Miss Zomboko
JF-Expert Member
- May 18, 2014
- 4,498
- 9,279
Bunge la Urusi limepitisha agizo la Rais Vladimir Putin la kutambua uhuru wa maeneo ya waasi mashariki mwa Ukraine, siku moja baada ya Rais Putin kutia saini agizo hilo na kuamuru wanajeshi kuingia katika maeneo hayo. Huku haya yakijiri Urusi inakodolea macho vikwazo kutoka nchi za magharibi kuhusiana na mgogoro unaoendelea kufukuta kati yake na Ukraine.
Agizo hilo limeungwa mkono kwa kauli moja katika baraza la wawakilishi mjini Moscow. Mabalozi wa Urusi katika mataifa kadhaa ya Ulaya, yakiwemo Austria na Uingereza, wametakiwa kufika katika wizara za mambo ya kigeni za mataifa hayo kujieleza kuhusiana na agizo la jana la Rais Vladimir Putin.
Taarifa kutoka kwa wakuu wa Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, na Charles Michel imesema umoja huo unatafakari kuwekea vikwazo benki za Urusi zilizo na matawi katika maeneo ya majimbo yanayodhibitiwa na waasi wa Ukraine ya Luhansk na Donetsk. Hata hivyo vikwazo hivyo vitahitaji ridhaa kutoka kwa nchi zote 27 wanachama.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema Uingereza itaweka vikwazo kwa benki tano za Urusi na watu watatu "wenye hadhi ya juu" kufuatia kutumwa kwa wanajeshi katika mikoa miwili inayoungwa mkono na Moscow.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ametangaza kuwa mchakato wa kuidhinisha matumizi ya bomba la gesi la Nord Stream 2 umesimamishwa. Ujenzi wa bomba hilo linaloziunganisha Ujerumani na Urusi kupitia chini ya bahari umekamilika, lakini utata unaolizunguka umelizuia kuanza kufanya kazi hadi sasa.
Aidha kansela Scholz amesema "Rais wa Ukraine Zelenskiy anastahili heshima yetu kubwa, kwamba nchi yake haikubali kuchokozwa na Urusi, kwa sababu ndicho hasa Rais wa Urusi anachosubiri, ili kuwa na kisingizio cha kuteka Ukraine nzima."