi, mwenyewe naneemeka,
  Tulia silipi kodi, la bure nalitamka,
  Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!

  Tulia mwana nitame, kaditamati nafika,
  Tulia msiniseme, ati nimeghafirika,
  Tulia kisu kichume, na mchuzi kumwagika,
  Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!

  Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Shamba)
   
 14. Waridi

  Waridi JF-Expert Member

  #14
  Apr 15, 2008
  Joined: Mar 30, 2008
  Messages: 1,027
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 135
  Mwanakijiji,
  Wakikwibia na wewe,nyamaa sipige yowe,
  mkuki si kwa nguruwe,ugeuziwe na wewe,
  au wakupige mawe,wakikukamata wewe,
  mleta kumbe ni wewe,hii tabu ya kijiji!

  Watashangaa ujiji,na vya jirani vijiji,
  kwamba tabu ya kijiji,mleta MWANAKIJIJI,
  kumbe ni chako kipaji,kwa jirani wanywa maji,
  ama kumbe ndiwe gwiji, wa kukwapua matunda!
   
 15. MwanaHaki

  MwanaHaki R I P

  #15
  Apr 26, 2008
  Joined: Oct 17, 2006
  Messages: 2,403
  Likes Received: 122
  Trophy Points: 145
  Safi sana! Laiti ningejua kutunga mashairi... ngoja nitajaribu! Imetulia sana hii!
   
 16. H

  Haika JF-Expert Member

  #16
  May 5, 2008
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 2,318
  Likes Received: 62
  Trophy Points: 145
  Jf Ina Hazina Kubwa,
  Moderator Tafadhali Weka/tenga Sehemu Ya Waswahili Wenye Kupenda Lugha Yetu Kuifaidi Na Kusoma Bashasha Za Malenga.
   
Loading...