Usalama wa Taifa wamvaa Dk Slaa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Usalama wa Taifa wamvaa Dk Slaa

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Kaa la Moto, Nov 5, 2010.

 1. Kaa la Moto

  Kaa la Moto JF-Expert Member

  #1
  Nov 5, 2010
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 7,666
  Likes Received: 164
  Trophy Points: 160
  Usalama wa Taifa wamvaa Dk Slaa Friday, 05 November 2010 08:15

  [​IMG]Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa,Jackie Zoka

  KATIKA hali isiyo ya kawaida, Idara ya Usalama wa Taifa jana ilijitokeza hadharani kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa ambaye alidai kuwa idara hiyo nyeti ilipika matokeo ya uchaguzi wa rais.Majibu ya Idara ya Usalama wa Taifa yametolewa katika siku ambayo Tume ya Uchaguzi (Nec) imekiri kuwa ilifanya makosa kwenye matokeo ya kura za uchaguzi wa rais kwa kumpa mgombea huyo wa Chadema kura chache kwenye jimbo alilolalamikia la Geita.
  Mkurugenzi wa uchaguzi wa Nec, Rajab Kiravu alisema jana kwenye mkutano na waandishi kuwa Tume ilichukuwa matokeo ya Jimbo la Nyang'wale na kuyatangaza kuwa ni ya Geita na kukiri kuwa ilifanya makosa, lakini ikasema matokeo ya Jimbo la Hai na Ubungo hayakuwa na makosa kama Dk Slaa alivyodai.
  Dk Slaa, ambaye aliibukia kuwa kivutio wakati wa kampeni za uchaguzi kutokana na mikutano yake kuvuta watu wengi, aliituhumu Idara ya Usalama wa Taifa juzi akisema kuwa ilihusika kuchakachua matokeo ya kura za urais kwa lengo la kumpa mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete ushindi wa kishindo.

  Katibu huyo mkuu wa Chadema, ambaye alikuwa na nyaraka zinazoonyesha matokeo yaliyokusanywa kwenye vituo na kwa wasimamizi wa uchaguzi ambayo alidai yanapingana na yale yanayotangazwa na Tume ya Uchaguzi, aliahidi kuyakataa matokeo na kuitaka Nec kuitisha uchaguzi upya.
  Katika moja ya mikutano yake wakati wa kampeni, Dk Slaa alisema imani yake kuwa wizi wa kura upo inatokana na hukumu ya mwaka 2008 ya mahakama kwenye kesi ya kupinga ushindi wake kwenye Jimbo la Karatu ambayo iliionyesha kuwa aliibiwa kura 5,000.

  Lakini jana, naibu mkurugenzi mkuu wa idara hiyo, Jackie Zoka alikutana na waandishi wa habari kujibu tuhuma hizo kali za kushiriki kuhujumu kura kinyume na utashi wa wananchi, akisema madai hayo yasipotolewa majibu, wananchi wanaweza kuyaamini.
  "Wananchi hawana budi kupuuza tuhuma zinazotolewa na Dk Slaa," alisema Zoka alipoongea na waandishi wa habari kuhusu madai hayo ya Dk Slaa. "Hizi ni jitihada za makusudi za kuichinganisha Idara ya Usalama wa Taifa na wananchi.
  “Tuhuma hizo ni nzito hasa kutoka kwa mtu anayewania kuwa kiongozi mkuu wa taifa letu. Kama zisipojibiwa, upo uwezekano mkubwa wa wananchi kuziamini. Hii itajenga hisia kuwa viongozi watakaotangazwa katika uchaguzi huu wamewekwa na usalama wa jambo ambalo sio kweli."

  Zoka alieleza kuwa hatua zote za uchaguzi mkuu, ikiwamo ni pamoja na upigaji wa kura, kuzihesabu na hata kutangaza matokeo, zinafanywa bila uficho hivyo haiingii akilini idara hiyo kuhusishwa kwa namna yeyote ile katika mchakato huo.
  Alizitaja hatua za upigaji kura kuwa ni pamoja na kupigwa vituoni bila uficho wowote, kuhesabu kura mbele ya mawakala, kujaza na kupewa fomu kwa mawakala wa vyama na kupelekwa kwa matokeo sehemu ya majumuisho, akasema katika hatua zote hizo, maafisa usalama wa Taifa huwa hawapo.

  “Katika utaratibu huo, haiingii akilini ni sehemu gani ambapo Maafisa usalama wa Taifa watapata nafasi ya kuchakachua. Hapana shaka tuhuma hizo zinalenga tu kuipaka matope idara,” alisema.
  Hata hivyo, kura hizo huhesabiwa kwa uwazi kwa wasimamizi wa uchaguzi na kutumwa Nec ambayo huamua kutangaza bila ya wawakilishi wa vyama kuhakiki kwanza matokeo kutoka kwa wasimamizi.

  Zoka alimtaka Dk Slaa kutoa ushahidi wa madai yake hayo akionya kuwa taratibu za Idara ya Usalama wa Taifa kufanya mambo yake kwa siri, zisitumike kama kigezo cha kuituhumu kwa mambo mazito na ya uongo.
  Kwa mujibu wa Zoka inawezekana Dk Slaa anadanganywa na watu wanaojifanya Usalama wa Taifa ambao wanampa taarifa za siri, lakini anapaswa kuwa makini kwani taarifa zingine ni za uongo na zinachochea uvunjifu wa amani.

  “Kwa lugha ya kawaida tunasema Dk Slaa ameingizwa mjini na yeye ameingia kichwa kichwa,” alisema Zoka.
  Zoka alieleza kuwa Idara ya Usalama wa Taifa ipo kwa lengo la kuhakikisha nchi inakuwa salama na sio kuwa chanzo cha kuhatarisha usalama wa Taifa hivyo tuhuma hizo hazina msingi.

  Alidokeza kuwa kimsingi idara hiyo ni rafiki wa vyama vya siasa na iko tayari wakati wote kushirikiana navyo katika kutekeleza majukumu yao.
  Hii ni mara ya kwanza kwa Idara ya Usalama wa Taifa kujitokeza kujibu tuhuma zinazoelekezwa kwake.
  Naye Dk Slaa alizungumza na waandishi wa habari jana na kuwaambia kuwa hashangazwi na lugha kali iliyotolewa na idara hiyo kujibu tuhuma zake.
  Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni, Dk Slaa alifafanua kuwa hashangazwi na hatua hiyo ya Usalama wa Taifa kwa kuwa ilishawahi kujaribu kuzuia kashfa ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) lisijadiliwe bungeni.

  "Kipindi kile limeibuka suala la EPA, Usalama wa Taifa waliingilia kati ili lisijadiliwe bungeni, sasa hawa ni Usalama wa Taifa gani wanaoficha maovu. Walisema nyaraka zangu za ushahidi wa EPA ni feki (za kughushi), lakini leo hii waliohusika katika sakata hilo la EPA wana kesi mahakamani," alisema Dk Slaa.
  "Katika ukurasa wa kwanza na wa pili wa tamko la Usalama wa Taifa walilolitoa baada ya kuwataja jana (juzi) kuwa walihusika kuchakachua matokeo, wamekiri wazi kuwa walisambazwa nchi nzima."
  Alisema idara hiyoi haihusiki na masuala ya uchaguzi na kwamba aliamua kuzungumza baada ya kuiona idara hiyo ikiingilia taratibu za uchaguzi.

  "Walitakiwa kuonyesha kwa nini nimepata kura kidogo katika maeneo ambayo rekodi zinaonyesha kuwa nilikuwa na kura nyingi, hiyo ndio kazi ya Usalama wa Taifa. Watanzania ndio waliowaajiri kwa kuwa wanalipwa kutokana na kodi za wananchi," alisema Dk Slaa.
  Dk Slaa, ambaye alitaja orodha ya mafisadi wakubwa nchini kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mwembeyanga, Tandika, alisema uchakachuaji wa kura ni ufisadi na kuweka bayana msimamo wake kuwa atazungumzia bila wowote kitu chochote kinachohusu ufisadi.

  "Mimi siogopi... waendelee tu, tutakutana mahakamani," alisema.
  "Hatuchonganishi jambo lolote bali tunaeleza ukweli... Usalama wa Taifa unaweza kutokuwa na manufaa kama haulindi haki za wananchi. Katika majibu yao wametueleza sheria, sisi ni watendaji inawezekana wakawa hawajui jinsi uchakachuaji wa kura unavyouma, labda na wao waje halafu wachakachuliwe ndio watajua ukweli," alisema Dk Slaa.
  Kuhusu madai kuwa ameingizwa mjini na watu wanaojidai kuwa ni maofisa wa Usalama wa Taifa, Dk Slaa alisema: "Ndio walishawahi kusema kuwa napewa nyaraka na Usalama wa Taifa 'feki', lakini iwe ndani au nje ya serikali wapo Watanzania wenye dhamira safi na wataendelea kutuletea taarifa tu."

  Alisema kuwa inachokifanya Chadema ni kueleza kuwa kuna matatizo ili yaweze kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi, lakini kuna watu hawataki.
  "Asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Huu ni msemo tu na mimi sio mkuu bali nazungumza kwa maslahi ya nchi yangu na watanzania kwa ujumla. Wananchi watakuja kukasirika na sisi tusilaumiwe kwa kuwa tunaeleza matatizo yaliyopo ili tukae kwa pamoja tuzungumze," alisema.

  Nao wasomi wameungana na madai ya Dk Slaa wakisema kuwa uchakachuaji matokeo ya kura nchini umekuwa aibu kwa taifa.
  Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, wasomi hao walisema kuna dalili zinazotia shaka kwamba matokeo ya urais yamechakachuliwa kwa kuwa hawaoni sababu kucheleweshwa kutangazwa.
  “Tunajua kuwa hata kama CCM ingeshinda, isingeshinda kwa kura nyingi kiasi hicho. Kwa nini tumsifie mtu kuwa ameshinda kwa kishindo na huku amechakachua matokeo?”alisema Dk Fairles Ilomo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa.
  Dk Ilomo alisema haiingii akilini kuelezwa kuwa matokeo yamechelewa kutangazwa kwa sababu ya matumizi ya kompyuta katika hatua ya kuhesabu kwani wakati wa upigaji, wananchi hawakutumia kompyuta.

  "Kwanini matokeo yasubiri kompyuta? Hakuna logic (mantiki) kusema kuwa kuingiza data kwenye kompyuta kulisababisha ucheleweshaji maana hata uchaguzi wa Marekani, walitumia kompyuta na matokeo yakawahi kutolewa," alisema Dk Ilomo.
  “Ni kweli uchaguzi ulifanyika vizuri na kulikuwa na amani lakini katika hatua ya kuhesabu kura na kutangaza matokeo kulikuwa na uchakachuaji hasa katika maeneo nyeti.
  “Rais aapishwe, lakini Dk Slaa ana haki ya kuendelea na malalamiko yake. Kama malalamiko hayo yakionekana yana ukweli, maamuzi mengine yafuate."
  Kwa mujibu wa Dk Ilomo pamoja na kwamba CCM imeshika hatamu kwa nafasi ya urais, wananchi wanapaswa kujua kuwa mfumo wa uongozi nchini ni wa uchakachuaji ambao kama mtu hauko kwenye mfumo huo, kushinda ni vigumu.

  Lakini Dk Ilomo alitahadharisha kwa kusema “kama hoja za Dk Slaa si za msingi au ni siasa tu, ni bora aache msimamo huu wa kukataa matokeo kwa sababu atajiharibia. Lakini kama ushahidi wake ni wa kutosha, aendelee."

  Mhadhiri mwingine chuoni hapo Harod Tairo alisema amestuka kuona matokeo hayo yanaonyesha kuwa watu wengi wamewapigia kura wabunge wa Chadema lakini si mgombea wake wa urais, yaani Dk Willibrod Slaa
  “Mimi naamini kwamba wabunge wengi wa Chadema walichaguliwa kwa juhudi za Dk Slaa. Wananchi hawawezi kuchagua mbunge wa Chadema halafu rais wamchague wa CCM. Mimi naona matokeo hayaakisi halihalisi,” alisema Tairo.
  Kwa mujibu wa Tairo matokeo hayo yanataka kuthibitisha tafiti za Redet na Synovate kwamba CCM bado iko juu kuliko vyama vingine.
  Mhadhiri huyo pia alizungumzia suala la ucheleweshaji matokeo akisema anashangazwa na sababu zilizotolewa.
  “Sababu za kuchelewesha matokeo haziingii akilini. Eti kuingiza mahesabu kwa siku mbili? Hapo hata mimi nina shaka.
  Kuna kuna kitu kilichokuwa kinaendelea," alisema Tairo na kutolea mfano wa msimamizi wa uchaguzi kwenye moja ya kata za Jimbo la Segerea aliyeripotiwa kukamatwa na nyaraka za Nec wakati wa majumuisho ya kura.
  “Wananchi walisimamia matokeo ya ubunge na kusahau ya urais ndio maana uchakachuliaji ulifanyika sana katika matokeo hayo,”alieleza.

  Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (Phd) wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Gasper Mpehongwa alisema Dk Slaa apeleke malalamiko yake Tume badala ya kulalamika nje ya utaratibu.
  "Kama ushahidi ni wa kweli, ni jambo la kusikitisha sana kwamba wananchi wanapiga kura kuonyesha maamuzi yao wakati system (mfumo) una maamuzi tofauti. Kulalamika hivi hivi tu hakusaidii. Dk Slaa apeleke malalamiko hayo tume,” alisema Mpehongwa
  mwisho
  Habari hii imeandikwa na Elias Msuya, Petro Tumaini na Fidelis Butahe
   
Loading...