Ushujaa na ukibaraka wa viongozi wa mwanzo wa Afrika

Comred Mbwana Allyamtu

JF-Expert Member
Jun 28, 2016
351
863
USHUJAA NA UKIBARAKA WA VIONGOZI WA MWANZO WA AFRIKA.

Na Comred Mbwana Allyamtu CMCA
Wednesday-9/11/2022
Mount Kilimanjaro, Tanzania

Mapema miaka ya 1920 mpaka 1975 Afrika ilichukua sura mpya, mageuzi mengi yaliivaa Afrika, kwanza ni vuguvugu la ukombozi (liberation of Africa), Pili ni harakati za uafrika na kudai uhuru (Africanism and Afrocentric nationalism), Tatu ni mageuzi ya muelekeo wa Dunia (Decolonization of Africa), Nne ni kuibuka kwa ushawishi mkubwa kwa ulimwenguni wa kijamaa (World of Socialism) na mengine mengi ambayo kwa namna moja au nyingine yaliathiri mueleko wa Afrika.

Sura hii iliibua Viongozi wakuu wa uhuru Afrika (Africa founding fathers) ambao kwa namna moja au nyingine waliibadirisha Afrika kutoka kuwa bara milikiwa (colonial State) mpaka kuwa nchi HURU (independent states).

Pamoja na Changamoto kadhaa lakini viongozi walifanikiwa kupindua utawala wa mataifa ya kibeberu mpaka kuleta mageuzi ya uhuru wa kisiasa, baada ya uhuru Changamoto nyingi sana ziliibuka na kuzalisha kile kilichoitwa "Zombwe la kibepari (Ukoloni Mamboleo)"

Viongozi kadhaa ambao majina yao yataandikwa kwa wino Afrika kwa miaka mingi walileta mchango mkubwa sana katika ukombozi wa kifikra, utu, utengamano na kuwaunganisha waafrika katika kufikia dhamila ya kijikomboa.

Kwanza, nataka niseme kuwa viongozi hao, ni tunu, wengi wao heshima zao ni kubwa mno duniani na hata kwa vizazi vyetu huku baadae.

Pili, si viongozi wote waliokuwa katika ukombozi wa kwanza wa Afrika walikuwa mahiri katika kupata uhuru, yani baadhi ya viongozi hao hawakuwa na haiba na ukubwa baada ya uhuru, maana wengine walibadirika nakuwa vibaraka na vikaragosi wa wazungu na mataifa ya kibeberu.

Wengine waligeuka na kuwa madikteta uchwara, waligeuza nchi kuwa mahala pa kujinufaisha.

Wengine kadhaa wakawa wabinafsi, walafi na kutaka kuishi maisha ya kizungu ambayo waliishi watawala wa kikoloni enzi za Ukoloni mkongwe, kundi hili halikufanya chochote kwenye nchi zao, bali waligeuza nchi zao kuwa masikini wa kutupa ndani ya ufukara wa kunuka.

Kundi jingine walikuwa wazarendo, kundi hili lilipata misukosuko mingi ikiwemo kuuwawa, kupinduliwa na hata kulazimishwa kulegeza misimamo yao ya kuilinda Afrika.

Tukumbuke kuwa Vichocheo vya uhuru kwa Afrika vilikuwa vya ndani na nje ya Afrika, Shinikizo la nje lilikuwa mageuzi ya mwelekeo wa ulimwengu (haswa mtazamo wa Ulaya juu ya makoloni yao Afrika) msukumo huu ulichagizwa na Marekani baada ya Vita vya pili vya Dunia, kupitia ile azimo la Atlantic la "Atlantic charter of 1941" ambalo ndio lilo unda Umoja wa Mataifa UN.

Pitia hapa kupata kuona namna hii ilivyo chagiza Afrika kupata uhuru... Atlantic Charter - Wikipedia

Basi bwana...

Kama nilivyosema awali, kuwa Viongozi wengi wazuri wa Kiafrika waliuawa au kupinduliwa na viongozi wabaya, hawa viongozi wabaya waliirudisha Afrika gizani kwa mgongo wa ubepari na msaada wa mataifa ya kibeberu.

Chaguo bora kwa kiongozi kuepuka kuuwawa au kupinduliwa ilikuwa ni kukaa bila kuegemea upande wowote.

Vita Baridi, nayo ikaleta mabadiriko kwenye mfumo mzima wa Siasa za dunia hasa Afrika, mivutano mikali ilitokea katika Dunia kuigombania Afrika, viongozi wengi walio egemea siasa za kijamaa waliuwawa, wachache waliponea chupuchupu lakini mataifa yao yalibaki taabani kiuchumi.

Viongozi kadhaa ambao walihisi kuwa vyama vya upinzani vinafadhiliwa na mataifa yenye nguvu huko ng'ambo ama Urusi, Marekani au mataifa yaliyokuwa ya Ulaya, walilazimisha mara nyingi mfumo wa chama kimoja cha kisiasa ili kupunguza hatari ya kuuwawa na kuingiliwa na mataifa ya nje.

Kwa ujumla wake ni kuwa nchi ambazo zilijipatia uhuru kupitia vita vya uhuru ziliishia kuwa na ombwe la madikteta wakatili Isipokuwa nchi ya Algeria pekee ndio ilisalimika na hilo.

Kati ya nchi 54 barani Afrika, ni nchi 11 zilizopata uhuru kupitia vita vya uhuru, Waliobaki walipata uhuru wao kupitia kura za maoni na njia nyinginezo zikiwepo za maridhiano au kugawa madaraka kwa vyama tanzu na Ukoloni.

Mpaka sasa kuna visiwa 10 kwenye bara la Afrika bado vinashikiliwa na mataifa ya kibeberu.

Nchi ya mwisho kupata uhuru kutoka kwenye mikono ya mataifa ya kibeberu ya Ulaya ni Namibia.

Sasa nataka nikupitishe Afrika nikuoneshe aina ya viongozi wa Afrika na Haiba ya ukombozi kwa mgawanyo wa viongozi mashujaa na wale vibaraka.

Tuanzie hapa.....

Angola...

Angola ilipata uhuru kupitia vita, Sura ya uhuru wa Angola ni António Agostinho da Silva Neto, ndio sura ya uhuru wa Angola, alizaliwa tarehe 17 Septemba 1922 na kufariki tarehe 10 Septemba 1979, alikuwa mwanasiasa na mshairi wa Angola.

Aliwahi kuwa rais wa kwanza wa Angola kuanzia mwaka 1975 hadi 1979, akiwa ndie kiongozi wa chama cha Popular Movement for the Liberation of Angola (MPLA) katika vita vya kupigania uhuru mwaka 1961 hadi mwaka 1974.

Hadi kifo chake, aliongoza chama cha MPLA katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mpaka mwaka 1975, vita hiyo ilikoma mwaka 2002 baada ya Jonas Savimbi kuuwawa.

Alikuwa mkomunisti aliyeponea chupuchupu kwenye ndoano za mabeberu, alipingwa na Marekani na mabeberu wote duniani, alipewa ushirika na Cuba na Urusi, Marekani iliongiza gege la UNITA kumpinga kwakua alifuata sera za kijamaa.

Anajulikana pia kwa shughuli zake za fasihi, anachukuliwa kuwa mshairi mashuhuri wa Angola, Siku yake ya kuzaliwa inaadhimishwa kama Siku ya Kitaifa ya Mashujaa, ni sikukuu ya umma nchini Angola, Mwili wake umehifadhiwa katika makumbusho jijini Luanda, tarehe ya kumbukumbu ya uhuru, kifo chake, mwisho wa vita na tarehe ya uzao wake makumbusho hiyo ufunguliwa wazi watu kwenda kutoa heshima.

Benin...

Benin, sura ya uhuru wa Benin ni Coutoucou Hubert Maga, Coutoucou alizaliwa mwaka 1916 na kufariki mwaka 2010, alianzisha chama cha "Rassemblement Démocratique du Dahomé" mwaka 1951, na kudai uhuru katika kuiongoza Benin, zamani iliitwa Dahomey, katika kuipatia uhuru august 1 1960.

Hurbert Maga ni kiongozi aliyokuwa mstari wa mbele katika kilimo, alihimiza vijana wote nchi nzima kwenda kulima mashamba ya umma ya Taifa, alipendelea mfumo wa ujamaa usio elemea siasa za kikoministi.

Mapema mwaka 1963, Maga alishutumiwa kumuua mpinzani wake mkubwa Christophe Bokhiri ambae alikuwa amemuachia kutoka gerezani siku chache nyuma, kufatia kifo hicho maandamano yalizuka nchi nzima.

Maandamano yakawa makubwa na hatimae mnadhimu mkuu wa jeshi (Chief of Staff of the Dahomeyan Army), Christophe Soglo, akafanya mapinduzi ya kumuondoa Maga madarakani mwezi 10.

Botswana...

Botswana, sura ya uhuru wa Botswana ni Sir Seretse Goitsebeng Maphiri Khama, GCB, KBE, alizaliwa tarehe 1 Julai 1921 na kufariki tarehe 13 Julai 1980, huyu alikuwa mwanasiasa wa Botswana ambaye aliwahi kuwa Rais wa kwanza wa Botswana, wadhifa alioshikilia kuanzia mwaka 1966 hadi kifo chake mwaka wa 1980.

Sir Seretse Goitsebeng Maphiri Khama anasifika kwa kuimarisha demokrasia nchini Botswana, alikuwa mwansiasa aliyeelemea kwenye siasa za ubepari.

Burknabe....

Burkina Faso, (zamani iliitwa Upper Volta) sura ya uhuru wa Burkina Faso ni Maurice Yaméogo alizaliwa tarehe 31 Desemba 1921 na kufariki tarehe 15 Septemba 1993.

Alikuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Upper Volta, ambayo sasa inaitwa Burkina Faso, kuanzia mwaka 1959 hadi 1966, Burkina Faso ilipata uhuru kupitia mageuzi yaliyotakiwa na Marekani baada ya Vita vya pili vya Dunia kama sehemu ya azimo la Atlantiki la mwaka 1941 iliyounda UN.

Katika azimo lile lilitaka nchi za Ulaya kutoa haki ya kujitawala kwa makoloni yao, ili wapatiwe unafuu wa mikopo ya kifedha, Hivyo Ilibidi kura ya maoni ifanyike, vyama viundwe, iundwe jamhuri na rais achaguliwe.

Pitia hii shajara ya Loi-Cadre-Deffere... Loi-cadre Defferre - Wikipedia

Cabo Verde...

Sura ya uhuru wa Cabo Verde ni Aristides Maria Pereira, alizaliwa tarehe 17 Novemba 1923 na kufariki tarehe 22 Septemba 2011, alikuwa mwanasiasa wa Cape Verde.

Huyu ndie alikuwa Rais wa kwanza wa Cape Verde, akihudumu kutoka mwaka 1975 hadi 1991.

Cameron...

Sura ya uhuru wa Cameron ni Ahmadou Babatoura Ahidjo alizaliwa tarehe 24 Agosti 1924 na kufariki tarehe 30 Novemba 1989, alikuwa mwanasiasa wa Kameruni ambaye alikuwa Rais wa kwanza wa Kamerun, akishikilia wadhifa huo kuanzia mwaka 1960 hadi 1982.

Ahidjo alichukua jukumu kubwa katika kulinda uhuru wa Kameruni hasa katika kuiunganisha eneo la Kameruni wanao zungumza kifaransa na kuwaunganisha wakameruni wanao zungumza Kiingereza.

Wakati wa muda wa Ahidjo madarakani, alianzisha mfumo wa kisiasa kufuta matabaka katika nchi, ili kufanikisha hilo akaanzisha nchi ya chama kimoja chini ya Muungano wa Kitaifa wa Cameroon (CNU) mwaka wa 1966.

Lakini mnamo mwaka 1972, Ahidjo alifuta shirikisho la Cameron ya kifaransa na kingereza na kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa ya kingereza, mpango huu ndio ulibadilika kuwa kuni kwake, ulimfanya apinduliwe.

Jamuhuri ya Afrika ya kati...

Sura ya uhuru wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) ilikuwa ni David Dacko alizaliwa mwaka 1927 na kufariki tarehe 21 Novemba 2003, alikuwa mwanasiasa wa Afrika ya Kati ambaye aliwahi kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuanzia tarehe 14 Agosti 1960 hadi 1 Januari 1966.

Na pia Rais kuanzia Septemba 21, 1979 hadi Septemba 1, 1981, Baada ya kuondolewa madarakani kwa mara ya pili katika mapinduzi yaliyoongozwa na Jenerali André Kolingba, alijishughulisha na siasa kama mwanasiasa wa upinzani na mgombea urais akiwa na wafuasi wengi lakini hakuwahi kushinda tena.

Dacko alikuwa mwanasiasa aliyedumu kwenye kisiasa ya nchi yake kwa zaidi ya miaka 50.

Chad...

Sura ya uhuru wa Chad ni François Tombalbaye (Kiarabu: فرنسوا تومبالباي Franswā Tūmbālbāy) alizaliwa tarehe 15 Juni 1918 na kufariki tarehe 13 Aprili 1975, anajulikana pia kama N'Garta Tombalbaye, alikuwa mwalimu wa Chad na mwanaharakati wa chama cha wafanyakazi ambaye aliwahi kuwa Rais wa kwanza wa Chad.

Alikuwa Kiongozi wa serikali ya kikoloni ya Chad na chama chake, Chama cha Maendeleo cha Chad, baada ya mwaka 1959, Tombalbaye aliteuliwa kuwa mkuu wa serikali ya taifa hilo baada ya uhuru wake tarehe 11 Agosti 1960.

Alitawala kama dikteta hadi alipotolewa madarakani na kuuawa na wanajeshi wa Chad Katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1975.

Comoro...

Sura ya uhuru wa Comoro ni Ahmed Abdallah Abderemane, au Ahmad Abd Allah Abd ar-Rahman, alizaliwa tarehe 12 Juni 1919 na kufariki tarehe 26 Novemba 1989, alikuwa mwanasiasa wa Comoro.

Alikuwa mjumbe wa Seneti ya Ufaransa kutoka mwaka 1959 hadi 1973, na Rais wa Comoro kutoka tarehe 25 Oktoba 1978 alipo pinduliwa aliishi Comoro hadi kifo chake mnamo mwaka 1989.

DRC....

Sura ya uhuru wa Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya (DRC) ni Joseph Kasa-Vubu, huyu ni Raisi wa kwanza wa Kongo DRC lakini alikuwa kibaraka wa Uberigiji na Marekani.

Alizaliwa mwaka 1915 na kufariki tarehe 24 Machi 1969, alikuwa mwanasiasa wa Kongo ambaye aliwahi kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutoka mwaka 1960 hadi mwaka 1965, alikuwa raisi aliyepachikwa na waberigiji kwa upendeleo wa chama chake cha kikabila cha ABAKO.

Kasavubu alitumiwa na mabeberu kama kinga ya kuizuia Kongo kudumkia kwenye mikono ya ukomunisti, alipoonekana zaifu mabeberu wakamtumia Joseph Mobutu (Mobutu Seseseko Kuku Ngwendu Wazabanga) Kumuondoa Kasavubu na kukaa yeye ili kuifanya kazi ya mabeberu.

Tishio kubwa la Kongo ilikuwa ni Patrice Lumumba na chama chake cha MNC.

Huyu Lumumba ni Sura nyingine ya uhuru wa Kongo, Patrice Emily Lumumba, ndie Waziri mkuu wa kwanza wa Kongo DRC, aliponzwa na misimamo yake ya Afrkanzasheni (Africazation) na ukomunisti, huyu aliuwawa na mabeberu baada ya kuwa na siasa za mrengo wa kikoministi wa Urusi.

Mpango wa kuuwawa kwake ulipewa jina (codename) Operation Barracuda (Yani misheni ya samaki wakubwa kumeza samaki wadogo)

Jamuhuri ya Kongo Brazzaville...

Sura ya uhuru wa Jamhuri ya Kongo ni Abbé Fulbert Youlou, huyu mwamba alikuwa ni Askofu, alizaliwa tarehe 29 Juni, 17 Juni au 19 Julai 1917 na kufariki tarehe 6 Mei 1972.

Huyu alikuwa ni kasisi wa Kanisa Katoliki la Brazzaville-Kongo, kanisa katoliki lilimpendekeza kuwa raisi wa Kongo Brazzaville ili kulinda masrahi yao kule, Ufaransa ilikubali azimio la Venice la kumfanya Abbé Fulbert Youlou kuwa raisi ili kudhibiti ukomunisti usiene eneo la Afrika ya Kati.

Alikuwa ni kiongozi wa chama cha kitaifa cha Kongo na mwanasiasa ambaye alikua Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kongo Brazzaville.

Côte d'Ivoire....

Sura ya uhuru wa Ivory coast ni Félix Houphouët-Boigny alizaliwa tarehe 18 Oktoba 1905 na kufariki tarehe 7 Desemba 1993, pia aliitwa jina lingine la "Papa Houphouët au Le Vieux ("Mzee").

Alikuwa rais wa kwanza wa Ivory Coast, akihudumu toka mwaka 1960 hadi kifo chake mwaka 1993.

Alikuwa ni Chifu wa kabila, alifanya kazi kama msaidizi wa matibabu na baadae kama kiongozi wa muungano kabla ya kuchaguliwa katika Bunge la Ufaransa.

Alihudumu katika nyadhifa kadhaa za mawaziri ndani ya serikali ya Ufaransa kabla ya kuiongoza Côte d'Ivoire baada ya uhuru mwaka 1960.

Katika maisha yake yote, alikuwa na mchango mkubwa katika siasa za ukombozi na kuondoa ukoloni wa Afrika.

Djibouti...

Sura ya uhuru wa Djibouti ni Hassan Gouled Aptidon (Kisomali: Xasan Guuleed Abtidoon; Kiarabu: حسن جوليد أبتيدون) alizaliwa Oktoba 15, 1916 na kufariki tarehe 21 Novemba 2006, huyu ndie Rais wa kwanza wa Djibouti kutoka mwaka 1977 hadi 1999.

Misri...

Sura ya uhuru wa Misri ni Mfalme Fuad I ambaye alitangaza uhuru kutoka kwa Uingereza kupitia mapinduzi ya Misri ya mwaka 1919

Equatorial Guinea.....

Sura ya uhuru wa Equatorial Guinea ni Francisco Macías Nguema jina lake halisi ni Masie Nguema Biyogo Ñegue Ndong, alizaliwa tarehe 1 Januari 1924 na kufariki tarehe 29 Septemba 1979, mara nyingi huitwa Macías, alikuwa mwanasiasa wa Equatorial Guinea ambaye aliwahi kuwa Rais wa kwanza wa Guinea ya Ikweta kutoka uhuru wa nchi hiyo mnamo 1968 hadi kupinduliwa mwaka 1979.

Anakumbukwa sana kama mmoja wa madikteta katili zaidi katika historia ya Equatorial Guinea, Equatorial Guinea ilipata uhuru kupitia vita.

Eswatini......

Sura ya uhuru wa Eswatini (zamani iliitwa Swaziland) ni Mfalme Sobhuza II, KBE, pia inajulikana kama Nkhotfotjeni au Mona alizaliwa tarehe 22 Julai 1899 na kufariki tarehe 21 Agosti 1982, alikuwa Chifu Mkuu na baadaye Ngwenyama wa Swaziland kwa miaka 82 na siku 254, ndio ufalme mrefu zaidi duniani unaoweza kuthibitishwa wa mfalme yeyote katika historia iliyorekodiwa.

Sobhuza alizaliwa tarehe 22 Julai 1899 katika Makazi ya Kifalme ya Zombodze, yeye ni mwana wa Inkhosikati Lomawa Ndwandwe na Mfalme Ngwane V.

Alipokuwa na umri wa miezi minne tu, baba yake alikufa ghafla wakati akicheza incwala, Sobhuza alichaguliwa kuwa mfalme mara baada ya hapo mama yake Labotsibeni na mjomba wake Prince Malunge waliongoza taifa la Swaziland hadi Sobhuza alipo kuwa mkubwa mwaka 1921.

Sobhuza aliongoza Swaziland kupitia uhuru hadi kifo chake mwaka 1982.

Alilithiwa kwa kufuatiwa na Mswati III, mtoto wake mdogo ambae jina lake halisi ni Inkhosikati Ntfombi Tfwala, aliye tawazwa mwaka 1986.

Gabon....

Sura ya uhuru wa Gabon ni Gabriel Léon M'ba alizaliwa tarehe 9 Februari 1902 na kufariki tarehe 28 Novemba 1967, alikuwa mwanasiasa wa Gabon ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa kwanza (1959-1961) na Rais wa kwanza (1961-1967) wa Gabon.

Gambia....

Sura ya uhuru wa Gambia ni Sir Dawda Kairaba Jawara GCMG, alizaliwa tarehe 16 Mei 1924 na kufariki tarehe 27 Agosti 2019, alikuwa mwanasiasa wa Gambia ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu kutoka mwaka 1962 hadi 1970, na kisha kama Rais wa kwanza wa Gambia kutoka mwaka 1970 hadi 1994.

Soma shajara yake hii kupitia hii Link

Ghana....

Sura ya uhuru wa Ghana ni Kwame Nkrumah, huyu aliiongoza Ghana kupata uhuru kupitia shinikizo la amani na kura ya maoni na uchaguzi.

Huyu alipinduliwa mwaka 1966 kupitia "Operation Cold Chop" baada ya kuonekana ni mwiba kwa mataifa ya magharibi.

Guinea...

Sura ya uhuru wa Guinea ni Ahmed Sékou Touré, ile hospital ya mkoa wa Mwanza imepewa jina kutoka kwake, huyu amefariki tarehe 26 Machi 1984, alikuwa kiongozi wa kisiasa wa Guinea na mwanasiasa wa Kiafrika ambaye alikua rais wa kwanza wa Guinea.

Akihudumu kuanzia 1958 hadi kifo chake mwaka 1984, Aliongoza Guinea kupata uhuru kupitia shinikizo la amani, kura ya maoni na uchaguzi, Touré alikuwa miongoni mwa wazalendo wa awali wa Guinea waliohusika katika kudai uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa Ufaransa.

Guinea Bissau...

Sura ya uhuru wa Guinea-Bissau ni Luís Severino de Almeida Cabral, huyu alizaliwa tarehe 11 Aprili 1931 na kufariki tarehe 30 Mei 2009, huyu alikuwa mwanasiasa wa Bissau-Guinea ambaye pia alikuwa Rais wa kwanza wa Guinea-Bissau.

Alihudumu kutoka mwaka 1974 hadi 1980, wakati mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na João Bernardo Vieira yalipomwondoa madarakani.

Luís Cabral alikuwa kaka wa kambo wa Amílcar Cabral mwasisi wa uhuru wa Guinea Bissau, Luìs alianzisha Chama cha Kiafrika cha Uhuru wa Guinea na Cape Verde (PAIGC) mnamo 1956 na kaka yake Amilcar Cabral.

Kenya....

Sura ya uhuru wa Kenya ni Jomo Kenyatta alizaliwa mwaka 1897 na kufariki tarehe 22 August 1978, alikuwa mwanaharakati wa kupinga ukoloni wa Kenya na mwanasiasa ambaye alitawala Kenya kama Waziri Mkuu kutoka mwaka 1963 hadi 1964 na kisha kama Rais wake wa kwanza kutoka mwaka 1964 hadi kifo chake mwaka wa 1978 kilicho tokea huko Mombasa akiwa usingizini.

Aliongoza chama cha Kenya African National Union (KANU) kuanzia 1961 hadi kifo chake.

Lesotho....

Sura ya uhuru wa Lesotho ni Chifu Sekhonyana Nehemia Maseribane, alizaliwa tarehe 4 Mei 1918 na kufariki tarehe 3 Novemba 1986, aliwahi kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Basutoland (sasa Lesotho) kutoka tarehe 6 Mei 1965 hadi tarehe 7 Julai 1965.

Liberia....

Sura ya uhuru wa Liberia ni Joseph Jenkins Robert, huyu alitokea Marekani na kuanzisha taifa la Liberia mwaka 1847.

Ndio mwanadamu wa kwanza kutumikia cheo cha uraisi ndani ya aridhi ya Afrika.

Libya.....

Sura ya uhuru wa Libya ni Mwana Mfalme Muhammad Idris bin Muhammad al-Mahdi as-Senussi, alikuwa ni Emir wa Cyrenaica na mtawala wa kwanza wa Libya huru iliyo kombolewa kutoka mikononi mwa Italia.

Wa pili ni Gaddafi aliyeongoza mapinduzi ya kumpindua mfalme Idris mwaka 1966.

Pitia shajara hii... Idris of Libya - Wikipedia

Madagascar....

Sura ya uhuru wa Madagascar ni Philibert Tsiranana aliye zaliwa tarehe 18 Oktoba 1912 na kufariki tarehe 16 Aprili 1978, alikuwa mwanasiasa na kiongozi wa Madagascar, ambaye aliwahi kuwa Rais wa kwanza wa Madagaska kuanzia 1959 hadi 1972 alipo pinduliwa.

Malawi....

Sura ya uhuru wa Malawi ni Hastings Kamuzu Banda alizaliwa mwaka 1898 au 1906/1907 na kufariki tarehe 25 Novemba 1997, alikuwa waziri mkuu na baadaye rais wa Malawi kuanzia 1964 hadi 1994, ilipopata uhuru mwaka 1964, Malawi ilikuwa chini ya Uingereza.

Mnamo mwaka 1966, nchi ikawa jamhuri na akawa rais, Utawala wake unajulikana kama "utawala wa kiimla uliokandamiza sana umma hasa wapinzani wake."

Mali......

Sura ya uhuru wa Mali ni Modibo Keïta alizaliwa tarehe 4 Juni 1915 na kufariki tarehe 16 Mei 1977, alikuwa Rais wa kwanza wa Mali (1960-1968) na Waziri Mkuu wa Shirikisho la Mali.

Aliunga mkono aina ya ujamaa wa Kiafrika ambao ulimponza na kupinduliwa madarakani.

Maulitania...

Sura ya uhuru wa Mauritania ni Moktar Ould Daddah (Kiarabu: مختار ولد داداه, ) alizaliwa Desemba 25, 1924 na kufariki Oktoba 14, 2003, alikuwa Rais wa Mauritania kuanzia mwaka 1960, wakati nchi yake ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa, aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi.

Mauritius....

Sura ya uhuru wa Mauritius ni Sir Seewoosagur Ramgoolam, GCMG LRCP MRCS alizaliwa Septemba 18, 1900 na kufariki tarehe 15 Desemba 1985, mara nyingi hujulikana kama Chacha Ramgoolam, alikuwa daktari wa Mauritius, mwanasiasa, na muhafidhina wa ubepari pekee Afrika.

Aliwahi kuwa waziri mkuu pekee wa kisiwa hicho, waziri mkuu wa kwanza, na gavana mkuu wa tano wa Mauritius.

Morocco....

Sura ya uhuru wa Morocco ni Mfalme Mohammed V (Kiarabu: محمد الخامس) alizaliwa tarehe 10 Agosti 1909 na kufariki tarehe 26 Februari 1961, alikuwa Sultani wa Morocco kuanzia mwaka 1927 hadi 1953, alitambuliwa kama Sultani tena aliporudi kutoka uhamishoni mwaka 1955, na kama Mfalme kuanzia 1957 hadi 1961.

Baada ya kifo cha baba yake, Yusef bin Hassan, alirithi kiti cha ufalme, alikuwa mwanachama wa nasaba ya 'Alawi, Morocco Ilipata uhuru kupitia vita vya ifni mwaka 1957.

Soma shajara hii kujua zaidi kuhusu Morocco na vita ya Uhuru ya Ifni... Ifni War - Wikipedia

Msumbiji (Mozambique)...

Sura ya uhuru wa Msumbiji ni Samora Moisés Machel alizaliwa tarehe 29 Septemba 1933 na kufariki tarehe 19 Oktoba 1986, alikuwa kamanda wa kijeshi wa Msumbiji na kiongozi wa kisiasa wa FRELIMO,

Alikuwa ni Msoshalisti katika mlengo wa Umaksi–Leninism, aliwahi kuwa Rais wa kwanza wa Msumbiji kutoka nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1975.

Machel alifariki dunia akiwa madarakani mwaka 1986 katika ajali ya ndege yake ya urais ilipoanguka karibu na mpaka wa Msumbiji na Afrika Kusini.

Ajali hiyo inatajwa kuhusishwa na njama za kibeberu, Msumbiji ilipata uhuru kupitia vita mwaka 1975.

Namibia...

Sura ya uhuru wa Namibia ni Samuel Shafiishuna Daniel Nujoma, alizaliwa tarehe 12 Mei 1929, ni mwanamapinduzi wa Namibia, mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi na mwanasiasa aliyehudumu kwa mihula mitatu kama Rais wa kwanza wa Namibia.

Alikuwa Raisi kuanzia mwaka 1990 hadi 2005.

Nujoma alikuwa mwanachama mwanzilishi na mwanasiasa wa chama cha SWAPO, pia rais wa kwanza wa Jumuiya ya Watu wa Afrika Kusini Magharibi (SWAPO) mwaka 1960.

Kabla ya 1960, SWAPO ilijulikana kama Ovambo People's Organization (OPO), Alichukua nafasi ya kiongozi wa vuguvugu la ukombozi wa kitaifa katika kampeni ya uhuru wa kisiasa wa Namibia kutoka kwa utawala wa Afrika Kusini.

Alianzisha Jeshi la Ukombozi la Watu wa Namibia (PLAN) mwaka 1962 na kuanzisha vita vya msituni dhidi ya serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini mnamo Agosti 1966 huko Omungulugwombashe, kuanzia baada ya Umoja wa Mataifa kuondoa mamlaka ya Afrika Kusini kutawala eneo hilo.

Nujoma aliongoza SWAPO wakati wa Vita vya muda mrefu vya Uhuru wa Namibia, vilivyodumu kutoka 1966 hadi 1989, na hatimae uhuru mwaka 1990.

Niger....

Sura ya uhuru wa Niger ni Hamani Diori alizaliwa tarehe 6 Juni 1916 na kufariki tarehe 23 Aprili 1989, alikuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Niger.

Mnamo mwaka 1946, alianza harakati za ukombozi wakati akifanya kazi kama mwalimu mkuu wa shule katika mji mkuu wa Niger wa Niamey, alikua mmoja wa waanzilishi wa Niger Progressive Party (PPN), tawi la kikanda la African Democratic Rally (RDA).

Baadaye mwaka huo huo, alichaguliwa kuwa mbunge wa Bunge la Kitaifa la Ufaransa.

Katika uchaguzi wa 1951, Diori alishindwa na binamu yake na mpinzani wake wa kisiasa Djibo Bakary, akarudi kuimalisha chama chake cha PPN na hatimae alichaguliwa tena katika bunge hilo mwaka wa 1956, na akachaguliwa kuwa naibu spika.

Mnamo mwaka 1958, baada ya kura ya maoni iliyoiruhusu Niger kujitawala, Diori alikua rais wa serikali ya muda, Kisha akawa Waziri Mkuu mwaka 1959.

Kisha aliteuliwa katika ofisi hiyo tena mwaka wa 1960, Niger ilipopata uhuru, Ingawa rushwa ilikuwa ni sifa ya kawaida ya utawala wake, alipata heshima ya kimataifa kwa nafasi yake kama msemaji wa masuala ya Afrika na kama msuluhishi maarufu katika migogoro mingi hasa mgogoro wa Nigeria, Egypt, Sahalawi na Kongo DRC.

Utawala wake uliisha na kufika kikomo baada ya mapinduzi mnamo mwaka 1974.

Nigeria (Giant of Africa)...

Sura ya uhuru wa Nigeria ni viongozi watano ambao ni Zik, Awolowo, Tafawa Balewa, Michael Okpara, Ahmadu Ibrahim Bello,

Huyu Nnamdi Benjamin Azikiwe, PC, alizaliwa tarehe 16 Novemba 1904 na kufariki tarehe 11 Mei 1996, kwa kawaida hujulikana kama "Zik", alikuwa mwanasiasa wa Nigeria na kiongozi wa kisiasa ambaye aliwahi kuwa Rais wa kwanza wa Nigeria kutoka mwaka 1963 hadi 1966.

Huyu ndie Baba wa uhuru wa Nigeria, anajulikana kama "baba wa taifa wa Nigeria".

Chifu Obafemi Jeremiah Oyeniyi Awolowo GCFR alizaliwa tarehe 6 Machi 1909 na kufariki tarehe 9 Mei 1987 alikuwa mzalendo wa Nigeria na mwanasiasa ambaye alikuwa ni kiongozi wa kimila na kiongozi wa machifu wote ambae alikuwa muhimu katika harakati za uhuru wa Nigeria.

Mwana wa mkulima wa Kiyoruba, na mtu anayeheshimika sana huko Nigeria.

Sir Abubakar Tafawa Balewa KBE PC, alizaliwa Desemba 1912 na kufariki tarehe 15 Januari 1966, alikuwa mwanasiasa wa Nigeria ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa kwanza na wa pekee wa Nigeria baada ya uhuru.

Aliuwawa mwaka 1966 katika vita ya kwanza ya Nigeria iliyotokana na kile kilichoitwa Operation Wi-ti-e Counter Coup (makakati wa laana ya mafuta na ukabila)

Michael Iheonukara Okpara huyu alizaliwa tarehe 25 Desemba 1920 na kufariki tarehe 17 Desemba 1984, alikuwa mwanasiasa wa Nigeria na Waziri Mkuu wa Nigeria Mashariki wakati wa Jamhuri ya Kwanza, kuanzia mwkay 1959 hadi 1966.

Akiwa na umri wa miaka 39, alikuwa Waziri Mkuu mdogo zaidi wa taifa hilo, Alikuwa mtetezi mkubwa wa kile alichokiita "pragmatic socialism" na aliamini kuwa mageuzi ya kilimo yalikuwa muhimu kwa mafanikio ya Umma wa Nigeria.

Ahmadu Ibrahim Bello, huyu alikuwa Sardauna (Emil) wa Sokoto alizaliwa tarehe 12 Juni 1910 na kufariki tarehe 15 Januari 1966, aliyejulikana kama Sir Ahmadu Bello, alikuwa mwanasiasa wa kihafidhina wa Nigeria ambaye aliongoza Nigeria ya Kaskazini kupitia uhuru wa Nigeria mwaka 1960 na aliwahi kuwa waziri mkuu wake wa kwanza wa kaskazini na wa pekee kutoka 1954 hadi kuuawa kwake mwaka 1966.

Rwanda...

Sura ya uhuru wa Rwanda ni Grégoire Kayibanda, huyu mwamba alizaliwa tarehe 1 Mei 1924 na kufariki tarehe 15 Desemba 1976, alikuwa mwanasiasa na mwanamapinduzi wa Rwanda ambaye alikuwa Rais wa kwanza kuchaguliwa wa Rwanda kuanzia mwaka 1962 hadi 1973.

Alikuwa ni muhafidhina wa Kabila la Hutu, alikuwa mwanzilishi wa Mapinduzi ya Rwanda na aliongoza harakati za kupigania uhuru wa Rwanda kutoka Ubelgiji.

Alichukua nafasi ya utawala kutoka kwa ufalme wa Watutsi na kubadili Rwanda kuwa na mfumo wa serikali ya jamhuri.

Rwanda ilipata uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1962, huku Kayibanda akihudumu kama rais wa kwanza wa nchi hiyo, akianzisha sera ya kuwaunga mkono Wahutu na mfumo wa chama kimoja unaosimamiwa na chama chake cha Parmehutu.

Alipinduliwa katika mapinduzi ya kijeshi mwaka 1973 na waziri wake wa ulinzi, Juvénal Habyarimana, na kufariki miaka mitatu baadaye akiwa gerezani alikofungwa, kifo chake kilitokana na njaa ya kunyomwa chakula.

São Tomé...

Sura ya uhuru wa São Tomé na Príncipe ni Manuel Pinto da Costa huyu aliyezaliwa tarehe 5 Agosti 1937 ni mwanauchumi na mwanasiasa wa Santomea ambaye aliwahi kuwa rais wa kwanza wa São Tomé na Príncipe kuanzia 1975 hadi 1991.

Alihudumu tena kama rais kutoka 2011 hadi 2016.

Senegal....

Sura ya uhuru wa Senegali ni Léopold Sédar Senghor amezaliwa tarehe 9 Oktoba 1906 na kufariki tarehe 20 Desemba 2001, alikuwa mshairi wa Senegal, mwanasiasa na mwananadharia wa ujamaa wa kitamaduni ambaye alikuwa rais wa kwanza wa Senegal kuanzia mwaka 1960 hadi mwaka 1980.

Shelisheli....

Sura ya uhuru wa Shelisheli ni Sir James Richard Marie Mancham KBE , alizaliwa tarehe 11 Agosti 1939 na kufariki tarehe 8 Januari 2017, alikuwa mwanasiasa wa Ushelisheli aliyeanzisha Chama cha Kidemokrasia cha Seychelles (DS) na alikuwa Rais wa kwanza wa Ushelisheli kutoka 1976 hadi 1977.

Sierra Leone...

Sura ya uhuru wa Sierra Leone ni Sir Milton Augustus Strieby Margai PC, alizaliwa tarehe 7 Desemba 1895 na kufariki tarehe 28 Aprili 1964, alikuwa daktari wa Sierra Leone na mwanasiasa ambaye aliwahi kuwa mkuu wa serikali ya nchi hiyo kuanzia 1954 hadi kifo chake mwaka 1964.

Alipewa cheo cha waziri mkuu kuanzia 1954 hadi 1960, na kisha waziri mkuu kutoka 1961 na kuendelea. Margai alisomea udaktari nchini Uingereza, na aliporudi nchini Sierra Leone akawa mwanaharakati mashuhuri wa afya ya umma.

Aliingia katika siasa kama mwanzilishi na kiongozi wa chama cha Sierra Leone People's Party.

Margai alisimamia kipindi cha mpito cha Sierra Leone kuelekea uhuru, kilichotokea mwaka wa 1961.

Alifariki akiwa ofisini akiwa na umri wa miaka 68, na akarithiwa na kaka yake Albert.

Sudan...

Sura ya uhuru wa Sudan ni Ismail al-Azhari alizaliwa tarehe 20 Oktoba 1900 na kufariki tarehe 26 Agosti 1969, alikuwa mzalendo na mwanasiasa wa Sudan.

Aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Sudan kati ya 1954 na 1956, na kama Rais wa Sudan kutoka 1965 hadi alipopinduliwa na Gaafar Nimeiry mwaka 1969.

Tanzania...

Sura ya uhuru wa Tanzania -ni Julius Kambarage Nyerere alizaliwa tarehe 13 Aprili 1922 na kufariki tarehe 14 Oktoba 1999, alikuwa mwanaharakati wa kupinga ukoloni, mwanasiasa, na mwananadharia wa siasa za kijamaa.

Aliitawala Tanganyika kama waziri mkuu kuanzia 1961 hadi 1962 na kisha akawa rais kuanzia 1962 hadi 1964, baada ya hapo akaongoza nchi ya Tanzania, kama rais kuanzia 1964 hadi 1985.

Alikuwa mwanachama mwanzilishi na mwenyekiti wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU), na kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi, kuanzia 1977 hadi 1990.

Kiitikadi alikuwa Mzalendo wa Kiafrika na mjamaa wa Kiafrika, aliendeleza falsafa ya kisiasa inayojulikana kama Ujamaa wa kujitegemea, alipata sifa kubwa Afrika kwa kuwa mstari wa mbele katika ukombozi wa Afrika.

Ndio kiongozi aliyesaidia nchi nyingi za Afrika kupata uhuru.

Togo.....

Sura ya uhuru wa Togo ni Sylvanus Épiphanio Olympio alizaliwa tarehe 6 Septemba 1902 na kufariki tarehe 13 Januari 1963, alikuwa mwanasiasa wa Togo ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu na kisha rais wa Togo kutoka 1958 hadi kuuawa kwake mnamo 1963.

Sylvanus anatoka katika familia muhimu sana nchini Togo ya Olympio, ambayo inamjumuisha mjomba wake Octaviano Olympio, ambae ni mmoja ya watu tajiri zaidi nchini Togo katika miaka ya 1900.

Sylvanus Épiphanio Olympio ndio raisi wa kwanza kuuwawa Afrika.

Tunisia....

Sura ya uhuru wa Tunisia ni Habib Bourguiba, Kiarabu tamka الحبيب بورقيبة, alizaliwa tarehe 3 Agosti 1903 na kufariki tarehe 6 Aprili 2000, alikuwa mwanasheria wa taifa la Tunisia toka mwaka 1950 na kiongozi wa taifa la Tunisia mwaka 1957.

Pia amekuwa waziri mkuu wa Ufalme wa Tunisia toka mwaka 1956 hadi mwka 1957…

Na kisha kama rais wa kwanza wa Tunisia (1957-87), Kabla ya urais wake, aliongoza taifa hilo kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa, na kumaliza ukaliwaji na Ufaransa kwa miaka 75.

Huko Tunisia amepewa jina la "Supreme Combatant".

Uganda....

Sura ya uhuru wa Uganda ni Apollo Milton Obote alizaliwa tarehe 28 Desemba 1925 na kufariki tarehe 10 Oktoba 2005, alikuwa kiongozi wa kisiasa wa Uganda aliyeongoza Uganda kupata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Uingereza mwaka 1962.

Kufuatia uhuru wa taifa hilo, aliwahi kuwa waziri mkuu wa Uganda kuanzia 1962 hadi 1966 nal Rais wa Uganda kutoka 1966 hadi 1971, kisha tena kutoka 1980 hadi 1985.

Zambia...

Sura ya uhuru wa Zambia ni Kenneth David Kaunda GCIH SCOT, alizaliwa tarehe 28 Aprili 1924 na kufariki tarehe 17 Juni 2021, pia anajulikana kama KK, alikuwa mwanasiasa wa Zambia ambaye aliwahi kuwa rais wa kwanza wa Zambia kuanzia 1964 hadi 1991.

Alikuwa mstari wa mbele katika harakati za kupigania uhuru katika kwa nchi hiyo na za kusini mwa Afrika.

Kwa kutoridhishwa na uongozi wa Harry Nkumbula wa Northern Rhodesian African National Congress (RANC), alijitenga na kuanzisha chama chake cha Zambian African National Congress, na baadaye United National Independence Party (UNIP).

Zimbabwe....

Sura ya uhuru wa Zimbabwe ni Robert Gabriel Mugabe alizaliwa tarehe 21 Februari 1924 na kufariki tarehe 6 Septemba 2019, alikuwa mwanamapinduzi na mwanasiasa wa Zimbabwe ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Zimbabwe kutoka 1980 hadi 1987 na kisha kama Rais kutoka 1987 hadi 2017.

Aliwahi kuwa Kiongozi wa Umoja wa Kitaifa wa Zimbabwe (ZANU) kuanzia mwaka 1975 hadi 1980 na kukiongoza chama cha siasa kilichorithiwa na ZANU cha Patriotic Front (ZANU–PF), kuanzia mwaka 1980 hadi 2017.

Kiitikadi ni mzalendo wa Kiafrika, na mjamaa, katika miaka ya 1970 na 1980 alijitambulisha kama Mmarx-Leninist, na kama mjamaa kindakindaki.

Baada ya miaka ya 1990 alijitambulisha kama mjamaa wa kiafrika.

Kwa kupata makala Zaidi wasiliana na Mimi WhatsApp 0679555526 uungwe group la Maktaba Kuu kwa gharama ya Tsh 3000/=.

Ukinakili kazi zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
Wako Mjoli wa Historia na diplomasia ya ulimwengu.

Ndimi: Comred Mbwana Allyamtu
Copyrights of this article reserved
written by Comred Mbwana Allyamtu
•Napatika Kwa mawasliano
Comred Mbwana Allyamtu

Kwa Tanzania
+255679555526 (WhatsApp).
+255765026057.
Email- mbwanaallyamtu990@gmail.com

Copyright 2022, All Rights Reserved.

Maktaba Kuu.View attachment 2411429View attachment 2411433View attachment 2411434View attachment 2411431View attachment 2411430View attachment 2411432View attachment 2411435View attachment 2411436
FB_IMG_1667973003232.jpg
FB_IMG_1667973005562.jpg
FB_IMG_1667973008902.jpg
FB_IMG_1667973000665.jpg
FB_IMG_1667972998045.jpg
FB_IMG_1667972995593.jpg
FB_IMG_1667972987165.jpg
FB_IMG_1667972989749.jpg
FB_IMG_1667972961738.jpg
FB_IMG_1667972950156.jpg
FB_IMG_1667972982045.jpg
FB_IMG_1667972984686.jpg
FB_IMG_1667972979248.jpg
FB_IMG_1667972967296.jpg
FB_IMG_1667972959219.jpg
FB_IMG_1667972955600.jpg
FB_IMG_1667972945002.jpg
FB_IMG_1667972942503.jpg
FB_IMG_1667972933934.jpg
 
Natamani ningepata muda wa kuisoma. Lakini it is disconcerting kusikia madini yetu yakichimbwa, tunapata 4%.
But who will bell the cat?
 
Yaani makala nzuri kama hizi hakuna hata wachangiaji JF
Lakini hadithi za kijinga na udaku zinajadiliwa kwa mapana na marefu utadhani ni mustakbali wa nchi
 
Back
Top Bottom