Usaili TFF, Wambura, Malinzi wang'aka

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,906
22,050
Usaili TFF, Wambura, Malinzi wang'aka

Na Sophia Ashery

USAILI kwa wanamichezo wanaowania nafasi za uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ulifanyika Dar es Salaam jana, huku baadhi ya wagombea wakiibuka na malalamiko mengine kuhusiana na vipingamizi walivyowekewa.

Usaili huo ulifanyika kuanzia saa tatu asubuhi, huku eneo la ofisi za shirikisho hilo kukiwa kumetanda askari polisi wenye sare na wale wasiokuwa na sare, ambapo hali ya utulivu ilikuwa kubwa, licha ya kuwepo mashabiki wengi kwenye eneo hilo, hasa wale wa Simba na Yanga maarufu kama Makomandoo.

Mwanamichezo wa kwanza kufanyiwa usaili alikuwa Rais wa sasa wa TFF, Leodeger Tenga, ambaye hakutumia muda mrefu na alipotoka, alisalimiana na watu mbalimbali, bila kutaka kuzungumza kwa kirefu na kuondoka eneo la usaili kwenye hosteli za TFF Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Lakini hali ilianza kubadilika alipoingia mgombea mwingine wa nafasi hiyo ya urais, Jamal Malinzi aliyetumia karibu dakika 45 akiwa ndani ya chumba cha usaili na alipotoka alilalamiki na kudai Kamati ya Uchaguzi ilihoji sababu ambazo nyingine ni za binafsi.

Alidai hali hiyo inamtia hofu na kuwa kama itaenda kama anavyohisi, basi viongozi wa zamani wataendelea kuongoza shirikisho hilo na kudai kuwa alihojiwa sababu ya kwenda mjini Lindi na kutuhumiwa kufanya kampeni, jambo alilosema ni la kushangaza.

Alidai anashangaa kuhojiwa uhalali wake wa kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine, wakati yeye ni mfanyabiasha anayeweza kusafiri sehemu yeyote ndani na nje ya nchi na kuongeza kuwa sheria za nchi ni kuwapa raia uhuru wa kusafiri popote hapa nchini bila kuvunja sheria.

Malinzi alizungumzia mambo kadhaa aliyodai alihojiwa ambayo kwake alidai hayana umuhimu mkubwa na nafasi anayoomba zaidi ya kushangaa kuwekewa pingamizi na watu wakihoji utendaji wake.

Baadaye aliingia aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa TFF wakati ikijulikana kama FAT, Michael Wambura anayewania nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye alihojiwa kwa saa moja na dakika mbili, ambapo alipotoka naye alitoa malalamiko yake, huku akidai kuna wagombea huenda hawatakiwi.

Alizungumzia kuhusiana na pingamizi alizowekewa na watu wanne kuwa ni moja ya fitina zilizowekwa ili asiweze kupenya katika kinyang'anyiro hicho na kudai baadhi ya mambo aliyohojiwa ni ya ndani ya TFF, hivyo ni vigumu kwa mtu aliye nje kuweza kuyazungumza.

"Lakini kamati imeshindwa vipi kutupa barua za pingamizi zilizowekwa, pia hao walalamikaji wangekuwepo pale kwenye usaili ili wazungumze maana hii ni kesi, nitaamini vipi kwamba hao watu kweli wapo?

"Sisi tulitakiwa ukichukua fomu kuomba uongozi udhaminiwe na chama cha mpira cha mkoa, lakini hawa walioleta barua zimepokelewa moja kwa moja TFF, kuna baadhi ya watu wamepeleka pingamizi kwa nia ya kuniondoa, lakini nitajua la kufanya baada ya uamuzi kutoka," alisema Wambura.

Naye wakili maarufu nchini anayewania nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais, Damas Ndumbaro, naye alitoa malalamiko akidai kushangazwa na baadhi ya mambo ikiwa ni pamoja na kuhojiwa uhalali wake wa kuwania nafasi hiyo kupitia Mtibwa badala ya Simba ambayo ni mwanachama.

Alitoa malalamiko mengine kuwa ni kutoonekana kwa baadhi ya makabrasha yenye wasifu wake, jambo alilodai limemfadhaisha sana.

Hata hivyo mgombea mwingine wa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema kamati hiyo ilifanya usaili huo kwa kufuata haki bila upendeleo wowote, ingawa naye alitumia muda mrefu kuhojiwa.

Kwa upande wa nafasi za juu, ukiacha Wambura, Malinzi na Kaburu, wagombea wengine walitumia muda mfupi zaidi katika usaili, ingawa walikuwa pia na mapingamizi. Juhudi za kuwapata wahusika wa Kamati ya Uchaguzi zilishindikana, ambapo hadi tukienda mitamboni walikuwa bado wakiendelea na usaili.

Ukiacha usaili huo, moja ya mambo yaliyopendezesha jana ni magari ya kifahari ya wagombea mbalimbali yaliyokuwepo kwenye usaili kiasi cha kuonekana kama kuna mashindano ya maonesho ya magari.

Lakini pia kuwepo baadhi ya mashabiki wa klabu za Simba na Yanga maarufu kama makomandoo, huku baadhi ya wagombea wakiamkia watu mbalimbali waliokuwepo kwenye usaili huo ilikuwa moja ya burudani hizo.

"Shikamoo ndugu yangu upo, tuwasiliane wakati ndio huu," zilikuwa moja ya salamu za baadhi ya wagombea.

Wanamichezo 46 walitarajiwa kusaili jana kwa nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo utakaofanyika Desemba 14, ambao ni Jamal Malinzi, Leodeger Tenga (Rais), Michael Wambura, Athumani Nyamlani, Lawrance Mwalusako, huku Makamu wa Pili wa Rais na Ali Mwanakatwe (Makamu wa Kwanza wa Rais), Lucas Kisasa, Damas Ndumbaro, Godfrey Nyange 'Kaburu' na Ramadhan Nassib (Makamu wa Pili wa Rais).

Wanaowania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Wallace Karia, Eliud Mvella, Shaibu Nandonde, Amir Roshan, John Kiteve, Samuel Nyalla, Ismail Rage, Joseph Mapunda, Khalfa Mgonja, Benedict Macha na Lameck Nyambaya

Wengine ni Nassoro Kipenzi, Mbasha Matutu, Tefrid Sikazwe, Abdul Sauko, Charles Mugondo, Titus Bandawe, Richard Rukambula, Athumani Kambi, Murtaza Mangungu, Vincent Majili, Muhsin Balhabou, Tumaini Kagina na Festo Mkemwa.

Pia wapo John Mwangakala, Ahmed Mgoyi, Rommel Hans Poppe, Hassan Othman 'Hassanoo', Juma Muruwa, Omar Abdulkadir, Charles Mchau, Castory Lugali, Mulamu Ng'ambi, Mohammed Nassoro, Israel Mwansasu na Hussein Mwamba.
 
Back
Top Bottom