Utafiti waonyesha rushwa imeongezeka Tanzania | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Utafiti waonyesha rushwa imeongezeka Tanzania

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Gudboy, Sep 25, 2009.

 1. Gudboy

  Gudboy JF-Expert Member

  #1
  Sep 25, 2009
  Joined: Aug 14, 2009
  Messages: 799
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 33
  Na Kizitto Noya

  WAKATI vita dhidi ya ufisadi ikionekana kupamba moto, tatizo hilo linaonekana kuongezeka kiasi cha kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi vinara wa rushwa barani Afrika, utafiti uliofanywa na shirika la Transparency International unaonyesha.

  Baadhi ya wabunge kutoka chama tawala na upinzani wamekuwa mstari wa mbele kuitaka serikali iwafikishe mahakamani viongozi na wafanyabiashara wanaowatuhumu kwa ufisadi, huku serikali ikiwafikisha mahakamani watu mbalimbali kwa tuhuma za kula njama, wizi na kutumia vibaya ofisi kwa maslahi binafsi.

  Karibu kesi 27 zinazohusiana na rushwa na matumizi mabaya ya ofisi zimeshafunguliwa katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne iliyoingia madarakani mwaka 2005.

  Lakini pamoja na Rais Jakaya Kikwete kujivunia mafanikio hayo aliyoyaita kuwa ni historia, utafiti wa taasisi hiyo ya kimataifa, unaonyesha kuwa rushwa ndio kwanza imeongezeka.

  Kwa mujibu wa utafiti huo, Tanzania imeporomoka kwa nafasi nne katika orodha ya nchi ambazo zimefanikiwa kuzuia rushwa kwa kiasi kikubwa.

  Utafiti huo unaonyesha kuwa Tanzania imeporomoka kutoka nafasi ya 12 mwaka juzi hadi nafasi ya 16 mwaka jana kati ya nchi 48 za barani Afrika na kutoka nafasi 94 mwaka juzi hadi 102 mwaka jana duniani.

  "Mwaka 2008 Tanzania imekuwa nchi ya 16 ikiwa imepata alama 3," inasema sehemu ya utafiti huo uliofanywa kwa kuwahusisha wafanyabiashara mbalimbali katika nchi husika na wachambuzi wa masuala ya uchumi.

  Utafiti huo ulifanywa mara 13 na matokeo yake kuchambuliwa kwa zaidi ya mara sita huku matokeo yanayofanana kwa zaidi ya mara tatu, yakitumika kuwa ndio jibu sahihi.

  Mwaka juzi Tanzania ilishika nafasi ya 12 kwa kuwa na viwango vidogo vya rushwa barani Afrika na nafasi ya 94 duniani. Nafasi hiyo ilishikiliwa na nchi ya Madagasca.

  Tanzania ilishika nafasi hiyo baada ya nchi za Botswana ikifuatiwa na Afrika Kusini, Cape verde, Mauritius, Namibia, Seychelles, Ghana, Senegal, Gabon, Swaziland na Lesotho.

  Hata hivyo wakati Botswana ikiendelea kushikilia nafasi yake ya kwanza mwaka jana Tanzania imeporomoka kutoka nafasi ya 12 hadi 16 pamoja na jitihada mbalimbali za serikali kupambana na ufisadi.

  Nchi zilizoifuatia Botswana mwaka jana ni Mauritius, CapeVerde, Afrika Kusini, Seychelles, Namibia, Ghana, Swaziland, Burkina Faso, Madagasca, Senegal, Lesotho, Mali Gabon na Bennin.

  Mbali na nchi hiyo kuwa ya 16 barani Afrika, pia imeshuka kutoka nchi ya 94 mwaka juzi hadi 102 mwaka jana duniani.

  Tangu serikali ya Kikwete iingie madarakani imeshapandisha kizimbani mawaziri wawili na katibu mmoja wa wizara, wafanyakazi wa taasisi nyeti za fedha na lundo la wafanyabiashara.

  Mawaziri hao, Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona (Nishati na Madini) wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutumia vibaya ofisi zao na kuisababishia serikali hasara ya Sh11 bilioni. Wameunganishwa pamoja na katibu mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.

  Pia balozi wa zamani wa Italia, Prof Costa Mahalu amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kupandisha gharama za ununuzi wa nyumba ya ubalozi.

  Zaidi ya watu 27, wakiwemo wafanyabiashara na maofisa waandamizi wa Benki Kuu (BoT) wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kula njama na kuiba fedha kutoka kwenye Akaunti ya malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

  Wiki mbili zilizopita, wakurugenzi wanne wa BoT walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kula njama, kufanya uzembe na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh100 bilioni katika uchapishaji wa noti, wakati mkurugenzi wa zamani wa utawala wa BoT, Amatus Liyumba anakabiliwa na kesi ya tuhuma za kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh200 bilioni.

  Katika mazungumzo yake ya moja kwa moja kwa njia ya redio na televisheni, Rais Kikwete alijivunia rekodi ya kumudu kufungua kesi nyingi za rushwa akisema kuwa ni ya kihistoria katika vita hiyo.

  Rais alidokeza kuwa kuna kesi nyingine kubwa tatu ambazo ziko tayari na zinaweza kufunguliwa wakati wowote.

  SOURCE: MWANANCHI
   
Loading...