Ushirikiano wa anga za juu kati ya China na Afrika watarajiwa kukua kwa kasi

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
VCG111407806213.png

Moduli ya majaribio ya Mengtian ya Kituo cha Anga za Juu cha China Tiangong hivi karibuni ilirushwa angani na kuunganishwa kwa mafanikio na moduli kuu ya Tianhe. Kwa hatua hiyo, ujenzi wa Kituo cha Tiangong kilichoundwa na moduli za Tianhe, Mengtian na Wentian umekamilika, na ukurasa mpya wa shughuli za utafiti wa China katika anga za juu umefunguliwa. Maendeleo ya kasi ya utafiti wa anga za juu nchini China yametoa fursa mpya kwa ushirikiano wa kimataifa, pamoja na Afrika.

Katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya anga ya juu imezidi kuwa sehemu muhimu katika ushirikiano kati ya China na Afrika. Pande hizo mbili zimepata mafanikio mazuri katika nyanja mbalimbali ikiwemo kujenga kwa pamoja miundombinu, matumizi ya pamoja ya data zilizotolewa na satelaiti, utafiti wa satelaiti mpya, na mafunzo maalum.

Mwaka 2017, Umoja wa Afrika ulitoa “Sera na Mkakati wa Afrika kuhusu Anga ya Juu”, na kuamua kuanzisha Shirika la Anga ya Juu la Afrika ili kuratibu ushirikiano wa kimataifa. Kutokana na umuhimu wa sekta ya anga ya juu katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na kuboresha uzalishaji na maisha ya watu, teknolojia ya kisasa ya anga ya juu inathaminiwa sana na nchi za Afrika. Maafisa wa Shirika la Anga ya Juu la Afrika wanasema, China ni mshirika na muungaji mkono wa lazima kwa Afrika ili kutimiza ndoto ya anga ya juu.

China imetangaza kuwa Kituo cha Anga za Juu cha Tiangong kitashirikisha nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa, na kundi la kwanza la nchi 17 ikiwa ni pamoja na Kenya zimechaguliwa kushiriki kwenye awamu ya kwanza ya majaribio ya anga za juu. Mradi wa majaribio ya sayansi ya anga ya juu uliowasilishwa na Kenya utatekelezwa kwenye Kituo cha Tiangong.

Ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na Kenya katika sekta ya anga za juu una historia ndefu. Mwaka 2003 wakati Chombo cha “Shenzhou 5” kiliporushwa, China ilianzisha kituo cha uchunguzi na udhibiti kwenye jimbo la Malindi nchini Kenya. Kama mojawapo ya vituo viwili vya kwanza vya kupima na kudhibiti vyombo vya usafiri wa anga za juu vilivyoanzishwa na China katika nchi za nje, kituo cha Malindi kilichangia maendeleo ya shughuli za anga za juu za China.

Misri ni nchi ya kwanza kufanya ushirikiano wa satelaiti na China chini ya mfumo wa ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Mwaka 2016, China na Misri zilisaini makubaliano kuhusu mradi wa kusaidia kujenga kituo cha kuunganisha na kupima satelaiti nchini Misri, na katika siku zijazo, Misri itakuwa nchi ya kwanza ya Afrika yenye uwezo wa kuunganisha na kupima satelaiti.

Hivi sasa, Idara ya Anga ya Juu ya China na Mamlaka ya Sayansi na Teknolojia ya Anga ya Juu ya Misri zimezindua miradi mipya ya ushirikiano, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la ofisi za Shirika la Anga ya Juu la Afrika, kituo cha satelaiti cha AIT cha urambazaji na mawasiliano, kituo cha utafiti na maendeleo, na jumba na maonesho.

Mbali na kutoa msaada wa vifaa na miundombinu, China pia inatoa mafunzo ya hali ya juu kwa watafiti wa Afrika katika kubuni, kutengeneza, kurusha na kudhibiti satelaiti. Kituo cha Elimu ya Sayansi na Teknolojia ya Anga ya Juu, kilichoko katika Chuo Kikuu cha Beihang, China, kinatoa elimu na mafunzo ya anga ya juu kwa wanafunzi wanaotoka barani Afrika. Tangu mwaka 2014, wanafunzi 32 kutoka nchi 8 za Afrika ambazo ni Algeria, Misri, Ethiopia, Togo, Cameroon, Msumbiji, Nigeria na Sudan wamehitimu kutoka kituo hicho baada ya kumaliza masomo ya shahada ya pili.

Anga za juu ni kwa binadamu wote, na ushirikiano kati ya China na Afrika katika utafiti wa anga za juu unaonyesha lengo na juhudi za pamoja za pande hizo mbili katika kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja. Kutokana na maendeleo ya kasi ya uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika, ushirikiano kati yao katika utafiti wa anga za juu utakua haraka.
 
Back
Top Bottom