Utafsiri wa Sheria na hatma ya Haki nchini Tanzania

Jul 8, 2015
31
39
MAKOSA YA JINAI YASIYO NA DHAMANA YANADHAMINIKA
(Non Bailable Offences are Bailable)
Obadia Kajungu, Esq.
ADVOCATE.

Dibaji (Forewords)

Sisi wanasheria ndiyo kikwazo cha haki nchini Tanzania na hii ni kwa sababu tumeacha kuzitendea haki sheria kwa kushindwa kuzitafsiri sambamba na matakwa ya falsafa na nadharia za kisheria(jurisprudence and legal theories). Matokeo ya kushindwa kwetu katika kazi yetu kumeleta maafa makubwa katika nchi yetu, kijamii, kisiasa na kiutamduni. Hii inaweza kupelekea maadui wa nchi kutumia upenyo huu kuyumbisha taifa. Ukweli ni kwamba mfumo wetu wa haki umekosa kitu ninachoweza kukiita mlinganyo wa kitaasisi (institutional equilibrium) katika mihimili ya kiserikali na hivyo serikali kuonekana haina ushirikiano na wananchi. Kukwama kwa mfumo wa sheria ikiwemo kukosa “public policy oriented approach to interpretation” kumesababisha madhara makubwa.

Watanzania wasio na hatia wanateseka gerezani kuliko jehanamu kwa sababu kesi zao hazisikilizwi. Ndoa zinavunjika na kupelekea watoto wa mitaani au watoto wa mzazi mmoja, kitu kinachopelekea serikali kuchangia kwa watoto wanaoweza kuwa na tabia za ushoga, kuwa wavuta bangi, wezi, makahaba, kwa sababu familia zao ziliparaganyika kufuatia wazazi wao kuwa gerezani bila kuhukumiwa huku serikali ikiendelea kuzishikilia kesi zao ikijua haina uwezo uwezo wa kuziendesha kwa upande mmoja na kwa upande mwingine mahakama ikishiindwa kufanya maamuzi pale haki inapoihitaji kufanya hiyo. Zote hizi ni hasara za kisosholojia (social costs) kwa watu na serikali. Lakini pia matokeo yake ni nchi kukosa kipato na ukosefu wa mzunguko wa pesa kwa sababu wale ambao wako jela bila hatia ndio wangekuwa wananunua, kuuza na kulipa kodi serikalini. Makampuni, mabenki na taasisi nyingine za kibiashara kufirisika na kusababisha ukosefu wa ajira, kodi za serikali, jamii kuyumba kwa sababu wamiliki ambao ndiyo taa za biashara hizo wamekaa jela kwa muda mrefu na haijulikani endapo wana hatia au la.

Kukoswa msimamo katika masuala ya haki na utafsiri wa sheria wenye mlengo wa sera za nchi (public policy oriented interpretation) ni sehemu ya sababu zinazokwamisha sera ya Tanzania ya viwanda kwa upande mmoja wakati jamii yetu ikiparaganyika kwa upande mwngine.

Kwa kweli kwa hali ya haki ilivyo nchini mwetu, sisi wanasheria ambao tulisomea na kuapa kutetea haki tulitakiwa tuwe tumekufa kwanza ili mambo yanayoendelea yasitokee mbele ya macho yetu, kwa maana Mwenyezi Mungu anatuona kwa mambo tunayowafanyia watu wake.

“Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.” Mt 16:25
Nadhani kila mwanasheria anatakiwa kuongozwa na mstari huu katika Injili ya Mathayo Mtakatifu, ili awe sadaka kwa ajili ya haki za watu wa Mungu.

Utangulizi
Sheria ni kama gari. Unaweza kuwa na gari jipya lakini usipojua kuliendesha, yaani kama wewe siyo dereva, basi utashindwa kumpeleka hospitali mgonjwa wako hadi mauti yamfikie kwa sababu huwezi kuendesha gari lako jipya ulilolinunua kwa pesa yako. Kwa hiyo shida siyo gari bali shida ni dereva. Sheria ni zana (tools) ambazo inabidi uzilinganishe kama mashine nyingine ambazo hutumiwa kufanya kazi au kutatua tatizo lakini zana hizo lazima ujue namna ya kuzitumia.

Sheria ndiyo mwanga wa serikali yoyote duniani na taifa lolote. Taifa likiyumba katika eneo la sheria lazima taifa lenyewe, serikali yake na jamii inayoishi ndani ya taifa hilo vitayumba na kuleta kitu kinaitwa “state instability” iwe kijamii (social unrest), kisiasa au kiuchumi au taifa kuanguka kabisa(state extinction).

Kazi ya sheria ni ngumu sana, na ni moja ya fani zinazohitaji kuwaza sana katika kutekeleza makusudio ya kisheria (object of the law). Walatini wana msemo wa kisheria (Latin legal maxim) kwamba “cessante ratione legis, cessat lex ipsa” [when the reason for a law ceases, the law itself ceases] ambayo ni kanuni ya kisheria inayosema kwamba tukiacha kuwazia sababu ya kutungwa kwa sheria hupelekea sheria yenyewe kufa. Hii inamaanisha kwamba, ili kufikia maamuzi katika kutafsiri sheria, ni lazima waamuzi na wanasheria wajiulize sababu ya kutungwa kwa sheria hiyo.

Waamuzi (majaji na mahakimu) na Mawakili huwa hawasomi sheria na kuzitafsiri kama zinavyosomeka katika karatasi bali huwa wanatumia mitindo ya utoaji maamuzi ya kimahakama (styles of judicial decisions making processes) kama vile grand style au unorthodox au unconventional au realism dhidi ya formal style au orthodox au formalism au literalism au conventional n.k.

Realism ni ile mbinu ya utafsiri wa sheria ambapo waamuzi huwa hawalengi sana maneno ya sheria kama yalivyoandikwa katika vitabu vya sheria za Bunge(Acts of Parliament) bali huangalia hasa athari ya maamuzi yatakavyoathiri jamii(social effect of law) wakati Formalism ni pale waamuzi wanaposoma na kuamua sheria kama ilivyoandikwa bila kutumia ubunifu(legal creativity) hata kama itakuwa na matokeo yasiyoleta mantiki kwenye jamii au hata kama italeta maafa.

Ili kufikia malengo hayo ya grand style na formal style katika maamuzi ya kimahakama, mahakama hutumia pia kanuni za ufafanuzi (cannons of statutory interpretation). Baadhi ya kanuni hizo ni “litera legis ita est scriptum” au (literalism) ikimaanisha kutafsiri kama ilivyoandikwa, “golden rule”, ambayo inataka mwamuzi asiende nje ya maana tasa ya neno la sheria ali mradi yasipotoshe mantiki(avoid absurdity), “mischief rule(rule in Heydon’s case)” ambayo inataka mahakama itafute kusudio la Bunge, na “purposive approach” au “purposivism” ambayo inataka mwamuzi avae viatu vya mbunge na kuamua kana kwamba angekuwa mbunge angemaanisha sheria ilete matokeo gani kwenye jamii.

Haiishii hapo katika hizo kanuni za utafsiri bado pia kuna mambo tunayaita misaada ya utafsiri (aids to interpretation). Misaada hii ya utafsiri yaweza kuwa ni zile zinazopatikana ndani ya kitabu cha sheria (intrinsic aids) kama vile “marginal notes”, “definitions”, long title, short title, n. k. Lakini pili pia, kuna misaada ya nje ya kitabu cha sheria (extrinsic aids to interpretation) kama vile travaux preparatoires, text books, hansadi za bunge, mijadala ya mabaraza ya mawaziri, taarifa za tume, machapisho, kamusi, taarifa za mawaziri, n.k.

Zaidi ya hapo, vile vile kuna mambo tunayaita misaada ya kimantiki (logical aids to interpretation) kama vile noscitur a sociis (kwa mujibu wa inayohusiana), ejusdem generis(kwa kadri ya inavyofanana na nyingine kinasaba), expressio unius est exclussio ulterius (ukitaja kitu kimoja chenye jamii ile ile una maanisha vyote vya jamii ile ile na kuacha kingine chenye jamii tofauti), dhahania(presumptions), n.k. Hayo yote ni sehemu ya jitihada za waamuzi (mahakama) kutafuta kusudio la sheria iliyotungwa na bunge(intension of Parliament), kazi ambayo kidogo inahitaji kuwaza sana lakini pia kufanya tafiti za vitabu mbalimbali nje ya kitabu cha sheria husika kwa nia ya kutenda haki. Usipozungukia milolongo yote hiyo basi hata kama ni mwanasheria utaendelea kuziona sheria kama anavyoziona mhasibu au mhandisi, kumbe sivyo zilivyo.

Kwa maana hiyo, mahakamani sheria hazitumii mantiki (logic) kwa sana, hivyo matokeo ya maamuzi ya sheria yanaweza kuwa ni tofauti na yale ambayo watu wengi waliyategemea.

Kwa ujumla wake waamuzi na wanasheria wanapotumia hizi mitindo ya kimaamuzi ya kimahakama (styles of judicial decision making processes) na kanuni za utafsiri (cannons of statutory interpretation) vikiwemo zikiwemo dhahania za kisheria (presumptions), n.k. katika kiingereza cha kisheria tunaviita “legal reasoning”.

Makosa Yasiyo na Dahamana Yanadhaminika.
Tukiachana na utangulizi huo hapo juu ninapenda kuwaambia kwa nini nasema kwamba kesi za jinai zisizokuwa na dhamana hasa utakatishaji pesa ambao umekuwa tishio la jamii na kupelekea janga la haki (justice crisis) katika nchi yetu ya Tanzania zinadhaminika.
Sheria za jinai ni za serikali na pia hazikusudii mtu apotee mbele ya mahakama, isipokuwa mahakama ina mamlaka yasiyoingiliwa kuweka mkataba kati yake na mshtakiwa ili aihakikishie kwamba atapatikana kipindi chote cha mashtaka na mahakama ina utashi wa kumpa au kumnyima dhamana mshtakiwa huyo hata kama kosa aliloshtakiwa nalo lina dhamana kisheria.

Kwa hiyo dhamana ni haki yenye masharti (conditional right) na tunaweza kusema kwamba dhamana ni amri ya mpito (interlocutory order) inayomruhusu mtu awe nje ya rumande huku akisubiria kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi ya msingi. Interlocutory orders siku zote ni “equitable remedies” yaani haki ambayo mahakama inaweza kumpa mshtakiwa au mlalamikaji/madaiwa au mdai kwa kufuata utashi wake usiongiliwa wa kutoa haki ili kuondoa usumbufu au kupunguza makali ya sheria yanayoweza kukwamisha utendaji haki.

Mamlaka ya mahakama kutoa equitable remedies yanatokana na mamlaka ya asili ya mahakama yaitwayo “inherent powers of courts” ambayo maana yake ni mamlaka zaidi ya yale yaliyotolewa na katiba. Ndiyo maana tunaona mahakama zina mamlaka ya kuhoji hata uhalali wa vifungu vya katiba yenyewe wakati katiba hiyo ndiyo inaanzisha mahakama husika na kuzipa mamlaka. Kwa hiyo inherent powers za mahakama huwa haziwezi kunyang’anywa na sheria za bunge. Yaani hakuna sheria ya bunge inayoweza kuinyang’anya mahama mamlaka ya kutenda haki.

Katika kesi ya Anisminic Ltd versus Foreign Compensation Commission [1969] 2 AC 147 sheria iliipatia Tume ya Ufidiaji mamlaka yote katika kutoa maamuzi ya kufidia makampuni ambayo mali zake zilikamatwa (sequestrated). Sheria hiyo ikaongeza kwa msisitizo kuwa “...hakuna mahakama yoyote ile itakayokuwa na mamlaka ya kuingilia wala kuhoji kwa namna yoyote ile maamuzi ya Tume….”

Hata hivyo, katika shauri hilo hapo juu, na kwa kuyatambua mamlaka yake ya asili (inherent powers) kuhusu utendaji haki, Mahakama iliamua kukwepa kifungu hicho na kuendelea kuhoji maamuzi ya Tume, bila kujali mazuio ya sheria (auster clause), kwa vigezo mbali mbali, vikiwemo kwamba tume inaweza kuwa imetoa maamuzi kwa nia ovu (acting in bad faith), au inaweza kuwa imetafsiri vibaya sheria (improper interpretation of the law), inaweza kuwa imetumia vibaya madaraka yake (acting ultra vires), inaweza kuwa imezingatia mambo yasiyohusika (considering irrelevant considerations), n.k. na hivyo ilisema kwamba kitendo cha kutoingilia maamuzi ya Tume, mahakama itakuwa imekwepa majukumu yake ya kutoa haki (derogation of its duties to dispense justice).

Kwa hiyo kama wanasheria wanafafanua maana ya dhamana katika makosa ya jinai kuwa ni mkataba kati ya mahakama na mshtakiwa ambapo mshtakiwa anatakiwa kupatikana kwa tarehe, muda na sehemu ambayo mahakama itapanga yakiwemo yakiwemo masharti mengine kama vile kutoingilia upelelezi, kutotenda kosa lingine linalofanana na lile analoshtakiwa nalo pamoja na msharti mengine ambayo mahakama itamwekea, basi hakuna sheria yoyote ya bunge ambayo inaweza kuiondolea mamlaka yake yaliyoko juu ya katiba wa kuingia mikataba (freedom to contract) kwa kuirahisishia kufikia utendaji haki. Dhamana siyo hukumu ni maamuzi ya mpito kama ilivyo kwenye mashauri ya madai ni “Temporary Injunction” ambazo pia zinatolewa kwa mujibu wa hisani chini ya inherent powers. Kamusi maarufu sana ya Sheria, Black's Law Dictionary; 782 (6th Edition 1990) inafafanua “inherent powers of courts” to mean:-
“powers over and beyond those explicitly granted in the Constitution or reasonably to be implied from express grants”

Kwa hiyo mahakama, katika kutoa au kukataa kutoa haki ya dhamana kwenye makosa ya jinai ni hisani (discretion) kutoa haki hiyo na ndiyo maana hata katika makosa yanayoruhusiwa kutolewa dhamana, kutokana na mazingira mahakama inaweza kulazimika kukataa kutoa dhamana. Vivyo hivyo, hata katika makosa yasiyo na dhamana kwa nini, kutokana na mazingira, mahakama isilazimike kutoa dhamana?

Ukitaka kujua kwamba kusudio la Bunge lilikusudia nini hadi kuyafanya makosa ya uhujumu uchumi yasiwe na dhamana au yawe na masharti magumu lazima utumie kanuni ya utafsiri inaitwa “mischief rule” na lazima ufuatilie historia ya matukio hadi kufikia kutungwa kwa hicho kifungu cha sheria kwa kuangalia kwanza sheria iliyokuwepo kabla ya kutungwa kwa sheria mpya, tatizo lililokuwepo wakati huo na ni nini suluhu ambayo sheria mpya ilikusudia.

Kimsingi ukiangalia makosa yasiyo na dhamana yameongezwa hivi karibuni ikiwemo utakatishaji pesa.

Ukiangalia historia basi ya makosa mengi ambayo sheria za jinai zimeyaweka kwenye kariba ya washtakiwa kutopewa dhamana si kwa sababu nyingine bali ni kwa sababu uzoefu umeonesha kuwa washtakiwa hasa wahujumu uchumi wamekuwa wakiitoroka mahakama au kuingilia upelelezi au kuingilia mashtaka na hivyo serikali kukoswa haki zake mbele ya mahakama zenyewe.

Kwenye sayansi ya Sosiolojia kuna kitu wanaita “institutional functionalism” ambayo inahusu mifumo ya kitaasisi kama ilivyo mihimili ya kiserikali. Nadharia hii inataka taasisi au mihimili ifanye kazi kwa kutegemena na kusisitiza kwamba lazima mihimili ya kitaasisi ifanye kazi japo kwa mbinu na mazingira tofauti lakini malengo yake ni kutimiza lengo moja(same objective). Kutokuwepo kwa milinganyo ya kitaasisi au kimihimili (instititutional equilibrium) hupelekea kutokea kwa kero za kijamii (social chaos). Katika utekelezaji wa majukumu ya kila mhimili ni lazima mihimili yote ishirikiane (institutional complimentality) ili kufikia lengo la Taifa vinginevyo kutatokea shida, kama vile kukwama kwa uhuru wa mahakama, kukwama kwa sera za nchi, na mengine mengi.

Serikali ni kama familia na kama wazazi hawaelewani lazima watoto watapata shida. Unakuta kwa mfano mama aki_misbehave libaba litajikuta linakuwa likatili hata kwa watoto kwa sababu “equilibrium” inakuwa “disturbed” (wataalam wa physics watanisaidia hapa kwamba “what will happen when the equilibrium is disturbed”?

Uhitaji wa ushirikiano wa kimihimili (institutional complimentality) ili kuleta mlinganyo wa kitaasisi (institutional equilibrium) katika mihimili yetu ya kiserikali unapatikana pia katika Ibara ya 9 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaznia inayosema kwamba:-

9. Lengo la Katiba hii ni kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au wa chochote kati ya vyombo vyake na udugu na amani kutokana na kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambayo inasisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa kwa kuzingatia mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha malengo ya Taifa(maneno yangu):-
(a) kwamba utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa; (b) kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa; (c) kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine; (d) kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa ulinganifu na kwa pamoja; (e) kwamba kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi, na kazi maana yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia mtu riziki yake; (f) kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu; (g) kwamba Serikali na vyombo vyake vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wake kwa waume, bila ya kujali rangi, kabila, dini au hali ya mtu; (h) kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini; (i) kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umaskini, ujinga na maradhi; (j) kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi; (k) kwamba nchi inatawaliwa kwa kufuata misingi ya demokrasia Ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea.

Katika tafiti zangu nimegundua chanzao cha ugonvi kati ya Mahakama na Utendaji ni ibara hii, pamoja na mambo mengine. Mahakama inashindwa kwenda sambamba na sera za nchi(public policy). Serikali inapoweka sera ya viwanda na uchumi wa kati lazima mahakama itafsiri sheria kuzielekeza kwenda kwenye viwanda na uchumi wa kati, serikali ikipanga kulinda uchumi wa nchi lazima mahakama itafsiri sheria kulinda uchumi wa nchi, seriakali ikibadilika na kuwa ya kijamaa, lazima sheria zitafsiriwe katika mitazamo ya kijamaa, n.k.
Mgawanyo wa madaraka wa Prof. Montesquieu (1689-1755) haukumaanisha kwamba kila mhimili ufanye mambo yake vululu vululu la hasha bali mihimili ishirikiane kufanya kazi japo kwa utengano lakini kwa nia ya kutimiza lengo moja la taifa. Mtafiti mmoja wa sheria huko nchini Pakistan (Mahmud, K; “Constitutional Paradigm of Societal Reconstruction and Rule of Law in Pakistan”;) aliwahi kusema
...in Pakistan. For this purpose, institutional justice under the core parameters of Rawlsian equality and equity is preferred to achieve egalitarianism. In this jurisprudential context, collaboration between legislature, executive and judiciary is required to accomplish the preamble and Objectives Resolution...

Ukosefu wa ushiriano katika mahakama dhidi ya mihimili mingine inajidhirisha kwenye maamuzi yake malimbali ambapo kesi za serikali hasa uhujumu uchumi watuhumiwa wamekuwa wakitoroka baada ya mahakama kuwapatia dhamana kwa masharti ambayo hayailindi serikali katika kuhakikisha mshtakiwa anapatikana hadi mwisho wa haki au hata akitoroka, au kuingilia mwenedo wa kesi ikiwemo kuingilia upelelezi na mwisho serikali ikawa inashindwa asilimia kubwa ya kesi zake.

Kufuatia uzoefu huu ndiyo umepelekea serikali kutunga sheria ngumu na za kikatili juu ya haki ya dhamana. Na matokeo yake mahakama imejikuta haiko huru. Waswahili wana msemo kwamba “ukitaka kufukuza inzi, kwanza ondoa mzoga”. Haiwezekani uhuru wa mahakama ukapatikana dhidi ya dola endapo mahakama yenyewe haijajitangazia uhuru dhidi ya mazingira ya kutoaminika katika maeneo mengine na hivyo kuendelea kuivutia serikali kuchungulia.

Kwa hiyo ieleweke kwamba serikali hadi inafikia hatua ya kutunga sheria ngumu na za kikatili juu ya dhamana si kwa sababu ya kuwakomoa wananchi wake bali ilikusudia kuibana mahakama ili wateja wake(waharifu) wasiikimbie na kuchakachua haki za serikali.
Wahaya wana methali inayosema kwamba “orw’otega muka sho rwija na nyoko” yaani kifo umtegacho mama yako wa kambo kitamnasa mama yako mzazi. Kwa hiyo misumari ya sheria za dhamana ambazo bunge lilizitunga zikilenga kuibana mahakama matokeo yake zimeugeukia na kuuumiza umma wa watu kipenzi wa serikali badala ya kuibana mahakama. Hii wataalama wa jusisprudensia wanasema ni “adverse social effect of the law.”

Ndoa zinavunjika, serikali inatengeneza watoto wa mitaani au watoto wa mzazi mmoja huku ikijua changamoto za ukuaji wa watoto katika dunia ya leo ikiwemo ubakwaji unaoweza kuwaletea ushoga, nchi imepoteza mzunguko wa pesa kwa sababu wafanyabiashara wameishia jela, huku mahaka haijui cha kufanya kujenga taifa kwa kusaidia watuhumiwa ambao kesi zao hazionekani kuwa na ushahidi huku serikali inaonekana kushindwa kuziendesha, n.k.. Ukifanya SWOT analysis ya mahakama kushindwa kutafsiri sheria hizi unakuta serikali inapata hasara kuliko makosa yenyewe, zikiwemo kutunza mahabusu ambao inajua haitawatia hatiani.

Baada ya kuona umuhimu wa mahakama kuhitaji kuzingatia historia ya sheria katika kuitafsiri na kupata kusudio lake niwapeleke sasa kwenye ni nini mahakama inatakiwa kufanya kuhusu makosa yasiyo na dhamana.

Kimsingi kukamilika kwa upelelezi tangu sheria za Kirumi si kazi ya mahakama na serikali haitakiwai kuwa na muda wa ukomo wa kushtaki chini ya msemo wa kisheria wa Kilatini unaoesema kwamba “nullum tempus occurrit regi” wakati mwingine kwa kifupi wanasheria wanasema ni “nullum tempus” ambayo ni kanuni ya kisheria inayoiondoa (exempts) serikali au taifa katika ukomo wa muda wa kushitaki. Kwa kiingereza wanasena, “no time runs against the King.” Hata Hivyo, kanuni hii haiipi serikali haki ya kufungia watu gerezani kwa muda usio na kikomo watu ambao hawajatiwa hatiani kwa mgongo wa mahakama.

Sasa ukiangalia kifungu cha 225 cha Sheria ya Mienendo ya Mashtaka ya Jinai Sura ya 20 utakuta, mashauri yote ambayo yako mahakamani zaidi ya siku 60 ni kwa utashi wa mahakama au mahakama kushindwa kufanya maamuzi. Kifungu kinasomeka hivi:-
225.—(1) Subject to subsections (3) and (6), before or during the hearing of any case, it shall be lawful for the court in its discretion to adjourn the hearing to a certain time and place to be then appointed and stated in the presence and hearing of the party or parties or their respective advocates then present, and in the meantime the court may suffer the accused person to go at large, or may commit him to prison, or may release him upon his entering into a recognizance with or without sureties at the discretion of the court, conditioned for his appearance at the time e and place to which such hearing or further hearing shall be adjourned.

(4) Except for cases involving offences under sections 39, 40, 41, 43, 45, 48(a) and 59, of the Penal Code or offences involving fraud, conspiracy to defraud or forgery, it shall not be lawful for a court to adjourn a case in respect of offences specified in the First Schedule to this Act under the provisions of subsection (1) of this section for an aggregate exceeding sixty days except under the following circumstances— (a) wherever a certificate by a Regional Crimes Officer is filed in court stating the need and grounds for adjourning the case, the court may adjourn the case for a further period not exceeding an aggregate of sixty days in respect of offences stated in the First Schedule to this Act; (b) wherever a certificate is filed in court by the State Attorney stating the need and grounds for seeking a further adjournment beyond adjournment made under paragraph (a), the court shall adjourn the case for a further period not exceeding, in the aggregate, sixty days; (c) wherever a certificate is filed in court by the Director of Public Prosecutions or a person authorized by him in that behalf stating the need for and grounds for a further adjournment beyond the adjournment made under paragraph (b), the court shall not adjourn such case for a period exceeding an aggregate of twenty four months since the date of the first adjournment given under paragraph (a).

(5) Where no certificate is filed under the provisions of subsection (4), the court shall proceed to hear the case or, where the prosecution is unable to proceed with the hearing discharge the accused in the court save that any discharge under this section shall not operate as a bar to a subsequent charge being brought against the accused for the same offence.

(6) Nothing in this section shall be construed as providing for the application of this section to any proceedings in a subordinate court in relation to any offence triable only by the High Court under the Economic and Organized Crime Control Act.
Ukiangalia kifungu kidogo cha 5 yaani 225(5) utakuta siku sitini zikipita na upelelezi ukawa haujakamailika na upande wa mashtaka ukawa umeomba maahilisho hadi DPP akawa pia ameomba kuahilisha hadi kupewa miezi ishirini na nne(miaka 2) basi mahakama inakoswa mamlaka kukaa tena na mshtakiwa zaidi ya miaka miwili hata kama ni mauaji.

Swali; Je, mbona sasa tunawaona watu wameendelea kuteseka gerezani kama mahabusu zaidi ya miaka miwili bila kuhukumiwa?
Jibu ni kwamba tatizo si sheria, bali tatizo liko kwenye utafsiri hasa baada ya kwamba mahakama zetu zimeendelea kutafsiri sheria kwa mtindo ambao hauhitaji usumbufu na niseme mfumo huu wa utafsiri uliorithiwa kutoka kwenye Sheria za Waingereza ambao pia waliurithithi kutoka katika sheria za Kirumi, unaoitwa literalism umeshapitwa na wakati. Nasema literalism hauhitaji usumbufu kwa sababu huhitaji kutumia mantiki kujua maana ya kifungu husika, hauhitaji kufanya tafiti nje ya kitabu kujua kusudio la bunge, hauhitaji kujali endapo sheria hiyo itakuwa na madhara gani kwenye jamii, n.k. Yaani literalism kwa kifupi hauhitaji kutumia “legal methods skills” kiasi kwamba si lazima uwe umesomea sheria kufanya kazi ya uamuzi wa kimahakama au uwakili, bali ni kwenda na kusoma makaratasi tu. Literalism imebaki makanisani ambao kabla msoma neno hajaanza kusoma anajionya kwamba “nitasoma kama ilivyoandikwa”; yaani haongezi neno wala hapunguzi neno.

Nchini India makosa yasiyodhaminika yapo na pia sheria zao nyingi ni kama za Tanzania, lakini mazingira ya kesi hasa kuendelea kuahilishwa kwa muda unaozidi siku sitini kunazipa mahakama za India kama zilivyo pia mahakama zetu utashi wa aidha kuondoa kesi au kama mahakama itaona Serikali itapoteza haki itampa dhamana mshtakiwa badala ya kufuta shauri mahakamani.
Hii iliamuliwa na mahakama ya juu ya nchini India katika kesi ya Anil Sharma v. State of Himachal Pradesh, (1997) 3 Crimes 135 (HP) ambapo Mahakama ilikuwa na haya ya kusema,“in non-bailable cases in which the person is not guilty of an offence punishable with death or imprisonment for life, the Court will exercise its discretion in favour of granting bail subject to sub-section (3) of section 437 of the Indian Code of Criminal Procedure, if it deems necessary to act under it; or the court may grant bail if the investigation exceeds sixty days without completion”.

Swali: Je, sheria ikisema kwamba kosa hili halitakuwa na dhamana ni kinyume na Katiba?

Jibu ni kwamba sheria yoyote inapotungwa hata kama itasomeka kama ilivyo kwenye karatasi lakini ikaonekana kupingana na katiba haitakuwa kinyume na katiba kwa sababu ilitungwa kwa nia ya kutimiza malengo ya katiba yenyewe. Kwa mfano kama malengo ya katiba yetu ni kujenga Tanzania yenye uchumi imara na uzoefu unapoonekana kwamba wanaohujumu uchumi wake wanatoroka na kukimbia adhabu wakiwa mikononi mwa mahakama, hivyo kukwamisha malengo ya kikatiba ya kiuchumi basi itakuwa ni halali bunge linapotunga sheria kuweka ugumu katika kupata dhamana, chini ya nadharia ya Jeremy Bentham (1748-1832) ya “utilitalianism” kwamba hakuna namna bali wateseke wachache watakaoingia kwenye mitego ya makosa yasiyo na dhamana kwa nia ya kuwanufaisha walio wengi kwa kulinda uchumi wa nchi yao ambapo katiba hiyo hiyo inayowapa watu haki ya kudhahaniwa chini ya dhahania ya utovu wa hatia(presumption of innocence). Ndiyo maana nimesema mahakama lazima ifanye mlinganisho (balance of equilibrium) na hivyo vifungu ambavyo vipo “restrictive” mahakama inatakiwa kuvitafsiri kwa kujionya.

Swali: Kama ni halali kutunga sheria za kubana dhamana katika jinai je, mahakama inatakiwa kufanya nini ili kulinda haki za washtakiwa endapo upande wa mashtaka utaitumia mahakama vibaya kwa kutokamilisha upelelezi?

Kama ilivyoamuliwa katika kesi ya Anisminc hapo juu, kwa kifupi, sheria inasema kwamba mahakama italazimika kutumia mamlaka yake ya asili pale sheria inapokuwa na mapungufu(lacuna), au ina maana tata(ambiguous), au kama kuna uwezekano wa upande mmoja katika kesi unaonekana kuisumbua mahakama(abuse of process) au matumizi mabaya ya nafasi ya mmoja wa wadaawa. Ukifika wakati wa mahakama kutumia mamlaka yake ya asili huwa inaweka pembeni vifungu vya sheria na kuangalia haki za watu na kuamua inavyoona inafaa kwa ajili ya haki.

Ronald Dworkin(1931-1913), mwanafalsafa wa kisasa(modern philosopher) Mmarekani anasema sheria lazima zitafsiriwe katika mitazamo ya kiuchumi(economic interpretation of laws) ili ziende sambamba na sera za kiuchumi za serikali ya wakati huo kwa upande mmoja, huku haki za wadaawa(Mshtakiwa na Mlalamikaji) na athari kwa umma vikizingatiwa kwa upande mwingine. Kwa mfano baada ya mahakama kujiridhisha kwamba, katika kuzuia dhamana, kusudio la bunge halikuwa kuwakomoa watu bali kuzibana mahakama ili washtakiwa wasizitoroke, au wasiingilie upelelezi, au wasiingilie mahakama, na kuifanya serikali kukoswa haki zake basi, cha kufanya ni kuangalia adhabu ya mshtakiwa endapo angetiwa hatiani. Kama kosa ni kukwepa kodi labda tuseme milioni kumi (10,000,000.00) na endapo mshtakiwa akitiwa hatiani atatakiwa kulipa faini milioni ishirini (20,000,000.00), basi hapa mahakama haitakiwi kuangalia Mlalamikaji na Mshtakiwa bali pia lazima iangaze pia nje ya mahakama kwenye serikali itapata nini kwa maamuzi yoyote yatakayotolewa!

Hapa mahakama inabidi iwaze mshtakiwa akipewa dhamana halafu akatoroka serikali itakosa pesa zake inazomdai. Kwa maana hiyo haitakuwa kinyume cha sheria mahakama kumwambia mshtakiwa aweke kwenye akaunti ya Mahakama pesa taslim Tshs. 20,000,000.00 au bondi yenye uhakika wa kuuzika na kupata Tshs. 20,000,000.00 pesa za serikali endapo mshtakiwa atavunja masharti ya dhamana. Pia mahakama itatakiwa kuwaza kuwa, huyu mshtakiwa akiwa nje kwa dhamana lazima atakuwa analipa kodi kwa sababu kushtakiwa kwa kosa lingine linalofanana na kosa unaloshtakiwa nalo ni sababu ya kufutiwa dhamana, na kwa hiyo wakati kesi inaendelea, serikali inakuwa inakusanya kodi isiyobishaniwa kutoka kwa mshtakiwa huyo pindi anapokuwa nje kwa dhamana. Lakini pia, kama mshtakiwa ataweka pesa taslim ya 20,000,000.00 kwenye akaunti ya mahakama ikiwa ni “security” ya dhamana, serikali itakuwa imepata mkopo usio na riba kwa muda wote ambao mahakama itakaa na pesa hizo mpaka kesi itakapoisha. Kama kesi itadumu labda miaka miwili na mshtakiwa nalipa Tshs. laki moja (100,000.00) kila siku utakuta serikali imevuna Tshs. milioni tisini (90,000,000.00) ambazo ingezikosa kama mshtakiwa angekaa mahabusu kwa kipindi chote hicho. Kwa upande mwingine wa shilingi watototo na wategemezi wa mshtakiwa ambao hawana hatia watakuwa wamelindwa na mahakama kuhusu haki zao za kutunzwa na kuishi. Hivi ndivyo mahakama katika nchi zenye uchumi wa viwanda zinavyotafsiri sheria.

Pia, utafsiri wa sheria kwenye dunia ya leo uko kwenye falsafa ya kizazi kipya zinazojulikana kama “postmodern generation of jurisprudence” au “postmodern interpretation of law” au “postmodernism.”

Nadharia hii ya utafsiri wa sheria inataka mahakama zitafsiri sheria kwa kuzingatia sheria yenyewe, kuzingatia haki za wahusika, na kuzingatia athari inayoweza kutokea kwenye jamii kutokana na matokeo ya utafsiri wa sheria hiyo, kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa huku ikizingatia uhalisia wa ndani ya jamii hiyo kama vile rangi (race), matabaka(classes), jinsia(sex), makabila(ethinicity), wategemezi (dependants), n.k ambao wanaweza kuathirika. Ninaweza kuifafanua kwa kiigereza kama hivi “legal postmodernism is the contempoaray approach to the interpretation of law where the courts are bound to consider a broad spectrum of social interests and diversity in the complicated society including but not limited to race, ethnicity, class, gender and other social multiplicity of standards”.

Kwa mfano siku hizi familia tegemezi zinazidi kupungua katika jamii zetu ambapo unaposhtaki mtu na kumnyima dhamana kwa kipindi kisichojulikana huku akiwa na watoto wachanga na wategemezi unatakiwa kujua kwamba hakuna ndugu au jamaa wa kuwatunza na kuwasomesha shule watoto na wategemezi hao hao kama ilivyokuwa zamani ambapo mtoto angeweza kuishi na kutunzwa na mjomba wake. Kitendo hiki pia kinakinzana na sheria za kimataifa juu ya haki za mtoto kwenye kanuni ya “the best interest of the child shall be the first to be considered”. Kwa sababu unawaweka watoto wa mshtakiwa katika hatari ya kufa kwa njaa, au kubakwa, au kukosa huduma ya shule, au kukosa malezi bora ya mzazi, au kukoswa matibabu, au hata kufa kwa sababu mbali mbali za “exposures” pale mzazi wao anapokuwa jela kwa kukoswa dhamana, mbaya zaidi pale anapokuwa hana kesi ya kujibu.

Athari zake haziishii hapo bali zinakwenda mbali na kukuta watoto hao hao wanakuja kuwa na tabia za ukubwani ambazo zitaigharimu mara dufu serikali hiyo hiyo kama vile kuwa wezi au mashoga au wavuta bangi, n.k. kutokana na magumu waliyoyapata wakiwa wadogo kwa sababu tu mahakama ilimnyima dhamana mzazi wao na huenda mzazi huyo wala hakuwa na hatia. Lakini hapa kwetu ni peleka twende hadi unakuta mahakama zinawaweka gerezani bila dhamana wanawake wajawazito.

Katika kesi nyingine iliyoamuliwa nchini India kati ya Ilaben Dipakkumar Dhanraj Shah vs State Of Gujarat (1993) 2 GLR 1148 ambapo kosa la mauaji ambalo halina dhamana kama ilivyo hapa Tanzania, lakini Mahakama kwa kuzingatia “diversity” au “postmodernism” katika kutafsiri sheria na kutoa haki, ilimpatia dhamana mwanamke aliyeua mume wake. Mahakama kabla ya kumpa dhamana ilizingatia mazingira ya mwanamke huyo, yaani alikuwa na watoto watatu ambao mkubwa alikuwa na miaka 13 na mdogo akiwa na miaka 6 huku wakiwa hawana ndugu mwenye uwezo wa kutunza watoto hao tofauti na mama huyo aliyekabiliwa na mashtaka ya mauaji yasiyokuwa na dhamana.

Mwisho kabisa huko huko nchini India, katika kesi ya Anil Kumar Sharma vs Enforcement Directorate, of Allahabad (9 December, 2020) mahakama ilimpatia dhamana mshtakiwa ambaye anashtakiwa kwa ufujaji udanganyifu, n.k. wa pesa nyingi yaani Rs. 6000/= kiasi ambacho hakiruhusu dhamana kwa sababu mshtakiwa alikuwa ni mkurugenzi na mmiliki wa Kampuni kubwa ya Real Estate na ikasema kwamba mshtakiwa kuendelea kukaa gerezani kampuni itafirisika na kusababisha upotevu wa ajira mitaani.

Hitimisho (Conclusion)
Wakati umefika sasa tujue watanzania kwamba kizazi hiki ni kizazi chenye jamii ambayo ni tata au niiite “complicated society”. Lakini pia ni kizazi kinachohoji uhalali wa mambo yanayofanywa na mihimili ya kiserikali kwenye nchi zao kwa sababu kila mtu au walio wengi wamepevuka nikimaanisha angalau kila mtu anajua kusoma na kuandika na anao uelewa walau wa hata kuhoji wasomi wanaweza au wanatakiwa kufanya nini. Kwa mfano, mtu aliyemaliza Form IV na aliwahi kusoma utangulizi katiaka Elimu ya Baiyologia, akiambiwa na Daktari kwamba kwamba UKIMWI unaambukizwa kwa njia ya hewa, asipokataa basi ataguna pamoja na kwamba yeye siyo Daktari hata kama jamii inamchukulia kwamba hajasoma. Mantiki yangu ni kwamba huu ni wakati ambao sasa kila wasomi wa fani zote wazitendee haki fani zao kwa kuzipenda, kuzielewa pasipo shaka na kuzingatia sheria na maadili ya kila fani ambayo mtu aliisomea ili kuleta matokeo chanya kwenye jamii(positive social effect). Kama ni Mhandisi, usichakachue “bill of quantites”; kama ni mwanasheria, linda haki; kama ni daktari, sema ukweli; kama ni mwandishi, usiandike uongo wala uchochezi, n.k.

Kwa maoni yangu, haya mambo kwa ujumla wake ndiyo yanayochangia kwa asilimia kubwa kuzifanya jamii zetu za kiafrika ziendelee kuyumba kisiasa, kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kimitazamo.
Mungu ibariki Tanzania.

_______________________
Obadia Kajungu, Esq.
ADVOCATE
+255 756 145 390
 
Asante ndugu Obadia, mimi nachukua huu uandishi wako kufanya katafiti kangu kadogo, ni wangapi wameusoma huu uzi wote mwanzo hadi mwisho?

Kama hujausoma uzi wote je sababu ni nini?
 
Back
Top Bottom