SoC01 Ushuhuda wa jinsi UKIMWI ulivyotesa familia, kuongeza umasikini na mateso. Tushukuru ARV na wadau wa afya

Stories of Change - 2021 Competition

Ngaliba Dume

JF-Expert Member
Oct 6, 2010
1,710
3,669
Hatukuwa tumewahi kufiwa na mmoja wa wanafamilia,kwa maana ya kaka au dada wa tumbo moja na baba mmoja.Misiba mingi ilikuwa ni kwa ndugu na jamaa tu wa karibu.Msiba huu wa dada yetu aliyekuwa "kichwa" na msaada mkubwa kwa familia ulitokea mwezi March 1993 wakati huo mimi nikiwa nimemaliza kidato cha nne nikisubiri matokeo ya kwenda kidato cha sita.

Huyu dada aliugua kwa muda mrefu sana na hata mimi nilipokuwa narudi likizo kijijini kwetu baada ya kufunga shule nilikuwa namkuta anazidi kudhoofika.Miaka hiyo wengi hatukuwa na uelewa juu ya mambo ya UKIMWI,dalili zake na hata uzoefu wa kuuguza mgonjwa huyu.Homa za hapa na pale na kikohozi cha muda mrefu kilimsumbua dada.Alikuwa tayari na mtoto mmoja ambaye naye bahati mbaya alizaliwa akiwa na maambukizi.

Hivyo baada ya dada kufariki huyu mjomba wangu alidumu kwa miaka miwili naye tukazika.A young talented boy!Alitumia mkono wa kushoto kuandika na kucheza mpira.Ama hakika UKIMWI umeenda na wapendwa wetu wengi na umekatiza ndoto za watu wengi. Kwa maisha ya kijijini na elimu duni ya afya na huduma mbovu ya afya kijijini,dada aliishua kupewa dawa za yale magonjwa nyemerezi tu lakini haikufua dafu.

Maana Kituo cha afya kilichokuwepo hakikuwa na vipimo.Ilikuwa ni kituo kilichojengwa kwa msaada wa Masista wa kanisa katoliki.Ambao zaidi ya kujitolea kwao sababu ya usista wao na nadhiri zao za kutumikia jamii inayowazunguka,hawakuwa na elimu darasa ya mambo ya tiba.Kama ilivyo ada ya maisha ya wengi vijijini wazo kubwa lilikuwa ni dada kurogwa.Haikuingia akilini mtu kuugua kiasi kile bila kupata nafuu na kudhoofu.

Sababu ya kukohoa sana,shangazi alitoa wazo kuwa inabidi dada akatwe kilimilimi maana mabibi pale kijijini wanasema hicho ndio kitakuwa kinamsababisha akohoe sana,na baada ya kukatwa ili kidonda kile kipone haraka alitakiwa kunyweshwa maji yaliyopatikana kwenye pango la mti na hasa mbuyu.Siku kadhaa akaja bibi wa pale kijijini ambaye ni mtaalamu wa kukata vilimi.Dada,siku moja alfajiri na wembe mpya wa topaz alikatwa kilimilimi,maana ilisemwa ni lazima kikatwe kabla ya jua kuchomoza.

Hata baada ya kukatwa na kunyweshwa maji ya pango la mti,dada aliendelea kukohoa sana sana.Akodhoofika na kukonda mno.Tukiwa wenye imani ya dini ya Katoliki kila jioni nilipokuwa likizo ya kidato cha nne dada aliniita na kusali nae rozari ili Mungu ampe afya njema.Hata kwa elimu yangu ya kidato cha nne nami sikuwa najuwa kuwa ule utakuwa ni UKOSEFU WA KINGA MWILINI.Dada aliteseka,alikonda na kuisha sana.Ilifikia wakati nami nikimtazama ninatoa machozi.Ama hakika UKIMWI na mateso yake ya wakati huo ya bila ARV yasikie tu kwa jirani.

Ziliuzwa ng'ombe na mbuzi kuzunguka kwa waganga kujua hasa "mbaya wetu" ni nani? Huyu mlozi wa familia ni nani? Hakuna hata mmoja aliyekuwa na wazo la kwenda mjini kwenye vipimo vikubwa.Na waganga wote tuliopita hakuna hata mmoja aliyeacha kutuambiwa kuwa "huyu karogwa kwa kutupiwa jini".Madawa na mitishamba ilijaa ndani kwa wingi bila kuleta matokeo chanya.Siku zikaenda na hali ya dada inazidi kuwa mbaya na ya kukatisha tamaa.Tulisafiri mpaka Morogoro sehemu za Vidunda kufuata mganga,lakini hakukuwa na uafadhali.

Wakati wote huu dada yangu mdogo na Mama ndio waliokuwa wauguzaji,ama hakika waliuguza bila tahadhari sababu hawakuwa na elimu juu ya mgojwa na namna ya kumuuguza.Baada ya kipindi kirefu cha mateso Dada alifariki.Naukumbuka mchana ule,mchana mgumu kuwahi kuuona katika maisha yangu ya ujana,ama kweli roho itokapo katika mwili mwnadamu hujijua.Dada isivyokawaida aliniita,niliitikia wito,akaniomba nikamate rozari na misale ya waumini,nifungue sala ya wagonjwa na tusali kwa moja.

Akiitikia kwa tabu na kwa kukoroma tulisali pamoja,baada kama ya dakika 15 niliona mtu amekaa kimya na baadae "kuhangaika" hapa na pale.Loooh!Kumbe ndio mwili ulikuwa unaacha roho na dada aliniita kuniaga,tuliagana kwa rozari na mishale ya waumini.Alasiri ya 08/03/1993.Upumzike kwa Amani.Baada ya kuzika maisha hayakuwa kama zamani,sehemu ya ng'ombe zilizotumika kunilipia ada zilipungua sana sbb ya mizunguko ya waganga na hali ya ugonjwa.

Hata anakufa hakuna aliyejua ulikuwa ni UKIMWI,wengi walilaani juu ya "uchawi" na jini lililotupiwa familia.Na ama hakika Waganga walisisitiza kuwa "jini" hilo bado linazungukazunguka,na litaondoka na mwingine.Bila kujua lolote Mama alianza nae kuugua,kwa dalili zilezile za Dada.Mama alikonda sana,nilirudi likizo ya kwanza ya kidato cha nne namkuta mama amelala nje juu ya mkeka amebaki kichwa tu,amekonda na kukondeana.Mtoto wa kiume nililia sana kwa hali ile ya Mama.Nikajisemea hili jini kweli litatumaliza wote.Baadae tena dada yangu aliyeshirikiana na Mama kumuuguza marehemu akaugua,dalili zilezile za Mama tukawa na wagonjwa wawili ndani ya nyumba,tuliuza mpaka ndama kuokoa maisha ya ndugu hawa.Hakuna wazo la hospitali,kila mtu ni kutegua mtego wa jini.

Siku moja akawa amefika Padre kigangoni kwetu,Padre huja mara moja kwa mwezi kusoma misa na kutembelea wagonjwa,baada ya misa ile nilimuomba Padre afike nyumbani kumuombea mama yangu na dada na hakika mama alistahili kuombewa sababu alikuwa mwanachama mzuri wa umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA),hivyo ilikuwa rahisi kwa Padre kufika na kuwaona.Ndani ya nyumba ya nyasi yenye giza hata mchana wa jua kali Baba Paroko akaingia.Alipowatazama wagonjwa akatokwa na machozi.

Akahimiza waondolewe haraka na atawakimbiza yeye mjini kwa gari yake wakapate vipimo vikubwa,wachache sana waliokubaliana na padre wakijuwa kuwa ule ni ugonjwa wa kurogwa sio wa hospitali,na kuwapeleka hospital ndio mwisho wa mchezo.Nguvu za paroko na ushawishi wake ziskashinda,Mama na dada haraka mjini,hadi kufikia jioni majipu yakawa ni TB kwa wote wawili,na baada ya udadisi wa madaktari ikabidi ni mtoto wa dada aende kupimwa,naye tukamsafirisha mpaka mjini.

Tobaaaa!Mtoto akakutwa na UKIMWI alioachiwa na mama yake,hivyo Mama na Dada waliambukizwa TB sababu hawakuwa na tahadhari ya kumuhudumia marehemu.Wakati huo hakukuwa na "Mpango wa kutokomeza Kifua Kikuu" wa kutoa dawa bure,hivyo ilihitaji kugharamia rundo la vidonge.Watu waliuza mifugo kununua dawa kwa shingo upande.Mama na dada wakawekwa hospitali na kunywa dawa kwa kuangalizi mkubwa sana,baada ya miezi mitatu afya zao zilirudi kwa kasi.

Kumbe haikuwa jini kama wale waganga walivyosema,ulikuwa ni UKIMWI kwa marehemu na kwa mama na fada ilikuwa ni TB.Maisha yakaenda na mama akarudi katika hali yake ya afya njema.Nikiwa mbioni kuingia kidato cha sita nikaanza kuugua sana nikiwa shuleni.Kikohozi na jasho kali wakati wa usiku.Kula sana chakula lakini ndani ya nusu saa nasikia njaa.Shule haina vipimo zaidi ya zahanati unayopewa dawa kulingana na dalili za ugonjwa.Niliugua sana sana kumbe nami ilikuwa TB,maana wote hatukuchukua thadhari wakati tukimuuguza dada,bahati nzuri shule ilinipeleka hospitali na kutibiwa mapema,ilibidi niahirishe mwaka mmoja ili nipate afya nzuri.Mwisho wa siku wote tukapona,haikuwa jini kwa dada wala kwa Mama,bali ni UKIMWI na TB.

Miaka miwili baadae mtoto wa dada akafariki,wakati huo hakukuwa na ujuzi wa kuzaliwa bila VVU hata kama mzazi anavyo,wala ARV hazikuwepo.Bwana mdogo alifariki katika mateso na mahangaiko makubwa sana.Tukamzika pembeni ya kaburi la Mama yake,na juu ya kaburi tukaandika "YEYE ANIAMNIYE MIMI HATAKUFA,BALI ATAISHI MILELE".Ni miaka zaidi ya 25 sasa,Wapendwa wetu wametangulia mbele za haki.

UKIMWI ulikatisha maisha yao,ama hakika balaa la ugonjwa huu lisikie kwa jirani.Jamani UKIMWI ni chanzo cha umasikini,lakini elimu ya msingi ya afya ni muhimu kusambaa mpaka vijijini.Isingalikuwa mtumishi yule wa Mungu,basi "ujinga" wa kuamini jini ungeendelea.Hii hali ipo sehemu nyingi,kuona UKIMWI kama ugonjwa wa kurogwa.Wasichekwe wazee wetuu kwa kuamini ktk waganga na tiba mbadala.Tuwaelimishe na kuokoa jahazi.Ninawapa pole wale wote waliowahi kupoteza wapendwa wao kwa UKIMWI.Tuwaenzi kwa kuepuka gonjwa hili,kuwa waaminifu,kuacha kabisa au kutumia kinga kwa wasioweza kujizuia.

RAHA YA MILELE UWAPE EEE BWANA,NA MWANGA WA MILELE UWAANGAZIE,WAPUMZIKE KWA AMANI AMINA.....KWAKE SISI TUMETOKA NA KWAKE TUTAREJEA.
 
Pole sana mkuu. Kwa hakika kabla ya ARV uliyoeleza ndiyo yalikuwa madhila yenyewe. Familia nyingi ziliguswa kwa namna kama ya kwenu mkuu.

IMG-20210725-WA0007.jpg


Kama ilivyo kuwa siku za Nuhu kwenye zama za Corona hali ni hiyo hiyo.
 
Unaweza kukuta anayelaani chanjo ya Covid, anashabikia arv na other western medicines

sad
 
Asante kwa ujum e mzuri..japo hii story ipo hapa JFkitambo Sana
Ni yangu mkuu...nimeileta tu huku kuchagiza mijadala!!uki-search utaona ni yangu.Na nimefanya hivi kuonyesha kuwa sio COVID tu inaweza kukumbana na changamoto za kutojua namna ya kuikabili, hata UKIMWI uliahidi kuwa hivyo.Tuzidi kuelimishana na kukumbushana
 
Back
Top Bottom