Elections 2010 Ushindi wa Mrema Vunjo waongezeka kwa asilimia 4

mdaumie

Member
May 12, 2008
77
1
UTATA katika ujumlishaji matokeo ya kura umezidi kuongezeka baada ya matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa Jimbo la Vunjo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) kutofautiana na yaliyotangazwa awali na msimamizi wa uchaguzi.
Kutangazwa kwa matokeo mapya ya jimbo hilo kumefanyika katioka kipindi ambacho Chadema imeamua kutotambua matokeo ya uchaguzi wa rais kwa madai kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu na wizi wa wazi uliolenga kukibeba chama tawala.

Katika kudhihirisha uzito wa tuhuma zake, Chadema ilitoa mfano wa matokeo ya urais ya majimbo ya Hai, Geita na Segerea na baada ya Nec kupitia upya ilikiri kuwa kulikuwa na makosa katika Jimbo la Geita.
Huku hali ikiwa haijatulia, Nec imetangaza matokeo mapya ya Jimbo la Vunjo yanayoonyesha kuwa mgombea wa TLP, Augustine Mrema alipata ushindi wa asilimia 54 na si 50 kama ilivyotangazwa awali.

Kadhalika katika matokeo hayo mapya ambayo Mwananchi inayo nakala yake, kura za mgombea wa CCM, Chrispin Meela zimeshuka kutoka 23,870 hadi 17,498, tofauti ambayo ni sawa na asilimia 39.
Katika matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi Moshi Vijijini, Annah Mwahalende mbele ya wagombea hao, Mrema alikuwa amepata kura 30,810 tofauti
lakini matokeo ya awali yanaonyesha alipata kura 29,047.

Kwa matokeo hayo mapya, Mrema alishinda kwa asilimia 54 huku Meela wa CCM akiibuka wa pili kwa kupata asilimia 32 na si 39. John Mrema wa Chadema alipata asilimia 12 na si 10, huku David Lyimo wa NLD akipata asilimia 2 badala ya 1.
Kwa mujibu wa matokeo hayo mapya, Mrema wa Chadema alipata kura 6,558 na si kura 6,316 zilizotangazwa mwanzo huku Lyimo wa NLD akiwa amepata kura 811 tofauti na kura 118 zilizokuwa zimetangazwa awali.
Hata hivyo kumekuwepo na mabadiliko katika idadi halisi ya wapigakura kutoka 55,013 iliyotangazwa awali hadi kufikia 55,102 ya sasa huku idadi ya kura halali sasa ikiwa ni 53,914 tofauti na kura halali 53,705 zilizotangazwa awali.
Kutokana na hali hiyo, Mrema ameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mazingira ya mabadiliko hayo ya kura, akisema kuwa anahisi kulikuwepo na njama za kuchakachua matokeo ambazo ziligonga mwamba.

“Nasikia kuna tajiri mmoja alikuja pale ule usiku akiwa na Sh100 milioni akitaka atangazwe mshindi anayemtaka, lakini nguvu ya umma ilishinda kutokana na watu kupaza sauti wakisema kama noma na iwe noma hawatakubali,” alidai Mrema.
Mrema alihoji kama karatasi ya matokeo mapya inaonyesha yalikuwa tayari saa 11:45 jioni, ilikuwaje yatangazwe usiku saa 4:00 na bado yakatangazwa matokeo ambayo hayakuwa sahihi na badala yake kurekebishwa kimyakimya.

Mbunge huyo, ambaye pia ni mwenyekiti wa TLP, alisema kutokana na mazingira hayo ana shaka kuwa hata idadi ya madiwani wa kambi ya upinzani walioshinda ikawa tofauti na akataka kura pia zimlishwe upya.
Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi wa Moshi Vijijini, Mwahalende aliliambia Mwananchi jana kuwa hapakuwepo na uchakachuaji wowote wa kura bali kilichosababisha tofauti hizo ni makosa katika kujumlisha matokeo hayo.
“Tulitumia calculator (mashine ya kuhesabia) kutokana na presha ya wananchi kwa kuwa walikuwa hawajui mfumo mpya tuliokuwa tukiutumia kwa hiyo baada ya kutangaza tuliendelea kuingiza kwenye mfumo ndio ulitupa matokeo sahihi,” alisema.

Msimamizi huyo alisisitiza kuwa matokeo hayo hayana tofauti kwa kuwa mshindi amebakia kuwa yule yule. Katika uchaguzi huo, Chadema ilipata madiwani wawili huku CCM ikipata madiwani sita na TLP madiwani saba.,

source : MWANANCHI Tuesday, 16 November 2010
 
Back
Top Bottom