Utajiri wenye uchungu

Madame S

JF-Expert Member
Mar 4, 2015
17,172
34,277
NYEMO CHILONGANI.
UTAJIRI WENYE UCHUNGU.

Sehemu ya Kwanza.

“All people who live at the beach have to leave immediately because tsunami will come. Once you hear this announcement, tell your colleague,” (Watu wote mnaoishi katika ufukwe mnatakiwa muondoke haraka iwezekanavyo kwa sababu tsunami itakuja. Unaposikia tangazo hili mtaarifu na mwenzako,)” ilisikika sauti ya mwanamke aliyekuwa akitangaza katika Kituo cha Redio cha Orange Fm nchini Marekani.
Watu wote waliokuwa wakiishi katika fukwe mbalimbali katika Jiji la New Orleans nchini Marekani walitakiwa kuondoka haraka iwezekanavyo kwani tayari mamlaka ya hali ya hewa ya nchini humo (National Weather Service) ilitangaza hali ya hatari ambayo ingelipata jiji hilo pamoja na majiji mengine yaliyokuwa katika fukwe mbalimbali ikiwemo Miami.
Hakukuwa na mtu aliyepuuzia taarifa hiyo, wengi wakaanza kuondoka kwa ajili ya kuyaokoa maisha yao kwani bado kumbukumbu juu ya kimbunga cha Katrina ambacho kilipiga miezi michache iliyopita bado ziliendelea kubaki vichwani mwao.
Mitaani kulikuwa na purukushani, kila mtu alitaka kuyaokoa maisha yake. Kumbukumbu juu ya tsunami zilikuwa vichwani mwao, walisoma kwenye historia miaka ya nyuma kwamba balaa hilo liliwahi kuikumba China na Japan na matokeo yake watu wengi walifariki dunia.
Serikali ya Marekani ikaagiza magari makubwa na kuwataka watu wote waondoke katika sehemu za ufukwe na kukimbia umbali wa kilometa ishirini kutoka ufukweni kwani pasipo kufanya hivyo ilikuwa ni lazima tsunami iwakumbe na kufariki dunia.
Watu waliondoka, helkopta zilipita kila kona ndani ya jiji hilo, mtu mmoja aliyekuwa akitangaza kwenye kipaza sauti alisikika akiwaambia watu kwamba huo ulikuwa ni muda wa kuondoka, kulikimbia jiji hilo kutokana na maafa ambayo yalitarajiwa kulikumba jiji hilo, tena saa mbili zijazo.
“Where is Catherine?” (Catherine yupo wapi?) alisikika mwanamke mmoja akiuliza.
“I don’t know . She told me that she would go to James, maybe she went there (Sifahamu. Aliniambia kwamba angekwenda kwa James, labda alikwenda huko) alijibu mwanaume mmoja.
Hakutaka kujali sana, kwa kuwa aliambiwa kwamba msichana huyo alikwenda kwa mwanaume aitwaye James, hakutaka kuuliza zaidi ya kuendelea na safari yao ya kuyaokoa maisha yao kwani lilikuwa limebaki saa moja kabla ya janga hilo kulikumba Jiji la New Orleans na miji yote ambayo ilikuwa karibu na bahari.
Mamlaka ya hali ya hewa nchini Marekani haikukaa kimya, bado iliendelea kutoa onyo kwamba watu wote waliokuwa wakiishi pembezoni mwa bahari ya Atlantic walitakiwa kuondoka kwani tsunami liliendelea kuja kwa kasi kwa kipimo cha 4.11 ambacho kilikuwa ni kikubwa mno huku mawimbi yake yakiwa na urefu wa mita mia moja kwenda juu ambayo yalikuwa yakienda kwa kasi ya kilometa 2 kwa dakika tano.
Huko lilipoanzia nchini China, Thailand na nchi nyingine barani Asia, liliacha vilio, zaidi ya watu milioni mbili walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya huku makazi ya watu wengi yakiharibiwa mno.
Maafa yaliyotokea nchini China kipindi hicho waliyaona kwenye televisheni, waliogopa na kuhisi kwamba inawezekana tsunami hilo lingefika mpaka nchini Marekani kwani hata wao kulikuwa na miji ambayo ilikuwa pembezoni mwa bahari, kweli ikawa hivyo.
“Mnatakiwa kuchukua vitu vilivyokuwa muhimu kwenu, ambavyo havina umuhimu viacheni na serikali itawasaidia kwa kila kitu,” bado tangazo lilikuwa likitolewa kutoka kwa mtu aliyekuwa kwenye helkopta ambaye alitumia kipaza sauti kilichosikika vizuri kabisa na kila mtu.
Muda ulizidi kwenda mbele, dakika arobaini na tano baadaye, ukimya mkubwa ulitawala kila kona ndani ya jiji hilo, hakukuwa na sauti yoyote iliyosikika, si binadamu tu bali hata wanyama hawakuwepo, watu walikimbia na kwenda katika Mji wa Gonzales uliokuwa kilometa ishirini kutoka hapo New Orleans.
“Jamani naomba mnisaidie, namtafuta binti yangu...” alisema mwanamke mmoja, kwa kumwangalia tu alionekana kuwa na hofu moyoni mwake, alikuwa akimwambia mmoja wa wanajeshi ambao waliwachukua watu kutoka New Orleans.
“Anaitwa nani?”
“Catherine, mara ya mwisho kabla tangazo halijatolewa, alikwenda kwa mpenzi wake, sijui kama yupo naye kwa sababu hata wazazi wa mpenzi wake tulionana nao wakasema kwamba hata kijana wao hayupo nao,” alisema mwanamke huyo.
Hiyo ilikuwa kazi nyingine kabisa, alichokifanya mwanajeshi huyo ni kuonana na wazazi wa huyo kijana ambaye alikuwa mpenzi wa Catherine aitwaye James na kuanza kuzungumza nao.
Kama alivyoambiwa na mama yake Catherine ndivyo alivyoambiwa hata na wazazi hao kwamba kijana wao aitwaye James hakuwa akionekana. Hiyo ikawatia hofu kwa kuhisi kwamba japokuwa mahali hapo waliona kwamba kila mtu alikuwa hapo kumbe kuna wawili ambao hawakuwa hapo.
Walichokifanya ni kuanza kuyaita majina yao kila kona kwa kupitia kipaza sauti. Kila aliyesikia, akabaki akimwangalia mwenzake kwa kuhisi labda huyo ndiye aliyekuwa akihitajika.
Zaidi ya watu milioni nne waliokuwa wamekimbia katika jiji hilo, ni watu wawili tu ndiyo ambao hawakuwa wakionekana, kwani familia zote zilikuwepo na kila moja walitimia isipokuwa familia mbili ambazo watu wawili hawakuonekana.
Tayari kukaonekana kuwa na tatizo sehemu, mwanajeshi yule akawapa taarifa wenzake kwamba watu wawili hawakuwa wakionekana mahali hapo hivyo walitakiwa kwenda kuwatafuta katika jiji hilo, hata kama kuwaita walitakiwa kufanya hivyo ilimradi wawapate na kuwaleta pale walipokuwa.
“Zimebaki dakika ngapi kabla ya Tsunami kuipiga New Orleans?” aliuliza mwanajeshi mmoja.
“Dakika ishirini!”
“Chukueni helkopta haraka muende kuwatafuta...”
Hicho ndicho kilichofanyika, hakukuwa na muda wa kupoteza mahali hapo, kwa haraka sana wanajeshi sita wakaingia katika helkopta moja kubwa na kuanza kurudi ndani ya jiji hilo kwa ajili ya kuwatafuta watu wawili tu, msichana mjauzito aliyeitwa Catherine na mwanaume aliyeitwa James.
Walipofika katika jiji hilo, wakachukua darubini na kuanza kuangalia, kila kona, hakukuwa na mtu yeyote, hakukuwa na mnyama, ni nyumba na magari machache ndivyo vilivyokuwa vimebaki.
Hawakukata tamaa, waliendelea kuwatafuta huku wakiita kwa sauti kubwa tena kwa kutumia kipaza sauti lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyeitikia au hata kutoka na kuwapungia mikono kuonyesha kwamba alitaka msaada.
Dakika ziliendelea kukatika, zilipofika dakika kumi na tisa tu, kwa mbali baharini likaanza kuonekana wimbi kubwa na zito likija kwa kasi. Waliliangalia wimbi lile, lilikuwa kubwa zaidi ya mita mia moja ambayo ilitangazwa na mamlaka ya hali ya hewa.
Lilikuwa likija kwa kasi mno na hata muungurumo wake ulikuwa mkubwa. Halikuwa likija peke yake bali lilikuwa likija na meli kadhaa kubwa zilizokuwa baharini ambazo nazo zilisombwa na tsunami hiyo.
“It is coming...it is coming...” (Linakuja...linakuja..) alisema mwanajeshi mmoja, rubani akageuza helkopta ile na kuanza kuondoka kwani kwa jinsi wimbi lile lilivyokuwa likija kwa kasi, tena huku likiwa kubwa namna ile, walijua kabisa wangeweza kupata tatizo, hivyo wakaondoka huku wakiahirisha kuwatafuta watu hao ambao ukweli wenyewe ni kwamba walikuwa hai, tena msichana Catherine akiwa kwenye uchungu mkubwa wa kujifungua mbele ya mpenzi wake, James.
 
NYEMO CHILONGANI
UTAJIRI WENYE UCHUNGU

Sehemu ya Pili.

Catherine alikuwa na tumbo kubwa, ujauzito huo tayari ulikuwa umetimiza miezi tisa na muda wowote kuanzia siku hiyo angeweza kujifungua. Kila alipokaa, alionekana kuwa na furaha mno, hakuamini kama siku chache au saa chache zijazo naye angeitwa mama.
Mwanaume aliyempa mimba alikuwa James Carthbert, mwanaume mwenye sura nzuri aliyekuwa na mchanganyiko wa rangi kwa maana ya baba kuwa mtu mweusi na mama Mzungu.
Siku hiyo Catherine hakutaka kukaa nyumbani kwao, alichokifanya ni kuondoka kuelekea nyumbani kwa kina James, alitaka kuonana na mwanaume huyo ili hata pale atakapoanza kujisikia uchungu basi apelekwe hospitali kwani mahali alipokuwa akiishi James kulikuwa karibu na Hospitali ya Cambodia Medical Center.
“I have come, I want you to take me to the hospital,” (Nimekuja, ninataka unipeleke hospitali) alisema Catherine huku akiteremka ndani ya gari.
“What time?” (Muda gani)
“Once I feel labor pains,” (Mara nitakapojisikia uchungu wa kuzaa) alisema Catherine.
“No hay problema mi ángel,” (hakuna tatizo malaika wangu) alisema James kwa Kihispania.
Akamchukua msichana wake na kuingia naye ndani. Wakaenda chumbani na kutulia kitandani. Walikuwa wakizungumza mambo mengi kuhusu maisha yao, walikwishajua kwamba mtoto ambaye angezaliwa alikuwa ni wa kiume hivyo walianza kupanga mipango yao namna ya kumlea na kumfanya kuwa miongoni mwa watoto waliokuwa na bahati duniani.
Waliyaandaa maisha yake angali yupo tumboni, wakajipanga vilivyo na kuhakikisha wanampa furaha ambayo hatoweza kuipata kutoka kwa mtu mwingine yeyote yule.
Walijifungia chumbani, hawakutaka kuingiliwa na mtu yeyote na kitu walichokisubiri wakati huo kilikuwa ni maumivu ya uchungu wa kuzaa kutoka kwa Catherine ambaye angekimbizwa katika Hospitali ya Cambodia ambayo wala haikuwa mbali kutoka hapo walipokuwa.
Baada ya kukaa kwa saa moja chumbani tena huku redio ikisikika, wakaanza kusikia tangazo kwamba watu wote walitakiwa kuondoka kwani tsunami ilikuwa njiani kulipiga Jiji la New Orleans.
Kwanza hawakuamini walichokisikia, Alichokifanya James ni kuifuata redio, akaongeza sauti kwa ajili ya kusikia vizuri kilichokuwa kikitangazwa, hakukuwa na mabadiliko, ni kweli mamlaka ya hali ya hewa ya nchini Marekani ilitangaza kuwepo kwa hali ya hatari dakika chache zijazo hivyo watu wote walitakiwa kuondoka.
“All people who live at the beach have to leave immediately because tsunami will come. Once you hear this announcement, tell your colleague,” (Watu wote mnaoishi katika ufukwe mnatakiwa muondoke haraka iwezekanavyo kwa sababu tsunami inakuja. Unaposikia tangazo hili mtaarifu na mwenzako,) ilisikika vizuri sauti ya mtangazaji huyo.
“We have to run,” (Inatupasa tukimbie) alisema James.
“I can’t James...” (Siwezi James..)
“Why?” (Kwa nini?)
“My time has come,” (Muda wangu umewadia) alisema Catherine huku akianza kujisikia uchungu kwani hata pale kitandani alipokuwa, alianza kujinyonganyonga.
Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya James ni kuchungulia dirishani, akaona watu wakianza kuondoka tena kwa kukimbia huku wengine wakitumia magari yao, alitamani kuomba msaada kwani kwa hali aliyofikia mpenzi wake ilionyesha kwamba muda wowote ule angeweza kujifungua.
Catherine akaanza kupiga kelele za maumivu, James akachanganyikiwa, alishindwa kuwaita hata watu waliokuwa nani ya nyumba hiyo kwani kila mmoja alianza kukimbia kufuatia tangazo lililotolewa kwamba watu wote walitakiwa kuondoka.
Hakutaka kukubali kirahisi, hakutaka kujiona akishindwa, hakuamini taarifa hizo japokuwa tayari helkopta zilianza kupita na kuwatangazia watu kwamba walitakiwa kuondoka kutokana na tsunami ambayo ilikuwa njiani kulipiga jiji hilo.
Dakika kumi mbele, ukimya mkubwa ulitawala, alipochungulia tena dirishani hakumuona mtu yeyote yule hali iliyomfanya kumsogelea Catherine pale alipokuwa na kuanza kuongea naye.
“Nitapambana mpaka unajifungua salama,” alisema James huku akimwangalia msichana huyo machoni.
“Nisaidie, naumia, nisaidie James...” alisema Catherine, tayari kijasho chembamba kikaanza kumtoka.
Alichokifanya James ni kuipanua miguu yake, na kuiingiza mikono yake katika njia ya kutolela mtoto na kumwambia aanze kusukuma. Hicho ndicho alichokifanya Catherine, akaanza kusukuma kama alivyoambiwa.
Alijitahidi, alipiga kelele, alisukuma kadiri alivyoweza lakini bado mtoto hakutoka, aliendelea kuambiwa asukume zaidi. Hakuacha, japokuwa alikuwa akisikika maumivu makali lakini aliendelea zaidi na zaidi.
Baada ya dakika kadhaa, James akaanza kusikia mlio wa helkopta kwa mbali, si mlio wa chombo hicho tu bali akaanza kumsikia mtu mmoja akiongea kwenye kipaza sauti akimtaka yeye na mpenzi wake wajitokeze kwani tsunami ilikuwa ikija.
“Siwezi kuondoka na kumuacha mpenzi wangu hapa,” alisema James huku tayari mtoto alianza kutoa kichwa.
James hakuacha, aliendelea kumvuta mtoto huyo huku Catherine akipiga kelele za maumivu makali. Ghafla kwa mbali akaanza kusikika sauti kubwa ikija kule walipokuwa, alijua fika kwamba hiyo ndiyo ilikuwa tsunami ikija lakini hakukimbia, kama kufa, alikuwa radhi kufa na familia yake lakini si kuiacha.
“Tunakufa James...” alisema Catherine kwa sauti ya chini, tayari mtoto alitolewa, alionyeshewa, japokuwa alikuwa mdogo lakini alionekana kufanana sana na James.
“Hatuwezi kufa....nitakulinda, kama utakufa, basi tufe wote,” alisema James huku akikikata kitovu cha mtoto.
Kwa haraka akakimbilia kabatini, akachukua taulo lake na kumfunikia mtoto, akamuweka pembeni, akalifuata friji lake dogo la chumbani na kuliangusha chini, akatoa vitu vyote na kisha kumuingiza mtoto wake.
“Catherine mpenzi....”
“Nipo hapa mpenzi...” aliitikia Catherine kwa sauti ya chini kabisa, sauti iliyosikika kama mtu aliyechoka mno.
“Kama tutakufa, acha mtoto wetu awe hai...”
“Yupo wapi?”
“Nimemuweka kwenye friji, tsunami inakuja, nitataka yeye aelee na anusurike,” alisema James huku akimshika mkono mpenzi wake. Muda wote huo mtoto yule alikuwa akilia tu.
Wala hazikupita dakika nyingi, maji yakawafikia, nyumba ikasombwa na maji hayo. Catherine, tena huku akiwa kwenye maumivu makali na mchoko mkubwa akaanza kupiga kelele za kuomba msaada, alikuwa akimuita mpenzi wake lakini hakuwa karibu naye na wala hakumuona.
Yeye na nyumba, vyote vikasombwa na maji na kuanza kupelekwa sehemu nyingine kabisa, maji mengi yenye urefu wa kwenda juu zaidi ya mita mia moja yakamchukua.
Kwa upande wa James, alijitahidi kupiga mbizi, kushikilia vyuma vya meli zilizosombwa na maji kutoka baharini, kote huko ilikuwa ni mishemishe ya kuyaokoa maisha yake.
“Catherine...Catherineeee...” alianza kuita mara baada ya kugundua kwamba alikuwa peke yake.
Alichanganyikiwa, aliangalia kila kona kumtafuta mpenzi wake, hakuweza kumuona. Maji yale yalikuwa na nguvu mno, yalimpeleka huku na kule, alijigonga kwenye vyuma, magari yaliyokuwa yakielea kiasi kwamba yakamfanya kuwa hoi, baada ya muda fulani, mikono yake ikaishiwa nguvu, hakuweza kushikilia hata vyuma vilivyokuwa vikielea.
“Bora nife...” alijisemea huku mikono yake ikiwa imeishiwa nguvu, akaangalia huku na kule, kote kulijaa maji, hata maghorofa makubwa yenye floo zaidi ya mia moja nayo yote yalizamishwa na maji hayo.
Alijiona akiwa baharini, hakuwa na nguvu tena, alikosa msaada hivyo kitu alichokiona ilikuwa ni lazima akubaliane na ukweli hivyo azame. Akaulegeza mwili wake, akajiweka tayari kwa kufa.
“Pokea roho yangu Mungu! Mlinde na mtoto wangu kwenye friji pasipo kumsahau mpenzi wangu, Catherine ambaye sijui yupo wapi,” alisema James huku akiwa hoi. Sasa akawa tayari kwa kufa.

Je, nini kitaendelea?
 
NYEMO CHILONGANI
UTAJIRI WENYE UCHUNGU

Sehemu ya Tatu.

Alikubaliana na ukweli kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya uhai wake, akakubali kufa kwani hakukuwa na chochote alichoweza kufanya zaidi ya kumruhusu Israeli achukue roho yake naye kuwa miongoni mwa watu waliokufa katika balaa la mafuriko la tsunami.
Wakati akiwa amekata tamaa kabisa, ghafla akaliona jengo moja refu, lenye floo zaidi ya mia moja na hamsini na lilijengwa katikati mwa Jiji la New Orleans, hilo lilikuwa ghorofa la vioo ambalo ndani yake kulikuwa na ofisi nyingi ikiwemo Studio ya Murder Inc ambayo ilikuwa ikivuma sana nchini Marekani kwa kurekodi nyimbo za wasanii wengi akiwemo Ashanti.
Akajikuta akipata nguvu mwilini mwake, hakutaka kuchelewa, huo ndiyo ulikuwa msaada wake wa mwisho, kama angeshindwa, basi alikuwa tayari kufa. Alichokifanya ni kuanza kupiga mbizi kulifuata ghorofa hilo.
Ilikuwa kazi kubwa lakini hakutaka kukata tamaa, aliendelea zaidi, alichoka lakini akajilazimisha kwani aliamini kwamba kama angefanikiwa kulifikia jengo lile basi angekuwa salama,asingekufa kama alivyotegemea.
Jengo lile lilikuwa mbali kama wa hatua mia moja kutoka pale alipokuwa, tena likiwa linaonekana kidogo sana, akakazana kupiga mbizi mpaka alipoanza kulifikia, akaongeza kasi kidogo, akalifikia na kudandia juu.
Akakaa kileleni, aliishiwa nguvu na hivyo kulala kwanza. Baada ya dakika kadhaa akapata nguvu na kuangalia kule alipotoka, maji yalijaa kila sehemu, ilikuwa ni vigumu sana kugundua kwamba sehemu hiyo iliyokuwa imejaa maji kulikuwa na mji, ilionekana kuwa moja ya bahari kubwa.
Hakutaka kuondoka katika jengo hilo, aliendelea kutulia huko juu huku macho yake yakiangalia huku na kule. Hilo ndilo lilikuwa jengo kubwa kuliko majengo yote kwa maana hiyo kwa kipindi hicho yeye ndiye alikuwa kileleni kuliko mtu yeyote katika jengo hilo.
Hapo ndipo kumbukumbu juu ya Catherine zilipomjia, moyo wake ulimuuma mno, alikuwa na lengo la kumsaidia mpenzi wake huyo lakini kitu cha ajabu, baada ya tsunami kupiga, hakuweza kubaki naye, akajikuta akitenganishwa yeye na mpenzi wake.
Mawazo yake hayakuishia kwa mpenzi wake tu bali hata kwa mtoto wake wa kiume aliyefikiria kumpa jina la Leonard. Alimkumbuka, alimuona mara moja tu, baada ya hapo akamuingiza ndani ya friji, kilichoendelea hakukijua, hakujua kama kweli alinusurika katika friji lile au la.
Siku hiyo ilikuwa ya mateso tele, alishinda katika jengo hilo, baridi lilimpiga sana na hakukuwa na dalili zozote za msaada kutoka sehemu yoyote ile kwani hata meli zenyewe ambazo zilitakiwa kutoa msaada, zilikuwa zimegeuzwa, chini juu, juu chini.
Muda ulizidi kwenda mbele, hakukuwa na dalili zozote zile za maji hayo kupungua, alipigwa na baridi usiku kucha, alikesha huku akiwa amelala katika jengo hilo juu kabisa, katika kila upande alioangalia, aliona maji, maji kila sehemu.
Siku hiyo ikakatika pasipo msaada wowote ule, kulipokucha, kidogo maji yakaanza kupungua, kutoka kwenye floo ya mia na hamsini aliyokuwepo mpaka mia na ishirini. Hapo akamshukuru Mungu, alichokifanya ni kuanza kushuka kwenda kwenye floo za chini, alifanikiwa kuvunja zaidi vioo vilivyovunjika na kuingia humo.
Hizo zilikuwa ofisi za Kampuni ya Madini ya Americanite ambayo ilikuwa ikipokea madini ya Tanzanite kutoka nchini Tanzania. Kwanza alipoona maneno yakiwa yameandikwa Americanite Company Limited, hakuamini, akaanza kusogea kulipokuwa na mlango wa kuingilia.
Akaingia kwenye mlango mmoja ambao ulikuwa kama sehemu ya kuingia katika mlango wa siri wa sehemu ya kuhifadhia madini ya bei kubwa. Kweli alipoufikia mlango huo, akaukuta ukiwa umefunguka kidogo kutokana na kupigwa sana na maji, akaufungua na kuingia ndani.
“Ooh! My God!” (Mungu wangu!) alijikuta akisema kwa mshtuko.
Kilichokuwa kikionekana mbele yake kwenye kabati kilikuwa ni madini ya almasi ya Americanite, alishtuka, yalikuwa mengi ambayo yangemfanya kuwa bilionea wa kimataifa. Aliyaangalia kwa tamaa lakini hakuwa na nguvu ya kuyachukua, kitu peke alichokihitaji kwa wakati huo ni chakula tu.
“Kwanza chakula, la sivyo nitakufa...” alijisemea huku akianza kuzungukazunguka humo ndani, bahati mbaya kwake, hakukuta chakula chochote kile.
****
Hali ilitisha, dunia ilitingishika, kile kilichotokea jijini New Orleans nchini Marekani kilimshangaza kila mmoja. Hilo halikuwa tsunami kama walivyolitegemea, lilikuwa kitu kingine ambacho kilikuwa tofauti na tsunami.
Hakukuwa na tsunami la hivyo, yaani la maji kusimama sehemu moja na kutengeneza mafuriko makubwa. Kitu kama hicho walizoea kukiona kwenye filamu mbalimbali za Kimarekani, ila leo hii, zile filamu zilionekana kuwa kweli, mafuriko yakaja na mali nyingi kuharibika.
New Orleans ikageuka na kuwa bahari kubwa, majengo hayakuonekana zaidi ya jengo moja tu ambalo lilikuwa refu kuliko majengo mengine jijini hapo. Waandishi wa habari wote walikwenda katika Jijini la Gonzalez ambalo lililokuwa kilometa ishirini kutoka katika Jiji la Orleans.
“Hii ni bahari,” alisema mwanaume mmoja, alionekana kushangaa, maji yalianzia hapo aliposimama mpaka ndani ya jiji hilo.
Taarifa zikatolewa kwamba miongoni mwa watu wote waliokuwa wakiishi katika jiji hilo, wote waliokolewa isipokuwa watu wawili tu, mwanaume aliyekuwa na mpenzi wake aliyekuwa mjauzito.
Hakukuwa na mtu aliyejua mahali watu hao walipokuwa kwani hata wanajeshi wa mwisho kabisa kwenda katika jiji hilo kuwatafuta, hawakuwapata japokuwa walikuwa na helkopta na kutangaza huku na kule lakini bado kulikuwa kimya.
Wazazi wao walikuwa wakilia tu, hawakuamini kama kweli watoto wao walikuwa wamekufa au la. Watu wengine waliwafariji kwa kuwaambia kwamba watoto wao walikuwa hai lakini hilo hawakukubaliana nalo hata kidogo, walichokuwa wakikiona mbele yao ni kwamba watoto wao walikufa katika maji yale.
Usiku hawakulala, sehemu waliyowekwa ambayo ilikuwa na maturubai mengi ilionekana kuwa salama na ndiyo sehemu ambayo serikali ya Marekani ilitoa kwa wahanga hao.
Ilipofika usiku wa saa nane, mwanaume mmoja akaingia katika turubai lao na kuwaita, mwanaume huyo alikuwa na taarifa mbaya ambayo alitaka kuwapa.
“Kuna nini?” aliuliza mama Catherine.
“Njooni huku,” alisema mwanaume huyo ambaye alikuwa mwanajeshi.
Hawakujua kuna nini lakini wakahisi kwamba inawezekana binti yao alikuwa amepatikana hivyo wakakaza miili yao kumfuata mwanaume huyo. Wakaenda katika turubai jingine alilokuwa akiishi baba yake James na kuwachukua wazazi wa mwanaume huyo na kuondoka nao.
Huko walipokwenda ilikuwa ni kwenye turubai la huduma ya kwanza ambapo wakaambiwa wasubiri kwani kulikuwa na mwili wa mtu mmoja ulipatikana.
“Ni mwanaume au mwanamke?” aliuliza mama yake Catherine.
“Subiri wala msijali, mtajua tu,” alisema mwanaume huyo na kuingia ndani.
Baadaya dakika chache akatokea mwanaume mwingine, alikuwa daktari aliyevalia koti refu jeupe, akawataka kuingia ndani na kuutambua mwili uliokuwa umepatikana, walipoingia, wakachukuliwa na kupelekwa katika chumba kimoja, huko kulikuwa na maiti iliyofunikwa kwa shuka la kijani. Wakaufuata mwili huo na kulitoa shuka.
Hawakuamini walichokiona mbele yao, shuka ile ilipofunuliwa na kuuangalia mwili huo, ilikuwa maiti ya binti yao, Catherine. Wakashindwa kuvumilia, hapohapo wakaanza kulia na hivyo wazazi wa James kuanza kuwabembeleza.
“Na kijana wetu yupo wapi?”
“Hatujui mpaka sasa! Huu mwili uliletwa na maji, kwa hiyo mwingine hatujui,” alijibu mwanajeshi mmoja.
Walipoambiwa kwamba binti huyo alikuwa mjauzito hata kabla ya tsunami kupiga, ndipo walipoanza kumchunguza na kugundua kweli alionekana kuzaa muda wa saa chache zilizopita kutokana na sehemu zake za siri zilivyokuwa.
“Inaonyesha kwamba alijifungua...” alisema daktari huyo.
“Mtoto wake yupo wapi?”
“Hatujui yupo wapi! Tulimpata mwanamke tu, mtoto hatufahamu chochote kile kama yupo hai au alikufa...” alijibu daktari huyo maneno yaliyowafanya watu hao kuanza kulia mahali hapo.

Je, nini kitaendelea?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom