Usidanganywe na stori za vijiweni, ijue Sheria ya Ndoa na Talaka

sajo

JF-Expert Member
Nov 8, 2010
3,021
5,253
marriage-pic JF.jpeg


NDOA NA MATOKEO YA NDOA (TALAKA, UGONI)

Mambo ya ndoa sio mageni sana masikioni mwetu kwani wengine tupo ndoani na wengine marafiki zetu wapo ndoani na hata wazazi wetu wamekuwa ndoani. Kwa hiyo baadhi yetu ni matokeo ya ndoa za wazazi wetu na wengine tumepata matokeo ya ndoa zetu wenyewe (watoto, mali nk). Hivyo nitafundisha juu ya ndoa na matokeo yake kwa urahisi ili tuweze kuelewa na kujua hatua za kuchukua pindi tutapotaka kufanya jambo fulani lihusianalo na mambo ya ndoa. Tanzania, masuala ya Ndoa yanatawaliwa au yanaongozwa na Sheria ya Ndoa Sura ya 29 Rejeo la 2019 (The Law of Marriage Act Cap 29 R.E 2019).

Naitwa Lusajo W. Mwakasege, ni Mwanasheria, namba yangu ya simu ni 0713-368153 (inapatikana whatsapp In WhatsApp teilen na telegram) na barua pepe yangu ni mwakasege@gmail.com. Tuanze somo letu:

A: Nini Maana ya Ndoa?
Ndoa ni muungano wa hiyari kati ya mwanamke na mwanaume kwa nia au dhumuni la kuishi pamoja mpaka mwisho wa maisha yao au ya mmoja wao. Yaani wanakubaliana kuishi pamoja mpaka kifo kitapowatenganisha.
Je, kuna aina ngapi za ndoa?
Kuna aina (kinds) mbili (2) za ndoa ambazo ni;
Ndoa ya mke mmoja (monogamous marriage) – ambapo mwanaume mmoja anamuoa mke mmoja tu
Ndoa ya wake wengi (polygamous) au huenda ikawa ya wake wengi (potential polygamous marriage) – ambapo mwanaume mmoja wakati wa kipindi cha ndoa yake ya awali anaweza kuoa mwanamke mmoja na kumwambia kuwa ataoa tena au kama alishaoa ni ile ambayo mwanaume anaoa wanawake wengine

Je, ndoa ni kweli kuwa ndoa ya kiislamu ni ya wake wengi?
Sio lazima iwe ya wake wengi - Ndoa iliyofungwa katika imani ya uislamu au kimila – hudhaniwa kisheria (presumption) kuwa ni ndoa ya wake wengi isipokuwa kama kutakuwa na uthibitisho kuwa sio ya wake wengi.
Hapa ni kuwa kama wanandoa wakati wa kusajili ndoa yao (katika cheti chao cha ndoa) walikubaliana na kusaini kuwa ndoa yao itakuwa ya mke mmoja, basi ndoa hii haitakuwa ya wake wengi hata kama ilifungwa kwa imani ya uislamu;

Je, ndoa ya kikristo ni ndoa ya mke mmoja tu? Mwanaume mkristo anaweza kufunga ndoa ya wake wengi?
Ndoa iliyofungwa kwa imani nyingine yoyote (ikiwa ni pamoja na ukristo) – itadhaniwa kisheria kuwa ni ndoa ya mke mmoja tu – isipokuwa kama kutakuwa na uthibitisho kuwa ni ya wake wengi;
Kama wanandoa wakati wa kusajili ndoa yao walikubaliana na kusaini kuwa itakuwa ya wake wengi kwenye cheti cha ndoa, basi ndoa ya kikristo inaweza kuwa ya wake wengi, ingawa ni amri ya dhehebu kuamua kuibali ndoa hiyo au la.

Je, Ndoa inatakiwa kudumu kwa muda gani? Umri wa Ndoa kudumu

Ndoa inapofungwa inatakiwa kudumu kwa maisha yote ya wanandoa mpaka kifo cha mwanandoa, au
👉🏿
Mpaka kutangazwa kwa dhana ya kifo cha mwanandoa mmoja; au
👉🏿
Mpaka itakapovunjika kwa kutolewa kwa talaka kisheria; au
👉🏿
Mpaka kufutwa kwa dhana ya ndoa (kwa wale ambao hawakufunga ndoa)

Umri unaoruhusiwa wa mtu kuingia kwenye ndoa
Ili mtu aruhusiwe kufunga ndoa na iwe halali,
  • Mwanaume anatakiwa kuwa na miaka 18 na kuendelea; NA
  • Mwanamke anatakiwa kuwa na miaka 15 na kuendelea
Chini ya umri huo, unaweza kuomba kibali cha mahakama na wazazi ili kupata ruhusa ya kuolewa. Lakini wanaharakati wa haki za watoto (hasa wa kike) pamoja na Umoja wa Mataifa wamekuwa wakipambana kuhakikisha umri huu wa wanawake kuolewa unaongezwa na kuwa miaka 18, rejea hukumu hii Attorney General vs Rebeca Z. Gyumi (Civil Appeal 204 of 2017) [2019] TZCA 348 (23 October 2019); | Tanzlii ya mwanaharakati REBECCA GYUMI (2019) iliyoeleza kuwa vifungu vya umri wa ndoa (Kifungu Na. 13 na 17) ni batili kwani vinakandamiza mabinti na vinatakiwa kurekebishwa na Serikali ndani ya mwaka 1 kutoka 2019. Japo mpaka sasa, bado Serikali haijarekebisha vifungu hivyo, hivyo vipo lakini ni kama visivyo na maana yoyote kisheria.


B: MAHUSIANO YASIYORUHUSIWA
Je, mtu anaruhusiwa kuoa au kuolewa na mtu yeyote yule ili mradi wameridhiana?


HAPANA, Kisheria, sio kila mahusiano yanakubalika kwani kuna baadhi ya mahusiano hayaruhusiwi kisheria. Mahusiano yasiyoruhusiwa ni kama;
  • Mtu kuoana na babu au bibi yake, mzazi wake, mtoto wake, mjukuu wake, kaka au dada yake, shangazi au mjomba, mtoto wa kaka au dada yake - yaani mpwa (niece or nephew),
  • vivyo hivyo mtu kuoa ndugu wa aina hiyo wa upande wa mwenza wake
  • Mtu kuoana na mwenza wa zamani wa babu au bibi, mzazi wake au mjukuu.
  • Mtu kuoana na ndugu wa kuzaliwa na mzazi mmoja (kuchangia baba au mama)

Haya yote ni mahusiano haramu na mtu anayekuwa na mahusiano ya namna hii anafanya kosa kisheria, na ikiwa itathibitishwa mahakamani anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka 2 jela. Ila mahusiano mengine kwa baadhi ya mila yanatambulika kama halali na hivyo yanaweza yasiwe haramu - japo hayaandikwa kisheria, mfano mtu mume kuoa mtu na dada yake nk


Je, mtu aliye na ndoa anaweza kuoa tena na ndoa ikawa halali? (Ndoa ndani ya ndoa)

HAPANA
, Mwanaume aliye na ndoa ya mke mmoja, hataruhusiwa kuoa mwanamke mwingine wakati wa uhai wa ndoa yake hiyo, na akifanya hivyo ndoa hiyo itakuwa ni batili

Vilevile, Mwanaume mwenye ndoa ya wake wengi, hataruhusiwa kufunga ndoa ya mke mmoja na mwanamke mwingine,

Upande wa Mwanamke Je?
Mwanamke aliyeolewa iwe kwa ndoa ya mke mmoja au ya wake wengi, hataruhusiwa kuolewa na mwanaume mwingine kwa ndoa ya aina yoyote ile wakati ndoa yake ikiwa hai.

C: UTARATIBU WA KUFUNGA NDOA;
Taarifa ya Ndoa (notice)
Ni lazima watu wanaotaka kuoana kutoa taarifa ya ndoa (notice) kwa msajili wa ndoa ya angalau siku 21 kabla ya tarehe ya kufunga ndoa, ingawa kukiwa na haraka sana kuna taarifa (notisi) ya siku 7 ambayo pia ni halali kisheria.
Taarifa hiyo,
  • Itaonesha umri wao, anuani zao za makazi, hali zao za kindoa (single nk), aina ya ndoa wanayotaka kufunga, kama ndoa ni ya wake wengi – majina ya wake waliotangulia, tarehe ya ndoa na mahali ndoa itakapofungwa
  • itasainiwa na wahusika wote (wanandoa watarajiwa)
Msajili wa Ndoa ataweka Taarifa ya ndoa hadharani kwa umma ili umma ufahamu juu ya ndoa inayotarajiwa na kama kuna mapingamizi basi yawasilishwe. Tangazo linaweza kubandikwa kwenye mbao za matangazo, kutangazwa gazetini, kwenye mitandao ya kijamii, kwenye redio au kwa njia yoyote ile ambayo jamii inatumia kupata habari kwa urahisi.

Ukitoa taarifa za uongo wakati wa kuandika tangazo la ndoa, unakuwa umefanya kosa la jinai na likithibitishwa mahakamani, utapata adhabu ya kifungo cha miaka 3 jela.

Mapingamizi ya ndoa
Baada ya tangazo la ndoa kuwekwa hadharani, mtu yeyote anaweza kuwasilisha pingamizi la ndoa kwa msajili wa ndoa akiwa na sababu za msingi kuzuia ndoa hiyo isifungwe;
Kama muoaji ni mume wa ndoa ya wake wengi, mkewe wa kwanza au mke yoyote kati ya wakeze anaweza kuwasilisha pingamizi kwa msajili kuzuia ndoa hiyo kwa sababu kama vile,
  • uwezo wa kifedha wa mumewe upo chini kiasi kwamba kuleta mke wa pili kutafanya maisha yawe magumu sana kwa mke mwenyewe na watoto,
  • Mwanamke anayetarajiwa kuolewa ni mkorofi (kipele),au mwenye ugonjwa wa kuambukiza ambao unaweza kuleta majanga kwenye familia

Watu wengine wanaweza kuja na sababu nyingine zozote wanazoona zinafaa kuzuia ndoa inayotarajiwa lakini muamuzi wa mwisho juu ya mapingamizi ya ndoa atakuwa ni msajili wa ndoa.

Mapingamizi yatayowasilishwa atayachambua na ikiwa anaona yana uzito atawaita wapingaji pamoja na wanadoa watarajiwa na kuyasikiliza na kuyatolea uamuzi.

Mapingamizi yanawasilishwa kwa njia ya barua (maandishi).

Aina au Namna (Manner) za ufungaji Ndoa
Ndoa inaweza kufungwa
👉🏿
Kiserikali (civil form) – mara nyingi kama sio zote, hufungwa katika ofisi za mkuu wa Wilaya maarufu kama bomani. Hapa watu wa imani mbili tofauti za kidini huweza kufunga ndoa bila kuathiri imani zao;
👉🏿
Kidini kama watarajiwa wa ndoa wote wanaamini dini moja, kwa imani ya dini hiyo
👉🏿
Kiislamu ,
👉🏿
Kimila, kama ni watu wanaoishi katika jamii moja au ni watu wanaofuata mambo ya kimila,
Ndoa iliyofungwa kimila ni lazima isajiliwe na msajili wa ndoa ili iweze kurasimishwa na kuingia kwenye daftari la ndoa.

Hata watu wa imani moja ya dini bado wanaruhusiwa kufunga ndoa ya kiserikali ikiwa wataona wanapendezwa kufanya hivyo.

Shuhuda wa Ndoa
Ndoa lazima iwe na mashahidi angalau wawili (2)
Ni lazima mashahidi wawe na umri ambao unaruhusiwa kwa mtu kufunga ndoa.
 
D: JE NDOA INAWEZA KUFUNGWA KISIRI?
HAPANA
, Ni lazima ndoa ifungwe hadharani (in public) ambapo umma unaruhusiwa kushiriki. Mtu yeyote anaruhusiwa kushuhudia ufungwaji wa ndoa, hakuna ndoa ya siri.
Ndio maana ni lazima ndoa itangazwe hadharani (magazetini, kwenye mbao za matangazo nk) kabla ya kufungwa.

Je, ni kwa mazingira yapi Ndoa iliyofungwa inaweza kuwa batili au haramu:
  • Kama mmoja wa wanandoa yupo chini ya umri unaoruhusiwa kisheria;
  • Kama wanandoa wapo katika uhusiano uliokatazwa kisheria (haramu);
  • Kama mmoja au wote wa wanandoa wapo katika ndoa nyingine (isipokuwa kama ni ndoa ya wake wengi);
  • Kama mwanandoa hakuridhia ndoa hiyo (alilazimishwa);
  • Kama wanandoa wote hawapo hapo mahali pa kufungia ndoa (isipokuwa kama muwakilishi wa mmoja wapo atakuwepo);
  • Kama mashahidi wawili hawatakuwepo;
  • Kama imeelekezwa kuwa itakuwa ndoa ya muda mfupi (mfano: ndoa ya mkataba);
  • kama ni mwanamke wa kiislamu, mjane au aliyeachika, akiolewa ndani ya muda wa eda (iddat) wa ndoa yake iliyokuwepo;
    Eda ni kipindi ambacho mwanamke wa kiislamu anatakiwa kupitia baada ya kifo cha mumewe au baada ya talaka ambapo hataruhusiwa kuolewa na mwanaume mwingine, ni siku 130 (miezi 4 na siku 10)

basi ndoa hiyo itakuwa ni batili / haramu na isiyokuwa na nguvu kisheria.


E: NDOA ZISIZO BATILI LAKINI ZITAZOTEGEMEA MAAMUZI YA MMOJA WA WANANDOA
Ikiwa wakati wa kufungwa ndoa:
  • Mmoja wa wanandoa alishindwa kufanya tendo la ndoa siku ya ndoa;
  • Mmoja wa wanandoa alipata kifafa au ugonjwa wa akili wa kujirudia rudia;
  • Mmoja wa wanandoa alipata ugonjwa wa zinaa wa kuambukiza;
  • Mke alikuwa na mimba ya mwanaume mwingine ambaye sio huyo mumewe

Ndoa hiyo itakuwa sio batili bali inayotegemea maamuzi ya mwanandoa kuibatilisha au kuendelea nayo. Ikitokea ameamua kuachana nayo basi mahakama itaibatilisha bila kujali kama imefikisha miaka miwili au la.

Ndoa hizo zisizo batili zitakuwa ni halali mpaka pale mahakama itakapotoa tamko la kuzibatilisha (decree of annulment)

Je, unaweza kuhakiki hali ya ndoa (status) ya mtu unayetarajia kuoana nae?
NDIYO
, kisheria unaweza kutafuta habari za kindoa za mtu kuomba upekuzi (search) kwa Msajili Mkuu wa Ndoa (RITA);
Msajili ana daftari (rejista) lenye majina ya watu wote waliosajili ndoa na atakuwa ndiye mtunzaji wa daftari hilo; Izingatiwe kuwa kila ndoa inapofungwa ni lazima taarifa zake ziingie katika daftari hilo (wafungishaji wa ndoa wameelekezwa kuwasilisha taarifa za ndoa wanazofungisha)

Mtu yeyote ataruhusuwa kutafuta habari za wanandoa waliosajiliwa katika daftari la msajili wa ndoa na ataweza kupewa nakala ya taarifa za wanandoa hao zikiwa zimetiwa muhuri wa uthibitisho na msajili. Hivyo ukioa au kuolewa na mtu aliye kwenye ndoa na ukasema hukujua, hiyo inakuwa imekula kwako, unakuwa umefanya uzembe kutomchunguza yule unayeoana nae (due diligence).

Je, unaweza kuhakiki talaka ya mtu?
NDIYO
, unaweza kufanya upekuzi wa talaka kwa Msajili wa Ndoa (RITA)
Kila nakala ya talaka au ubatilisho wa ndoa inapotolewa nakala yake hutumwa kwa msajili wa ndoa ili aisajili na kuihifadhi. Gharama ya kusajili hati ya talaka ni Tshs. 20,000/=
Mtu yeyote ataweza kuomba taarifa za talaka kutoka kwa msajili (kwa kulipia ada - kama Tshs. 20,000 hivi)

Kwa hiyo ni vyema kufanya upekuzi wa ndoa na talaka kwa pamoja ili kujua status halisi ya mtarajiwa wako.

Ushahidi wa uwepo wa ndoa
Ushahidi ufuatao utapokelewa mahakamani kuthibitisha uwepo wa ndoa. Izingatiwe kuwa wepo wa Ndoa haimaanishi kuwa ndio uhalali wa ndoa. Ushahidi huo ni ufuatao;
  • Cheti cha ndoa;
  • Nakala ya cheti cha ndoa iliyothibitishwa na msajili wa ndoa anayekitunza cheti halisi;
  • Hati ya Uthibitisho wa ndoa kutoka kwa maombi ya kujua hali ya ndoa kwenye daftari la msajili wa ndoa – yawe yamethibitishwa na msajili wa ndoa

Je, nini haki za wanandoa kuhusu upatikanaji na utumiaji wa mali?
Wanandoa wote wana haki sawa ya kutafuta, kumiliki na kutumia mali.
Mke atakuwa na sifa na haki ya kutafuta, kumiliki na kuiuza mali, kuingia mikataba mbalimbali, kushtaki na kushtakiwa kwa jina lake au la familia sawa na mume ambaye nae pia ana haki hizo zote.

Je, ikiwa ni ndoa ya wake wengi, Haki juu ya mali ipoje?
Je, Mke mkubwa na hadhi zaidi ya wake wengine?
HAPANA
, Ingawa imezoeleka kuwa mke mkubwa huwa na hadhi kubwa kuliko wake wengine.
Hata hivyo, kisheria, Kama mwanaume yupo kwenye ndoa ya wake wengi, kila mke atakuwa na hadhi sawa, majukumu sawa na haki ya kufurahia mali za mumewe sawa.
Wake wote watakuwa na hadhi sawa bila kujali yupi ni mkubwa na yupi ni mdogo,au yupi alitangulia na yupi amechelewa kuolewa;


F: JE, MWANANDOA ATAWEZA KUMILIKI MALI BINAFSI?
Ndoa haitaondoa haki ya mwanadoa kumiliki, kuiuza au kukodisha mali yake binafsi aliyoipata kabla ya ndoa, na wala haitaondoa haki ya mwanandoa kutafuta, kumiliki na kuuza mali binafsi akiwa ndani ya ndoa; Hivyo mwanandoa anweza kumiliki mali binafsi aliyoipata kabla ya ndoa au baada ya ndoa.

Umiliki wa mali zilizopatikana katika ndoa
Mali yoyote iliyopatikana kipindi cha ndoa na :-
  • Ikawa imeandikishwa jina la mwanandoa mmoja tu basi kutakuwa na dhana, au itaaminiwa kwamba mali hiyo ni mali binafsi ya ya mwanandoa huyo tu – isipokuwa kama kutakuwa na ushaidi wa kuonesha kinyume chake (Mfano mwenza akithibitisha kuwa iliandikwa jina la mwanandoa mmoja lakini ilipatikana kwa wanandoa wote kushirikiana);

  • Ikawa imeandikishwa majina ya wanandoa wote, basi kutakuwa na dhana au itaaminiwa kwamba ni mali ya wanandoa wote (matrimonial property) na wote wana haki sawa ya umiliki wa mali hiyo (50% kwa 50%), isipokuwa kama kutakuwa na ushahidi wa kuonesha kinyume chake.
Haki za wanandoa kwenye nyumba ya familia (matrimonial home)
Nyumba ya familia (a matrimonial home) ni nyumba ile ambayo wanandoa wanamiliki na kuishi humo. Ni tofauti na nyumba inayomilikiwa na wanandoa lakini imepangiishwa kwa watu wengine au haitumiki kwa makazi (ipo tupu).

Kuna nyumba ya ndoa (matrimonial home) na mali za machumo ya pamoja au mali za ndoa (matrimonial property), hivi ni vitu viwili tofauti.

Nyumba ya familia (matrimonial home) haitaweza kuuzwa, kukodishwa au kuhamishwa umiliki (kukopewa) na mwanandoa yoyote bila ruhusa ya mwenza wake.
Mwanandoa atakuwa na haki ya kuweka zuio la uuzwaji au uhamishaji wa umiliki uliofanywa bila ruhusa au ridhaa yake. Hii ni hata kama ilikuwa ni mali binafsi ya mwanandoa, bado mwenza atakuwa na haki ya kupinga.

Ikitokea mwanandoa ameuza au kukodisha sehemu ya umiliki wake wa nyumba ya familia, mwenza wake atakuwa na haki ya kubaki katika nyumba hiyo mpaka pale ndoa itakapokuwa imevunjika au pale mahakama itakapotoa amri ya kutengana (separation)

Ikiwa mwanandoa atamtelekeza mwenza wake katika nyumba ya familia, mwenza wake aliyebaki atakuwa na haki ya kubaki katika nyumba hiyo isipokuwa mpaka pale kutapokuwa na amri ya kuuza mali ikiwa ni utekelezaji wa hukumu dhidi ya mwanandoa (mume au mke)

Je, mali walizopeana wanandoa kama zawadi ni za nani?
Ikiwa wakati wa ndoa, wanandoa walizawadiana mali, basi mali hizo zitakuwa na dhana kuwa ni za aliyepewa zawadi. Utachotakiwa kuthibitisha, ni kuwa ulipewa mali hiyo kama zawadi Mfano kama mume alimpa (expressly) mke zawadi ya gari, basi gari hilo litadhaniwa kuwa ni mali ya mke. Ni tofauti na gari hilohilo angepewa mke awe analitumia kwa mizunguko, kwamba gari ni la mume ila mke amepewa alitumie kwa mizunguko, hii sio zawadi.

Dhana (Presumption) – maana yake ni kuwa fikra inaweza kubadilika ikiwa kutakuwa na uthibitisho wa tofauti.
 
G: NANI ANA JUKUMU LA KUMLEA MWENZA?

Ni jukumu la mwanaume (mume) kumlea mke au kuwalea wake zake kwa kuwapa chakula, mavazi na malazi sawa na hadhi na kipato chake katika maisha.

Vipato havilingani kwa kila mwanaume, hivyo hakuna kiwango maalumu kilichowekwa na sheria.

Vivyo hivyo, ikiwa mwanamke ndiye mwenye kipato na mumewe ni mgonjwa au mlemavu asiyejiweza, litakuwa ni jukumu la mwanamke kumlea na kumuwezesha mumewe kwa mavazi, malazi na makazi kama ambavyo mume angefanya kwa mke.

Isipokuwa kukiwa na amri ya kutengana (separation) na yenye kuondoa jukumu hilo la wanandoa kutunzana,


Vipi kuhusu mikopo? Je ni kweli mwanamke anaweza kukopa kwa jina la mumewe?
NDIYO
, Sheria inaruhusu mwanamke kuchukua mkopo kwa jina la mumewe, kutumia fedha yoyote aliyopo nyumbani au chini ya uangalizi wake, kuuza mali yoyote na kutumia pesa hizo kwa ajili ya kununulia chakula kwa ajili yake na watoto wa ndoa sawa na hadhi ya maisha ya mumewe.

Lakini dhana hii, ni kwa mazingira haya:
  • Wanandoa lazima wawe wanaishi pamoja,
  • kama wanandoa wametengana kuwe na makubaliano ya kuwa mume atahudumia familia na mume akashindwa kutimiza wajibu wake;
au
👉🏿
ikiwa mume amemtelekeza mkewe au kamfanyia visa ili mkewe aondoke;

Dhana hii itakufa endapo mwanamke atakuwa akiishi maisha ya waziwazi ya kinyumba na wanaume wengine.


Je, Mwanaume anaweza kupinga ukopaji au uuzwaji wa mali na mwanamke?
NDIYO
, ikiwa atatoa uthibitisho ufuatao basi mwanamke hataweza kukopa kwa jina lake:

Mwanaume akithibitisha kuwa,
  • Alimpa mwanamke vyakula vya kutosha kwa matumizi;
  • Alimpa Mwanamke fedha ya kutosha kukidhi matumizi tajwa;
  • Bidhaa zilizokopwa zilizidi uwezo na hadhi ya mwanaume, mwanamke alikopa kwa kukomoa.

Je, mume anaruhusiwa kumpiga mkewe?
Kisheria, mume haruhusiwi kumpiga mkewe,au mke kumpiga mumewe, Hairuhusiwi kabisa. Lakini hii isifanye mwanandoa kuwa na kiburi kwa mweza wake, atapigwa mpaka ashangae.

Kukaa Tofauti (living Apart)
Wanandoa wanaweza kukubaliana na kusaini makubaliano kuwa waishi tofauti na huduma za matunzo zitakubaliwa zitatolewaje na bado wakatambulika kisheria kuwa ni wanandoa.


H: JE, MTU ANAWEZA KUSHTAKIWA MAHAKAMANI KWA KUVUNJA AHADI YA NDOA KWA MPENZI WAKE?
NDIYO
, mtu anaweza kufungua kesi ya madai ya fidia kwa kuvunjwa kwa ahadi ya ndoa iliyotolewa na mpenzi wake;
▪️
Mtu atadai fidia ya fedha ya kiasi chochote kile afikiriacho lakini kiasi hicho hakitazidi gharama halisi mtu alizoziingia au kutumia kuhusiana na ahadi ya ndoa;

Mfano: baada ya kuahidiwa ndoa, mtu akaanza kumsomesha mchumba wake, au akajenga nyumba ili waje waishi wote nk – hivi vitu maana yake asingevifanya kama kusingekuwa na ahadi ya ndoa – kwa hiyo kuvunjika kwa ahadi kunakuwa kumeleta hasara ya kifedha inayoweza kuthibitishika.

Angalizo:
  • Hakutakuwa na kesi itayofunguliwa dhidi ya mtu, ikiwa mtu huyo wakati akitoa ahadi ya ndoa alikuwa na umri wa chini ya miaka 18;
  • Muda wa kufungua kesi ya jambo hili hautakiwi kuzidi mwaka mmoja toka tarehe ya kuvunjika kwa ahadi ya ndoa kulipotokea.

Je, zawadi zilizotolewa kwa mpenzi uliyeachana nae bila ndoa zinaweza kudaiwa?
NDIYO
, mtu anaweza kudai zawadi alizotoa kwa mpenzi wake ambaye hawakuoana (uchumba ulivunjika) ikiwa atathibitisha kuwa zawadi hizo zilitolewa, huku lengo zikiwa ni moja ya masharti ya wao kufunga ndoa.


I: UGONI
Je, mkeo anachepuka? Ukimfumania mgoni wako, uchukue hatua zipi?

Mara kadhaa tumeshuhudia mitandaoni, video za watu kufumaniana na varangati zinazofuata baada ya kufumania. Wafumaniaji wengi wamekuwa wakiwapiga wagoni wao, kuwarekodi video za lengo la kuwadhalilisha, na wengine wamefika mbali kwa kuwakodia kikosi kazi cha kuwafundisha kazi hao wagoni wao kwa kuwabaka na kuwalawiti (mara nyingine kavukavu bila hata kilainishi- mafuta). Matokeo ni kuwa baada ya video kusambaa kwenye mitandao ya jamii, kibao humgeukia mfumanizi. Jeshi la Polisi humkamata na kumshtaki mahakamani kwa makosa chungu nzima ikiwemo kujeruhi, kusambaza video za ngono au udhalilishaji, ubakaji nk – matokeo ni mfumanizi kukutwa na hatia na kisha kufungwa jela huku akimuacha mumewe au mkewe pamoja na mgoni wake mtaani wakiendelea kula raha.

Sasa nini kifanyike ukifumania?

Wasilisha madai ya Fidia mahakamani dhidi ya mgoni wako.
Mke au Mume anaweza kuwasilisha madai ya fidia iliyosababishwa na ugoni dhidi ya mgoni wake. Hii ndio njia pekee ya kisheria ambayo haitamsababishia mfumanizi matatizo ya kisheria bali kidogo itamfuta machozi.
▪️
Fidia haina kiwango maalumu, ni kiasi chochote mtu anachojisikia – ili mradi aweze kukielezea na kukithibitisha mahakamani ni kwa nini amekitaja.

Madai ya fidia yanaweza kuwasilishwa peke yake au yanaweza kuwasilishwa ndani ya hati ya maombi ya talaka kutoka kwa mwenza wake.

Angalizo:
  • Hakuna fidia itakayolipwa ikiwa itahibitika kuwa mke au mume alijua kuhusu ugoni huo na akaridhia ( fumanizi la mchongo)
  • Madai ya fidia peke yake yataondoloewa mahakamani ikiwa itathibitika kuwa madai ya aina hiyo yalikwishaombwa na mfumanizi kwenye maombi ya talaka.
  • Mgoni ataweza kufutiwa madai na mahakama ikiwa atathibitisha kuwa hakuwa akijua na asingeweza kujua kuwa alikuwa anatoka kimapenzi na mke/mume wa mtu;

KUMBUKA:
Ugoni ni kwa wanandoa tu, sio wapenzi.
 
J: MADAI YA TALAKA NA UTENGANISHO (DIVORCE AND SEPARATION)
Ikumbukwe lengo la watu kufunga ndoa ni kuishi pamoja kwa maisha yao yote yaliyobaki. Lakini si mara zote lengo hilo hutimia, mambo yanapobadilika na mapenzi kutokuwa mapenzi tena – wanandoa huona ni vyema kila mmoja kuchukua ustaarabu wake. Na kwa kuwa watu hawa walifunga ndoa kisheria, basi kuachana kwao pia hufanywa kisheria kupitia TALAKA.

Mwanandoa yoyote anaweza kuomba mahakama itoe amri ya talaka au utenganisho ikiwa tu atathibitisha kuwa ndoa yake imeharibika kiasi cha kutoweza kutengenezeka tena.

Mahakama haitatoa talaka isipokuwa pale itakapokuwa imejiridhisha kuwa kweli ndoa imeharibika kwa kiwango cha kutoweza kutengenezeka (kutengamaa) tena.

Masharti ya Kuomba Talaka
👉🏿
Ni lazima ndoa iwe na miaka miwili na kuendelea – chini ya umri huo mtu hataruhusiwa kuwasilisha maombi ya talaka;
👉🏿
Hata hivyo, mahakama inaweza kutoa talaka kwa ndoa yenye umri wa chini ya miaka miwili ikiwa mwanandoa atathibitisha kuwa anapata madhara ya kupitiliza (exceptional hardship) katika ndoa hiyo.


Hatua za Kufanya
Kabla ya kufungua madai ya talaka mahakamani, Ni lazima kuwasilisha mgogoro wa ndoa katika baraza la usuluhishi wa ndoa ili mgogoro uweze kusuluhishwa. Migororo huwasilishwa kwa njia ya mdomo au maandishi, ni vile mtu atapenda.

Kazi kuu ya Baraza ni kuwasuluhisha wanandoa ili wapatane na kuendelea na ndoa yao na sio kutoa talaka wala kugawa mali. Kama Baraza likishindwa kusuluhisha basi litatoa maelezo kwa mahakama kuwa mgogoro umeshindwa kusuluhishwa na ndoa imeharibika kiasi cha kutoweza kutengenezeka. Baraza litatoa kwa wanandoa fomu maalumu (Fomu Namba 1).

Fomu hiyo itatumika mahakamani kama ushuhuda kuwa wanandoa walijaribu kusuluhisha ndoa lakini ikawa imeshindikana.

Fomu hiyo ya Baraza la Usuluhishi wa ndoa inatakiwa kuwasilishwa ndani ya miezi 6 kutoka usuluhishi uliposhindwa.

  • Mawakili hawaruhusiwi kuwawakilisha wanandoa katika Baraza hili na kama mwanandoa hataweza kufika mbele ya baraza basi Baraza linaweza kutoa ruhusa awakilishwe na nduguye wa familia yake tu.

Baraza hili la usuluhishi wa Ndoa linapatikana wapi?
▪️
Kama ndoa ilifungwa kwa imani ya ukristo – wanandoa huenda katika kanisa walilofungia ndoa au huelekezwa na kanisa walilofungia ndoa kwa tawi la kanisa hilo lililo karibu nao; huko mchungaji akiwa na wazee wenye hekima huwaita wanandoa na kusuluhisha mgogoro;
▪️
Kama ndoa ilifungwa kwa imani ya uislamu – wanandoa huenda kwa Kadhi ambaye huita pande zote na kujaribu kuzisuluhisha; Kivitendo, mara nyingi wanandoa huenda BAKWATA ambao huwasuluhisha,
▪️
Na ikiwa ndoa ni ya kiserikali au ya kimila, Basi Baraza la Kata mahali wanapoishi wanandoa ndipo usuluhishi hufanyika. Mabaraza ya kata yapo katika kila kata na mara nyingi vikao vyao hufanyika katika majengo ya ofisi ya Afisa mtendaji wa Kata.

Hata kama pande zimepitia kwenye mabaraza ya imani zao za dini, hushauriwa kutumia pia baraza hili la Kata ili kupewa kibali cha kwenda mahakamani na kuepusha mapingamizi ya kisheria na kuweka milolongo isiyo na sababu.



K: UWASILISHAJI WA MAOMBI YA TALAKA MAHAKAMANI
Maombi ya Talaka huwasilishwa mahakamani kwa njia ya hati ya maombi ya talaka (divorce petition).
Uandaaji wa hati ya maombi ya talaka ni wa kitaaluma, kwa hiyo inashauriwa mwanandoa anayetaka kuomba talaka mahakamani awaone wanasheria ili wamsaidie kuandaa hati na kuiwasilisha mahakamani.

Je, Maombi hayo ya talaka yanawasilishwa katika Mahakama ya ngazi ipi?
Mahakama zenye uwezo wa kusikiliza mashauri ya ndoa ni mahakama ya mwanzo, ya wilaya au mahakama Kuu. Hizi zote zina mamlaka sawa ya kupokea shauri la ndoa, kwa hiyo unachagua tu upeleke wapi.

Ushahidi wa Ndoa kuharibika kwa kiwango cha kutowezeka kutengenezeka
Mambo yafuatayo huwa ni ushahidi kuwa ndoa imeharibika kabisa na haiwezi kutengenezeka kuwa kama mwanzo;

  • Uzinzi – ukiwa umefanyika zaidi ya mara moja au ikiwa unaendelea kufanyika licha ya mwenza kuupinga;
  • Sexual Pervesion – yaani matendo ya kingono yasiyo ya kawaida na yasiyokubalika kwa mwenza (spouse);
  • Ukatili wa kihisia au wa kimwili kwa mwenza au kwa watoto wa ndoa;
  • Kutomjali (wilful neglect) kwa makusudi mwenza (spouse);
  • Kumtelekeza mwenza (desertion) kwa miaka 3 na kuendelea;
  • Kutengana (separation) kwa amri ya mahakama au kwa hiyari, ikiwa kutafika miaka 3 na kuendelea;
  • Ikiwa mwenza atahukumiwa kifungo cha miaka 5 na kuendelea gerezani au kifungo cha maisha;
  • Ugonjwa wa akili (mental illness) wa mwenza uliothibitishwa na angalau madaktari 2 na mmoja wa madaktari akiwa ni bingwa (specialized) wa afya ya akili – wakithibitisha kuwa hakuna dalili za mgonjwa kupona;
  • Kubadili dini kwa mwanandoa ikiwa wakati wa kufunga ndoa, wanandoa wote walikuwa ni waamini wa dini moja;


L: KAZI YA MAHAKAMA KUHUSIANA NA TALAKA NA MALI ZA WANANDOA
Ni jukumu la mahakama
👉🏿
kuchunguza na kujiridhisha kuwa kweli ndoa imeharibika na haiwezi kutengamaa tena.

Wakati mwingine mahakama inaweza kuona kuwa ni kweli ndoa imeharibika lakini kuna uwezekano wa kutengenezeka, katika mazingira hayo mahakama haitatoa talaka.

👉🏿
Ni jukumu la mahakama kutoa talaka kwa muombaji

👉🏿
Ni jukumu la Mahakama kufanya mgawanyo wa mali za machumo ya pamoja (matrimonial properties) ikiwa mwombaji ameomba hivyo

👉🏿
Ni jukumu la mahakama kutoa amri ya matunzo ya watoto ikiwa mwombaji atakuwa aliweka maombi haya katika hati ya maombi.

👉🏿
Ni jukumu la mahakama kuelekeza mahali watakapoishi watoto (custody) baada ya kutolewa kwa talaka.

Ni jukumu la mahakama kutoa amri ya kgoni kulipa fidia kwa mwombaji;

MUHIMU:
Mahakama peke yake ndiyo chombo chenye uwezo na mamlaka ya kutoa talaka na kufanya magawanyo wa mali za machumo ya pamoja kwa wanandoa. Baraza la Kata, Kanisani au BAKWATA hawana mamlaka ya kutoa talaka kwa wanandoa au kugawanya mali zao, kazi za mabaraza hayo ni kusuluhisha tu wanandoa ili waendelee na ndoa yao na sio kuvunja ndoa.


M: NINI TOFAUTI YA TALAKA NA AMRI YA UTENGANO?
Talaka ( divorce) inakuwa imehitimisha ndoa iliyokuwepo baada ya siku 30 toka amri ilipotolewa na ikiwa hakuna rufaa; WAKATI
Amri ya Utengano (decree of separation
) ni amri ambayo haibatilishi hali ya ndoa ya wanandoa isipokuwa inatoa zuio la wanandoa hao *kukutana kimwili, kusaidiana na kupeana kampani.

Amri ya utengano ikitolewa, kama hakuna amri ya kutunzana, wanandoa hawatakuwa na jukumu la kutunzana ila bado watatambulika kama wanandoa.

Vipi wanandoa wakipatana na kuzika tofauti zao baada ya amri ya talaka kutolewa?
Je wanaweza kufufua ndoa yao au itabidi waoane upya?

Talaka ikishatoka, na hakuna rufaa iliyofunguliwa na mrufani kushinda, hakuna namna ya kuibatilisha talaka hiyo, na hivyo waliokuwa wanandoa hawataweza kutambulilka kama wanandoa tena, isipokuwa kwa kuoana upya kwa taratibu za kisheria au kwa dhana ya ndoa.

Vipi kwa amri ya utengano (decree of separation)?
Kwa amri ya utengano, mahakama italazimika kutengua amri yake ikiwa wanandoa wote kwa pamoja watawasilisha maombi ya kutenguliwa kwa amri hiyo;

Ikiwa mwanandoa mmoja atawasilisha maombi ya amri ya utengano kutenguliwa, mahakama itatengua amri yake ikiwa itajiridhisha kuwa ilitoa amri hiyo kwa kujielekeza vibaya au kwa makosa ya kuchambua maelezo yaliyotolewa na wanandoa (misrepresentation or mistake of the facts);

N: JE, MAHAKAMA INAWEZA KUTOA AMRI YA MUME KUMTUNZA MKE AU MKE ALIYEMWACHA?
NDIYO
, Wakati ikiwa inatoa amri ya talaka au utengano, Mahakama inaweza kutoa amri ya mume kumtunza mke anayeachana nae, kwa mazingira haya;
  • Ikiwa mume alimtekelekeza mke kwa muda mrefu;
  • Ikiwa mume kwa makusudi, hakumjali mkewe;
  • Wakati kesi ya talaka ikiwa in,aendelea kusikilizwa;
  • Kipindi cha iddat (eda) ikiwa wanandoa ni waislamu na walioana katika uislamu;
  • ikiwa mke alitamkwa kuwa amekufa kwa dhana ya kifo na sasa amepatikana akiwa hai;

Mke pia anaweza kuamriwa kumtunza mumewe ikiwa mume ataonekana ni asiyejiweza kabisa (mlemavu), au mwenye ugonjwa wa akili au ugonjwa mwingine wowote wa kufisha;

Amri hii itakufa pale ambapo mwanandoa tegemezi atakapoolewa na mtu mwingine;
 
O: DHANA YA NDOA (Presumption of Marriage)
Je, Nini maana ya dhana ya ndoa?

Dhana ya Ndoa ni ile hali ambayo watu huitwa wanandoa kwa kuwa wameishi pamoja kama mume na mke kwa kipindi cha miaka miwili na kuendelea;

Wanawake wengi wamekuwa wakiaminishwa vibaya kuwa akikaa na mwanaume kwa miezi 6 tu basi hapo mwanamke anatambulika kama mke halali wa huyo mwanaume, jambo hili si sahihi, sababu Sheria inatambua kipindi cha miaka miwili (2) mfululizo kuishi kama mke na mume, hapo ndipo dhana ya ndoa hutambulika.

Dhana ya Ndoa humalizikaje? Je nayo huombewa talaka?
HAPANA
, dhana ya ndoa huvunjwa na mahakama kwa kutolewa kwa amri ya kubatilisha dhana hiyo (decree of annulment) na sio talaka. Talaka hutolewa kwa wanandoa rasmi tu.

Vipi kuhusu mali na mgawanyo wa watoto waliopatikana katika dhana ya ndoa?
Mgawanyo wa mali, na uangalizi wa watoto pamoja na matunzo yao hufanyika kwa kuzingatia mambo yaleyale yanayozingatiwa wakati wa utoaji wa talaka.

P: UANGALIZI WA WATOTO NA MATUNZO YAO:
Wakati wa kutoa talaka au utengano Mahakama ina uwezo wa kuamuru mtoto akae chini ya uangalizi wa baba au wa mama na ikiona mazingira hayaruhusu kwa mtoto kukaa kwa baba au mama yake mzazi, basi inaweza kuamua mtoto akakae kwa ndugu yeyote wa mtoto au kwenye kituo cha kijamii kinacholea watoto;

Mahakama katika kuamua ukaaji wa watoto huzingatia maslahi ya mtoto kwa kuangalia;
  • Maombi ya wazazi wenyewe;
  • Maombi ya mtoto ikiwa ana umri wa kuweza kujielezea;
  • Mila na desturi za mahali wanapoishi wanandoa;
Mtoto wa umri chini ya miaka saba hudhaniwa kuwa ni vyema akikaa kwa mama yake, ingawa sio lazima akae huko kulingana na mazingira yatakavyokuwa;

Sambamba na hilo, mahakama itaangalia:
  • Haki za kimasomo za mtoto, kama kumhamisha kutaharibu masomo yake au la;
  • Itaweka utaratibu wa mzazi aliyenyimwa uangalizi kumtembelea mtoto huyo;
  • kuweka zuio la mtu aliyepewa uangalizi wa mtoto kutoka naye nje ya Tanzania bila ruhusa ya mzazi mwenza na pia ya Mahakama.


Q: DHANA YA KIFO (Presumption of death):
Wakati mwingine watu hupotea na kutopatikana waliko au habari zao, jamii hufikia kuamua kuwa mtu huyo alishakufa huko alikopotelea na baadhi ya jamii hufanya ibada ya mazishi kana kwamba wana mwili wa huyo mtu (marehemu). Hii fikra ndio inayoitwa dhana ya kifo

Kisheria, mtu asipowasiliana na mtu yeyote ambaye kwa kawaida wangepaswa kuwasiliana mfano baba, mke, kaka nk kwa kipindi cha miaka 5 na zaidi, basi kutakuwa na dhana kuwa mtu huyo alikwishafariki dunia.


R: MAKOSA YA JINAI YAHUSIANAYO MAMBO YA NDOA
  • Ukizuia isivyo kisheria kufungwa kwa ndoa ambayo wanandoa tarajiwa wamepitia hatua zote na wana sifa za kufunga ndoa, ama ukienda kufanya vituko kwenye sherehe ya harusi ya wanandoa kwa lengo la kuwadhalilisha au kuwafedhehesha unakuwa umefanya kosa la jinai na likithibitishwa unaweza kuapata adhabu ya kifungo cha miezi 3 jela.

  • Kuolewa na mtu ambaye uhusiano wake umekatazwa kisheria;

S: Sheria za Kimila za mwaka 1963 – Tangazo la Serikali (GN.) Na. 279 la 1963
Hizi zilipangwa kutumika katika wilaya za Handeni, Kahama, Kondoa, Lushoto, Musoma, Ngara na Pangani – Lakini kwa sasa zinachukuliwa kutumika kwa jamii yote Tanzania.

Vipi sasa watu wakikaa pamoja bila ndoa na kuamua kutengana kabla miaka 2 haijafika?
Ikiwa watu watakua na mahusiano ya kimapenzi yenye muelekeo wa kindoa, wakakaa pamoja na kuvunja mahusiano yao kabla ya miaka 2 ambayo wangetambulika kuwa wanandoa ksheria (kwa dhana ya ndoa) basi mali walizochuma pamoja hutambulika kama mali za ushirika ( partnership properties).

Mali hizi za ushirika hugawanywa na Baraza la Kata kwa kuzingatia taratibu za kijamii za mahali husika. Kwa kuwa sheria ya kimila iliyorasimishwa ni hili tangazo la Serikali namba 279 la 1963, basi ndio linalozingatiwa wakati wa ugawaji. Mgao huwa ifuatavyo:

👉🏿
Mifugo, vyakula vilivyomo ghalani, mazao ya biashara, mazao ambayo hayajavunjwa, hugawanywa sawa sawa kwa hao watu wawili.
👉🏿
Nyumba hupewa mwanamume na mwanamke huchukua vyombo vya jikoni.
👉🏿
Baada ya mavuno, shamba huwa mali ya mume.
👉🏿
Kila mtu atachukua vitu vyake binafsi anavyovimiliki kama vile nguo mapambo n.k. pamoja na zawadi alizopokea toka kwa mwenziwe.

▪️
Kama mwanamke amemfuata mwanamume katika nyumba yake na wakaishi pamoja na kama wote wawili wameshirikiana kuendesha kazi hapo kwao na kupata mali, ama kama wote walikuwa na kazi rasmi, basi mwanamke ana haki ya kupata robo ya vitu vyote au mali zote zilizopatikana kwa msaada wake isipokuwa vitu vyake mwenyewe (mali binafsi)
▪️
Kama mwanaume amemfuata mwanamke katika nyumba yake na wakachuma mali pamoja, ana haki ya kupata robo ya vitu vyote vilivyopatikana kwa msaada wake isipokuwa vitu vyake binafsi.


T: MIRATHI

Hili ni somo pana ambalo litahitaji siku nyingine kulizungumza, ila hapa nitazungumza kwa ufupi sana kuhusu mirathi ya mali za marehemu kwa wajane na watoto.

Je, ikiwa anayefariki ni mume, kina nani wanastahili kuwa warithi wake?
Sheria inasema kuwa warithi ni wale watu walioandikwa katika wosia wa marehemu. Ikiwa marehemu hajaacha wosia, basi watu wa karibu ya marehemu (ndugu) wanaweza kuwa warithi wake. Watu hao ni mke, watoto, wazazi na wengine ikiwa ni pamoja na wale waliomuuguza kipindi cha mwisho cha uhai wake.

Je, ni kila mke anayeweza kurithi mali za marehemu (mume)?
Hapana
. Sio kila mke atakuwa na uhalali wa kurithi mali za marehemu, bali ni mke halali tu wa marehemu ndiye atayeweza kurithi.

Ikiwa wamejitokeza wake wawili wa marehemu na wote wana vyeti vya ndoa, yupi atakuwa ni mke halali?
Ikiwa ndoa ilikuwa ni ya mke mmoja, mke aliyeolewa kwanza ndio atakua halali na ndiye atakastahili kurithi. Huyu mwingine hatahesabika kama mke wa marehemu bali kama hawara tu. Ikiwa walichuma pamoja na marehemu basi atapata mali hizo kwa mtindo wa ushirika (partnership) na sio kwa mtindo wa mirathi.

Je, watoto waliozaliwa hapo kwenye ndoa inayoonekana kuwa ni haramu, watahesabiwa urithi?
Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 (The Law of the Child Act, CAP 13 R.E 2019) , watoto hawa wataweza kutumia na kufurahia mali za baba yao, sheria hiyo haijawekwa wazi kama wataweza kurithi (kumiliki) pindi baba atakapokufa. Maamuzi ya karibuni ya mahakama kuu ya Tanzania chini ya Jaji Mlyambina yalionesha kuwa watoto hawa (maarufu kama haramu) wanaruhusiwa kurithi mali za marehemu baba yao.

Hata hivyo maamuzi haya bado yanaendelea kufanyiwa tathmini ya kisheria kwa kuwa tayari kulikuwa na maamuzi ya Mahakama ya Rufaa ambayo yalitamka wazi kuwa mtoto wa nje ya ndoa hawezi kurithi isipokuwa tu kama baba wa mtoto huyo alimkomboa huko kwao na kumtambulisha kwenye ukoo wake kwa tamaduni za ukoo husika, na kwamba mtoto huyo alikuwa akihusika na shughuli za kijamii kwa ukoo wa baba yake.

Mahakama ya Rufaa kupitia kesi ya VIOLET ISHENGOMA KAHANGWA AND JOVIN MUTABUZI v THE ADMINISTRATOR GENERAL AND MRS. EUDOKIA KAHANGWA 1990 TLR 72 (CA) - (KISANGA JJA, MAKAME JJA na MFALILA JJA) iliamua kuwa mtoto haramu anaishia kufurahia mali za baba yake mpaka pale baba yake atakapofariki dunia na hataweza kugusa mali hizo mara baada ya kifo cha baba yake. Wazee wa Mahaka ya Rufaa wakasema kama baba anapenda mwanae wa nje ya ndoa asisumbuliwe pindi yeye baba atakapokufa, basi amfanyie mwanae mambo yote akiwa hai, maana hakuna mtu anayeweza kumzuia baba kufanya vitu kwa mwanawe. Hukumu hiyo mpaka leo hii haijabatilishwa, hivyo ndio msimamo wa Sheria Tanzania.

Ahsanteni sana ninaishia hapa.
Ninakaribisha maoni, mjadala, maswali, ufafanuzi, nyongeza nk ruksa kuja DM na Whatsapp
 
Kuna maelezo mengi umechanganya kwa uandishi, labda kwa sababu ya kukopi na kupesti
 
Sasa za kimila kwenye ulimwengu wa kisasa zinakua halisi kweli?
 
Back
Top Bottom