Utajiri wenye uchungu

Mfyuu James unaharaka sana yakufinyana,lazima tu mwisho utakuja kulizwa na kuherehere chakujiita young billionaire kitakuisha
 
NYEMO CHILONGANI.
UTAJIRI WENYE UCHUNGU.

Sehemu ya Sita.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kila kitu, maisha yao yakabadilika na James hakuwa radhi kuondoka, alizoeleka ndani ya nyumba hiyo na kitu pekee alichokibakiza ni kufunga ndoa na msichana Claire ambaye alikuwa na mimba yake.
Hakuwakumbuka wazazi wake, kichwa chake kilimwambia kwamba tayari wazazi wake nao walikuwa marehemu kutokana na tsunami lilivyopiga na hivyo vingi vingi kuharibika.
Hakutaka kujali sana, mtu ambaye alikuwa akimfikiria kwa wakati huo alikuwa msichana wake tu. Siku zikaendelea kukatika, hakutaka kumwambia Claire kuhusu zile almasi alizokuwa nazo, alikuwa msiri na alitaka kuzungumza naye kuhusu hilo mpaka pale atakapomuoa na kuwa mke wake wa ndoa.
Maisha hayakuwa mepesi, yalikuwa magumu lakini akavumilia sana, kuna wakati alitamani kumwambia msichana huyo juu ya kile kilichofichika nyuma ya pazia lakini wakati mwingine aliona kwamba muda haukuwa tayari.
Siku zikaendelea kukatika, katika kipindi chote hicho alikuwa mtu wa kukaa kimya, japokuwa alikuwa na msichana Claire ambaye alimpa mimba lakini bado kumbukumbu za Catherine ziliendelea kukisumbua kichwa chake.
Miezi ikakatika kwa kasi na baada ya miezi tisa, msichana Claire akajifungua mtoto wa kike na kumpa jina la Catherine kama kumbukumbu ya msichana wake aliyekufa kwenye janga la tsunami.
Kwake ilikuwa furaha tele, kila alipomwangalia mtoto huyo, alifanana naye sana. Muda wote James alikuwa na furaha tele, alimshukuru Mungu kwa kile kilichotokea na kila Jumapili alihakikisha anakuwa mtu wa kwenda kanisani tu.
“Ninakupenda, ninataka kukuoa,” alisema James, kwa kumwangalia tu ingekuwa rahisi kugundua kwamba mtu huyo alichanganyikiwa kwa furaha.
Hayo ndiyo maneno aliyokuwa akimwambia mara kwa mara. Kwa Claire, hiyo ilikuwa furaha tele, alijua ni kwa jinsi gani wasichana wa hapo kijijini walitamani kuolewa ila hawakuwa na bahati ya kupata wanaume kutokana na idadi ndogo ya wanaume mahali hapo.
Ili kumuonyesha msichana huyo kwamba alimaanisha, baada ya mwezi mmoja, wawili hao walikuwa kanisani, mchungaji alisimama mbele yao huku kukiwa na idadi ya watu ishirini ambao walifika kwa ajili ya kuishuhudia harusi hiyo.
“Ndiyo nimekubali...” alijibu Claire huku akiachia tabasamu pana.
Jioni ya siku hiyo wakaondoka na kuelekea mjini ambapo wakachukua chumba katika hoteli moja na kutulia huko. Usiku wa siku hiyo walikesha huku wakiwa wamekumbatiana, hawakuamini kwamba mwisho wa kila kitu hatimaye wangekuwa pamoja na kufunga ndoa na kuwa mume na mke.
Kwa kuwa alipanga kwamba angemuweka wazi Claire siku ambayo angemuoa, siku hiyo ndiyo aliuona wakati muafaka wa kumwambia ukweli juu ya utajiri mkubwa aliokuwa nao ambao aliuficha ndani kwa kipindi cha miezi kumi.
Alipomwambia mke wake kwamba kulikuwa na kitu alitaka kuzungumza naye, mwanamke huyo akaonekana kuogopa kwa kuhisi kuwa inawezekana kulikuwa na jambo baya lilitokea na hivyo alitaka kumpa taarifa.
“Mbona unaonekana kuogopa?” aliuliza James.
“Unataka kuzungumza nami kuhusu nini mpenzi?”
“Usiogope, ni habari njema!”
“Ipi?”
“Nikuulize swali?”
“Niulize...”
“Unakumbuka baba yako aliponiuliza siku ya kwanza nilimjibu mimi ni nani?” aliuliza James huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
“Ulimwambia wewe ni bilionea kijana...”
“Unaamini hilo?”
“Hapana!”
“Kwa nini?”
“Tumeishi kwa kipindi kirefu, sijauona huo ubilionea wako hata kidogo...”
“Leo nataka kukwambia kile nisichowahi kukwambia....”
“Kitu gani?”
“Kwamba mimi ni bilionea, tena bilionea wa kumi Marekani...”
“Unasemaje?”
“Huo ndiyo ukweli...”
Kwanza Claire akabaki kimya, akamwangalia mume wake huku akionekana kutokuamini kile alichomwambia, mara ya kwanza alifikiri ni utani lakini kila alipomwangalia mume wake huyo alionekana kumaanisha alichokuwa akikisema. Akajiweka vizuri kitandani na kumwangalia vizuri mume wake.
“Sijakuelewa....”
“Mimi ni bilionea, kuanzia kesho, tutanunua nyumba nzuri na kubwa, tutaendesha magari ya kifahari, tutafungua biashara nyingi na kubwa, nitakufanya uwe malkia wangu maisha yangu yote....” alisema James.
“Yote yanawezekana vipi haya?” aliuliza Claire.
Hapo ndipo James alipoanza kumuhadithia mke wake kile kilichotokea nyumba wakati tsunami ilipopiga. Hakutaka kumficha kitu, alimhadithia ukweli wa mambo na hakutaka kudanganya hata neno moja.
Claire alibaki kimya akimsikiliza, hakuamini kile alichokisikia. Aliukumbuka mzigo ambao aliubeba mwanaume huyo, alikuja nao nyumbani na hakumuachia mtu yeyote aone kile kilichokuwa ndani.
Moyo wake ukawa na furaha mno, hakuamini kama huo ndiyo ulikuwa mwisho wa umasikini waliokuwa nao, akamsogelea mumewe na kumkumbatia.
Huko katika fungate yao walikaa kwa muda wa wiki moja na ndipo wakarudi. Walipofika nyumbani, jambo la kwanza kabisa alilolifanya James ni kumuonyeshea mke wake ule mzigo aliokuwa nao, alipoufungua, Claire hakuamini alipoona madini ya Americanite, moja ya madini ghali zaidi duniani.
Huo nao ukawa mwanzo wa utajiri wao. Alichokifanya James ni kuwasiliana na watu waliohusika na madini kisha kuyauza kwa gharama kubwa. Hakuyauza yote, mengine alibaki nayo kwani yalikuwa mengi mno, kilo mbili hayakuwa madogo hata mara moja.
Mpaka robo ya madini yale yanamalizika, tayari alijitengenezea zaidi ya dola bilioni ishirini, zaidi ya trilioni arobaini. Maisha yake yakabadilika, akaanza kuingia kwenye utajiri mkubwa, akanunua majumba ya kifahari na kuanzisha biashara mbalimbali, akanunua ndege, akaanzisha kampuni zake mbalimbali.
James akawa bilionea, hakuwa masikini, akaanza kujulikana kwa Wamarekani kwamba alikuwa bilionea kijana ambaye alibadilisha maisha yake baada ya kuuza madini ya Americanite. Heshima ikawa kwake, wazazi wa Claire hawakuwa masikini tena, walinukia pesa, alihakikisha anabadilisha maisha ya kila mtu aliyehusika naye mara baada ya maafa makubwa kutokea jijini New Orleans.
“Where did this guy come from?” (Huyu jamaa ametoka wapi?) aliuliza jamaa mmoja.
“I don’t know where he came from,” (Sijui ametoka wapi)
Hilo ndilo lilikuwa swali la Wamarekani wengi, utajiri wake ulikuwa ni wa kushtukiza sana, wengi wakajiuliza juu ya mahali James alipotoka lakini hakukuwa na aliyejua. Akawaajiri wafanyakazi wengi katika kampuni zake ambazo kwa mwaka zilionekana kumuingizia zaidi ya dola bilioni ishirini, zaidi ya shilingi trilioni arobaini.

Je nini kitaendelea?
 
NYEMO CHILONGANI.
UTAJIRI WENYE UCHUNGU.

Sehemu ya Nane.

Wote walishtuka baada ya kupewa taarifa na dada wa kazi kwamba Catherine alikuwa amepoteza fahamu chumbani kwake. Wazazi wake wakatoka chumbani na kwenda chumbani kwake, walichoambiwa ndicho walichokutana nacho.
Kompyuta yake ilikuwa mbele yake, hawakutaka kujali sana, walichokiangalia ni afya ya binti yao hivyo walichokifanya ni kumchukua na kuanza kumpa huduma ya kwanza huku dada wa kazi akipewa jukumu la kumpigia simu daktari wa familia ili aweze kufika mahali hapo haraka iwezekanavyo.
Catherine alikuwa kimya kitandani alipolazwa, hakukuwa na aliyejua kitu gani kilikuwa kimetokea, walichanganyikiwa, huyo ndiye alikuwa binti yao wa kwanza, walimpenda mno kwa hiyo kitendo cha kupoteza fahamu hakika kiliwashtua na kuwauma mno.
Wote wakatulia wakimsubiri daktari wa familia aweze kufika, hawakuondoka chumbani humo, walikuwa pembeni yake huku kila mmoja akiwa na hofu moyoni mwake kwa kuhisi kulikuwa na jambo baya lilitokea kwani haikuwa rahisi hata kidogo kwa Catherine kuzimia, hakuwa na historia mbaya au ugonjwa wowote ule, sasa ni kitu gani kilimpekea kuzimia?
Kila walichojiuliza, hawakupata jibu, waliendelea kumsubiria daktari ambaye baada ya dakika kumi na tano, akawa ndani ya nyumba hiyo. Kwa haraka sana akaanza kuchukua vipimo kwa Catherine na kugundua kwamba msichana huyo alikuwa amepata mshtuko ambao uliupelekea moyo wake kupokea damu nyingi, tena kwa haraka sana hivyo kuzimia.
“Ila hana historia yoyote mbaya...” alisema Bwana James.
“Sawa! Ila inawezekana kuna kitu....”
Daktari akamtundikia dripu ya maji na kisha kumpa muda wa kupumzika huku kiyoyozi kikiendelea kupuliza. Baada ya dakika arobaini na tano, vidole vya Catherine vikaanza kutingishika hali iliyoonyesha kwamba alikuwa amerudiwa na fahamu.
“Mwacheni kwanza apumzike,” alisema daktari.
Kama walivyoambiwa ndivyo walivyofanya, wakampa muda zaidi wa kupumzika mpaka baada ya saa mbili ndipo wakaingia chumbani humo ambapo wakamkuta Catherine akiwa amejikunyata huku akilia kitandani mwake.
Wazazi hao wakamsogelea huku mioyo yao ikisikia maumivu makali mno, walipomfikia, nao wakakaa kitandani na kumuuliza tatizo lilikuwa nini mpaka kulia namna ile.
“Nimefeli...” alisema Catherine huku akiendelea kulia.
“Umefeli?” aliuliza baba yake.
“Ndiyo baba.”
Bwana James hakutaka kukubaliana na hilo, kwa kuwa matokeo yalikuwa wazi, akaichukua simu yake na kuanza kuperuzi, alitaka kuona kama kweli binti yake alikuwa amefeli kama alivyosema au kulikuwa na kingine kwani hakuamini kama kuna siku binti yake huyo angeweza kufeli mtihani.
Alipoangalia matokeo, akapigwa na mshtuko, japokuwa binti yake alisema kwamba alifeli lakini matokeo yalionyesha kwamba alikuwa mtu wa pili huku nafasi ya kwanza ikishikiliwa na mwanafunzi aliyeitwa Dylan
Matokeo yale yalionekana kuwa mazuri, baba yake aliyafurahia lakini kitu cha ajabu kabisa Catherine aliyakasirikia na ndiyo hayohayo yalimfanya kuzimia na hata kulia kipindi hicho.
“Nilitaka kuwa wa kwanza baba....” alisema Catherine huku mama yake akimbembeleza.
“Usijali mwanangu, matokeo si mabaya sana....”
“Kwa nini nimekuwa wa pili? Kwa nini nimeshuka? Kwa nini kuna mtu ana akili zaidi yangu? Kwa nini baba?” aliuliza Catherine.
“Huyu aliyeshika namba ya kwanza, hana akili zaidi yako, alikuwa mjanja katika vitu vichache tu binti yangu, amini kwamba wewe una akili zaidi yake,” alisema Bwana James.
“Kweli baba?”
“Ndiyo Catherine, wewe una akili mno...”
Yalikuwa maneno yenye faraja, yaliamsha ari mpya moyoni mwake, japokuwa wakati mwingine alikuwa na huzuni lakini kila alipokumbuka maneno ya baba yake yaliyomwambia kwamba alikuwa na akili mno, yalimpa nguvu mpya.
Matokeo hayo hakutaka kuyaangalia tena, alitaka kuyasahau kabisa, siku zikaendelea kukatika, kitu kilichousumbua moyo wake ni huyo mtu aliyeitwa kwa jina la Dylan ambaye matokeo yalionyesha kwamba alikuwa na akili kuliko yeye.
Alitaka kumuona, alifananaje, alikuwaje, kiu yake kubwa ikawa ni kumuona tu. Alitamani kwenda shuleni kwao, ila ilikuwa uswahilini sana, sehemu ambayo kulikuwa na wahuni wengi, kutoa bunduki lilikuwa jambo la kawaida na hata ukisikia mtu amechomwa visu vingi, hakuna kushangaa kwani mambo kama hayo yalikuwa yakitokea sana tu.
Kwa sababu waliambiwa kwamba watu kumi watakaofanya vizuri wangepata nafasi ya kwenda ikulu na kuonana na rais, alitaka kumuona huyo Dylan kwa kuamini kwamba ile kiu aliyokuwa nayo hakika ingepoa kabisa.
Siku zikaendelea kukatika huku akiendelea kuwa na kiu kubwa ya kumuona huyo Dylan, baada ya mwezi mmoja kukatika ndipo akapokea mualiko maalumu kwamba alikuwa akihitajika katika ikulu ya Marekani kama miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri.
Siku ya kwenda huko, mama yake, bi Claire ndiye aliyekuwa msindikizaji mkuu, Bwana James hakutaka kwenda kwa sababu alikuwa bize na mambo yake ya biashara kwani siku hiyohiyo ndiyo aliyosafiri mpaka jijini Texas na kusaini mkataba na Wamexico kwa ajili ya kusambaza maji nchini humo.
Walipofika katika geti la ikulu, likafunguliwa na kisha kuingia ndani hasa baada ya shughuli zote za kupekuliwa zilipokamilika. Humo ndani, kulikuwa na sehemu maalumu iliyoandaliwa vizuri, watu walitakiwa kuwa huko.
Kulikuwa na wageni waalikwa, waandishi wa habari na watu wengi, wakatafuta sehemu iliyokuwa na viti viwili na kutulia hapo. Watu walizidi kuongezeka na baada ya dakika kadhaa, hafla ikaanza.
Muda wote Catherine alikuwa na shauku ya kuangalia huku na kule, bado alitaka kumuona huyo Dylan alikuwaje. Wakati rais akiwa amesimama, akaanza kuwaita wanafunzi hao kwa ajili ya kuchukua zawadi, akaanza kwa mtu wa kumi na kushuka chini.
“Naitwa Catherine, ninamshukuru Mungu kwa kufanya vizuri...” alisema Catherine huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
Alipomaliza akashuka na ndipo jina la Dylan likatajwa. Catherine akajiweka vizuri, mtu aliyekuwa akitaka kumuona ndiye aliyeitwa, alitaka kumuona alifananaje mpaka awe na akili kuliko yeye.
Kijana huyo aliposimama na kwenda mbele, Catherine alimkazia macho, hakumuona kwa mbele, kwa kuwa alikuwa akielekea jukwaani, akabaki akiangalia mgongo tu, kijana huyo alipofika mbele, akapeana mkono na rais na kuwageukia watu waliokuwa mahali hapo.
Kitu cha ajabu kabisa, Catherine na mama yake wakapigwa na mshtuko mkubwa, walipomwangalia kijana huyo, alifanana sana na Bwana James, yaani kama wangesimama pamoja, ilikuwa ni rahisi kusema kwamba watu hao walikuwa mapacha.
“Mmmh!” wote walijikuta wakiguna kwa pamoja.
**
Kwa jina aliitwa Leticia Bullock Christopher, alikuwa miongoni mwa watu masikini waliokuwa wakiishi katika Jiji la Kenner. Watu wengi mahali hapo walimtambua kwa jina la widow yaani mjane.
Miaka michache iliyopita, mume wake ambaye aliyafanya maisha yake kuwa afadhali alifariki katika ajali iliyojaa utata mkubwa hali iliyowafanya watu wengi kuhisi kwamba kulikuwa na mkono wa mtu nyuma ya pazia.
Lilikuwa tukio baya, lililomhuzunisha, taarifa zikatolewa katika kituo cha polisi hapo Kenner kwa ajili ya kufuatilia kwa ukaribu chanzo cha ajali hiyo lakini hakuna kilichofanyika. Hakutaka kukata tamaa, akatoa taarifa mpaka katika Shirika la Upelelezi ndani ya nchi ya Marekani, Fideral Bureau of Investigation (FBI) lakini hakukuwa na kilichoendelea.
Alisikitika sana, pamoja na hayo, moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akipitia maisha hayo, aliwachukia polisi wote, akawachukia wapelelezi wote nchini Marekani na wakati mwingine alihisi kwamba kulikuwa na mtu aliyeyafanya yote hayo, kumsababishia maumivu makubwa moyoni mwake.
Wakati akiwa katika huzuni kubwa juu ya kifo cha mume wake, mtoto wake aliyekuwa akimpenda ambaye alikuwa ndiye mfariji wa maisha yake, Carlos aliyekuwa na miaka minne, naye akafariki kwa ugonjwa wa polio ambao ulimtesa tangu kuzaliwa kwake.
Moyo wake ukaumia, maumivu aliyoyapata hayakuweza kuelezeka, alikuwa mtu wa kulia kila siku, kila kilichotokea katika maisha yake aliona kama alikuwa katika moja ya ndoto ya kusisimua ambapo baada ya muda fulani angeamka na kujikuta akiwa kitandani.
Kilichoendelea hakikuwa ndoto, yalikuwa matukio yaliyoendelea katika maisha yake halisi, maisha yake yaliendelea kuwa na huzuni mpaka pale alipofanikiwa kukabidhiwa mtoto mdogo, aliyekuwa amefunikwa ndani ya friji, huyo ndiye akawa furaha yake kwa mara nyingine.
Alimpenda mtoto huyo aliyempa jina la Dylan, alimlea katika malezi mazuri, hakutaka aishi kama watoto wengine wa mitaani ambao walikuwa na tabia mbaya, kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kumpeleka sana kanisani kila alipohitajika.
Miaka ikakatika, Dylan akaendelea kukua katika mikono ya mwanamke huyo, hakujua kama aliokotwa, hakujua kama mwanamke huyo aliyemuita mama hakuwa mama yake, kila kitu kilichotokea kipindi cha nyuma kilikuwa siri kubwa sana.
“Mom...” aliita Dylan.
“Yes my son...” (Ndiyo kijana wangu)
“I want to be a pastor when I grow up,” (Nataka kuwa mchungaji nitakapokua) alisema Dylan.
“You will be my son, what you have to do is praying to God, anything can be possible through Him,” (Utakuwa tu kijana wangu, unachotakiwa kufanya ni kuomba, kila kitu kinawezekana kwake) alisema bi Leticia huku akimwangalia Dylan usoni mwake.

Je, nini kitaendelea
 
15 Reactions
Reply
Back
Top Bottom