UPORAJI WA RASILIMALI: Viongozi wageukia udalali (Bakari M Mohamed) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

UPORAJI WA RASILIMALI: Viongozi wageukia udalali (Bakari M Mohamed)

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Ng`wanakidiku, Jan 11, 2012.

 1. Ng`wanakidiku

  Ng`wanakidiku JF-Expert Member

  #1
  Jan 11, 2012
  Joined: Apr 18, 2009
  Messages: 1,196
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  ENZI za TANU, uongozi ulikuwa ni utumishi wa umma! Viongozi wa chama na serikali walilelewa na kuelekezwa na utashi wa kuwatumikia wananchi kwa minajili ya maendeleo ya watu.
  Hapa ndipo Azimio la Arusha lilipozaliwa na zaidi, azimio lile lilisisitiza juu ya hakikisho la umiliki wa njia kuu za uchumi kuwa mikononi mwa wananchi kwa kupitia serikali ya watu.
  Kwa ujumla, njia kuu za uzalishaji mali zilimilikiwa na umma na rasilimali za nchi zilikuwa mikononi mwa viongozi waliodhaminiwa na chama.
  Ukiachilia mbali matatizo ya utekelezaji wa maazimio kadha wa kadha juu ya ujenzi wa jamii ya watu waliyo sawa na huru katika kuinua hali za uchumi wa wananchi na maendeleo ya nchi kadhalika, rasilimali nyingi za Tanzania zilikuwa zikitumika kwa uangalifu mkubwa katika kuhakikisha kwamba matumizi yake yanawanufaisha wananchi.
  Na pale ilipobainika kwamba uwezo wa maarifa, sayansi na teknolojia ya matumizi ya rasilimali hizo haujafikia kiwango cha uvunaji wake; uongozi wa chama na serikali uliziacha rasilimali hizo kwa matumizi endelevu yatakayozingatia utashi wa watu na maendeleo yao.
  Hata hivyo, muda ulipita na TANU (na ASP) kama vyama vilivyoendesha harakati za uhuru viliunganisha siasa na sera zao na kuzaliwa Chama cha Mapinduzi (CCM). CCM, kama chama cha wakulima na wafanyakazi, kilirithi maazimio yote yenye taathira ya kulinda na kuendeleza rasilimali za Tanzania.
  Japokuwa dunia ilikuwa inabadilika kisiasa, kiuchumi na kijamii; CCM iliendelea na sera ya uchumi hodhi na hususan pale ilipokuwa inalinda matumizi ya rasilimali za Tanzania.
  Mabadiliko yaliyofanywa na viongozi wa CCM miaka ya 1980 na 1990 yaliyotiwa munda na mabadiliko ya mfumo wa siasa, uchumi na jamii wa dunia yalivuruga mujtamaa wa mizania ya matumizi makini ya rasilimali za nchi.
  Kwa kuwa viongozi wengi wa CCM (chama kilichoshika hatamu na chama kinachoongoza serikali kwa sasa) ni watu binafsi wenye ubinafsi na wanaoongozwa na choyo, roho mbaya na ubinafsi kayaya; kwa pamoja na bila ya kutafakari taathira hasi ya kuingia kwenye uchumi holela (soko huria) waliamua kuliweka kando Azimio la Arusha na kuanzisha mfumo wa uchumi unaozingatia udalali dhidi ya rasilimali za Tanzania.
  Kwa jinsi hii, Tanzania imefanywa “shamba la bibi” kwa viongozi kuendesha shughuli za udalali wa kiuchumi na hata kuivuruga jamii kwa mfumo wa uchumi unaoendeshwa pasipokuwa na mizani ya uhuru, haki na uadilifu.
  Muktadha wa makala umeanza kwa jinsi ya kuonyesha upotovu wa uongozi wa siasa ulivyopoteza mwelekeo juu ya umiliki, matumizi na menejimenti ya rasilimali za Tanzania katika kufikia malengo ya vita dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi (maadui watatu wa taifa waliyotangazwa baada ya uhuru).
  Hakuna asiyefahamu kwamba Tanzania ya sasa (miaka 50 baada ya uhuru) bado ingalipo kwenye umasikini, ujinga, maradhi, na sasa ameongezeaka adui mwingie mbaya zaidi, yaani ufisadi! Ufisadi ndio zao la “udalali” wa viongozi wa CCM waliyeshika nafasi za uongozi ndani ya chama na serikali yake.
  Uongozi umeacha kuongoza kwa uhuru, haki na uadilifu; wote kwa jinsi yao, wanafanya ufisadi (uharibifu) kwenye siasa, uchumi na jamii.
  Tanzania ni nchi ya kilimo. Na kwa jinsi hiyo sehemu kubwa ya uchumi wa wananchi wake wanategemea kilimo kama “uti wa mgongo” wa kuendesha maisha ya watu na nchi kadhalika. Kwa vyovyote vile, kilimo hutegemea ardhi na tabia nchi.
  Tanzania, kwa sehemu kubwa ya kijiografia, imejaaliwa ardhi inayofaa kwa kilimo cha aina zote kwa mujibu wa utashi wa kilimo cha mazao mbalimbali. Na kwa kulijua hili, Tanzania iliwekeza kwenye kilimo na wananchi wake walishajihishwa wawekeze kwenye kilimo.
  Pamoja na ukweli wa uwekezaji mdogomdogo wa wakulima wadogo; serikali (ya TANU/CCM) iliwekeza kwenye kilimo cha mashamba makubwa kama vile ngano, mpunga, mahindi na ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa.
  Shughuli za uchumi zilizotegemea ardhi zilitengewa maeneo maalum yaliyoainishwa kwa sheria na kanuni za kilimo na ufugaji unaozingatia sayansi na teknolojia ya kisasa katika kuzalisha mazo yenye ubora na kiasi cha kutosha.
  Serikali ya CCM iliposhindwa kwenye menejimenti ya shughuli za uzalishaji kwenye kilimo na mifugo aidha iliamua kuzitelekeza au kuziendesha kwa hasara. Hapa ndipo lilipozuka wazo la ubinafsishaji! Uoni butu wa uongozi wa kisiasa uliona njia ya kutoka hapo kwenye mkwamo wa hama kusindwa kusimamia uchumi ni kubinafsisha. Lilikuwa kosa kubwa la kimkakati. Kwa upande mmoja; ubinafsishaji ulikuwa ni mpango wa kuwanyang’anya wananchi umiliki wa rasilimali na kuwafanya wawe “vibarua” na au “manamba” kwenye ardhi yao.
  Ardhi, kama rasilimali ya pekee waliyorithishwa wananchi na Mwenyezi Mungu, imeporwa na inaendelea kuporwa na wawekezaji wenye uchu na uroho wa kuzalisha ziada kwa gharama ya wananchi wasiyekuwa na uwezo kiuchumi.
  Viongozi wa kisiasa badala ya kusimamia uhuru na haki ya wananchi juu ya umiliki wa rasilimali wamekuwa wa kwanza kufanya kazi ya udalali wa kuuza rasilimali za Tanzania!
  Kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21 (Longhorn, 2011 ukurasa wa 74) neno dalali limepewa maana ya “mtu anayeuza vitu kwa njia ya mnada, mtu anayenadi vitu, mtu anayepanga kuuza kitu cha mtu mwingine ili apate asilimia fulani ya mauzo kama malipo yake; au mtu kati anayeshiriki katika kunadi bidhaa ili apate natija.”
  Kwa jinsi ya kadhia ya Tanzania, viongozi wa CCM waliyepewa dhima ya uongozi wa nchi wamechukua maana zote kama zilivyoainishwa kwenye maana hii! Rasilimali za Tanzania zilinadiwa, ziliuzwa, na faida ya mauzo ya udalali ilikwenda moja kwa moja kwa madalali (viongozi wa CCM) walioshiriki katika mnada wa kuiuza Tanzania.
  Wapo baadhi ya wachambuzi wa siasa, uchumi na jamii katika Tanzania wanaodai nchi imeuzwa; yaani, Tanzania imeuzwa kwa wawekezaji! Kwa sehemu kubwa nakubaliana na dhana na au hoja hii kwa vile uongozi wa chama kinachotawala (kinachounda serikali) hauonyeshi dhamira ya uhuru, haki na adilifu katika kujenga jukwaa la utetezi dhidi ya uporaji wa rasilimali za wananchi unaofanywa na wawekezaji jeuri, wenye uchu na uroho wa kumiliki njia za uchumi kwa gharama ya umasikini wa watu wa Tanzania.
  Viongozi wa kisiasa wamekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha mipango yote ya ubinafsishaji hata pale wananchi walipoonyesha hasira za kuchukia uninafsishaji huo!
  Ukiachilia mbali uporaji wa ardhi kwa kilimo kunakosimamiwa na viongozi wa serikali wanaofanya udalali dhidi ya rasilimali ya ardhi; kuna uporaji unaosimamiwa na viongozi kwenye ardhi inayotumika kwa uchimbaji wa madini. Wananchi wanaomiliki maeneo ya migodi na yanapopatikana madini mbalimbali wamekuwa wakiporwa uhuru na haki yao ya umiliki wa maeneo ya rasilimali zinazopatikana kutoka ardhini.
  Hali hii imewapa wawekezaji nguvu ya kisheria wakiwa nyuma ya viongozi wa kisiasa katika uvunaji wa rasilimali bila kuzingatia uwiano wa watu na mazingira yanayovurugwa kwa uvunaji holela unaozingatia faida zaidi kuliko athari za kimazingira.
  Ni viongozi wa kisiasa waliyesimamia unyang’anyi wa maeneo yenye madini kama vile Bulyanhulu, Buzwagi, North Mara, Kabanga, Tulawaka na kadhalika na ni viongozi hao hao waliyeshiriki kwenye uuzaji holela wa machimbo ya madini yaliyokuwapo na kumilikiwa na serikali.
  Kuna mifano ya Kiwira (mgodi wa makaa ya mawe) na mgodi wa Buhemba uliyefisidiwa na kampuni ya Meremeta na kuachwa na au kutelekezwa na hata kuhujumiwa huku viongozi wa serikali wakishiriki kwa jinsi moja na au nyingine.
  Uongozi wa kisiasa umekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha udalali na hatimaye kuuzwa kwa rasilimali pasipo kuwa na aibu ya uwajibikaji.
  Ukiangalia ardhi iliyoporwa na viongozi wa kisiasa na kwa jinsi ambayo hata umiliki wake unatia mashaka ni vema tujikumbushe uporaji wa mashamba ya miwa ya Mtibwa na kiwanda cha kusindika sukari! Angalia uporaji wa mashamba ya miwa ya Kilombero na kiwanda cha kusindika miwa cha Kilombero. Haitoshi, angalia uuzaji wa nyumba za serikali na mashirika ya umma ulivyofanywa na uongozi wa kisiasa (hususan Awamu ya Tatu).
  Huu ulikuwa uporaji wa kutisha uliyoambatana na udalali uliyokuwa ukifanywa kimkakati na kwa kuzingatia ufisadi wa kimfumo kwa vile waliyekuwa wakihusika na ujambazi huo ni walewale waliopewa dhamana ya kusimamia menejimenti ya shughuli za serikali kwa manufaa ya umma.
  Viongozi, kama watu wenye dhamana, walihusika sana na uporaji. Kwa kuwa wengi wa viongozi wa serikali wanatokana na CCM na watendaji wenye mafungamano ya ndani kwa ndani na wenye dhamana katika siasa zinazoongoza na kutawala uchumi wa Tanzania.
  Kwa jinsi hii, CCM imeacha kuwatetea wananchi kwenye njia ya umiliki wa rasilimali kwa uwiano wenye mizani ya kuwaletea hali bora watu wa Tanzania kama chama kimegeuka chama cha madalali wa uporaji! Wawekezaji wanapora na kuvuna utajiri wa Tanzania huku viongozi wa CCM wakifaidika na natija ya udalali, siyo?
  Kama hawaoni vile, viongozi wanaotawala siasa na kuendesha serikali wamekuwa mstari wa mbele katika kuongoza uporaji na umilikishwaji wa rasilimali za wananchi kwenye mikono ya watu wachache wanyonyaji na wasiyezingatia uhuru, haki na usawa wa wananchi wa Tanzania.
  Tanzania imekuwa kama nchi isiyokuwa na wenyewe! Hii ni dhana mbaya sana kudhaniwa na wananchi wenye haki ya umiliki wa nchi yao. Nchi inapokosa umiliki wa moja kwa moja wa rasilimali zake; nchi inapokosa satwa ya kutawala uchumi wake kwa matumizi makini; na hata pale, nchi inapotawaliwa na kuongozwa na viongozi wanaotamani kuuza nchi kwa faida ya watu wachache, ni hatari inayoweza kuzusha hamkani kisiasa, kiuchumi na kijamii.
  Dalali ni dalali; na mbaya zaidi dalali akiwa kiongozi mtawala na mwenye satwa ya menejimenti ya shughuli za serikali! Kiongozi asiyeweza kupanga wala kusimamia umiliki, uchakataji na menejimenti jumla ya shughuli za kiuchumi kwa utumizi wa rasilimali chache za nchi hafai kuongoza nchi.
  Na kama akipewa nafasi ya kuongoza; basi, mwendo wa uongozi wake utakuwa ni kuiuza nchi anayoiongoza.
  Kumbukizi inaonyesha kwamba mwaka 2003 wakati wa songombingo la uuzaji wa benki ya makabwela (National Micro Finance Bank, NMB) kiongozi wa nchi alisisitiza, “benki ya makabwela lazima iuzwe kwa kuwa inaendeshwa kwa hasara.”
  Japokuwa ulikuwa uongo mpevu, kiongozi wa nchi alikuwa dalali na alihakikisha benki hiyo inaporwa!
  Wengi wa viongozi wanaoutamani udalali kwa kutumia nafasi za uongozi wamekuwa wakitafuta nafasi za kuwa madalali ili waweze kutekeleza azima ya kutumia udalali katika kufanikisha uporaji wa rasilimali za Tanzania.
  Tanzania imepoteza rasilimali nyingi kwa njia hii na hata sasa, wengi wa viongozi wanaotamani kuiuza nchi wanatarajia kuzifisidi rasilimali chache zilizobakia kwa mfumo wa wawekezaji wa ndani ambao wanabebwa na madalali viongozi waliyemo ndani ya serikali ya CCM. CCM imegeuka dalali wa uuzaji wa nchi!
  Udalali kwa viongozi wa CCM umekuwa ni sehemu ya “itikadi” mpya ya kimkakati katika kufikia malengo ya kifisadi juu ya kuwawezesha viongozi wenye inda, hila na choyo ya kupata faida kwa gharama ya wananchi wasiyekuwa na mtetezi pale chama kilichodhaniwa kuwa mtetezi wao kupoteza madhumuni yake ya “asili” na kuwa wakala na dalali wa uporaji.
  Uporaji unaofanywa na waporaji wawekezaji unalenga kuhitimisha azma ya unyonyaji na unyanyasaji unaofanywa na wawekezaji kwa usaidizi wa nguvu za viongozi madalali ndani na nje ya chama na serikali.
  Uporaji na udalali unafanya kazi kwa kutegemeana waporaji wanapora huku madalali wanafaidika na mapato ya uporaji kwa uwiano wa mapato ya kazi ya udalali.
  Unapowaangalia viongozi wanaotawala siasa, uchumi na jamii kwa sasa hakuna hata mmoja mwenye ghera na uchu wa kusimama kidete katika kutetea uhuru, haki na usawa wa wananchi wanyonge waliyenyang’anywa haki ya matumizi ya rasilimali za nchi.
  Wao (viongozi) wa siasa wanadhani hakuna atakayewawajibisha, kuna kila sababu ya wao kujikumbusha kwamba wayafanyayo katika “biashara” ya udalali wa kuuza rasilimali za Tanzania kwa faida ya umasikini wengi wanayatambua na kuna siku “nguvu ya umma” itatumika kuwaadabisha kwa jinsi ya ujambazi wa kiserikali uliyofanywa.
  Udalali wa kuuza rasilimali za nchi ni ujambazi wa kiserikali; na ni ufisadi mbaya sana. Na ni wajibu na haki kwa wananchi kuchukua hatua za makusudi katika kukomesha hali hiyo!
  Ombwe linaloonekana sasa la uongozi wa kisiasa kushindwa kushughulikia ufisadi uliyosababishwa na udalali wa kuuza rasilimali za nchi linatokana na ukweli kwamba sehemu ya viongozi waliyopo sasa (kwenye utawala na menejimenti ya chama na serikali) ni walewale waliokuwamo kwenye awamu za uongozi zilizotangulia.
  Kwa jinsi hiyo, kuna kulindana kwa kiasi kikubwa na kuna kila sababu ya kulinda maslahi ya mfumo uleule wa kijambazi uliorithiwa kutoka awamu moja kwenda nyingine! Tanzania ndipo ilipofika, uongozi unafanya udalali kama dhana na falsafa ya kuendesha ujambazi wa kiserikali huku wakilindwa na sheria na kanuni za kifisadi.
  Tamaa, uchu, uroho, na roho mbaya zimewafanya viongozi wengi wa kisiasa watumie siasa kwa maslahi ya uchumi unaoendeshwa kwa nguvu ya soko holela lenye mashiko yanayozingatia uporaji wa rasilimali za wananchi pasipo na malipo ya haki dhidi ya matumizi yake.
  Kama nchi ina utajiri mkubwa wa rasilimali; kwa nini nchi ingalipo kwenye umasikini wa kutupwa? Nadhani suala hili halina majibu muafaka na ya yanayokidhi utashi wa uhuru, haki na usawa kwa wananchi waliyo wengi.
  Uongozi wa CCM kwa sasa hauna majibu ya moja kwa moja kwa vile tayari umeshashindwa kujenga jamii ya watu waliyo sawa na huru kwa matumizi mazuri ya rasilimali za Tanzania.
  CCM imekuwa na maneno marefu; ilhali vitendo vyake vifupi! Nchi inaingia kwenye mikono ya watu binafsi wachache kwa kumilikishwa sehemu nyeti na muhimu ya rasilimali na njia za uzalishaji mali huku matumizi ya rasilimali hizo hayawanufaishi wananchi wengi masikini wa Tanzania.
  Rasilimali zinatafunwa na wajanja, maendeleo ya watu na nchi yanaongezeka kwa kasi isiyolingana na matumizi ya rasilimali. Kwa ujumla, nchi inanyonywa na wanyonyaji wa nje wakisaidiwa na wale madalali wa ndani wakiongozwa na sera mbovu za matumizi endelevu ya rasilimali kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.
  Viongozi wengi wa tangu kale, kama Sultan Magungo wa Msowero (Kilosa), walifanya udalali wa kuuza miliki na maeneo yao ya utawala; hata hivyo, wapo wachache waliokataa kuuza utu wao kama kina Mtwa Mkwawa na Mtemi Milambo.
  Umefika wakati sasa wananchi tuwakatae viongozi wanaotumia nafasi za uongozi kwa manufaa ya udalali na au kuuza nchi kwa gharama ya umaskini wetu.
  Tanzania, kama tunasimama kwenye uongozi bora, tuna kila sababu ya kupunguza umasikini, kufuta ujinga, kuboresha afya ya mwili na akili ya watu wetu, na kupambana na aina zote za ufisadi.
  Ni maamuzi magumu ya kukataa uongozi wa kifisadi na kuweka viongozi watakaojali uhuru, haki, usawa na uadilifu kwa uwiano wa maendeleo ya watu na vitu kadhalika. Kwa hili, Tanzania inahitaji mabadiliko ya kweli ni sasa, na si wakati mwingine; tumechelewa sana!
  Source:UPORAJI WA RASILIMALI: Viongozi wageukia udalali
  My note: Watanzania wanahitaji elimu kama hii kabla ya 2015. Great Thinkers tuungane kuelimisha haswa wale wapokea kanga na kofia na T-shirt kule vijijini.
   
 2. Ng`wanakidiku

  Ng`wanakidiku JF-Expert Member

  #2
  Jan 11, 2012
  Joined: Apr 18, 2009
  Messages: 1,196
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Pia kuna umuhimu kuhakikisha serikali inawajibika kwa maamuzi ya umma kabla ukoloni mambo leo haujagraduate na kuwa kama DRC Congo.
   
 3. R

  RMA JF-Expert Member

  #3
  Jan 12, 2012
  Joined: Oct 10, 2010
  Messages: 409
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Kikwete ndio chaguo la Mungu ili watanzania mjifunze!! Ni vema maisha yaendelee kuwa magumu zaidi ili mpate akili. Safari nyingine msifanye ushabiki wa Yanga na Simba katika siasa bila kutazama uhalisia wa mambo! Mnapiga kura kama vipofu halafu mnalalama kama vichaa! Maisha duni kwa kila mtanzania ni haki yenu! Mnastahili kwa kuwa huyo rais mnayemlalamikia ni ninyi mliomchagua!
   
 4. Mwanyasi

  Mwanyasi JF-Expert Member

  #4
  Jun 15, 2017
  Joined: Nov 16, 2010
  Messages: 5,761
  Likes Received: 1,895
  Trophy Points: 280
  Hii thread ilitupiliwa mbali mwaka 2012,lakini ukweli ni kwamba bado inaishi.
   
Loading...