Upinzani wataka Sheria Makosa Kimtandao, Takwimu zifanyiwe marekebisho kwa kuwa zinaminya uhuru wa mawasiliano

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,498
9,279
KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imetaka serikali kupeleka bungeni miswada ya marekebisho ya Sheria ya Makosa ya Kimtandao, Sheria ya Takwimu na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari kwa kuwa inaamini sheria hizo zimesababishwa kuminywa kwa uhuru wa mawasiliano.

Akiwasilisha bungeni maoni ya kambi hiyo kuhusu Muswada wa Sheria ya Serikali Mtandao ya Mwaka 2019, Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Ruge, alisema pamoja na malengo mazuri ya uanzishwaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, kambi hiyo inaona yatakwama ikiwa serikali haitafanya marekebisho ya sheria hizo.

Ruge ambaye aliwasilisha maoni hayo kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa kambi hiyo katika Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ruth Mollel, alisema sheria hizo zinadhibiti mawasiliano ya kimtandao na upatikanaji wa taarifa.

"Ili sheria inayopendekezwa iweze kufanya kazi na kufikia malengo yaliyokusudiwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri na kupendekeza serikali ilete miswada ya marekebisho ya sheria nilizozitaja hivi punde ili vipengele pingamizi vinavyozuia uhuru wa mawasiliano ya kimtandao na upatikanaji wa taarifa na takwimu za serikali vifutwe.

"Kwa kufanya hivyo, kutatoa mwaya kwa sheria inayopendekezwa kufanya kazi. Ikiwa jambo hili halitafanyika, basi sheria hii inayopendekezwa itakuwa imetungwa tu kuweka kumbukumbu kwamba kuna Sheria ya Serikali Mtandao lakini kimsingi utekelezaji wake utakuwa ni changamoto kubwa.

"Pia, serikali itambue kwamba wajibu wake mkubwa ni kutoa huduma kwa wananchi ambao wengi wao takribani asilimia 70 wanaishi vijijini ambako kuna changamoto za mawasiliano ya kimtandao.

"Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaikumbusha serikali kushirikiana na sekta binafsi hususan kampuni binafsi za simu, kujenga miundombinu ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini ili wananchi waishio vijijini waweze kunufaika na mfumo huu wa Serikali Mtandao," alisema.

Awali, akiwasilisha muswada huo bungeni jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki, alisema kutungwa kwa sheria hiyo kutaisaidia serikali kuongeza udhibiti wa kuboresha utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini.

Alisema sheria hiyo pia itasaidia kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali, usimamizi wa matumizi ya rasilimali Tehama katika taasisi za umma, kuboresha mazingira ya biashara (mifumo ya leseni, kodi, benki, usimamizi wa ardhi na utoaji wa hati za kusafiria) na kuimarisha utendaji kazi serikalini.

======

MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI (NA. 4) YA MWAKA 2019 [THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 4) ACT, 2019
(Yanatolewa chini ya kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Januari 2016)
__________________________

A. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kabla ya yote naomba kumshuruku Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, kuniwezesha kuwa mwenye afya njema, kusimama mbele ya Bunge hili ili kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu hoja iliyo mbele yetu. Sambamba na hilo nishukuru kwa kupewa fursa hii na Kiongozi wangu wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kuniamini katika jukumu hili.
2. Mheshimiwa Spika, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (No. 4), ya Mwaka 2019, unapendekeza marekebisho ya sheria mbalimbali kumi na moja (11). Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Mawakili, (Sura ya 341), Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo, (Sura 108), Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai,(Sura ya 20), Sheria ya Urejeshwaji wa Wahalifu, (Sura ya 368), Sheria ya Mashauri dhidi ya Serikali,(Sura ya 5), Sheria ya Mahakama za Mahakimu Wakazi (Sura ya 11), Sheria ya Taifa ya Mashitaka, (Sura ya 430), Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (Sura ya 329), Sheria ya Mapato yatokanayo na Uhalifu, (Sura ya 256), Sheria ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, (Sura ya 268) na Sheria ya Chama cha Msalaba Mwekundu, (Sura ya 66).
3. Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kuwa marekebisho yanayopendekezwa yanahusu sheria nyingi, ambazo zina athari za moja kwa moja kwa wananchi. Kutokana na Sheria hizo kugusa maisha na shughuli za wananchi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitegemea kuwa Serikali ingewashirikisha kwa utoshelevu wadau wote ambao wanaguswa na marekebisho ya sheria hizo ili watoe maoni yao na hatimae Bunge liweze kutunga sheria bora ambayo ni rafiki kwa wadau wote na hivyo kurahisisha utekelezaji wake.
4. Mheshimiwa Spika, tofauti na mategemeo hayo; ushiriki wa wadau ulikuwa duni jambo ambalo mosi, linatoa picha kuwa hakuna nia njema katika marekebisho yanyopendekezwa; lakini pili utekelezaji wa sheria ambayo haina maridhiano kwa wadau wote utakuwa mgumu.
5. Mheshimiwa Spika, kutokana na upungufu huo wa ushiriki hafifu wa wadau ambao matokeo yake ni kutungwa kwa sheria ambayo itaanza kupingwa hata kabla ya kuanza kutekelezwa na hivyo kusababisha kuleta muswada mwingine wa marekebisho ndani ya muda mfupi jambo ambalo ni hasara kwa Serikali; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri na kupendekeza kwamba; Serikali itanue wigo wa ushiriki wa wadau ili sheria inayotungwa ipokelewe na kutekelezwa vyema na wananchi wanaoguswa na sheria hiyo (compliance) na hivyo kupunguza gharama za kufanya marekebisho ya sheria mara kwa mara kutokana na sheria husika kuwa na mapungufu mengi yanayotokana na ukosefu wa mawanda mapana wa maoni ya wadau.
6. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, ufuatao ni uchambuzi wa baadhi ya vifungu vinavyopendekezwa kufanyiwa marekebisho na maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu mapendekezo hayo.

B. UCHAMBUZI WA VIFUNGU VYA MUSWADA
i. Marekebisho ya Sheria ya Mawakili, (Sura ya 341)
7. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 39 cha sheria mama kinarekebishwa kwa kuongeza kifungu kipya cha “(2) kinachosomeka kama ifuatavyo: “A law Officer or State Attorney shall not, for the whole period of service as a Law Officer or State Attorney be issued with a practicing certificate”.
8. Mheshimiwa Spika, kifungu hiki kinatoa zuio kwa mawakili wa Serikali kupewa hati au kibali cha kufanya shughuli za uwakili nje ya mfumo wa Serikali kwa kipindi chote watachokuwa katika utumishi wa umma.
9. Mheshimiwa Spika, kifungu hiki kinawabana mawakili wa Serikali wasiweze kufanya shughuli zozote za uwakili nje ya ajira ya Serikali kwa lengo la kujiongezea kipato. Kwa mantiki hiyo, licha pendekezo hilo kuwaathiri kiuchumi, lakini pia linawaondolea motisha wa kufanya kazi bila msongo wa mawazo (stress) unaotokana na ugumu wa maisha. Aidha, pendekezo hili linapoka haki ya wananchi kupata msaada wa kisheria kutoka kwa mawakili wa Serikali kama vile viapo, kushuhudia mikataba na makubaliano nk.
10. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kuwa taaluma ya sheria ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine, na kwa sababu hiyo, mawakili wa Serikali wana haki ya kufanya shughuli binafsi za kiwakili baada ya muda wa kazi kama ambavyo waajiriwa wengine wa Serikali wanavyoruhusiwa kufanya shughuli binafsi zinazohusiana na taaluma zao baada ya muda wa kazi.
11. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuikumbusha Serikali kuzingatia kaulimbiu yake ya “Hapa Kazi Tu” na pia msisitizo wake kwa wananchi kujiajiri na kujipatia kipato ili kuondokana na umaskini kwa kuwaruhusu mawakili wa Serikali kufanya shughuli binafsi za uwakili ili kutimiza azma hiyo. Hapa tunasisitiza kuwa muda wa mwanataaluma yoyote kujiajiri ni wakati akiwa na nguvu ya kufanya kazi. Kuwazuia mawakili kufanya kazi hizo kwa kipindi chote cha ajira yao ni kuwadhulumu kwa kuwa hawataweza kufanya shughuli hizo kwa ufanisi baada ya kustaafu ajira ya Serikali.
12. Mheshimiwa Spika, sababu iliyotolewa kuhalilisha pendekezo la kuwazuia mawakili wa Serikali kufanya kazi ya uwakili wa kujitegemea ni pamoja na kuondoa mgongano wa maslahi ikiwa wakili huyo atakuwa anamwakilisha mtu mwenye shauri dhidi ya Serikali ilhali wakili huyo ni mwajiriwa wa Serikali. Hoja inaweza kuwa na pande mbili; ukweli na uongo, kwani yapo matukio kadhaa ambapo imeshuhudiwa maslahi binafsi yakipewa kipaumbele hasa katika teuzi mbalimbali. Kwa mfano wapo mawakili binafsi waliowahi kuteuliwa kuwa majaji wa Mahakama Kuu; au kuwa watendaji wakuu katika Ofisi na Idara za Serikali.
13. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inapenda kufahamisha Serikali kwamba; sio mara zote mawakili wa Serikali watakuwa wanafanyakazi wa kuitetea serikali tu. Kwa sababu hiyo, mawakili wa Serikali waruhusiwe kufanya uwakili wa kujitegemea ilimradi katika utekelezaji wa shughuli hiyo kusiwe na maslahi ya Serikali. Hivyo, ni vyema kazi ambazo hazina uhusiano na kuitetea Serikali wakaruhusiwa kuzifanya.
14. Mheshimiwa Spika, Kinachokwenda kutokea ikiwa kifungu hiki cha kibaguzi hakitafutwa; kazi ya Uwakili wa Serikali itakosa mvuto kwa wanataaluma wa Sheria kutokana na maslahi duni; jambo ambalo linaweza kusababisha upungufu wa mawakili wa Serikali au Serikali kuwa na mawakili wasio na sifa stahiki (competent lawyers) na hivyo kupelekea Serikali kushindwa katika mashauri mengi dhidi yake.
ii. Marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (Sura ya 20)
15. Mheshimiwa Spika, dhana ya makubaliano baina ya mwendesha mashitaka na mtuhumiwa wa kosa la jinai kukiri kosa ili kupunguziwa adhabu (Plea Bargaining) ni nzuri kwa ujumla wake kutokana na sababu zilizo wazi.
16. Mheshimiwa Spika, kifungu cha cha 16 cha Muswada kinachoanzisha kifungu kipya cha 194F kimeorodhesha makosa ambayo hayatahusika na utaratibu wa makubaliano ya kupunguziwa au kufutiwa adhabu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina inapendekeza kwamba; makosa yaliyoainishwa katika kifungu cha 194F (b),(c ),(d) na (e) ambayo yanahusu uhaini, umiliki na ufanyaji wa biashara ya dawa za kulevya, ugaidi na umiliki wa nyara za Serikali kinyume cha Sheria yaingizwe katika utaratibu wa Plea Burgaining.
17. Mheshimiwa Spika, msingi wa pendekezo hili ni kutokana na ukweli kwamba makosa tajwa katika vifungu hivyo yanahusu mtandao hatari, hivyo ni muhimu sana kuufahamu mtandao husika kupitia kwa Mtuhumiwa. Kama mtuhumiwa asipoingizwa kwenye makubaliano na Mwendesha mashtaka au na wakili wake kuna uwezekano mkubwa walioko nje wakaendelea na uhalifu mbaya zaidi. Kwa mfano, kama unataka kufahamu wale wanaoleta madawa ya kulevya, unatakiwa uingie makubaliano na wanaotumia ili kujua wanauziwa na nani ili kuubaini mtandao mzima unaojishughulisha na dawa za kulevya.
18. Mheshimiwa Spika, halikadhalika ili kutokomeza ugaidi ni lazima kushughulika na mtando mzima na sio mtuhumiwa mmoja. Ni vigumu kuvunja kambi au makundi ya siri yaliyo kimya (sleeping cells) au hata kama kuna uhaini hautaweza kufika mwisho wa mzizi, kama hapatakuwa na watu wa kutoa taarifa kwa njia hii ya Plea Bargaining.
19. Mheshimiwa Spika kitendo cha Serikali kuyaondoa makosa yanayohusisha mtandao hatari kama vile uhaini, ugaidi na biashara ya dawa za kulevya katika orodha ya makosa yanayoweza kushughulikiwa kwa makubaliano katika ya mtuhumiwa na mwendesha mashtaka ni sawa na Serikali kujifunga na kujizuia kubaini wahalifu wa mitandao hatari na kuwachukulia hatua ili kukomesha kabisa makosa ya aina hiyo.
iii. Marekebisho ya Sheria ya Mashauri dhidi ya Serikali, (Sura ya 5)
20. Mheshimiwa Spika, Sheria hii ni muhimu sana katika dhana ya haki na usawa mbele ya sheria. Aidha, ni muhimu wananchi wakafahamu kwamba Serikali inaweza kushtakiwa iwapo itakiuka misingi ya utawala bora na utowaji wa haki katika utekelezaji wa shughuli zake.
21. Mheshimiwa Spika kifungu cha 22 cha kinaanzisha kifungu kipya cha 6A ambacho kinampa mamlaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuingilia kati shauri lolote lililofunguliwa na Serikali au dhidi ya Serikali kwa wizara, idara au taasisi yoyote ya umma.
22. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina mtazamo kwamba kifungu hiki kinaondoa dhana ya uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa umma kwa makosa watakayoyatenda kwa kuwa wanajua Mwanasheria Mkuu wa Serikali atasimama badala yao. Kwa kuwa idara na taasisi za Serikali zimepewa mamlaka kamili kwa mujibu wa sheria ya kushtaki na kushtakiwa; zinatakiwa kutumia mamlaka hayo vile vile kuwajibika pale zinapokabiliwa na mashitaka. Ili kujenga dhana ya uwajibikaji, Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kwamba ikiwa watendaji waliopewa dhamana katika ofisi za umma watafanya mambo ambayo ni kinyume cha sheria na wakawajibika wao binafsi bila kuhusishwa kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuleta nidhamu katika utendaji wa umma.
23. Mheshimiwa Spika, kitendo cha taasisi za umma kujificha kwenye kivuli cha mwanasheria Mkuu wa Serikali kunapotokea mashauri dhidi ya taasisi hizo kinatoa taswira kwamba wanasheria katika taasisi hizo dhaifu hawawezi kusimama na kutetea taasisi zinapokabiliwa na mashauri ya kisheria. Kama Serikali itang’ang’ania Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuingilia mashauri ya kisheria katika idara na taasisi za umma; basi wanasheria walioajiriwa katika taasisi hizo wafutwe kazi au wabadilishiwe majukumu kwa kuwa watakuwa wanalipwa mishahara kwa madaraka ambayo hawayafanyii kazi.
iv. Marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (Sura ya 329)
24. Mheshimiwa Spika, marekebisho kama yanavyoelekezwa kwenye kifungu cha 29 cha muswada, kwa kuongeza kifungu kidogo kipya cha 2 kinachohitaji utoaji wa idhini au kibali toka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa mashauri ya rushwa ambayo hayahusiani na makosa yaliyoelezwa katika kifungu cha 15 cha sheria mama ya TAKUKURU.
25. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina mtazamo kwamba; kitendo cha TAKUKURU kutokuwa na mamlaka ya kupeleka mahakamani mashtaka ya rushwa kubwa kadiri ya mapendekezo yanayoletwa na Serikali kinatoa picha kwamba, taasisi hiyo ya kiuchunguzi haiaminiki katika utendaji wake na ndio maana inakuwa ni taasisi ya kupewa maelekezo ya nini cha kufanya na wakati gani.
26. Mheshimiwa Spika, Ukiangalia kifungu cha 9 cha sheria ya Taifa ya Mashtaka kinachofafanua aina ya mashtaka ambayo DPP anatakiwa kupewa taarifa au kushirikishwa, ni dhahiri kuwa TAKUKURU itabakia kuwa taasisi isiyokuwa na meno. Kambi Rasmi ya Upinzani inashangazwa sana na mapendekezo haya kwani yanatoa taswira kwamba TAKUKURU haina uwezo kiutendaji wa kuweza kuwafungulia mashtaka watuhumiwa wa makosa ya rushwa mpaka ipate kibali cha Mwendesha Mashtaka wa Serikali. Aidha, mapendekezo hayo yanakwenda kinyume na bango linalobebwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuwa inapambana na Rushwa ilhali inaidhibiti TAKUKURU kufanya kazi kwa uhuru kwa kupoka madaraka yake na kuyahamishia kwa mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.
27. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali; kama kweli inataka kupambana na rushwa kwa vitendo; basi ilete muswada wa sheria utakaoifanya TAKUKURU kuwa taasisi huru. Kifungu hiki kinachopendekezwa katika muswada huu kinainyima TAKUKURU uhuru wa kufanya kazi.
28. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 9 cha Sheria ya Taifa ya Mashitaka kinaonyesha jinsi ambavyo TAKUKURU imepokwa mamlaka ya kushughulikia mafisadi na wala rushwa. Kifungu hicho kinasomeka kama ifuatavyo; naomba kunukuu:-
9.-(l) Notwithstanding the provisions of any other law, the functions of Director shall be to-
(a) decide to prosecute or not to prosecute in relation to an offence;
(b) institute, conduct and control prosecutions for any offence other than a court martial;
(c) take over and continue prosecution of any criminal case instituted by another person or authority;
(d) discontinue at any stage before judgement is delivered any criminal proceeding brought to the court by another person or authority; and
(e) direct the police and other investigative organs to investigate any information of a criminal nature and to report expeditiously.
(2) The functions referred to in sub-section (1) shall include institution conducting of summary proceedings, committal proceedings or a preliminary hearing under the Criminal Procedure Act, the Magistrates' Courts Act or any other law relating to criminal proceedings.
(3) Nothing in this section shall prevent the Director to take over and continue proceedings in the name of the person or authority that instituted those proceedings.
(4) The Police Officer or the Officer of any other investigative organ in-charge of any area or authority to be specified by the Director shall, in respect of offences alleged to have been committed within that area, report to the Director any-(a) offence punishable with death;
(b) offence in respect of which a prosecution is by law required to be instituted with the consent of the Director;
(c) case in which a request for information is made by the Director;
(d) case in which it appears to such Police Officer or the Officer of any other investigative organ that the advice or assistance of the Director is desirable; or
(e) other offence specified by the Director to be an offence in respect of which a report under this section is necessary.
(5) The term "area" or "authority" as used in subsection (4) means and includes a geographical jurisdiction of a police post, station, district, region or zone, a corresponding office of any other investigative organ or a person to whom a command or a directive may be issued as the case may be.
29. Mheshimiwa Spika, kitendo cha kutoipa TAKUKURU uhuru wa kujitegemea kimamlaka kitasababisha mwendelezo wa vitendo vya rushwa, kwani makosa yote ya rushwa kubwakubwa yataishia ofisini kwa DPP na TAKUKURU haitakuwa na uwezo/ mamlaka ya kuhoji chochote kuhusu mwenendo wa mashauri hayo.
30. Mheshimiwa Spika kama hofu ya Serikali ni kupoteza au kupunguza madaraka ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri na kupendekeza kwamba, Serikali ifanye utafiti katika nchi nyingine kuona ni namna gani Ofisi za Waendesha Mashtaka wa nchi hizo wanafanya kazi zao bila kuathiri mamlaka nyingine zenye majukumu ya usimamizi wa utekelezaji wa sheria.
v. Marekebisho ya sheria ya Mapato yatokanayo na Uhalifu, sura ya 256.
31. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 37 cha muswada kinafanyia marekebisho kifungu cha 22 cha sheria mama, kwa kufuta kifungu cha 4 na kukiandika upya. Kifungu hicho kinachohusu adhabu kwa makosa ambayo yanakiuka vifungu vya sheria yoyote ya ndani au nje ya nchi na adhabu zake ni kifo au kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na mbili; na pia utaifishaji mali iliyopatikana kutokana na makosa hayo. Kwa muktadha huo, kifungu cha 4(c) kinasema kuwa pale maombi ya adhabu yanapotolewa dhidi ya mtuhumiwa wa makosa tajwa “serious offense”, mali ya mtuhumiwa kukamatwa, itahusu pia mali ambayo alikuwa anamiliki miaka mitano nyuma kabla ya pale kosa alilohukumiwa nalo halijatendeka.
32. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kifungu hiki kina nia ovu ya kuwalenga baadhi ya watu hususan wenye mtazamo tofauti na Serikali ili kuwabambikizia kesi za uhujumu uchumi na kuwafilisi kwa kutaifisha mali zao kabla hata ya kesi hizo kutolewa uamuzi na mahakama.
33. Mheshimiwa Spika, ukitazama kwa makini mapendekezo ya Serikali utagundua pia kwamba Serikali inataka kujiwekea kinga ya kisheria ya kutolipa madeni makubwa inayodaiwa na watu na pia kuwahujumu watu wenye mgogoro na Serikali kwa kuwa itakuwa ni rahisi kwa Serikali kuwageuzia kibao watu wenye mgogoro nayo au wenye madai dhidi yake na kuwafilisi mali zao kupitia sheria hii.
34. Mheshimiwa Spika, jambo la kushangaza zaidi ni pale Serikali inapopendekeza kutaifisha mali halali iliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitano nyuma kabla kosa halijatendeka. Jambo hili halikubaliki kwa kuwa litaathiri familia nzima ilhali aliyetenda kosa ni mmoja. Kama ilivyo desturi mali za familia huchumwa pamoja kwa maana ya mke na mume au ndugu wa familia, hivyo kama ni mtu mmoja ametenda kosa inahalalisha vipi ufilisi wa mali ambazo ni za familia? Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo ni kwa namna gani itatenganisha mali binafsi za mtenda kosa na mali za familia ili kutoiingiza familia nzima kwenye adhabu kwa kosa la mtu mmoja. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kifungu chote cha 4 kifutwe kabisa kwani ni kifungu ambacho badala ya kuangalia ustawi wa nchi yetu, kinalenga kuwavizia watu wenye mtazamo tofauti na Serikali na kuwafilisi mali zao na pia kitapunguza morali ya wawekezaji hapa nchini kwa na hofu ya kufilisiwa kutokana na hila za kisiasa.
vi. Marekebisho ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, Sura ya 66.
35. Mheshimiwa Spika, lengo la marekebisho haya ni kutaka kuifanya sheria hii kutumika katika pande zote mbili za Muungano, na vile vile kuongeza mawanda ya nembo ya Msalaba mwekundu kuwa pia ni mwezi mwekundu. Hata hivyo, uko mkanganyiko kuhusu ya matumizi ya sheria hii kwa kuwa sheria itatumika pande zote mbili za Muungano, lakini waziri anayepewa dhamana ya kuisimamia sheria hii ni Waziri wa Katiba na Sheria – wizara ambayo si ya Muungano. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza waziri atakayekuwa na dhamana na sheria hii awe waziri wa Mambo ya ndani ya nchi ambayo ni wizara ya Muungano na sio waziri wa sheria kama muswada unavyopendekeza.
C. HITIMISHO
36. Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia hotuba yangu kwa kuiasa Serikali kwamba; utunzi wa Sheria una lengo kuweka utaratibu wa uendeshaji wa mambo katika jamii. Ili utaratibu huo uweze kufanya kazi ni lazima uwe unafahamika na uwe unakubalika na jamii nzima. Kwa sababu hiyo, ipo haja kubwa ya kuishirikisha jamii katika mchakato mzima wa utunzi wa sheria ili jamii iweze kuziheshimu sheria hizo ili ziweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.
37. Mheshimiwa Spika, tofauti na dhana hiyo ya ushiriki mpana wa wananchi katika utunzi wa sheria, kumekuwa na desturi mbaya kwa Serikali kuwaita wadau wachache kuchambua miswada huku idadi kubwa ya wananchi ambao ndio walengwa wa sheria husika, wakiwa hawajui chochote kuhusu sheria hizo.
38. Mheshimiwa Spika, kwa kuutambua upungufu huo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia chadema, imeweka bayana katika sera yake ya Utawala Bora (Sura ya 2.1) kuhusu ushirikishwaji wa wananchi katika kutunga sheria. Sehemu ya sera hiyo inasema kwamba; naomba kunukuu. “Chadema itawashirikisha wananchi kutoa maoni na mapendekezo katika mchakato wa kutunga sheria zote za nchi ili kurahisisha usimamizi na utekelezaji wa sheria hizo”.
39. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.

Latifah H Chande (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA
5 Septemba, 2019
 
Hizi Sheria za kishamba zinapelekea nchi hii kukosa fursa za kibiashara na uwekezaji Kati yetu na wazungu ndiyo maana kila siku Yale matumaini ya Tanzania ya viwanda inazidi kufifia
 
Back
Top Bottom