SoC01 Urithi Unaotutenganisha

Stories of Change - 2021 Competition

Kaka Junior

Member
Sep 15, 2015
13
4
Nakusalimu ndugu usomaye makala hii. Makala hii haikusudii kumlazimisha mtu akubaliane na mtazamo ulioandikwa ndani yake, kila msomaji ana uhuru wa kukubali au kukataa chochote kilichoandikwa katika makala hii, au hata makala nzima. Makala hii ni ndefu ila ni vema ukijitahidi kuisoma yote. Ukiona yaweza kuleta badiliko katika jamii yetu kama itafanyiwa kazi, usisite kuipigia kura.

Hebu fikiria! Ni vipi kama mtu umpendaye sana angekupa zawadi nzuri ya kitu ambacho unakihitaji sana maishani mwako, lakini kwa zawadi hiyo uhusiano wenu unapaswa upungue sana au kwisha kabisa? Je, bado ungeipenda na kuipokea hiyo zawadi? Je, ungefurahia zaidi zawadi hiyo au uhusiano pamoja na zawadi ambayo haitetereshi uhusiano wenu? Bila shaka ungependa sana kupewa zawadi, lakini ungependelea zaidi zawadi ambayo haitachangia uhusiano kutetereka.

Sasa ni vipi kuhusu watoto wetu? Tunawapatia zawadi nzuri sana iitwayo elimu, lakini bahati mbaya wazazi wengi wa kizazi hiki tumelemewa zaidi na mzigo wa kuwapa watoto zawadi hii kiasi kwamba mahusiano yetu na watoto yako hatarini sana, wengine yakiwa yamevunjika tayari. Hebu tusonge pamoja na kushauriana kupitia makala hii kuona jinsi ambavyo tunaweza kuweka vizuri jambo hili ili tusiishie kuzaa na tukajikuta hatuna watoto.

Karibu kila mzazi, kwa uwezo na hadhi yoyote aliyonayo, anatamani ampatie mtoto wake elimu bora. Hii hasa inatokana na dhana ambayo inaaminiwa na watu wengi, kwamba elimu ndio urithi mkubwa zaidi unaoweza kumwachia mtoto wako. Na kwa sababu hiyo kila mmoja anajitahidi kupambana ili amwachie mwanaye urithi mzuri kwa kumpatia elimu bora. Pamoja na kuwa na lengo zuri katika hili, urithi huu umekuwa mtego na kuaza kusababisha utengano badala ya kutuunganisha. Ziko sababu nyingi zinazopelekea hilo, lakini hapa tutachambua mbili kuonyesha jinsi jambo hili muhimu linavyotutenganisha na kuharibu mahusiano kwa kasi sana.

  1. Umri wa mtoto kuazishwa shule
Nyakati hizi ni kama hakuna umri rasmi wa kupeleka mtoto shule, tofauti na huko nyuma. Kwa sasa mtoto akiwa hata na miaka miwili unaweza kukuta ameanzishwa shule. Ziko sababu kadhaa katika hili ikiwemo mzazi kutokuwa na muda wa kuweza kukaa na mtoto au kumwacha mtoto nyumbani kutokana na majukumu ya kikazi au mengineyo. Lakini pia watoto wengine wanapelekwa shule mapema sana kwa sababu mzazi anaona mtoto ni mtundu sana kwa hiyo inabidi asishinde nyumbani. Ipo pia dhana ya mtoto kuwahishwa kuanza shule ili apate muda wa kutosha kusoma akiwa bado umri unaruhusu na ahitimu ngazi muhimu za kielimu akiwa bado na umri mdogo. Zote hizi pamoja na sababu nyingine zinaweza kuwa sababu nzuri na zenye mashiko, lakini je, ni kwa kiwango gani tumetathmini matokeo yake kabla hayajatokea?

Huyu mtoto anayepelekwa shule akiwa mdogo sana na wengine wanapelekwa hata kuongea vizuri hawajaweza, je, ameshakaa mtaani vya kutosha? Je, ameshawajua wazazi wake na kuhusiana nao kwa kiwango cha kutosha? Kwa sababu mtoto huyu kuna uwezekano wa kutumia muda mwingi akiwa shule kuliko akiwa na wazazi au jamii yake. Mtoto yeyote anahitaji ukaribu sana na mzazi, lakini mtoto wa mpaka miaka mitano anahitaji ukaribu zaidi. Anamhitaji mzazi labda kuliko mtu mwingine yeyote. Anapopelekwa shule anabadilishiwa mazingira, anabadilishiwa watu, na pia anabadilishiwa mahitaji. Na kwa hiyo taratibu anaanza kuwa sehemu ya shule zaidi ya alivyo sehemu ya nyumbani.

Kumbuka na zingatia jambo moja la msingi; wewe umeishi hapa duniani na kuna namna unaijua dunia. Kamwe usi- assume kwamba mtoto anajua vitu au atahusiana na mzazi na jamii automatically. Yeye kila kitu ni kipya kwake na anahitaji utulivu wa kuvi- study na kuvipokea. Hajawahi kuwa duniani hapo kabla (wale wanaoamini vinginevyo mtanisamehe) na anahitaji mwongozo wa kutosha wa mzazi kabla ya mtu mwingine yeyote, wa jinsi ya kuishi na kuhusiana hapa duniani, hajui chochote.

Kwa hiyo unapomtoa kwako mapema wakati ambapo anakuhitaji sana, ni kwa kiwango hicho hicho utamkosa maisha yako yote. Kwa sababu hajawahi kujifunza kuishi na wewe, wala kuhusiana na wewe. Atapata elimu mapema, tena labda elimu nzuri sana, lakini imemuondoa kwako kabla moyo wake haujakumeza na kuimeza jamii, na kujua kwamba kwa kiwango chake chochote cha elimu, yeye ni jamii na mwanajamii. Kitu pekee anachojua vizuri tangu amepata akili ya kujitambua ni shule (elimu) mana ndiko alikojikuta huko. Atakwenda shule na tangu hapo hatawahi kurudi kama mwanadamu huru kwenye jamii yake, ila kama mwenye majukumu mazito, ama ya kielimu au ya kimaisha baada ya elimu.

Ni kweli shule kutakuwa na likizo lakini hata katika hizo atakuwa ni mwanafunzi. Na kimsingi likizo za siku hizi ni kama tu kuwafanyia watoto uhamisho kutoka kuwa wanafunzi wa shule kuwa wanafunzi wa tuition. Huyu mtoto anakuwa hajapata muda wa kutosha wa kuwa huru mtaani kucheza, kukimbizana na kufanya kila ujinga anaoweza kufanya kwa ngazi ya mtaani/ nyumbani. Hii ni hatua muhimu sana ambayo kila mtoto anaihitaji kwa sababu kabla ya kupata elimu rasmi anahitaji sana hii isiyo rasmi ya mtaani. Anahitaji kuipata hii kwa upekee wake kabisa bila kuingiliwa kwanza na ile rasmi ya shuleni, imsaidie kumjenga na kumfanya kuwa mmoja wa wanajamii. Aijue jamii na kujihusisha nayo, na ku- belong kwa jamii yake, halafu sasa ndio aende shule. Wengi wa mnaosoma makala hii mtakuwa mashahidi (kwa wale ambao umri umesonga kidogo) kuwa mlilelewa namna hii na mkawa jamii kabla ya kuwa wanafunzi, na hilo bila shaka mnaweza kukiri kuwa munaona faida yake. Mtoto anapoanza shule, anakuwa ndio ameanza maisha mengine. Hata kama anakwenda asubuhi na kurudi mchana au jioni, ni wa shule na shule ndio maisha yake. Anapomaliza ngazi moja anakwenda nyingine moja kwa moja, mpaka anapokuja kutulia kabisa ni baada labda ya kuhitimu chuo (kama amepata fursa hiyo). Anapohitimu chuo au ngazi yoyote ile, harudi tena nyumbani kufanya yale aliyoyakosa akiwa mtoto, isipokuwa anatumbukizwa moja kwa moja kwenye harakati za maisha, aanze kupambana kutoka kwenye utegemezi wa wazazi/ walezi ili awe yeye.

Swali ni je, tangu ajitambue amewahi kupata nafasi ya kuishi kwa uhuru bila kuwaza masomo au anaendeshaje maisha? Kwa watoto wengi wa kizazi hiki jibu linaweza kuwa ni hapana. Elimu ameipata nzuri lakini amekosa wazazi na jamii.

  1. Bweni au kutwa!
Hii pia ni changamoto nyingine linapokuja suala la elimu kwa watoto wa kizazi hiki. Ni kawaida sana mtoto wa shule ya msingi kupelekwa shule ya bweni kwa sasa, wengine hata kuanzia chekechea. Lengo linaweza kuwa zuri sana, lakini matokeo yanaweza yasiunge mkono uzuri wa lengo.

Wengi tunaamini kwamba mtoto akipelekwa bweni atapata utulivu wa kutosha kusoma tofauti na akiwa kutwa. Lakini swali langu kwako mzazi, huyu mtoto wa shule ya msingi uliyempeleka bweni ni nani anamlea kwa nafasi yako? Ni mwalimu? Matroni? Au ni wanafunzi wenzake? Na je, malezi unayoamini wanampatia ndio ambayo unataka ayapate mwanao na kwa kiwango hicho anachopata?

Kwa kawaida malezi ya mtoto yanapaswa kuwa ya muunganiko wa wazazi/ walezi, jamii, na walimu. Je, unapompeleka shule ya bweni anapata dozi kamili? Waswahili wakasema, asiyefunzwa na mamaye (mzazi/ mlezi) hufunzwa na ulimwengu. Hii inaonyesha ukubwa wa kiwango cha umuhimu wa mafunzo ya kutosha ya mzazi/ mlezi kwa mtoto kabla ya kumtoa na kumkabidhi kwa ulimwengu. Kila mtu anapozaa mtoto, kuna mtu fulani anamtarajia kutoka kwa huyo mtoto miaka mingi ijayo. Na yule unayemtarajia atokeze kutoka kwa mtoto huyo anatengenezwa na wewe. Mwalimu au matroni unayempa mtoto hataweza kukuletea matokeo unayoyataka, na kimsingi anashughulika na watoto wengi sio wako tu. Yeye anapaswa kuchangia matokeo na sio kuwa mzalishaji mkuu wa matokeo.

Mimi ninaamini kitu kimoja, Mtoto anazaliwa, lakini mtu anatengenezwa. Unaweza kuzaa mtoto wa kiume lakini usitengeneze mwanaume kulingana na malezi utakayompatia. Jinsi/ jinsia mtoto anazaliwa nayo, uanaume au uanamke hutengenezwa. Hilo labda tutalitazama kwa kirefu wakati mwingine kama mada inayojitegemea.

Kwa hiyo, kunaweza kuwa na lengo zuri la kupeleka mtoto shule ya bweni ilia pate elimu bora kutokana na mazingira au jina la shule, lakini je, ataendelea kuwa mtoto wako baada ya kupata elimu yake? Kwa sababu umri wa shule ya msingi ni kipindi ambacho mtoto anamhitaji sana mzazi na anahitaji vingi kutoka kwake zaidi ya pocket money na kutembelewa kwenye visiting day. Anahitaji kujua taratibu na desturi za jamii yake na familia yao. Anahitaji kupata mwongozo wa kimaisha wa familia yao, anahitaji kuwa mtu wa hiyo familia kwa kila namna. Anahitaji ku- belong, kuwa part ya familia. Nina mifano kadhaa ya watu waliojikuta wanatoa machozi baada ya kuwatembelea watoto shuleni na kukuta watoto baada ya kupokea zawadi walizowapelekea hawakuwa na shughuli nao tena, kwa sababu watoto hawakujua kama wanapaswa kurudi kuendelea kukaa na wazazi baada ya kupeleka zawadi zao bwenini. Hawajafundishwa kuhitaji hiyo moment.

Tulipoanza kulikuwa na swali la kama ungekuwa tayari kupewa zawadi unayoihitaji sana lakini iwe kwa gharama ya kukuondolea uhusiano na anayekupa zawadi hiyo. Watoto wetu wangependa sana tuwape elimu bora, lakini si kwa kuwafukuza nyumbani mapema au kuharibu uhusiano baina yetu na wao. Waswahili husema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Kila hatua unayochukua juu ya mtoto wako inatafsirika kama malezi, hata kama inamuweka mbali na wewe, unamlea na atakua kwa kuwa mbali na atahakikisha anakaa mbali kweli kweli. Ni kweli tuna kazi na majukumu mengi sana, lakini tafadhali sana, yasitutenge na watoto wetu hasa wakati huu wanapotuhitaji sana, kwa sababu wakati tutakapowahitaji sana hatutawapata na wao. Kwa sababu tuliwafundisha kutokupatikana wala kuwepo kwa ajili yetu. Ni kweli tunatafuta kwa ajili yao, lakini tusije tukajikuta tunatafuta sana kwa ajili yao ili baadaye tuje kuwatafuta na wao. Elimu ni zawadi na urithi mzuri sana, lakini isitutenge na wanetu.

Mwandishi wa makala hii ni Junior J. Mkilindi. Hairuhusiwi kunakili au kutumia makala au sehemu yoyote ya makala hii bila ruhusa ya mwandishi.
 
Back
Top Bottom