Ushirikishwaji wa wadau katika utekelezaji wa mradi

Jul 3, 2016
19
13
Mradi huwa na mafanikio pale unapofikia/timiza malengo yake mahsusi na pia lengo kuu (project objectives/Project goal) na kukidhi matakwa ya wadau (meeting stakeholders’ expectations) kwa maana hii wadau wanakuwa na ushawishi mkubwa sana katika kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mradi.

Wadau ni akina nani?

Hawa ni watu ambao wana maslahi (interests) na ushawishi (influence) juu ya mradi unaotekelezwa, si hivyo tu pia wana umuhimu (importance) . Kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mradi kunategemea sana jinsi hawa watu watakavyoshirikishwa katika mradi. Watu hawa hupata athari chanya au hasi (positively/negatively affected). Kwa mfano unapofanya mradi wa ujenzi wa miundo mbinu ya maji (water infrastructures development project) katika eneo fulani, wakazi wa eneo hilo ambao ni watumiaji wa maji watakuwa miongoni mwa wadau wa mradi huu, hii ni kwa sababu wataathirika moja kwa moja na matokeo ya mradi (positively affected), kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mradi huu kutategemea sana watu hawa. Lakini si hawa tu, pia makundi mengine kama vile wasambazaji wa vifaa vya ujenzi, mamlaka zinazotoa vibali n.k pia ni wadau wa mradi huu.

Pia ni vyema ikafahamika kwamba, haijalishi mradi umekuwa timilifu kwa kiasi gani (meeting project’s specification parameters), bado watu hawa wana uwezo wa kukwamisha mafanikio ya mradi, hivyo ni kiungo muhimu sana.

Uchambuzi wa wadau (Stakeholders analysis)

Hichi ni kitendo cha kufanya uchambuzi juu ya ushawishi (influence) waliyo nayo wadau wa mradi husika. Si tu ushawishi pia uchambuzi huu huwa na lengo la kutambua maslahi ya hawa wadau na umuhimu wao pia, na baada ya kutambua ushawishi , maslahi na umuhimu wao ni jukumu la wasimamizi wa mradi kuhakikisha wanaathiri maslahi yao ili yaendane na maslahi ya mradi kiujumla.

Njia mbalimbali huweza kutumika katika kufanya uchambuzi huu, miongoni mwa njia ambazo hutumika kufanya uchambuzi wa wadau ni njia ya majadilliano (focus group discussion), pia njia ya mashauriano hutumiwa (basic consultation). Aina ya njia hutegemea na mazingira ya mradi husika (nature of the project), hivyo ni jukumu la timu ya utekelezaji wa mradi (project team) kuamua ni njia ipi nzuri katika uchambuzi wa wadau.

Matokeo ya chambuzi wa wadau huja na makundi makubwa manne ya wadau ambao wana athari katika mafanikio ya mradi kiujumla, makundi hayo ni:

1. Wadau ambao wana ushawishi kiasi kwa kidogo katika utekelezaji na mafanikio ya mradi lakini umuhimu waliyonao juu ya mradi ni mkubwa. Wadau hawa ni muhimu sana kwa mafanikio ya shughuli za mradi lakini hawana uwezo wa kuathiri mchakato wa shughuli katika mradi. Kwa mfano mradi wa uchaguzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali, mafanikio yake hutegemea sana ushiriki wa wanawake na makundi mengine tengwa, lakini ukweki ulio wazi ni kwamba haya makundi hayana uwezo hata kidogo wa kurekebisha au kuathiri mchakato wa uchaguzi.

2. Wadau ambao wana ushawishi mkubwa katika utekelezaji na mafanikio ya mradi lakini umuhimu waliyonao juu ya mradi ni mdogo. Wadau hawa wakati mwingine huweza kuleta vikwazo katika utelkelezaji wa mradi ijapokuwa umuhimu wao ni mdogo.

3. Wadau ambao wana ushawishi kiasi kidogo katika utekelezaji na mafanikio ya mradi pia umuhimu waliyonao katika mradi ni mdogo . Hawa ni wadau ambao kuwepo au kutokuwepo kwao hakuathiri sana matokea na mafanikio ya mradi , mfano waangalizi wa Kimataifa (International observer groups) katika miradi ya kiuchaguzi.

4. Wadau ambao wana ushawishi kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji na mafanikio ya mradi pia umuhimu waliyonao katika mradi ni mkubwa . Wadau hawa ni muhimu zaidi na wanapaswa kushirikishwa kuanzia katika uibuaji wa mradi (project planning). Mfano wa wadau wanao angukia kundi hili ni vyama vya siasa katika miradi ya kiuchaguzi.

Wakati mwingine huwa kuna kasumba au tabia ifanywayo na watendaji wakuu wa mradi kutokuwahusisha baadhi ya wadau wa mradi, na hii hutokea sana kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa (complex projects). Makundi tengwa (marginalized groups) na jamii masikini vijijini hazishirikishwi katika utekelezaji wa miradi kwa sababu watendaji wa miradi huwa na dhana kwamba jamii hii ya watu haina elimu, ujuzi na taarifa ambazo ni muhimu katika utekelezaji wa mradi. Hii dhana ni mbaya na inaweza kusababisha mradi kutofanikiwa na kukosa hali ya uendelevu (sense of sustainability)

Kuwashirikisha wadau katika utekelezaji wa mradi huepusha migogoro na vikwazo ambavyo vinaweza kuathiri utekelezaji wa mradi, pia ushirikishaji huo hutoa fursa ambazo hunufaisha katika utekelezaji wa mradi.


Call +255 719 518367 (Kwa ushauri au huduma ya uandishi wa mchanganuo wa biashara, mradi au mpango mkakati)
 
Back
Top Bottom