Utafiti kuhusu maadili na uwajibikaji wa viongozi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,801
11,961
Habari wakuu,

Hii hapa ni Taarifa kuhusu Utafiti wa maadili na uwajibikaji wa Viongozi.
Utafiti pic.PNG

Taarifa hii ya utafiti inahusu maadili na uwajibikaji wa viongozi. Moja ya hoja iliyojitokeza sana katika mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya ni maadili na uwajibikaji wa viongozi. Hivyo utafiti ulijaribu kuangalia changamoto mbalimbali zinazohusu maadili na uwajibikaji kuhusiana na taasisi kadhaa za umma na baadaye kutoa mapendekezo. Utafiti umepitia Katiba mbalimbali, sheria, maamuzi ya kimahakama, maandiko ya wanazuoni pamoja na taarifa mbalimbali. Hali kadhalika, utafiti ulijaribu kuangalia ni namna gani nchi nyingine zimejaribu kuzitatua changamoto zinazofanana na zile za Tanzania, halafu kuangalia kama utatuzi huo unaweza kufaa katika mazingira halisi ya Tanzania.


Taarifa hii imegawanywa katika sehemu kumi. Sehemu ya Kwanza inadodosa dhana ya uwajibikaji na kuangalia changamoto za kiuwajibikaji kwa ujumla wake. Inajaribu kuangalia umuhimu wa Katiba kuimarisha mifumo ya maadili na uwajibikaji. Sehemu ya Pili inaongelea maadili na miiko ya viongozi wa umma. Inaelezea changamoto zilizopo na kupendekeza namna ya kuimarisha maadili na miiko ya viongozi wa Umma. Sehemu ya Tatu inahusu uwajibikaji wa viongozi wakuu wa mhimili wa Serikali. Inaanza na kungalia mfumo uliopo na kumuwajibisha Rais na hasa utaratibu wa Rais kushtakiwa na Bunge (impeachment). Inaonekana utaratibu wa mashtaka ya Rais na Bunge (impeachment) una changamoto nyingi ambazo zinafaa kuangaliwa katika mchakato wa kutunga Katiba mpya. Baada ya hapo Taarifa inaongelea mfumo na changamoto za kuwawajibisha Mawaziri (akiwemo Waziri Mkuu na Manaibu Waziri).


Sehemu ya Nne inahusu “Taasisi za Uwajibikaji” ambazo ni taasisi zilizoundwa mahsusi kwa ajili ya kuleta uwajibikaji katika taasisi za umma na zingine. Taasisi zilizozungumziwa katika Taarifa hii ni pamoja na TAKUKURU, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai. Taarifa inabainisha changamoto zinazozikabili taasisi hizo na kutoa mapendekezo ya namna Katiba inavyoweza kuzikabili.


Sehemu ya Tano inahusu uwajibikaji wa Mahakama. Kama ilivyoelezwa katika Taarifa ya Tume ya Bomani[1], changamoto zinazoukabili mhimili wa Mahakama ni nyingi lakini taarifa hii imeangalia maeneo ambayo yanaweza kutatuliwa kikatiba tu kama kuimarisha uhuru wa Mahakama na kuimarisha usimamizi wa maadili ya Majaji na Mahakimu. Sehemu ya Sita inazungumzia uwajibikaji wa Bunge kwa ujumla wake na Wabunge mmoja mmoja. Inapendekeza namna ya kuimarisha udhibiti na urari wa madaraka (checks and balances) miongoni mwa mihimili mitatu ya dola ili iweze kuwajibishana, kuimarisha uwajibikaji wa wawakilishi (Wabunge) kwa wapiga kura wao, na kuwapa wapiga kura haki ya kuwawajibisha wawakilishi wao kabla ya uchaguzi.


Sehemu za Saba na Nane za Taarifa hii zinahusu Serikali za mitaa. Zinaangalia uwajibikaji kuhusu wawakilishi wa wananchi (madiwani) na watendaji wa Halmashauri za Serikali za mitaa. Sehemu ya Tisa inahusu uwajibikaji kuhusiana na Maliasili za Taifa. Wananchi wengi wametoa maoni mbalimbali wakionyesha kutoridhishwa na uwajibikaji katika usimamizi na uvunaji wa maliasili zilizopo. Taarifa imebainisha changamoto mabalimbali zinazohusiana na uwajibikaji katika usimamizi na uvunaji wa maliasili za nchi na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kukabiliana nazo. Katika kutoa mapendekezo hayo jitihada zilifanyika ili kupata uzoefu wa nchi zilizofanikiwa kukabiliana na changamoto kama hizo. Sehemu ya Kumi ni muhtasari wa mapendekezo yaliyotolewa sehemu mabalimbali katika Taarifa hii. Sehemu hii ina lengo la kumsaidia msomaji kufanya marejeo kwa urahisi zaidi. Hata hivyo, sababu na mantiki ya kila pendekezo zimeainishwa katika sehemu husika.



United Republic of Tanzania, Financial and Legal Management Upgrading Project (FILMUP): the Legal Sector Report, Dar es Salaam.

Naomba ufungue kiambatanisho hiki kujisomea zaidi.
 

Attachments

  • utafiti - maadili na uwajibikaji.pdf
    1.2 MB · Views: 102
Back
Top Bottom