Urais wa Kikwete hauna ubia, mafisadi washughulikiwe’

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,825
287,849
jk.JPG

Rais Jakaya Mrisho Kikwete

Urais wa Kikwete hauna ubia, mafisadi washughulikiwe’
Oscar Mbuza
Daily News; Monday,April 28, 2008 @20:04

Rais Jakaya Kikwete.

“NAMUONEA sana huruma Rais Jakaya Kikwete,” hiyo ni kauli ya utangulizi ya Mbunge wa Hai, Fuya Kimbita, akizungumzia kukithiri kwa tuhuma za ufisadi zinazowaandama viongozi mbalimbali wa serikali.

Kimbita ni miongoni mwa Wabunge wa Bunge la Tanzania, waliotoa maoni yao kuhusiana na kukithiri kwa tuhuma hizo za ufisadi na kutoa ushauri wa nini kifanyike katika kukabiliana na hali hiyo.

“Kama mwenyewe (Rais Kikwete) alivyosema kwamba Urais wake hauna ubia. Ni lazima Rais asimame juu ya maneno yake, kama kweli ameazimia kukabiliana na vitendo vya ufisadi,” anasema Kimbita.

Kimbita anasema kama Rais Kikwete, hatakuwa na dhamira ya dhati katika kukabiliana na vitendo vya ufisadi ni wazi kwamba mustakabali wa Chama cha Mapinduzi na serikali kwa ujumla, itakuwa hatarini.

“Upo uwezekano mkubwa wa kuzuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Tofauti ya maisha imekuwa kubwa, huku masikini wakizidi kuongezeka, hali hii ni hatari kwa mustakabali wa Taifa,” anasema Kimbita.

Mbunge huyo wa Hai anasema ni lazima viongozi wa serikali, waheshimu rasilimali za Taifa na waepuke kuweka maslahi yao binafsi mbele kama ilivyo sasa.

“Viongozi wawe na dhamira ya dhati ya kuwaondolea wananchi umasikini. Hakuna sababu ya Watanzania, kuwa masikini wakati wana rasilimali nyingi, kama vile madini, ardhi yenye rutuba, bandari, mifugo, wanyamapori na nyinginezo.

“Nchi kama Singapore wamekuza uchumi wao kwa kutumia bandari tu na Botswana wao wamenufaika na madini na mifugo. Sisi tupo nyuma kiuchumi huku viongozi wetu wachache wakijilimbikizia mali nyingi, hii ni hatari kubwa,” anasema Kimbita.

Hata hivyo, Kimbita anasema kwa kiongozi kujihusisha na vitendo vya ufisadi ni dalili ya wazi kwamba kiongozi huyo anatumiwa na shetani na haridhiki na kile anachokipata.

“Historia itatuhukumu, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na kiasi na ndio maana hakutaka kujilimbikizia mali. Katika suala la ufisadi ni lazima urafiki na undugu, vikae pembeni. Watanzania tuwe kitu kimoja katika kukabiliana na vitendo hivi,” anasema.

Anasema yeye binafsi ana imani na Rais Kikwete, kwamba ana dhamira njema katika kukabiliana na vitendo hivyo, lakini anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa viongozi wa chini yake, ambao wameathiriwa na tabia ya ufisadi.

Anasema ingawa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, lakini kwa hali iliyofikiwa sasa ni lazima Tanzania iwe nchi ya kidikteta ili kurejesha nidhamu kwa viongozi wa serikali.

“Mimi naona hakuna sababu ya kusubiri uamuzi wa Mahakama. Kiongozi anapohusishwa na vitendo hivi na kukawa na ushahidi wa kutosha wa kimazingira, kitu cha kwanza ni Rais Kikwete kuagiza fedha za kiongozi huyu kushikiliwa wakati uchunguzi unafanyika.

Unakuta mfanyakazi wa serikali ana nyumba 30 hadi 40, lakini mshahara wake hauwezi kujenga nyumba hizo, sasa huyu mtu anapata wapi fedha hizi?” anahoji Kimbita.

Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro, anasema vitendo vya ufisadi vimeshamiri sana hivi sasa lakini msingi wake mkubwa ukianzia katika serikali za awamu ya pili na tatu.

“Serikali ya awamu ya nne haiwezi kukwepa hili, lazima wahusika wachukuliwe hatua mara moja wanapohusika na vitendo vya ufisadi.

Ni lazima Rais Kikwete ajitenge na kundi hili la ufisadi. Nakumbuka maneno yake mwenyewe aliwahi kusema Urais wake hauna ubia. Ni Watanzania ndio waliompa urais na si mafisadi ni lazima awashughulikie hawa watu,” anasema Kimaro.

Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa, anasema vitendo vya ufisadi vimechukua uelekeo mbaya hivi sasa na kwa kiasi kikubwa vinaathiri imani ya wananchi dhidi ya CCM na serikali yake.

“Ni vitendo vilivyoanzia kwenye serikali za awamu ya pili na tatu, lakini mpasuko wake umeangukia katika serikali ya awamu ya nne.

Si siri kuona sasa viongozi wetu, wanabainika kuhusika katika uingiaji wa mikataba mibovu kama ile ya IPTL, BoT, Richmond, Buzwagi na hata katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira,” anasema.

Mwambalaswa anasema anamhurumia Rais Kikwete, kwa vile katika miaka mitatu tangu aingie madarakani, amekuwa akijishughulisha na migogoro zaidi, badala ya kushughulikia maendeleo ya jamii.

“Hii ni hatari kwani inafanya utekelezaji wa Ilani ya CCM kuwa ngumu. Kama kweli tunalenga kutimiza ahadi zetu kwa wananchi ni lazima serikali ishughulikie suala la ufisadi na kulimaliza haraka iwezekanavyo.

Ni vizuri kama Rais Kikwete atawaondoa mara moja viongozi ndani ya Baraza la Mawaziri na maofisa wa juu serikalini, ambao wana dalili za kuhusika na vitendo vya rushwa,” anasema Mwambalaswa.

Mbunge huyo anaonyesha wasiwasi wake, kwamba matukio ya vitendo vya ufisadi dhidi ya viongozi waandamizi wa serikali, yatapunguza imani ya wananchi kwa serikali yao.

Mwambalaswa anasema anaamini kwamba vyombo maalumu, vinavyotumika kuchunguza maadili ya viongozi wa serikali, vinawafahamu fika viongozi wenye tabia za ufisadi na ni vizuri vyombo hivyo vikamsaidia Rais Kikwete katika kuwachuja viongozi hao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Koani, Haroub Said Masoud anasema ni vizuri kama itaundwa Kamati Maalumu ya Bunge ili kukabiliana na vitendo vya ufisadi vinavyowahusisha viongozi wa serikali.

“Bunge lina kamati nyingi ambazo kazi yake ni kufuatilia kwa kina sekta mbalimbali za serikali. Nadhani sasa wakati umefika wa kuundwa kwa Kamati ya kushughulikia ufisadi,” anasisitiza Masoud.

“Nadhani dhamira ya Rais ni nzuri na ndio maana hivi karibuni alivunja Baraza la Mawaziri, kutokana na tuhuma za ufisadi, lakini ni lazima Rais asaidiwe na vyombo mbalimbali na hasa Bunge,”anasema.

Hata hivyo hoja hiyo ya Masoud aliyoitoa bungeni hivi karibuni, ilikosa nguvu baada ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kuipinga akisema imetolewa wakati usio mwafaka. Mbunge huyo ameahidi kuiwasilisha hoja hiyo upya.

Mbunge wa Kalambo, Ludovick Mwananzila, anasema ingawa hana majibu ya moja kwa moja kuhusu sababu zinazowafanya viongozi wengi wa serikali kujihusisha na vitendo vya ufisadi, lakini anasema tabia hiyo ilikuwapo tangu dunia ilipoundwa.

Hata hivyo anasema ni lazima Rais Kikwete atumie nguvu zake zote ili kuweza kukabiliana na vitendo hivyo vya ufisadi, ambavyo vinawahusu viongozi wa juu katika serikali yake.

“Naamini Rais anaweza kurekebisha hali hii. Ipo mifano inayoonyesha wazi kwamba anakerwa na vitendo hivi na anayo dhamira ya dhati ya kukabiliana navyo,” anasema Mwananzila.

Anasema kushamiri kwa matukio hayo ya ufisadi, kwa kiasi kikubwa kumepunguza imani ya wananchi dhidi ya serikali yao, ingawa ukweli ni kwamba ni viongozi wachache sana ndio wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Kwa pamoja, Wabunge hao, wanamtaka Rais Kikwete kusimama juu ya kauli aliyoitoa kwa Watanzania kwamba Urais wake hauna ubia na mtu yeyote.
 
Source ni Daily News; Monday,April 28, 2008 @20:04 kweli mkuu?
JK ana wakati mgumu wa kuwatoa 'wabia' wake kwenye Urais......kama watu walimwaga fedha 'zao' nyingi na kutumia muda wao mwingi kukusaidia ushinde ndani ya chama, ni vigumu kuwaondoa katika uendeshaji wa serikali.
Lets see if he has the guts and he is firm on issues.
 
Sasa hivi hana jinsi inabidi awatoe au watamtoa yeye, ila anatakiwa kuwa makini kwani wanaweza kumtanguliza badala ya yeye kuwatanguliza.
 
Source ni Daily News; Monday,April 28, 2008 @20:04 kweli mkuu?
JK ana wakati mgumu wa kuwatoa 'wabia' wake kwenye Urais......kama watu walimwaga fedha 'zao' nyingi na kutumia muda wao mwingi kukusaidia ushinde ndani ya chama, ni vigumu kuwaondoa katika uendeshaji wa serikali.
Lets see if he has the guts and he is firm on issues.

Kwa nini aruhusu kuwa na wakati mgumu?Katiba ipo inamlinda kila analotaka kufanya.Yeye atende kama alivyoapa pale Uwanja wa TAIFA mwezi Decemba 21, 2005?Urafiki ktk kuongoza nchi ni kutumbukia shimoni.
Ukiona unazama majini na unataka kujiokoa inabidi uvue viatu,nguo na vyote vinavyoweza kukufanya uzame.Avue mafisadi wote
Kwa nini akae na watu ambao ni irrespossible tena wanadharau wale waliowaajiri(wananchi).Wananchi wakigoma wote au wasifike nusu kupiga kura kutakuwepo uongozi?
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom