Usikate Tamaa, Jifunze haya kutoka Kwa Mengi na Bakhresa

Drop shipping Tanzania

Senior Member
Jun 15, 2020
198
500
HABARI WAKUU,

KARIBU KWENYE MADA;

UKWELI ambao pengine una kushangaza ni kuwa matajiri wengi hupenda kusimulia nyakati zao za giza. Kipindi ambacho maisha yalikuwa magumu, yenye mateso, manyanyaso na taadhira.

Upande wa pili, maskini wengi hujitahidi kwa kila namna kuficha aibu zao. Watu wakiwa kwenye utafutaji huwa hawataki wajulikane kama ni wajaa dhiki wakubwa. Wapo hudanganya hata mahali walipotoka ili kukwepesha ramani.

Ni kwa nini matajiri wengi hupenda umaskini wao wa zamani ujulikane wakati maskini hupambana kuficha hali halisi ya maisha yao hususan ukweli wa dhiki ndani ya familia zao?

Heshima; Neno hili moja tu linajibu swali hilo katika pande zote mbili. Tajiri hutaka asemwe kuwa alikuwa maskini kwa sababu ya heshima. Maskini hukataa asijulikane kwa sababu ya heshima.

TAJIRI NA HESHIMA

Siyo uongo kuwa unaposema mtu fulani alikuwa maskini wa kutupwa katika kipindi ambacho anakuwa ameshabadili kibao cha maisha ni heshima. Yaani ule umaskini wake unakuwa unazungumzwa kama historia, hapo unamuongezea thamani.

Kuna tofauti kubwa kati ya utajiri wa kurithi (Inherited wealth) na ule wa kuuvujia jasho (self made wealth). Kwa maana ule wa kuupigania kwa njia halali mpaka kuupata ni kielelezo cha ushujaa wa mtu.

Mohamed Dewji ‘Mo' ndiye tajiri namba moja nchini kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za fedha na uwekezaji. Amefanya kazi kubwa mno kuanzia nyakati za mwisho wa miaka ya 1990 mpaka sasa.

Mo ni mrithi bora, maana alichukua mikoba kutoka kwa baba yake, Gulam Dewji na kuunda Mohamed Enterprises, kisha kuleta matokeo makubwa kupindukia, akiwazidi mpaka wababe wa kibiashara nchini akina Reginald Mengi, Said Salim Bakhresa, Rostam Aziz na wengine.

Hivi sasa Mo ndiye mfanyabishara za halali anayeongoza kifedha, kwa maana kupitia ule uwekezaji unaoonekana. Utajiri wake ni mkubwa, unaokuwa kwa kasi. Anafanya kazi kisasa, kiuchapakazi na kiteknolojia.

Hata hivyo, pamoja na hatua ambazo Mo anapiga na heshima ambayo anastahili kwa namna alivyozipaisha mali alizorithi kutoka kwa baba yake, lakini anabaki tu kuwa mtoto wa tajiri mwenye akili.

Mengi, Bakhresa na Rostam, heshima kubwa ambayo wanakuwa nayo ni kwamba wao hawajarithi. Utajiri wanaomiliki umetokana na kuanzia sifuri, wakavuja jasho, wakatokwa machozi mpaka kuufikia ‘ubabe' wa kifedha walionao.

Hivyo basi, ukikutana na Mengi anakueleza kuwa alilala na ng'ombe pamoja na mifugo mingine ni kwa sababu anataka ushike adabu zako unapomuona amekaa pazuri, kwa maana maisha ya nyuma yalikuwa magumu hasa.

Bakhresa akikwambia alikuwa anauza maandazi, maana yake anataka unavyoona miliki kubwa alizonazo sasa, ujue kuwa zimetokana na ushujaa wake binafsi, siyo kitu kingine.

Rostam akisema alikuwa anabana sehemu ya ada mpaka akapata mtaji wa kuanzia kabla ya kuvuja jasho kwa malengo, anataka ukisikia anamiliki Vodacom Tanzania na uwekezaji mwingine ndani na nje ya nchi, umpigie saluti.

Kwa manti hiyo, matajiri wengi hupenda wajulikane walipotoka kama kielelezo cha kutambulika kwa ushujaa wao. Kutoka kuchangia malazi na ng'ombe mpaka ubilione wa mfano Tanzania kwa nini usimpe utukufu wake Mengi?

Na ndiyo maana Mo ni tajiri mkubwa ambaye historia yake haina mvuto sana kwa sababu alikuta baba yake alishafanya kazi kubwa, kisha yeye akapokea kijiti. Akina Rostam na Bakhresa hawakuanzishiwa mwendo na mtu.

MASKINI NA HESHIMA

Maskini anayeendelea kuuishi umaskini wake anakuwa hana ushujaa wowote, hivyo anaona hali halisi ya maisha yenye asili yake yakijulikana, yatamvunjia heshima na pengine kumharibia fursa mbalimbali.

Na ndiyo maana maskini wengi huishi maisha ya urembo yenye ubandia (synthetic life), hasa nyakati wanapokuwa wanatafuta. Wapo wengi tu wanaotafuta maisha wakijitahidi kuficha hali halisi za umaskini wao lakini wanapofanikiwa hujaa ushujaa wa kusimulia walipotoka.

Tajiri akisema "nilikuwa na chawa au funza", kwake ni ufahari kwa mageuzi aliyofanya. Maskini hufikiria akisema atadharaulika na kupuuzwa moja kwa moja.

Tajiri husema nyumbani kwao kulikuwa na nyumba ya tembo (full suit), yaani udongo kila upande au iliyoezekwa nyasi kwa sababu ukirudi nyumbani kwao hukuti tena suti, unakuta mjengo wenye thamani kubwa na wa kisasa alioujenga.

UMASKINI NI MAPITO

Hata wewe hapo ulipo unaweza kusimama kifua mbele, pamoja na umaskini wako, simama useme kuwa nyumbani kwenu ni shida lakini hayo ni mapito tu ya maisha.

Sema: "Sisi ni maskini, nyumbani kwetu paa ni nyasi, mvua ikinyesha tunaogelea, maana nyumba inageuka bwawa nje, ndani mpaka vyumbani, ila yatakwisha. Mungu yupo."

Usiache kumtanguliza Mungu mbele kwa maana yeye ndiye mfanikishaji wa kila jambo. Nia jumlisha juhudi kisha ukamuomba Maulana akufanyie wepesi, hakuna kinachoshindikana.

Jiulize, wao wamepata kwa nini, kisha ukose kwa upungufu gani ulionao? Mungu ni wa kila mtu. Huhitaji mtu wa kati kumfikia Muumba wako, sema naye usiku na mchana huku ukipambana.

Nikuhakikishie; Kwa hali yoyote uliyonayo Mungu anao mpango wake mzuri tu na wewe. Usikate tamaa, ni dhambi. Yeye aliyekuumba anajua fungu lako lipo na anatambua utalifikia kwa kujituma kwako huku ukimuomba yeye. Unapokuwa hai, elewa kuwa Mungu amekubakiza kwa sababu zaidi ya milioni, kwa hiyo USIKATE TAMAA.


Toa Maoni yako hapo chini.
 

Kabaino Tanzania

JF-Expert Member
Oct 22, 2015
2,337
2,000
Una vimaneno fulani amaizing
Mzee we unaweza waambia watu walime
Tikiti maji kwa mtaji wa million 2,
Kwamba watapata million 13 , baada ya mavuno🤣🤣🤣🤣🤣🤣🤣🤣
Na waka kuamini kindaki ndaki.
 

Pichukodada

JF-Expert Member
Oct 14, 2020
247
250
Tushike lipi sasa jamani nyie walimwengu mboni mnatuchanganya? ukifanya kazi sana ili upate sana utasikia

''acha tamaa ridhika na unachopata''

pesa zoote hizo bado anataka zangu!

'' huyu nae haridhiki?. mara utasikia

''Tamaa mbaya"" au

'' Tamaa mbele mauti nyuma!!

Tamaa ilimponza fisi. unalinganishwa na mnyama hayawani. yaani majina mabaya mabaya km hayo!!

Ukisoma saana ''utasikia umetumwa na kijiji.

Wewe unakuja na slogan za ''Usikate tamaa''
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom