Urais nyuma ya mgogoro mpaka Tanzania na Malawi

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Felix Mwakyembe

Mbeya
Toleo la 254
15 Aug 2012



  • Malawi ni 2014 wakati Tanzania ni 2015
  • Kambi za Urais zatumia kete ya mgogoro
  • Wamalawi waishangaa Tanzania kukimbilia vita


KUNDI la wakazi wa jijini Mbeya waliovuka mpaka kuingia nchini wakitokea Mzuzu, Malawi walikokwenda kuhudhuria harusi wamepatwa na mshituko kukuta taarifa za maandalizi ya vita dhidi ya majirani zao hao.
Mshituko wa wakazi hao wa jijini Mbeya ulitokana na ukweli kwamba katika siku zile tatu walizoishi nchini Malawi kwa tukio hilo la kijamii, hawakuwahi kusikia kauli na tambo za vita kutoka kwa viongozi wa nchi hiyo au wananchi wao.

"Hali ilikuwa tete huku (Tanzania) kuliko Malawi, hatukusikia wananchi wakilizungumzia, hata Rais wao katika mkutano aliofanya tukiwa huko alisema hakuna tatizo watamaliza kwa kuzungumza. Tulikuwa huru kutembea na kufurahia maisha wakati wote tukiwa kule," anasema mmoja wa wakazi hao waliokuwa nchini humo hivi karibuni.


Mbali ya wananchi hao wa kawaida, juma lililopita aliyepata kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karonga nchini Malawi, Felix Mkandawire ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Chikwawa alikuwa jijini Mbeya kwa matembezi binafsi akiwa amefuatana na marafiki zake.


Mkuu huyo wa Wilaya ya Chikwawa iliyopo Kusini mwa nchini hiyo, ni miongoni mwa viongozi na wananchi wa Malawi wenye kawaida ya kuja nchini kwa matembezi na kukutana na ndugu zao Watanzania, na hiyo pia ndivyo ilivyo kwa Watanzania kutembelea Malawi, ni jambo la kawaida sana.


Mgogoro wa mpaka kati ya Malawi na Tanzania uliibuka kufuatia hatua ya Malawi kuanza utafiti wa mafuta katika Ziwa Nyasa huku mmoja wa viongozi wake akitoa kauli iliyodai kuwa ziwa lote hilo linamilikiwa na Malawi, kauli ambayo haikuipendeza Serikali ya Tanzania.


Lakini katika hali iliyoshangaza wengi, hususan wananchi mkoani Mbeya, ni hatua ya viongozi nchini kukimbilia kutoa kauli kali ikiwamo kuwa tayari hata kwa vita endapo majirani zao hao, Malawi, wataendelea na utafiti wao wa mafuta ziwani humo pamoja na madai ya umiliki wa ziwa lote.


Katikati ya mkanganyiko huo wa mpaka wa nchi mbili hizi kunajitokeza kambi zenye kujiandaa kukamata dola katika chaguzi za mwaka 2014 nchini Malawi na 2015 nchini.


Kauli zenye tambo zilizotolewa na mawaziri watatu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya Bunge linaloendelea huko Dodoma, zimetazamwa na wachambuzi wa siasa za nchi hii kwa tahadhari kubwa huku zikibainishwa kuwa na sura ya harakati za mbio za urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, 2015.


"Hawa wote wako kwenye kambi zenye kuwania Urais katika uchaguzi ujao wa 2015, wanautumia huu mgogoro kama kete yao ya kisiasa, wanalazimisha kuaminika na wananchi kwamba wao ni majasiri, si weak candidates (si wawania dhaifu wa urais)," anasema mkazi mmoja jijini Mbeya.


Hisia za mgogoro huo kutumika kama mtaji wa kisiasa kwa kambi zenye kuwania urais katika chaguzi zijazo katika nchi hizo mbili, zipo kwa baadhi ya wananchi nchini Malawi ambapo baadhi wanamtaja Waziri wa Mambo ya Ndani na Uhusiano wa Kimataifa kwa Mambo ya Kiusalama nchini humo, Uladi Musa kuwamo kwenye kambi ya Rais wa sasa kati uchaguzi ujao.


Musa ambaye yupo kwenye chama cha Rais Joyce Banda cha Peoples Party, anaelezwa kuwania nafasi ya Makamu wa Rais kwa Mkoa wa Kati wa Malawi huku Rais wake akiwa hana mpinzani.

Katika uchaguzi ujao nchini humo kutakuwa na makamu wa Rais watatu mmoja kutoka kila eneo, kwa maana ya Kusini, Kati na Kaskazini.

Tayari Musa anatajwa kuwa na upinzani mkubwa ndani ya chama hicho akielezwa kuwa ni mgeni kwenye chama hicho, wakati wapo waliokipigania hadi hapo kilipo ambao wanajiona kustahili zaidi kugombea nafasi hiyo.

Ni katika mazingira hayo ambapo inaelezwa kuwa anatumia kila nafasi kuweza kujiweka karibu na wapiga kura, hivyo mgogoro wa mpaka ulioibuka hivi karibuni anautumia kama moja ya karata zake muhimu.

Hapa nyumbani, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta alikuwa wa kwanza kutoa tahadhari kwa Serikali ya Malawi juu ya hatua yake ya kuendelea na utafiti wa mafuta kwenye Ziwa Nyasa na kwamba Tanzania iko tayari kulinda mipaka yake kwa gharama zozote zile.


Sitta alitoa kauli hiyo pale wabunge waliposhinikiza kupewa kauli ya Serikali kuhusu taarifa walizozipata za Malawi kudai Ziwa lote la Nyasa kuwa mali yake hivyo kuanzisha utafiti wa mafuta ziwani humo pasipo mashauriano na majirani zake wanaolizunguka ziwa hilo.


Mbali ya Tanzania na Malawi, nchi nyingine inayopakana na Ziwa Nyasa ni Msumbiji ambayo hata hivyo katika mgogoro unaoendelea imekaa pembeni.


Baada ya kauli hiyo ya Serikali kupitia kwa Waziri Sitta aliyekuwa akikaimu nafasi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wananchi waliendelea kusikia matamko yenye tambo zenye kuashiria utayari wa Tanzania kuingia vitani na Malawi, jambo lililoshangaza wananchi wengi hususani mkoani Mbeya ambao ndio walio jirani na nchi hiyo huku wakiwa na maingiliano makubwa ya kiuchumi na kitamaduni.


Waliofuata baada ya Sitta ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambaye naye alitoa kauli rasmi ya Serikali kuhusiana na mgogoro huo huku akisisitiza kauli yake kwa kurudia mara tatu, lakini akihitimisha kwa kuwasihi wabunge kuacha diplomasia kuchukua nafasi yake.

Sinema ya tambo za viongozi nchini ziliendelea na safari hii akajitosa Mbunge wa Monduli na Mwenyekiti wa

Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa naye akisema Tanzania iko tayari kuingia vitani na Malawi.


Akizungumza mjini Dodoma, Lowasa alisema Tanzania imejiandaa kiakili na kivifaa kuingia vitani na Malawi kama italazimika na kwamba Kamati yake imeridhishwa na maandalizi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Katika maelezo yake, Lowasa alirudia mara kwa mara kuhusu utayari wa Tanzania kuingia vitani na Malawi kama vile majirani hao walitangaza vita na Tanzania.

Kauli ya utayari wa vita iliwafadhaisha zaidi wananchi waishio mpakani, mikoa ya Mbeya na Ruvuma ambao mbali ya kuwa waathirika wa moja kwa moja na vita hiyo inayohubiriwa na wanasiasa nchini, wamekuwa na maingiliano ya kindugu na ndugu zao wa Malawi ya karne na karne.


Hadi sasa Serikali ya Malawi haijatoa tamko lolote lenye kuashiria nia ya vita zaidi ya kusimamia hoja yake kwamba Ziwa Nyasa, ambalo wao kwa miaka mingi sasa wanaliita Ziwa Malawi, kuwa ni lao kwa asilimia 100.


Serikali ya Malawi inasimamia hoja hiyo wakitumia mikataba iliyowekwa wakati wa ukoloni ambayo Tanzania inakataa kuitambua, lakini pasipo kuweka hoja za msingi mezani na badala yake kutumia vitisho vya vita.


Maoni ya wananchi wa Malawi yanaonyesha kuishanga Tanzania kusogeza askari mpakani, wakisema Malawi inaamini kuwa njia iliyo sahihi ni kukaa pamoja kwenye meza ya majadiliano na kumaliza tofauti zilizopo.


Hata Rais wao, Bi Banda hajatoa kauli ya serikali zaidi ya kusema hakuna tatizo kwani ni jambo la majadiliano na zaidi kuelezea hisia zake kuwa yuko tayari kuifia Malawi.


Hoja ya mgogoro huo kutumika kama mtaji wa kisiasa kuelekea chaguzi kwenye nchi hizi mbili jirani, inaelezwa pia kuthibitishwa na hatua ya viongozi hao kutoa misimamo mikali wakati wakifahamu fika kwamba baadaye mwisho wa mwezi huu, watakutana mjini Mzuzu kwa ajili ya majadiliano kuhusu suala la mpaka huo.


Miongoni mwa wanasiasa wasiokubaliana na kauli za viongozi wenye kuhubiri vita, ni pamoja na Richard Kasesela ambaye mbali ya kuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi ni mwenyeji wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ambaye anaziona kauli za vita kuwa zisizowatakiwa mema wananchi wa nchi mbili hizo.


Kasesela anashangaa kuona diplomasia inawekwa pembeni na wanasiasa, tena wenye matamanio ya Urais 2015.

"Kuna ngazi katika mazungumzo ambazo hazijatumika bado. Tunakimbilia kutangaza vita, si sahihi kabisa, kwanza watu mnakaa chini, mnajadiliana mkishindana kuna usuluhishi ambao unaleta upande wa tatu kusimamia majadiliano. Na hapa hutumika watu wenye busara, suala la kutangaza vita haipo," anasema Kasesela.

Shughuli za utafutaji mafuta kwenye Ziwa Nyasa kwa upande wa Malawi zilianza miaka miwili iliyopita na muda wote huo hakukuwapo kauli zozote zenye kutishana kati ya mataifa haya mawili masikini duniani.


Wakati mgogoro huo ukishika kasi, mwezi uliopita nchi hizo mbili zilizindua Mpango mkubwa wa Mto Songwe ambao unatarajiwa kuwanufaisha zaidi wananchi masikini wa nchi hizo kupitia miradi yake ya kilimo cha umwagiliaji, umeme na uvuvi.











 
Kwakweli hata mimi nimewashangaa sana viongozi wetu kwa kuona kwamba vita ndio suluhisho pekee. Tunatakiwa kutumia busara na sio kukurupuka. Ni bora njia za kidiplomasia zikatumika kwa manufaa ya nchi zote mbili. Ninakubali kabisa kwamba katika hili, Malawi wameonyesha ukomavu na busara za hali ya juu kuliko sisi.
 
Back
Top Bottom