Stories of Change - 2021 Competition

Boniface Evarist

JF-Expert Member
Nov 26, 2010
1,147
512
KUJIAJIRI.png

Daima wazo la mtu ndiyo kitu pekee anachoweza kutumia kubadilisha mfumo mzima wa maisha yake, ninaandika andiko hili nikiwaangalia vijana kama Maxence Melo aliyeanzisha JamiiForums na Milladi Ayo mwanzilishi wa Ayo Tv, hawa ni baadhi ya watu walioamua kutengeneza ajira za wengine badala ya wao kusubiri kuajiriwa. Ninatamani kuona kila Mtanzania wa leo na wa miaka ijayo anakuwa na uthubutu wa aina hii.

Ninaanza kwa kusema ili kuweza kuwa mtu wa ushawishi na mleta mabadiliko katika jamii inatakiwa akili ya kipekee inayotekeleza maamuzi uliyoyafanya kama ndiyo maono au njozi yako. Na maono ya mtu mmoja mmoja ndiyo husababisha maendeleo ya kundi, chama au nchi. Uwezo binafsi wa mtu mmoja mmoja ndiyo unaosababisha uwezo wa timu yote. Ukiona timu ya mpira inafanya vizuri sana tambua ni uwezo binafsi wa mtu mmoja mmoja unaotokana na wachezaji wa timu hiyo, ndivyo ilivyo pia kwenye mafanikio ya taifa lolote, maendeleo yanategemea sana uwezo wa kila mwananchi, Tanzania inatuhitaji sisi tuweze kubadilisha fikra kutoka kutamani kuajiriwa na kufikia maamuzi ya kujiajiri na kusababisha ajira kwa wenzetu na vizazi vijavyo.

Mafanikio ya mtu ni kufikia kilele cha ukubwa wa ndoto au maono yake, na hakuna anayefika kileleni pasipo kuamua kufanya jambo lilelile mara kwa mara mpaka ainuke. Kwa kufikia hapo, ninataka nikueleze mambo muhimu ya kuzingatia ili kuleta mabadiliko ya mtu binafsi na kundi (taifa) kwa ushirika wa mtu mmoja mmoja.

Kugundua unachopenda na kujitoa kukifanya: uwezo wa mtu daima unajificha na kudhihirika kupitia kile tu anachokipenda sana. Mfano mzuri ni mafanikio ya Christiano Ronaldo yanatokana na kugundua kwake mapema kuwa yeye ubadaye wake uko kwenye mpira na ndipo akaamua kuweka malengo ya hicho alichogundua. Unapofanya kile unachokipenda hufanya ili kupata hela unafanya ili Kusababisha matokeo, uzuri ni kwamba matokeo hayatakuacha maskini.

Kuwa na hamu na shauku ya kupenda kusoma vitabu: inasemekana daima kuwa mara zote viongozi wakubwa ni wasomaji wakubwa, kabla hujaanza kufanyia kazi kile unachokipenda kwanza soma maisha ya watu wakuu waliowahi kufanya kazi kama unayoipenda, hii itakusaidia sana kujua waliweza na kushindwa wapi, na unawezaje kufanya zaidi yao. Siku moja David Oyedepo aliwaambia vijana kuwa kama hutaki kudharaulika katika ujana wako, wekeza umakini wako katika usomaji
David Oyedepo (Chanzo: nobelie.com)  kama hutaki kudharaulika katika ujana wako, wekeza umakini wako katika usomaji.

David Oyedepo (Chanzo: nobelie.com) "kama hutaki kudharaulika katika ujana wako, wekeza umakini wako katika usomaji".

Tunaona pia Marehemu Reginald Mengi alikuwa msomaji sana wa vitabu vya maswala ya biashara na aliweza kuandika pia kitabu cha “I can, I must, I will – the spirit of success” ambacho kinatoa siri kubwa za mtu anayeweza kufanikiwa anakuwa na roho ya uthubutu na kuona ushindi tangu mwanzo.

Ishi kulingana na uwezo wako: kuna usemi unasema “maisha ni hatua kwa hatua”. Huu ni mtihani mwingine ambao kijana wa kitanzania anapaswa kuufaulu, yaani unakuwa msomi lakini huna hela, ni bora ukae nyumba ya kawaida ya bei nafuu ili uweze kuinuka na kuhamia viwango vikubwa, kuliko unalazimisha kuishi nyumba ya kodi ya laki tatu kwa mwezi, wakati mshahara wako ni laki tano. Usipande Uber au Bolt kama uwezo wako unaruhusu daladala. Usiige maisha ya mtu mwingine, nenda hatua kwa hatua ili ufikie hatua ya kuweza kuishi kwa utoshelevu.

Kutunza kukumbukumbu vizuri: kumbuka kila kitu kuanzia tarehe yako ya kuzaliwa, tarehe uliyopata wazo au maono uliyonayo, siku uliyoanza kujifunza juu ya ndoto yako, hatua zote ulizowahi kupitia katika hiyo ndoto yako. Kila wazo unalolipata litunze, kila jambo unalifanya liandike kuwa ulianza lini na hii itakusaidia kujifanyia tathmini ya kila baada ya muda fulani ili kujua wakati gani umeenda vizuri au umekwama. Kuna Mwandishi anaitwa Lailah Gifty Akita, katika kitabu chake kiitwacho Think Great: Be Great, anasema:

“Historical gap is created due to missing written records.” Akiwa na maana kwamba tunakosa taarifa za kihistoria kwa sababu ya kukosekana kwa taarifa zilizoandikwa.

Fanya vitu, tunza kukumbukumbu kimaandishi, na kwa kufanya hivi taarifa zako zitasimuliwa kwa ujasiri, kumbuka hata Mungu anatunza kumbukumbu.

Tenda kile unachokisema: nimegundua sisi watu wa Tanzania ni watu ambao tunaongea sana, inaniuma sana kuona nguvu tunazo, akili tunazo lakini hatuchukui maamuzi magumu kusimamia mipango yetu. Njia pekee ya kufanikiwa ni kukubali kuumia kwa ajili ya kile ambacho umeamua kukifanya, hii tabia wanayo sana Wachaga, ndiyo maana huonekana kama hufanya biashara zaidi, ufike wakati kila mmoja ahamasike kulisimamia jambo lake kwa bidii sana, kwa kufanya hivi itasababisha wakulima kuanza kilimo kikubwa na cha malengo, wavuvi kuvua kwa malengo, Waalimu kufundisha kwa malengo. Mtu akisema nimeamua kuwa mcheza mpira, ni vema sana kujinoa kwa mazoezi kila wakati, ukiamua kuwa utakuwa mwanasiasa – isiwe kwa sababu ya kipato bali tamani kusoma zaidi habari za wanasiasa mashuhuri ambao wamefanya mambo makubwa na mazuri duniani. Imezoeleka kuwa wana siasa ni waongo mimi sikubaliani na hii kauli ila mtu husika aliye katika siasa anaweza kuwa muongo. Amua kusimamia kwa vitendo unachoongea. Hii natamani iwe ni tabia mpya ya kila Mtanzania, China waliamua kusimamia wanachoongea leo limekuwa miongoni mwa mataifa yenye nguvu zaidi duniani.

Kamwe usikope: Naomba nieleweke kwa umakini hapa, simaanishi kukopa ni kosa, ila ninachotaka kukwambia msomaji ni kwamba kamwe usianze mradi au biashara kwa pesa ya mkopo. Hii ndiyo sababu hata benki haiwezi kukukopesha kama hujatimiza muda kadhaa na hiyo biashara yako. Anza na ulicho nacho, kama unataka mtaji ni bora uuze mali yoyote uliyo nayo ndipo uanze biashara kwa huo mtaji lakini usikope kwa mtu yeyote ili huo mkopo uwe ndiyo mtaji, mara nyingi utaishia kuchanganyikiwa na ukishindwa kufanikiwa kwa mara ya kwanza utakosa nguvu ya kurudia huo mradi maana mdai wako atakunyanyasa kisaikolojia. Mkopo unaondoka uwezo wa ubunifu na upambanaji wa mazingira ili kuielewa vizuri kazi. Ukianza mradi kwa hela ya mkopo, wewe utakuwa si mjasiriamali bali ni mtumishi wa aliyekukopesha.

Elewa kwa undani kusudi na maono ya kuishi kwako: kuna kila sababu ya watu kufundishwa toka shule ya msingi kuwa kila mmoja amezaliwa ili kutimiza wajibu fulani (maono), mfano tunaweza kusema Nyerere alikuja kuikomboa Tanzania, Reginald Mengi alikuja kutuonesha njia Watanzania kuwa ukisema inawezekana, ukathubutu na kufanya inatokea. Watu kama Akina Bakheresa walizaliwa ili kutuambia kuwa hapa nchini kwetu tuna utajiri wa kila namna, na wengine wengi. Sasa huu uwe ni wakati wa kila mmoja hasa vijana kuamua kuchukua hatua ambayo unasikia msukumo ndani yako, inawezekana, jambo la kwanza angalia unachojisikia amani kufanya, hiyo ndiyo ajira yako ya kweli na si kila msomi kuwaza kwenda kwenye taasisi za umma na asasi za kiraia. Ifike mahali uwe na Shilingi elfu moja leo lakini unaona unamiliki mabilioni ya hela miaka thelathini ijayo. Tuanze kujituma kwa ajili ya ile ndoto au maono, hakuna haja ya kuvaa vizuri, kula vizuri au kufanya starehe wakati hata ndoto yako huijui na kama unaijua hujaanza kuitekeleza.

Zingatia kupita kawaida: Kuna usemi usemao kuwa “kama unawakimbiza panya wawili basi utawakosa wote”. Ili kubadilisha maisha yako na taifa letu kila mmoja asimamie kile ambacho amepata msukumo moyoni mwake kuwa atasimamia hicho, hauwezi kuwa nyota wa muziki wakati huo huohuo ukawa nyota wa mpira. Muziki una gharama yake ya kulipa ili kufikia hatua ya ubora na mpira pia, njia pekee ya kukufikisha kileleni ni wewe kuamua kuzingatia (to focus) jambo unalofanya wakati wote, iwe usiku au mchana, umelala au unatembea, waza hilo. Usiwe mtu wa kujaribu kila fursa kila inapokuja akilini mwako, fanya kile ambacho unaweza kutoa huduma kwa ubora zaidi, wanadamu tunategemeana sana, rais wa nchi anahitaji wahudumu, walinzi, wataalamu, washauri na wengineo, sasa kama wewe unataka kila kitu ujue hutakuwa na utaalamu kwa lolote, maana kuzingatia kimoja ndiko kunaunda ujuzi na utaalamu zaidi wa hilo ufanyalo. Mfano, Bill Gates alipokuwa anasoma chuo kikuu cha Harvard alipoona kama ana maono na kitu aliona bora aacha chuo ili apate muda wa kuzingatia katika uundaji wa mifumo ya kompyuta, mwingine ni Mark Zuckerberg ambaye pia aliamua kuacha chuo kikuu cha Harvad ili azingatie zaidi kile anachokifanya na leo dunia nzima tunatumia kile walichoamua kukipa muda zaidi maishani mwao. Ukishagundua kusudi la kuzaliwa kwako achana na mengine yote, zingatia kwa kuwekeza nguvu, muda, akili na mali katika hilo.

Fanya kazi, Fanya kazi, Fanya kazi, hakuna mbadala. Nimeweka hiyo sentensi kuonesha msisitizo wa namna ya kubadilisha ndoto yako iwe ndiyo maisha yako. Amua kufanya kazi kwa bidii sana, ifike sehemu hata ukiweza kulala masaa 6 na 18 fanyia kazi, ni bora ukavunja kanuni za kitaalamu za kulala ili kusababisha mambo kubadilika maishani mwako. Siku moja nilisikiliza akihojiwa Diamond Platinumz katika majibu yake alijibu kuwa kuna wakati wimbo anaufanyia mazoezi kwa muda wa siku tatu bila kulala, ila wimbo huo ukitoka unakuwa wa dakika 3 hadi 5. Ni tabia za watu wakuu kuwekeza zaidi kwenye muda wa kazi na mazoezi kuliko kujionea huruma.

Endapo tutaamua kuishi kwa mtindo huu wa maisha hata unapokuwa shule akilini utazingatia kusoma ili kuendesha ndoto yako na si kusoma ili uwe mwajiriwa bali uwe mwajiri, zama zimebadilika, mtindo wa maisha unahitaji ubunifu zaidi, umia hata miaka kumi ila fikia ndoto yako, na ukiinuka vijana wengi walioko vyuoni watafanya mafunzo (internships) kwako.

Mwisho, jifunze kuishi na wanaokukosoa bila kuwachukia na kuanza kujibizana nao, kila mtu mkuu anakutana na changamoto ya kusemwa vibaya, nyamaza bali endelea kutimiza ndoto yako. Heshimu kufundishwa (mentorship), hili litakufanya usome, usikilize au uhuduhurie mafundisho ya wanaokushawishi zaidi, kila mwenye maono makubwa hafi kabla hayajatimia.
Rejea:
  1. Mengi, Reginald. I Can, I Must, I Will: The Spirit of Success. IPP Limited, Dar Es Salaam, Tanzania, 2018.
  2. Oyedepo, David. Pillars of Destiny: Exploring The Secrets Of An Ever Winning Life. Dominion Publishing House, Lagos, Nigeria, 2008.
 
Sawa kabisa lakini naweza kuwa na maswali machache tu kwako

Je naweza kuajiri watu huku nimeajiriwa?
Unaweza kabisa, tena wewe unakuwa na nafasi kubwa sana ya kutengeneza ajira kuliko wale wasio na ajira kabisa.

Unaweza kutumia kipaji chako ambacho unacho au maono yako na kuyawekea mpango mkakati ukaanza jambo kwa muda wako wa ziada na huku unaandaa mtu wa kukusaidia ukiwa kwenye ajira yako, na kwa kadri mradi wako unavyokua ndivyo unavyoongeza fursa kwa wengine watakao kuwa wanapata nafasi ya kusaidia majukumu ya mradi wako. Kazi ni kubwa ni kuwaza, kuamua na kufanya kwa bidii.
 
Naomba kura yako ndugu msomaji wa andiko hili.

Kama kuna mahali sijaeleweka kwenye comment naweza kufafanua maana kwenye mada ilitakiwa iwe kwa kifupi ili yasizidi maneno 1500
 
“Chochote ambacho akili ya binadamu inaweza kuumba na kufikiri, inaweza kukikamilisha pia.”
Napoleon Hill
 
Ndiyo mkuu, tumaini langu hakuna mshindi aliyefanya plagiarism. Maana katika kupitia pitia leo hii nimekutana na plagiarism kadhaa na nimegundua ndizo zilikua na votes nyingi za wasomaji.
 
Ndiyo mkuu, tumaini langu hakuna mshindi aliyefanya plagiarism. Maana katika kupitia pitia leo hii nimekutana na plagiarism kadhaa na nimegundua ndizo zilikua na votes nyingi za wasomaji.
Na kwa Tanzania plagiarism haipewi sana jicho. Aisee wenzetu hili swala hasa vyuo vya US unapewa zero kabisa wanaheshimu sana citations
 
Na kwa Tanzania plagiarism haipewi sana jicho. Aisee wenzetu hili swala hasa vyuo vya US unapewa zero kabisa wanaheshimu sana citations
Ni kweli kabisa, tena kuna mdau mmoja nimeona amebeba jarida kama lilivyo na kulipakia kwenye mashindano. Ila najua wasimamizi wa zoezi hili walimtambua tu.
 
8 Reactions
Reply
Back
Top Bottom