#COVID19 UTAFITI: Wanaopata COVID-19 Tanzania wana umri chini ya miaka 61

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,006
9,872
Utafiti wa kwanza kuripoti sifa zawaliougua Ugonjwa wa Virusi vya Korona(UVIKO-19) pamoja na matokeao ya tiba walizopatiwa nchini Tanzania umebaini kuwa takribani robo tatu ya wagonjwa wote ni wenye umri chini au sawa na miaka 60.

Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa Januari 6 mwaka huu katika mtandao wa IJID Regions, jarida rasmi la Jumuiya ya Kimataifa ya Magonjwa ya Kuambukiza (ISID). Wanasayansi walitafiti wagonjwa wa UVIKO-19 katika miezi ya mwanzo ya janga hili nchini Tanzania.

“Tulifanya utafiti huu wakati ambao hakukuwa na takwimu kamili za kitafiti kuhusu UVIKO-19,” anasema kiongozi wa utafiti huo Profesa Sayoki Mfinanga, Mtaalam wa Afya ya Jamii na Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Umri wa waliougua UVIKO-19 nchini Tanzania unaakisi takwimu za watu wengi walioambukizwa ugonjwa huu barani Afrika, utafiti unasema. Pia, matokeo haya yanaweza kubadili mitazamo ya watu wengi waliodhani kuwa ugonjwa huu huwapata wazee pekee.

Iliwachukua muda wa miezi miwili (Aprili 1 hadi Mei 31, 2020) kumaliza utafiti huo, ambapo wagonjwa 121 waliandikishwa kutoka hospitali mbili zenye hadhi ya rufaa Jijini Dar es Salaam na kufuatiliwa kwa siku 21. Hatahivyo, mtaalamu wa Six-Sigma, taaluma inayohusika na maboresho ya utendaji katika mifumo ya utoaji huduma, Godbless Baluhya, anasema matokeo ya utafiti huu yangeboreshwa zaidi endapo sampuli kubwa ya watu na katika uwanda mpana zaidi kitabia na umri ingehusishwa kutoka vituo mbalimbali vya kutolea huduma.

“Kwa ufahamu wangu, kulikuwa na visa vingi[vya UVIKO-19] wakati wa wimbi la kwanza, labda utafiti ungehusisha angalau hospitali mbili hadi tatu katika kila mkoa ungetoa picha tofauti,’’ anasema. Baluhya. Watafiti walifuatilia wagonjwa 112 na kati ya hao, asilimia 92.6 walikuwa wamelazwa, huku wagonjwa 9 ambao ni sawa na asilimia 7.4 ni wale waliotibiwa na kurudi nyumbani.

Sita kati ya 10 ya wagonjwa walioandikishwa kwaajili ya utafiti ni wanaume wakifuatiwa na wale wenye magonjwa yanayohusisha mfumo wa upumuaji kama vile pumu na kifua kikuu. Wastani wa umri wa wagonjwa wote ni miaka 41 ambapo ni sawa na kusema wagonjwa walioandikishwa kwenye utafiti walikuwa na miaka kuanzia 30 hadi 54.

Wastani huo ni sawa na ule ulioripotiwa Afrika Kusini lakini chini kidogo ya ule ulioripotiwa China, Libya, Marekani(New York) na Italia, ambapo huko wastani ulikua juu zaidi yaani walioathirika alikuwa na umri mkubwa ukilinganishwa na Tanzania na Afrika Kusini.

Utafiti huo ulizingatia pia dalili ambazo wagonjwa walikuwa nazo kabla ya kufanya vipimo na miongoni mwa dalili zote walizobaini, maumivu ya kichwa ndio dalili iliyobeba takribani asilimia 55 ikifuatiwa na homa kwa asilimia 49. Profesa Mfinanga anasema kuwa
dalili walizozibaini katika utafiti wao ni sawa na zile zilizoripotiwa duniani kote.

“Kwahiyo wataalamu wa afya wanatakiwa watoe uangalizi wa karibu kwa wagonjwa wenye dalili sawa na hizo katika kudhibiti janga la UVIKO-19,” amesema Mfinanga

Dalili nyingine zilizobainika katika utafiti huo ni pamoja na kikohozi, maumivu ya kifua, homa, mwili kuchoka pamoja na matatizo ya pumzi. Mpaka sasa Shirika la Afya Duniani WHO limeripoti vifo 5,658,702 vilivyotokana na wagonjwa walioripotiwa duniani kote.

Wakati wa utafiti huu, kati ya wagonjwa 121 waliofanyiwa uchunguzi wa karibu, 18 kati yao walipoteza maisha ambapo wastani wa umri wa wagonjwa waliopoteza maisha ni miaka 58 sawa na kusema kuwa walifariki watu wenye umri kuanzia miaka 54 hadi 61.
Hali hiyo inaashiria kuwa waathirika wakubwa wa janga la UVIKO-19 ni watu wenye umri mkubwa pamoja ma wale wenye magonjwa sugu na ya kudumu kama vile magonjwa ya moyo, kisukari, UKIMWI na kadhalika.

Prof. Mfinanga amesema kuwa katika kupambana na kuzuia janga hilo la UVIKO-19 kwa njia mbali mbali kama vile utoaji wa chanjo, watu wenye magonjwa sugu ya kudumu pamoja na wazee na wale wenye umri mkubwa wapewe kipaumbele zaidi ili kuepusha
idadi kubwa ya vifo itakayoendelea kutokea kutokana na kuathirika kwa afya zao.

Mpaka kufikia Januari 25, 2022 jumla ya watu milioni 1.9 milioni sawa na asilimia 3.33 ya Watanzania walikuwa wamepata chanjo kamili. Hii ni sawa na kusema watu wanne tu katika kila kundi la Watanzania 100 ndio waliopata chanjo ya UVIKO-19. Profesa Mshiriki wa Uuguzi wa Rheumatology katika Shule ya Afya na Ustawi wa Jamii Bristol nchini Uingereza Mwidimi Ndosi, anaeleza kuwa utafiti
huu ni wa muhimu kutokana na kwamba umefanyika nchini Tanzania, mahali ambapo takwimu za ugonjwa huo hazikuwa wazi na habari zinazohusiana na UVIKO-19 zilitolewa na serikali katika mlengo wa kisiasa zaidi.

“...utafiti huu unawafungua akili baadhi ya watu waliokuwa wakiamini kuwa huu ni ugonjwa unawapata wazee tu,’’ anasema Ndosi

CHANZO: MWANASAYANSI
 
Wanashindwa tu kusema ila hapo wanataka watu wote tuchanje hamnishawishi hata kidogo.Mwanzon walisema miak 50 kuelekea 100 na sahz 6o kushuka. Sichanjwi
 
Back
Top Bottom