Usipotoshwe na watu wasioelewa maana na utaratibu wa kuwa na raia pacha. Angalia hapa maelezo ya uraia pacha na niulize swali lolote nitakujibu

Synthesizer

JF-Expert Member
Feb 15, 2010
11,143
18,774
Nimekuwa nikisoma maoni na hoja za watu kuhusu Tanzania kuruhusu uraia pacha, na nimeshangaa sana na kugundua watu wengi sana wanaotoa maoni kuhusu uraia pacha hawaelewi kabisa inakuwaje mtu anakuwa na uraia pacha. Na hili nimeona hata toka kwa wanasiasa wanaopinga uraia pacha, na kuona kwamba wengi hawaelewi kabisa hili suala na wanaliongelea bila kuwa na ufahamu nalo.

Sasa nimeona ni vema kuwa na thread ambayo itasaidia kuelimisha watu juu ya suala hili. Na nitaanza na maswali ya msingi juu ya uraia pacha, na kujibu mengine yatakayofuta.

1. Tanzania ikiruhusu uraia pacha, ni kwa ajili ya Watanzania pekee?
Hapana. Unaporuhusu uraia pacha inakuwa ni kwa ajili ya Watanzania wanaotaka kuchukua uraia wa nchi nyingine, na watu wa nchi nyingine wanaotaka kuchukua uraia wa Tanzania. Ni lazima Tanzania na nchi hiyo nyingine zote ziwe zinaruhusu uraia pacha. Masharti na vigezo huzingatiwa na hutofautiana.

2. Inakuwaje hadi mtu anakuwa na uraia pacha?
Kimsingi, huombi kuwa raia pacha, bali unaomba uraia wa nchi ya pili, na kama ukikubaliwa ndio unakuwa raia pacha, kwa kuwa sasa utakuwa na uraia wa nchi zaidi ya moja.

Jambo la msingi ni kwamba sio rahisi mtu kupata uraia pacha. Mara nyingi, mtu anapewa uraia pacha ikiwa ameishi kihalali mfululizo katika nchi ya pili kwa muda usiopungua miaka mitano. Na nchi nyingine zitataka upitie kwanza hatua ya kuwa mkazi wa kudumu (permanent resident) kabla ya kuomba uraia na kuwa raia pacha. Kwa hiyo basi, mtu toka Kenya hawezi kuja Tanzania leo na kuomba uraia pacha, sio rahisi.

Hivyo ieleweke wazi kwamba wewe Mtanzania ambaye hujawahi hata siku moja kuishi South Africa, huwezi kuondoka Tanzania leo hii kwenda bondeni ukaombe uraia ili uwe raia pacha. Vivyo hivyo mtu wa South Africa ambaye hajawahi kuishi Tanzania, hawezi kuja Tanzania leo ili apewe uraia wa Tanzania na kuwa raia pacha.

3. Nini hasa baadhi ya vigezo vya msingi vya kuwa raia pacha?
Inategemea nchi inaweka vigezo gani kwa raia wa nchi nyingine kuomba uraia pacha. Sharti kubwa la nchi nyingi ni kwamba usiwe na rekodi ya uhalifu (criminal record) ya nchi uliyotoka au nchi unayoishi na unaomba uraia, na uwe umeishi kwa muda fulani katika nchi unayoomba uraia ili uwe raia pacha. Nchi nyingine hata zinaweka sharti la kwamba lazima uongee lugha ya nchi , kama hapa kwetu Kiswahili, ili uwe raia wao.

Kama nilivyosema katika swali la kwanza, kigezo cha kawaida ni kuwa umeishi kihalali (sio kuzamia) katika nchi nyingine kwa zaidi ya miaka mitano. Sasa kuna nchi nyingine, ikiwa umeoa au kuoelewa na raia wa nchi hiyo basi unapata uraia wa nchi ya mume/mke wako na kuwa raia wa nchi hiyo, hivyo kuwa raia pacha. Sasa kuna baadhi ya nchi ziliona hili lilitumika vibaya, watu walioa au kuoelwa ili tu kupata uraia. Hivyo walibadilisha huu utaratibu na kusema lazima uishi katika ndoa, na kuthibitisha unaishi na mumeo/mkeo kwa angalau miaka 3 kabla ya kuomba uraia.

Kwa hiyo kila nchi inakuwa na vigezo vyake, na Tanzania tukiamua kuruhusu uraia pacha lazima tutaweka vigezo vyetu. Hatuwezi kutoa uraia kama sadaka ili watu wawe raia pacha.

4. Kuna watu wanakuwa na uraia pacha wa kununua?
Ndio, zipo nchi zinauza uraia. Kwa mfano, kuna nchi zinaweza kusema ukiingiza katika nchi hizo mtaji kuanzia Dola 250,000 basi una haki ya kupewa uraia. Kwa hivyo nchi kama hizo zitasemwa zinauza uraia. Tanzania hatulazimishwi na mtu yeyote kuuza uraia wa Tanzania, kwa hiyo tunaweza kuruhusu watu wa nje kuwa na uraia wa Tanzania bila kuwa na kigezo cha kununua uraia wa Tanzania

5. Je, Tanzania tunaweza kuwawekea Watanzania masharti ya kuwa na uraia pacha na nchi nyingine?
Sio rahisi, kwa sababu ni sawa na kusema tutaziwekea hizo nchi masharti ya wao kumpa Mtanzania uraia wa nchi hizo. Ila sasa, Tanzania tunaweza kuweka masharti kwa Watanzania walio na uraia pacha ili kulinda vitu kama usalama wa nchi yetu, nk

6. Je uraia pacha hauwezi kutuletea athari za usalama wa Tanzania?
Hii ni hoja potofu na imetumika vibaya na watu wengi. Ili mtu kusababisha athari za usalama wa nchi yetu sio lazima awe raia pacha. Na pia kama kuna maeneo ambayo tunaona uraia pacha unaweza kuhatarisha usalama wa Tanzania basi tutawawekea watu wenye uraia pacha masharti fulani ili kuzuia hilo. Kwa mfano, tunaweza kusema Mtanzania mwenye uraia pacha haruhusiwi kugombea nafasi za kisiasa kama ubunge na uraisi, au kutumika katika vyombo vya usalama kama JW, Polisi, na TISS.

7. Uraia pacha unakuwaje na manufaa za kiuchumi kwa Tanzania?
Hili ni swali la msingi sana. Jambo la kukumbuka ni kwamba unapokuwa wa nchi ya kigeni, kunakuwa na masharti yanayokuzua kufanya mambo fulani katika nchi nyingine. Kwa mfano, si rahisi kwa Mtanzania kutuma fedha za kigeni kwenda nchi nyingine, na ndivyo isivyo rahisi kwa mtu aiye Mtanzanaia katika nchi ya nje kutuma fedha za kigeni Tanzania. Sasa unapokuwa unaishi nchi ya kigeni na una uraia wa Tanzania, moja kwa moja unakuwa na kitu tunaita haki ya kutuma faida kwenye nchi yako (repatriation of profits) bila masharti magumu. Na kumbuka kwamba, kwa upande wa Tanzania, unakuwa na urahisi wa kuwekeza ukiwa na uhakika kwamba investments zako Tanzania ziko salama kwa kuwa unalindwa kwa haki za kuwa raia. Mtu kama Aliko wa Dangote huwezi kumlinganisha katika uhuru wa investments zake kama alionao MO kwa kuwa MO kama raia wa Tanzania ana wigo mwepesi na mpana zaidi wa kufanya biashara Tanzania kuliko Dangote.

Kwa hiyo Watanzania waliochukua uraia wa nje watajisikia huru zaidi kuhamisha mitaji yao kuja Tanzania wakijua kwamba wanahamishia mitaji Tanzania kama raia wa Tanzania bila kuhofu kubadilika kwa upepo wa kisiasa au hata kutaifishwa mali zao

Lakini zaidi, raia wa nje wenye uraia pacha na Tanzania wanakuwa na uhuru zaidi wa kuwekeza Tanzania ikiwa watakuwa na uraia wa Tanzania. Itakuwa rahisi sana na kutompa hofu yoyote Dangote kuhamishia mtaji mkubwa Tanzania akijua anafanya hivyo kama raia wa Tanzania

8. Vipi ikiwa nchi ya nje ambayo una uraia pacha nayo inataka uihujumu Tanzania, sio rahisi hilo kufanyika kama raia pacha?
Suala la nchi uliyonayo kukutaka uihujumu nchi yako ya kuzaliwa ni suala la uhalifu kama uhalifu mwinginme wowote wa kimataifa, na linaweza kufanywa na mtu yeyote hata asiye na uraia pacha. Nikiukana uraia uraia wa Tanzania na kuchukua tuseme uraia wa Burundi, kama Burundi watataka kunituma kuihujumu Tanzania sio lazima niwe raia pacha. Bado wanaweza kunituma kufanya hujuma hata bila kuwa na uraia pacha. Na kimsingi, ni rahisi mie kukataa kuja kuihujumu Tanzania nikiwa na uraia pacha kuliko kama niliukana uraia wa Tanzania kwa kushurutishwa ili nipate uraia wa Burundi. Kwa hiyo ni hoja poofu kuhusianisha uraia pacha na watu kuihujumu nchi yao ya kuzaliwa.

9. Je uraia pacha hauathiri uzalendo wako kwa nchi yako ya kuzaliwa?
Kwanza nini hasa maana ya mzalendo, na uzalendo au kutokuwa mzalendo kunathibitishwa na matendo gani? Je ndio tuseme mtu akiwa na uraia pacha na anaishi Tanzania atakuwa fisadi, mwizi, mhujumu uchumi, mvivu na mtoro kazini kuliko yule Mtanzania asie na uraia pacha? Hii pia ni hoja potofu inayotumiwa vibaya na watu wengi. Wengi watakubali kwamba Tanzania kwa sasa inapigika sana, watu wanafuja fedha za serikali na wanafisadi sana nchi hii. Sasa ndio tuseme watu wanaofanya haya ni raia pacha? Jambo moja la kuelewa ni kwamba, ni raisi kwa mtu asiye na uraia pacha kufanya ufisadi katika nchi yake kuliko yule aliye na uraia pacha.

10. Vipi raia pacha akifanya uhalifu na kukimbilia nchi nyingine aliko na uraia wa pili?
Dunia ya sasa ni kama kijiji. Unapofanya uhalifu wa aina yeyote ukiwa raia pacha, usidhani kwamba kukimbilia nchi nchingine kutakuokoa. Kumbuka katika masuala ya uhalifu kuna Interpol, polisi ya kimataifa, ambayo ni rahisi Tanzania kuitumia na wewe kukamatwa hata ukiwa umekimbilia nchi nyinge. Ukiiba gari Tanzania ukakimbilia USA ambako una uraia pacha, usidhani kwamba utapona. Na kumbuka kwamba, nchi nyingi zinaruhusu uchukue uraia wao kwa masharti ya kutokuwa na rekodi ya kihalifu (criminal record). Kwa hiyo sidhani kwamba utafanya ubakaji Tanzania ukimbilie USA na kuwa salama. USA watatengua uraia wako wa USA na utarudishwa Tanzania kwa nguvu (deportation) kwa sababu tayari umekiuka mashart ya kutokuwa na criminal record. Dunia ni kijiji siku hizi.

11. Je ukiwa uraia pacha, Tanzania inaweza kuutengua?
Inawezekana. Kama vile tu USA wanaweza kuutengua uraia wa Mtanzania kule USA kwa sababu ya makosa ya jinai, ndivyo Tanzania tunavyoweza kutengua uraia wa Tanzania wa Mchina ambaye anafanya makosa au uhalifu akiwa anaishi hapa Tanzania kama raia pacha. Ila sidhani kama haki za binadamu zinaruhusi kutengua uraia wa asili wa mtu na kumfanya stateless.

12. Je kuna Watanzania wenye uraia pacha kwa sasa?
Sio rahisi, hasa ikiwa waliupata uraia wa nchi nyingine ukubwani. Mara nyingi ili uwe raia wa nchi nyingine, lazima nchi hiyo ipeleke taarifa za ombi lako la uraia kwenye ubalozi wa nchi yako. Tanzania wanapopata ombi hilo basi wataubatilisha uraia wako wa Tanzania. Kuna nchi mtu unakuwa raia kwa kuzaliwa katika nchi hiyo. Ndio maana Tanzania kwa watu waliozaliwa nje, wenye birth certificate za nje, lazima uthibitishe uraia wako wa Tanzania ukifikisha miaka 18. Hiki ndicho tumesikia katika nyanja za siasa kwamba fulani sio faia wa Tanzania. Hii ni mara nyingi kwa wale waliozaliwa nje ya Tanzania.

Na suala la kuthibitisha uraia linakuja kwa kuwa kuna nchi zinakupa uraia ukizaliwa kwenye hizo nchi, hata kama wazazi wako sio raia. Kimsingi, watoto wanaozaliwa nje ya Tanzania wapo ambao ni kama wana uraia pacha ikiwa nchi walikozaliwa iliwapa uraia kwa msingi wa kuzaliwa huko. Ndio maana wakifikisha miaka 18 Tanzania inataka wathibitishe uraia wao wa Tanzania au waende nchi walikozaliwa ambako wanaweza kutambuliwa kama raia. Unaweza usithibitishe uraia, lakini huenda siku moja ukakwama pale itakapoonekama una birth certificate ya nje na hukuthibitisha uraia wako wa Tanzania ulipofika miaka 18. Ndio utasikia fulani hana sifa za kugombea ubunge kwa kuwa sio Mtanzania ingawa wazazi wake wote unakuta ni Watanzania.

13. Nini tofauti ya ukazi wa kudumu (permanent residency) na uraia pacha?
Ukazi wa kudumu ni kwamba wewe unakuwa mkazi wa nchi fulani, na unaruhusiwa kufanya kila kitu kama vile tu raia isipokuwa baadhi ya vitu hasa kugombea nafasi za kisiasa, kupiga kura na nchi nyinge huruhusiwi kumiliki ardhi.

Huruhusiwi kujihusisha na siasa. Huhitaji visa kuingia hiyo nchi, na unaruhusiwa hata kufanya kazi bila kibali cha kazi (work permit) na hata kufanya kazi serikalini. Na ukazi wa kudumu unaweza kuupoteza ikiwa hutaishi katika nchi ya ukazi wako wa kudumu kwa kipindi cha muda fulani. Kwa hiyo ukazi wa kudumu huwezi kabisa kuulinganisha na uraia pacha. Uraia pacha unakupa uhuru zaidi na hauna kikomo wala masharti ya kuendelea kukaa katika nchi muda wote.

14. Vipi kwa walioukana uraia wa Tanzania na sasa ni raia wa nchi nyingine, wanaweza kupata uraia pacha?
Hili ni jambo gumu kidogo, na litahitaji ufikirio maalum wa kibinadamu (special consideration on humanitarian grounds) wa serikali. Uraia pacha si kwa ajili ya raia wa Tanzania ambaye aliukana uraia wa Tanzania na sasa anaishi nje ya Tanzania kama raia wa nchi nyingine. Ikiwa Mtanzania alishaukana uraia wa Tanzania na sasa anaishi nje ya Tanzania, kimisingi, ili aweze kuwa raia pacha inabidi aombe uraia wa Tanzania upya kama mtu mwingine tu ambae sio raia wa Tanzania. Huenda kwanza arudi Tanzania, na labda aishi kwa kibali (residence/permanent permit) nchini kwa muda usiopungua miaka mitano, na ndio ataomba tena kuwa raia wa Tanzania na kumfanya awe raia pacha - ikiwa nchi ambayo ni raia wake kwa sasa inamruhusu kuwa raia pacha, na Tanzania itakubali kumpa tena uraia. Sasa ndio maana nimesema serikali inaweza kutoa ufikirio, kwa sababu kimsingi huyu mtu ni mzaliwa wa Tanzania, na hivyo wakasema hawa watarudishiwa uraia wa Tanzania kwa msingi wa kuzaliwa Tanzania ili wawe raia pacha na nchi ambayo wana uraia kwa sasa.

15. Hadi sasa, ni nchi ngapi katika Afrika zinaruhusu uraia pacha?
Ni rahisi zaidi kuongelea ni nchi ngapi katika Afrika haziruhusu uraia pacha kuliko ni ngapi zinaruhusu uraia pacha, kwa kuwa karibu nchi zote za Afika sasa zinaruhusu uraia pacha isipokuwa Tanzania, Ethiopia, Eritrea, DRC, Malawi, Zambia, Liberia, Lesotho, Sao Tome na Cameroon, kama ramani hapa chini inavyoonyesha.

1628326239668.png

Maswali mengine yanakaribishwa japo nahisi vipengele nilivyoweka vinajitosheleza

Malamula atoa kauli kuhusu uraia pacha!!!!!!!

Mweleko mpya kwa uraia pacha​

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema Serikali inalifanyia kazi suala la uraia pacha na kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha, litakuwa limepatiwa ufumbuzi.

Pia, alisema wizara yake iko tayari kuwawezesha Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) kupiga kura endapo watapata ridhaa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa sababu ni rahisi kwa kutumia teknolojia.

Balozi Mulamula alisema hayo katika mahojiano maalumu na wahariri wa gazeti hili alipotembelea Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) jijini Dar es Salaam jana kwa lengo la kuimarisha ushirikiano.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imetambua suala la uraia pacha linakwenda sambamba na ushiriki wa diaspora; na watu wengi, wakiwamo wabunge wamekuwa wakionyesha utayari wao.

“Tukiwa bungeni kuna mbunge mmoja aliondoa shilingi mpaka tumpe majibu, wakati ule zamani tukienda bungeni walikuwa wanasema ‘bwana wee usituambie habari za diaspora, wanakula kuku kwa mrija, wachague wanataka wapi, huwezi kupata huku ukapata kule’. Sasa mtazamo umebadilika, wao ndio wanaotaka,” alisema Balozi Mulamula.

“Wabunge wengi wametoka diaspora, nikawaambia kama mnalitaka hili basi, na ninyi ni watunga sheria, sisi tunalifanyia mkakati wa kisera, lakini likija kwenye sheria ninyi wabunge ndiyo mtusaidie tuipitishe.”

Balozi Mulamula alisema tangu akiwa balozi, msisitizo wake ni kwamba huwezi kumwondolea mtu haki ya kuzaliwa katika nchi aliyozaliwa.

Alisema Watanzania wengi walio nje ya nchi wamekwenda kutafuta maisha na wako kwenye fani tofauti, ukiwamo udaktari na biashara, hivyo, wana mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.

“Ningekuwa na uwezo ningelimaliza hata jana, ingekuwa imenipa amani sana, hasa kukuza ushiriki wa diaspora. Mtazamo umebadilika, si kama huko nyuma, kwa hiyo mimi naamini kabla ya mwisho wa mwaka huu, tutakuwa tumelipatia suluhu hili la uraia pacha,” alisema.

Alisema suala la uraia pacha lilitakiwa lipite katika mchakato wa mabadiliko ya katiba, lakini ilionekana si suala la kuingia kwenye katiba, bali kuliwekea sheria maalumu kama zilivyofanya Ethiopia na India.

“Kubadilisha Katiba ni mlolongo mrefu, lakini ikishaingia kwenye katiba halafu ukaja utawala mwingine hauitaki, unaitoaje? Kwa hiyo kukiwa na sheria inawalinda zaidi.

“Sasa tumesema tunavyoainisha hii sera yetu ya mambo ya nje, tuko kwenye mkakati wa kuweza kuja na programu maalumu wanayoita hati maalumu zinazowatambulisha Watanzania walioko nje,” alisema Balozi Mulamula.

Suala la uraia pacha ni miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa na wananchi wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC) inakusanya maoni ambayo yaliwekwa kwenye rasimu ya pili ya Katiba kisha kupitishwa kwenye Katiba inayopendekezwa.

Ibara ya 72 ya Katiba Pendekezwa inasema: “Bila kuathiri masharti yaliyomo kwenye sura hii, mtu yeyote mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano kwa kupata uraia wa nchi nyingine, atakapokuwa katika Jamhuri ya Muungano, atakuwa na hadhi maalumu kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.”

Wadau wazungumza

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema nchi zilizoruhusu uraia pacha duniani kote zimepiga hatua kiuchumi kwa sababu zimewajengea diaspora kujiamini na kupata haki kama raia wa nchi zao.

Mbatia alitolea mfano Kenya akisema mwaka jana fedha zilizotoka kwa diaspora kwenda Kenya zilikuwa ni Dola 4.4 bilioni za Marekani ukilinganisha na Dola 380 milioni ambazo diaspora walirudisha hapa Tanzania.

“Ili kujenga confidence ya diaspora, uraia pacha ni muhimu. Kutojiamini ndiyo sababu ya kuwekea vikwazo suala hili, tuangalie mizania ya kiuchumi zaidi ili tufanye maamuzi sahihi,” alisema Mbatia.

Diaspora kupiga kura

Balozi Mulamula alisema suala la diaspora kupiga kura linahitaji utaratibu na miundombinu, hasa kwa kutumia teknolojia kama zinavyofanya nchi nyingine zilizofanikiwa kwa kutumia mifumo ya kimtandao.
 
Hili la uraia pacha hatulitaki. Lilishindwa wakati wa kikwete na litashindwa hata sasa. Hatuhitaji raia mamluki wenye kuweza kua wazalendo kwa nchi nyingie au kuweza kutumiwa na adui wa nchi au kuweza kuisaliti nchi au kuihujumu uchumi wake. Hao wanaokupa uraia nao wana malengo yao.
 
Kama sheria ya uraia ya Tanzania ya sasa inasema kwamba mtanzania wa kuzaliwa (pigia mstari ...sio wa kuandikishwa) ambaye wazazi wake wawili wote ni watanzania wa kuzaliwa hawezi kuupoteza uraia wake kwa kupata uraia wa nchi nyingine isipokuwa kwa kibali cha wazazi wake ambacho kinapaswa kuombwa na waziri wa mambo ya nje wa Tanzania kwa wazazi wa mtanzania huyo anayeutaka uraia pacha... sasa je ni masharti gani mengine ambayo mtanzania wa namna hiyo anaweza kuupoteza uraia wake ikiwa wazazi wake wa kuzaliwa hawataki ?

2. Ikiwa maifa ya nje huwa hayamshurutishi mtu kuuna uraia wake wa asili wa Tanzania au nyingine, je Tanzania inatumia vigezo gani kusema kwamba mtu kauna utanzania wake ili hali hajaukana mahali popote kimaandishi au kimaneno? Na vigevyo hivyo vipo katika sheria ipi ya uraia? Nazungumzia Section 13 ya sheria ya uraia ya renounciation hapa:
http://citizenshiprightsafrica.org/wp-content/uploads/2016/08/Tanzania-Citizenship-Act-1995.pdf

Uraia nao-uzumngumzia hapa ni ule wa kuzalia na sio wa kujiandikisha taadhari kabla hamjanirukia maana waziri mwenye dhamana hana uwezo wa kuufuta uraia wa kuzaliwa isipokuwa tu kwa ruhusa ya wazazi wa mtanzania huyo wa kuzalia. Uraia wa unaowezwa kufutwa ni ule tu wa kujiandisha... na hata huo, una mlolongo mrefu.. sijui athari za kumfutia mtu uraia na kumfanya stateless... je wamekwisha futiwa wangapi, lini na mahali gani? Tupeni records.
 
Hili la uraia pacha hatulitaki. Lilishindwa wakati wa kikwete na litashindwa hata sasa. Hatuhitaji raia mamluki wenye kuweza kua wazalendo kwa nchi nyingie au kuweza kutumiwa na adui wa nchi au kuweza kuisaliti nchi au kuihumu uchumi wake. Hao wanaokupa uraia nao wana malengo yao.
Hivi sheria ya uraia umeisoma? unaijua inavyosoma? watu wote wenye umri chini ya miaka 18 hata sasa wanaruhusiwa kuwa raia pacha . Sasa unaposema kwamba haamtaki uraia pacha , ni akina nani hao unaowasema waovunja sheria zetu za sasa ?
 
Swali ....mwanao kazaliwa nchi flani. Ila soon after ukarrud bongo ukaanza kushuulikia passport ya bongo ukapata. Je kuna chochote cha kufanya kisheria? au automatically baada ya kupata passport tayar ni mtanzania? Ikumbukwe huna nia ya kurudi alikozaliwa mwanao na ku claim uraia wa Kule.
 
Hapana Mkuu, bado akifika miaka 18 itabidi athibitishe uraia wake wa Tanzania. Suala kubwa hapo ni kuwa na birth certificate ya nje ya Tanzania, ambapo inaweza ikawa inampa uraia wa nchi hiyo kwa kuzaliwa, na Tanzania wanataka ku-confirm uraia wake akifika miaka 18. Hilo linafanya kama ana uraia wa hiyo nchi nyingine kwa kuzaliwa, basi anakuwa anaukana huo uraia akifika miaka 18
 
Hili la uraia pacha hatulitaki. Lilishindwa wakati wa kikwete na litashindwa hata sasa. Hatuhitaji raia mamluki wenye kuweza kua wazalendo kwa nchi nyingie au kuweza kutumiwa na adui wa nchi au kuweza kuisaliti nchi au kuihumu uchumi wake. Hao wanaokupa uraia nao wana malengo yao.
Hulitaki wewe, na sisi tunalitaka. Kwa hiyo tufanyeje sasa?
 
Hapana Mkuu, bado akifika miaka 18 itabidi athibitishe uraia wake wa Tanzania. Suala kubwa hapo ni kuwa na birth certificate ya nje ya Tanzania, ambapo inaweza ikawa inampa uraia wa nchi hiyo kwa kuzaliwa, na Tanzania wanataka ku-confirm uraia wake akifika miaka 18. Hilo linafanya kama ana uraia wa hiyo nchi nyingine kwa kuzaliwa, basi anakuwa anaukana huo uraia akifika miaka 18
Safi kabisa. Jibu murua.
Ila birth certificate itaendelea kuwa ya kule ughaibun??? maana RITA eti hawatoi birth certificate ya aliyezaliwa nje.
 
Uraia pacha ni kitu cha muhimu,sijui kwanini unamnyima mtu uraia pacha

Tena sio pacha tu,mtu awe na uraia wa manchi kibao atakayo yeye

Mengine ni kunyima watu haki tu mamaeee

Bado miakili ya cold war yapo kichwani mwa sisi waTZ
Hakuna point za maana wanazotoa, ndio maana mara nyinge ni inaonekana ni wivu tu unawasumbua watu. Binadamu mara nyingi hapendi kuona mtu mwingine anafaidika na kitu ambacho yeye hatakaa apate.
 
Kama sheria ya uraia ya Tanzania ya sasa inasema kwamba mtanzania wa kuzaliwa (pigia mstari ...sio wa kuandikishwa) ambaye wazazi wake wawili wote ni watanzania wa kuzaliwa hawezi kuupoteza uraia wake kwa kupata uraia wa nchi nyingine isipokuwa kwa kibali cha wazazi wake ambacho kinapaswa kuombwa na waziri wa mambo ya nje wa Tanzania kwa wazazi wa mtanzania huyo anayeutaka uraia pacha... sasa je ni masharti gani mengine ambayo mtanzania wa namna hiyo anaweza kuupoteza uraia wake ikiwa wazazi wake wa kuzaliwa hawataki ?

2. Ikiwa maifa ya nje huwa hayamshurutishi mtu kuuna uraia wake wa asili wa Tanzania au nyingine, je Tanzania inatumia vigezo gani kusema kwamba mtu kauna utanzania wake ili hali hajaukana mahali popote kimaandishi au kimaneno? Na vigevyo hivyo vipo katika sheria ipi ya uraia? Nazungumzia Section 13 ya sheria ya uraia ya renounciation hapa:
http://citizenshiprightsafrica.org/wp-content/uploads/2016/08/Tanzania-Citizenship-Act-1995.pdf

Uraia nao-uzumngumzia hapa ni ule wa kuzalia na sio wa kujiandikisha taadhari kabla hamjanirukia maana waziri mwenye dhamana hana uwezo wa kuufuta uraia wa kuzaliwa isipokuwa tu kwa ruhusa ya wazazi wa mtanzania huyo wa kuzalia. Uraia wa unaowezwa kufutwa ni ule tu wa kujiandisha... na hata huo, una mlolongo mrefu.. sijui athari za kumfutia mtu uraia na kumfanya stateless... je wamekwisha futiwa wangapi, lini na mahali gani? Tupeni records.
Hili la aliloeleza la kufuatiwa Uraia inabidi aliongezee nyama. Ni kwa sheria ipi au ibara ipi ya katiba inatoa rukhsa ya kufuta Uraia wa kuandikishwa.
 
Hili la aliloeleza la kufuatiwa Uraia inabidi aliongezee nyama. Ni kwa sheria ipi au ibara ipi ya katiba inatoa rukhsa ya kufuta Uraia wa kuandikishwa.
Nimeona nchi nyingi zina-revoke uraia wa kuandikishwa. Sasa sijui inakuwaje ikiwa mtu alipata unaia wa kuandikishwa kwa kuukjana uraia wa nchi yake. Watam-deport kumpeleka wapi?
 
Maswali yamekwisha? Ningependa sana maswali ya hoja za hawa wanaopinga uraia pacha. Nahisi wakisoma hii thread wanakimbia kujificha
 
Uraia pacha kwa Tanzania naona Kama ujinga tu uraia pacha unawafaa wazungu,wahindi na waarabu na wachina kwa sababu wana faida kwenye zao kiuchumi na kibiashara wakiwa Nchi sio zao

Mfano mhindi wa Tanzania ndio importer mkubwa wa bidhaa za India kuleta Tanzania

Mwarabu pia ndie importer mkubwa wa bidhaa za Uarabuni Kama mafuta nk kuleta Tanzania

Mchina vivyo hivyo

Diaspora wa kwetu wa nini kikubwa wanacho import kwenye Nchi zao waliko watafute masoko huko?

Uraia pacha kwa watanzania hawana maana yeyote ninkujaza tu mipassport tu kwenye kabati

Diaspora wetu was kitanzania Ni choka mbaya

Mhindi,mwarabu na mchina diaspora yeye huwaza tu namna ya kuleta bidhaa toka nchini kwake kwenye country of origin kuuza aliko tofauti na midiaspora mitanzania .Ni kelele tu ohhh tunataka uraia pacha kwa kipi Cha maana walichonacho wanachosaidia Nchi?
 
Nimeongeza swali

14. Vipi kwa walioukana uraia wa Tanzania na sasa ni raia wa nchi nyingine, wanaweza kupata uraia pacha?

Hili ni jambo gumu kidogo, na litahitaji ufikirio maalum wa kibinadamu (special consideration on humanitarian grounds) wa serikali. Uraia pacha si kwa ajili ya raia wa Tanzania ambaye aliukana uraia wa Tanzania na sasa anaishi nje ya Tanzania kama raia wa nchi nyingine. Ikiwa Mtanzania alishaukana uraia wa Tanzania na sasa anaishi nje ya Tanzania, kimisingi, ili aweze kuwa raia pacha inabidi aombe uraia wa Tanzania upya kama mtu mwingine tu ambae sio raia wa Tanzania. Huenda kwanza arudi Tanzania, na labda aishi kwa kibali (residence/permanent permit) nchini kwa muda usiopungua miaka mitano, na ndio ataomba tena kuwa raia wa Tanzania na kumfanya awe raia pacha - ikiwa nchi ambayo ni raia wake kwa sasa inamruhusu kuwa raia pacha, na Tanzania itakubali kumpa tena uraia. Sasa ndio maana nimesema serikali inaweza kutoa ufikirio, kwa sababu kimsingi huyu mtu ni mzaliwa wa Tanzania, na hivyo wakasema hawa watarudishiwa uraia wa Tanzania kwa msingi wa kuzaliwa Tanzania ili wawe raia pacha na nchi ambayo wana uraia kwa sasa.
 
Uraia pacha kwa Tanzania naona Kama ujinga tu uraia pacha unawafaa wazungu,wahindi na waarabu na wachina kwa sababu wana faida kwenye zao kiuchumi na kibiashara wakiwa Nchi sio zao

Mfano mhindi wa Tanzania ndio importer mkubwa wa bidhaa za India kuleta Tanzania

Mwarabu pia ndie importer mkubwa wa bidhaa za Uarabuni Kama mafuta nk kuleta Tanzania

Mchina vivyo hivyo

Diaspora wa kwetu wa nini kikubwa wanacho import kwenye Nchi zao waliko watafute masoko huko?

Uraia pacha kwa watanzania hawana maana yeyote ninkujaza tu mipassport tu kwenye kabati

Diaspora wetu was kitanzania Ni choka mbaya

Mhindi,mwarabu na mchina diaspora yeye huwaza tu nna ya kuleta bidhaa toka nchini kwake kwenye country of origin kuuza aliko tofauti na midiaspora mitanzania .Ni kelele tu ohhh tunataka uraia pacha kwa kipi Cha maana walichonacho wanachosaidia Nchi?
Hapo ndipo unapokosea. Tunaposema uraia pacha sio kwa Watanzania pekee, bali ni kwa Watanzania kuwa na uraia pacha na nchi nyingine na wasio raia wa Tanzania kuwa na uraia pacha na Tanzania. Haiwezi ikawa suala la upande mmoja kama unavyosema
 
Similar Discussions

Back
Top Bottom