Ushauri mwingine wa Bure kwako mheshimiwa Magufuli

brazaj

JF-Expert Member
Jul 26, 2016
27,819
35,809
Miye ni mmoja wa waliokuwa waungaji mkono wako na mashabiki wakubwa na ningependa kuendelea kuwa hivyo hata baada ya 2025 utakapokuwa umerejea Chato (Inshallaah mnyazi Mungu atujalie uzima); kama wengine walivyorejea Mwitongo na Msoga.

Ninaamini kuwa waliokuwa na mtazamo kama wangu na ambao wangependa kuendelea na mtizamo huo bado wangalipo wengi tu na hasa kama ungeweza kufanya marekebisho ya msingi katika uongozi wako kwani ninaamini hujachelewa na kutereza mheshimiwa si kuanguka.

Mheshimiwa, naomba nami nikuase kuwa ubabe ubabe si katika uongozi wa nchi. Ubabe ubabe una mahali pake. Ni kutokana na ubabe ubabe huu usiokuwa na tija wakuonao tokea nje waliwahi kukuwekea wazi kuwa ulifaa zaidi kwenye unyapara. Waliosema hivyo si kuwa wanakuchukia au kuwa walikurupuka. Hiyo ilikuwa ni tathmini ya wakuonavyo wao tokea nje kutokana na matendo yako yanavyoakisi. Matendo yako ndiyo yanayowapa maoni hayo au mrejesho huo. Ni jukumu lako kubadilika inavyopaswa ili maoni kama hayo yaweze kubadilika pia. Kimsingi ni kuwa kiini cha maoni hayo ni wewe mwenyewe ndiyo unayoyajenga kwao. Haiwezi kuwa vingine. Mbona hawakusema hivyo na Mkapa, Mwinyi, Kikwete au Nyerere?

Usiwaone watoao maoni hawa kuwa wanakuchukia. Hawa ni watu wanaokusaidia kubadilika. Wengine waliokuwa wafuasi wako wamefika mahali wanashangaa. Ikumbukwe kuwa maoni ya wananchi ni ya muhimu sana katika kuongoza nchi yoyote kwa haki. Vinginevyo ndiyo yale ya udikteta uchwara yanapozaliwa. Kuongoza nchi kwa haki ndiko kunakoitwa kuongoza nchi ki demokrasia. Kuongoza nchi zikiondolewa kero kwa wananchi ndiyo yanayotumainiwa na wote wala siyo kuongoza nchi kwa kuongeza kero.

Huwezi kuiongoza nchi kama unavyotaka wewe bali kama wananchi unaowaongoza wanavyotaka. Haya katika lugha rahisi ni kuwa unapaswa uongoze nchi kwa mujibu katiba na ndiyo maana uliapishwa. Katiba ni ya wananchi na ndiyo sheria mama ya wao wanavyotaka nchi yao iwe. Sasa mheshimiwa ukija unasema unataka kunyoosha nchi kivyako vyako hili linakuwa jipya na ni jambo la hatari sana kwa yeyote mwenye uelewa au kujitambua. Unataka kunyoosha nchi mheshimiwa kwa maoni yako? Hili mwalimu (rip) alisema laweza kuwa sawa na bahati kubwa kama mnyoosha nchi akiwa genious ikiwa sivyo ni hatari sana. Alisema mwalimu kesho akitokea mwenda wazimu naye akawa ananyoosha nchi kivyake vyake itakuwa je? Kupisha haya kwa hekima kabisa alisema mwalimu tuzingatie katiba peke yake. Mheshimiwa zingatia katiba uone kama malalamiko na manung’uniko ambayo kwa hali ya sasa yamekuwa mengi mno yataendelea kuwapo.

Kwamba labda huendeshi kwa mujibu wa katiba, mheshimiwa lingekuwa jambo la tija kweli kweli kuwataka wanaokukosoa wakupe listi hiyo nawe ujiridhishe. Hiyo itakuwa kudhihirisha ukuu wako wala si unyonge wako. Achana na hawa wanaokusifia kwa kila jambo ili kupalilia ulaji wao kumbuka hao wako kimaslahi zaidi na kesho mambo yakiwa tofauti watakuruka kimanga. Kama huwajui hawa wanaokusifia kwa kila jambo mheshimiwa omba wanaokukosoa wakupe listi yao pia.

Leo hii kwenye utawala wako tumekuwa hatujui kesho na hii si tu tokea kwako bali pia kwa wawakilishi wako mikoani na wilayani, polisi nk. Imekuwai kila mwenye madaraka yake anakuja na matamko yake na yanakuwa sheria tokea siku hiyo hiyo. Polisi anaye simamia sheria tangu lini akawa na matamko yake na yakawa sheria hapo hapo? Hii ni katika Tanzania ya Magufuli peke yake.

Ni dhahiri kuwa yatakikana mtu kuwa mwuungwana kweli kweli kufahamu kuwa maoni ya wananchi unaowaongoza yanazingatiwa. Mheshimiwa, u heri kusikia wakukosoao kuliko wanaokusifia. Ninaamini mheshimiwa katika usomi wako unayo katika kumbukumbu zako ya Yule mfalme aliyekuwa uchi ambapo ni mtoto mdogo tu ambaye haswaa kwa utoto wake alithubutu kumfahamisha mfalme kuwa alikuwa yu-uchi kwenye kadamnasi na si mawaziri, spika, na manaibu spika waliokuwa pale. Kimsingi mheshimiwa hawa unaowasikia wakitakiwa kwenda kupimwa mikojo; ni watu wa msaada zaidi sana kwako kuliko hata hao wanaokesha wakiwanyanyasa kwa nia ya kujipendekeza kwako ili uendelee kuwapa ulaji (wachumia tumbo).

Mheshimiwa pana kundi hili kubwa ambalo kwa jitihada zako ingekuwa ni busara kuliona halikutupi mkono hasa kabla ya 2020. Ninasema hivi kwa dhati kwani vinginevyo mheshimiwa nachelea kusema usipochukua tahadhali za mapema kuendelea kwako kipindi cha pili utakuwa wewe mwenyewe unakuweka rehani.

Staili yako ya uongozi imekuwa ikiwakwaza wengi hasa wenye uelewa au wenye kujitambua hata kwa kiasi kidogo tu. Mashabiki wako kwa sasa wamebakia kuwa wale unaowapa ulaji madarakani na wale wasiokuwa na uelewa au kujitambua kabisa. Kundi hili la wasiojielewa au kujitambua ndio pekee ambalo linaendelea kukushangilia kila unapotumbua au kuwaongezea watu katika maisha uliyoyaita wewe ya “ushetani” bila ya yao kuona kuwa hiyo haiwasaidii wao kuondokana na hayo maisha ya “kishetani”. Kudhihirisha hili mheshimiwa fika benki yoyote au pata takwimu uone pana wateja wangapi mstarini kwa siku.

Kumekuwa na maneno mengi ya kukuasa na muelekeo wako ambayo umeendelea kuyafumbia macho. Umekuwa ukiambiwa unaminya demokrasia. Kuminya demokrasia maana yake ni kuwa hutendi haki na hili si jambo heri wala kuendekezwa. Tanzania ilikuwa imepiga hatua kubwa sana katika demokrasi (haki) kulinganisha na nchi nyingi kama Rwanda ambako wewe leo umekuwa ukijaribu kuiiga. Mahakama zina maana tu katika nchi za kidemokrasia ambako haki hupatikana. Maamuzi ya mahakama katika nchi ya kidemokrasia huheshimiwa na kuthaminiwa vilivyo. Leo wewe una matatizo na maamuzi tokea mahakama hata za kimataifa. Vyombo huru vile vinaposhangazwa na sisi kutokufuata mikataba ni kutufunza kuheshimu makubaliano. Kutufunza sisi tuweke misingi ya haki katika jamii zetu ambayo sasa hivi imemong’onyoka kwa kasi ya ajabu.

Leo hii mahakama zetu umezitaka hadharani kuwa zinapaswa kuegemea kwako. Umetamka mahakama zikusaidie. Maamuzi ya mahakama yasiyokupendeza hayaheshimiwi. Leo hii kuna nyumba zinabomolewa kukiwa na mazuio ya mahakama. Polisi nao leo wanatunga sheria ambazo wanawashurutisha wananchi kuzifuata. Wananyima watu dhamana. Wewe na wao tofauti imekuwa haipo. Nchi unaipeleka wapi?

Mifano iko mingi mno kama nilivyoonyesha kama unapenda kupewa mifano kwa kila hoja onyesha hivyo utapata mlolongo mrefu tu ambao ni wa haki usio na kupendelea wala kumwonea mtu.

Hakika ulipofikia mheshimiwa wahitaji muda kutathmini utawala wako wewe kama wewe.
 
Kuna mamillioni ya Watz ambao hawakukupigia kura lakini ni walipa kodi tena wengine ni wakubwa, kodi ambayo unatamba nayo nchi nzima.
Toa mawazo kuwa ,wewe ni kiongozi wa mashabiki wako tuu. Huna monopoly ya akili
 
Kuna mamillioni ya Watz ambao hawakukupigia kura lakini ni walipa kodi tena wengine ni wakubwa, kodi ambayo unatamba nayo nchi nzima.
Toa mawazo kuwa ,wewe ni kiongozi wa mashabiki wako tuu. Huna monopoly ya akili

Nadhani ni RAIS wa wanaCCM kwa uhalisia ila kwa mdomo ni RAIS wa wote.
 
Ushauri wako ungelipokelewa kwa mikono miwili kama angeliutoa Bashite kipenzi cha Mheshimiwa. Sasa wewe mwananchi mwenzangu sijui hata kama atausoma.

Mwafaaa!!!!!
"Aaah Bastola ya nini tena jamani " In Nape's Voice
 
Nadhani ni RAIS wa wanaCCM kwa uhalisia ila kwa mdomo ni RAIS wa wote.

Mkuu sidhani kuwa wanaCCM wana nafuu tumewaona wengi tokea kwa mheshimiwa Dialo hadi bwana Nape. Huko barabarani ambako polisi wamekuwa wakija na ya kutokea kwenye tinted, speed limit za ajabu ajabu hadi kulazimisha mabasi kulala majiani yanatuathiri sote na wana CCM.

Ninadhani ni kwa maslahi ya kila mtu na hata mkuu mwenyewe kuachia demokrasia (haki) ishamiri na sote bila kujali lolote tuwe sawa mbele ya sheria na mahakama zetu ziwe huru kwa maana yake halisi.

Tunapotozwa faini na kushikiwa madege ni kwa sababu hatukuwatendea wenzetu haki. Tuwe tayari kuelekezwa tuna pokesea na mahakama hii ndiyo ilikuwa hasa kazi yake. Mahakama pia ichukue jukumu lake la kukataa kuwepo kwa muhimili ulio chimbiwa zaidi.

Nadhani sote tunayo sehemu ya kufanya kwenye hili. Tusimwache mtu kuichezea katiba na kutuulia Demokrasia iliyokuwa imeshamiri vile hata kama katokea mbinguni.
 
Ushauri wako ungelipokelewa kwa mikono miwili kama angeliutoa Bashite kipenzi cha Mheshimiwa. Sasa wewe mwananchi mwenzangu sijui hata kama atausoma.

Mwafaaa!!!!!
"Aaah Bastola ya nini tena jamani " In Nape's Voice

Mkuu ninakusoma lakini kama ataupuuza ushauri huu atakuwa hajitendei haki yeye mwenyewe na akumbuke mpanda ngazi hushuka. Walikuwapo kina Kikwete leo wako Msoga naye siku moja atakuwa Chato kutenda haki ni jambo la msingi sana labda kuliko lingine lolote. Walikuwapo kina Sumaye leo tuko nao uraiani.
 
Back
Top Bottom