Upinzani 2009: Tutakata mbawa za Rais | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Upinzani 2009: Tutakata mbawa za Rais

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Jan 1, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Jan 1, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,609
  Likes Received: 82,187
  Trophy Points: 280
  Upinzani 2009: Tutakata mbawa za Rais

  Mwandishi Wetu Disemba 31, 2008
  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  MABADILIKO ya Katiba kuomba madaraka ya Rais yapunguzwe na hatua kali zaidi dhidi ya watuhumiwa ufisadi ni kati ya mambo ambayo wanasiasa kadhaa wanataka yafanyike mwaka 2009.

  Hatua hizo zimo katika tathmini ya viongozi hao ya mwaka unaokwisha wa 2008 na matarajio yao kwa mwaka 2009.

  Baadhi ya viongozi hao wameutafsiri mwaka 2008 kuwa mwaka wa mshituko kwa Taifa, ulioamsha Watanzania wengi kuanza kufuatilia uwajibikaji wa viongozi wao, hasa viongozi waliowapigia kura.

  Lakini pia, viongozi hao wanautazama mwaka ujao (2009) kama mwaka wa mabadiliko zaidi. Na katika kuhakikisha mabadiliko hayo yanatokea, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohammed, anatarajiwa kuwasilisha hoja binafsi kutaka mabadiliko ya Katiba.

  Hamad ambaye ni Mbunge wa Wawi kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), atawasilisha hoja yake akitaka Bunge kuridhia azimio la mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano ujao wa Bunge, ili hatimaye Rais apunguziwe kile anachokiita mzigo wa madaraka aliyonayo Rais sasa.

  Ameiambia Raia Mwema katika mahojiano kwamba tayari amekwisha kuwasilisha taarifa ya kuwasilisha hoja hiyo kwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta.

  "Mwaka 2009 tunatarajia mabadiliko zaidi na msingi wake ni kubadilisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," anasema Hamad katika mazungumzo yake na Raia Mwema, wiki hii.

  Kwa mujibu wa maelezo hayo ya Kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani, kati ya mambo yanayolengwa kubadilishwa katika Katiba ni pamoja na vifungu vinavyompa Rais mamlaka makubwa ya uteuzi wa viongozi wanaotumikia wananchi.

  Akitathmini mwaka 2008, Hamad alisema Bunge kwa nafasi yake na hasa Kambi ya Upinzani wamefanya kazi kubwa ingawa juhudi zaidi zinahitajika.

  Akifafanua alisema juhudi zaidi katika Bunge zinahitajika ili kumalizia viporo vya ufisadi katika ujenzi wa majengo pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), malipo ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ununuzi wa rada ya kijeshi na ndege ya Rais, aina ya Gulf Stream iliyonunuliwa wakati wa utawala wa Awamu ya Tatu.

  Kwa upande mwingine, aliunga mkono uamuzi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutaka Serikali ipunguze matumuzi yasiyo ya lazima, yakiwamo ya ununuzi usio wa lazima wa magari ya kifahari, semina na malipo ya posho.

  "Tumekuwa masikini wenye matumizi ya kitajiri, wakati wenzetu wa nchi tajiri wamekuwa matajiri wenye matumizi ya kimasikini," anasema Hamad.

  Alipendekeza katika mwaka 2009, sheria za uchaguzi pamoja na muundo wa Tume ya Uchaguzi, hasa Zanzibar, ziangaliwe upya, ili kulinda uhuru katika mchakato wa uchaguzi akiamini kuwa hilo halikufanyika katika mwaka wa 2008.

  Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, katika mazungumzo yake na Raia Mwema anasema mwaka 2008 unakwisha kwa chuki na fitina, ufisadi ukiwa umeshamiri na pengo kati ya masikini na matajiri likizidi kupanuka.

  "Maisha yamezidi kuwa magumu katika mwaka 2008, Pato la Taifa (GDP) limeshuka kwa takriban asilimia moja wakati idadi ya watu ikiongezeka kwa asilimia kati ya mbili hadi tatu," anasema Mbatia na kuongeza:

  "Katika hali kama hiyo ni wazi kuwa jamii ipo katika mgogoro, na jamii inapokuwa katika mgogoro haiwezi kustawi."


  Kwa mujibu wa Mbatia, Taifa limejitoa katika kujadili masuala ya msingi na badala yake mjadala umeelekezwa kwa watu binafsi.

  "Hatutajadili mfumo wetu wa elimu ambao ndiyo msingi wa matatizo yetu. Tunapaswa kuwapa elimu watoto wetu yenye kukabili mazingira ya sasa ya teknolojia. Hatupaswi kuendelea kubaki katika mfumo wa sasa ambao ni rasmi," anasema.

  Anafafanua: "Mfumo rasmi wa elimu ninaozungumzia ni mtaala wa miaka ya nyuma kuendelea kufundishwa leo shuleni na vyuoni. Mtoto wa darasa la tatu unamtaka ataje gavana wa kwanza wa Benki Kuu, taarifa hizi zote zipo kwenye mtandao wa kompyuta leo hii…tunawapa watoto wetu maarifa ya enzi za ujima.'

  Mbatia anasikitishwa na kulaani mauaji ya albino akisema: "Kwa bahati mbaya, jamii imerejea katika maisha ya karne ya tisa. Maisha ya kuamini ushirikina."

  Kuhusu mwaka 2009, Mbatia anaamini kuwa utakuwa mwaka wa giza kwa Taifa kama mjadala rasmi kuhusu mustakabali wa Taifa hautaitishwa.

  "Kama hakutakuwa na mjadala wa kitaifa utakaoshirikisha wadau mbalimbali ndani na nje ya mfumo wa Serikali ni wazi kuwa tutarajie Taifa lililoshiba chuki, fitina na uadui kati ya makundi, yawe ya kisiasa na hata kiuchumi," anasema.

  Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, anasema mwaka 2008, umekuwa mwaka wa mshituko na kwa mara ya kwanza katika miaka 47 ya Uhuru, Watanzania wameanza kuona mwanga na kutambua mamlaka waliyonayo juu ya viongozi wa umma.

  "Tangu yalipoibuka masuala ya ufisadi BoT (Benki Kuu ya Tanzania) na Zitto (Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini – Chadema) kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge, Watanzania wameamka sana," anasema Dk. Slaa na kuongeza:

  "Watanzania wamekuwa hodari, wameisukuma Serikali na kuifikisha hapa ilipo…baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi sasa wanafikishwa mahakamani. Katika ziara za baadhi ya mawaziri na hata Rais, wananchi wamekuwa wakiwapokea kwa mabango ya kudai haki zao…haya ni mambo ambayo hayakuwapo awali."

  Anasema jambo jingine la kujivunia mwaka 2008 ni kushuhudia viongozi waliokuwa na jeuri hadi kufikia hatua ya kutamka maneno ya kejeli kwa Watanzania wakifikishwa mahakamani.

  "Tulijengewa tabaka la kada fulani ya viongozi kuwa ni miungu watu na baadhi wakalewa madaraka na kufikia kusema maneno ya kejeli kwa Watanzania…sasa waliosema hivyo nao wamebeba ndoo za maji gerezani. Kwa hiyo haya ni mafanikio…Watanzania wameanza kujenga imani kuwa hakuna kiongozi aliyejuu ya sheria," anasema Dk. Slaa.


  Hata hivyo, anasisitiza kuwa katika mwaka 2009 Watanzania wanahitajika kuweka shinikizo zaidi ili viporo vya ufisadi vikamilishwe kwa wahusika kufikishwa mahakamani.

  Mwenyekiti wa Chama Cha United Democratic (UDP), John Cheyo, anautathmini mwaka 2008 kuwa ni wa mambo ambayo hayakutarajiwa kutokea akirejea kashfa ya Richmond, wizi katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), vilivyotikisa Bunge.

  "Katika mwaka 2008, Bunge limefanya kazi yake ya kuisimamia na kuishauri Serikali na matokeo yake ni Serikali kulazimika kuingia katika utekelezaji wa matakwa ya Bunge," anasema Cheyo.

  Hata hivyo, Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kinachoundwa na vyama vya siasa vyenye wabunge, haridhishwi na mwenendo wa siasa nchini na hususan tabia za baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa.


  Anarejea kampeni za uchaguzi mdogo katika Jimbo la Tarime, mkoani Mara akisema baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ambao, hata hivyo, hakuwataja walikiuka ustaarabu wa kisiasa ambao umebainishwa katika kanuni za TCD.

  Anashauri katika mwaka 2009 kuwa ushindani wa kisiasa uwepo lakini kwa malengo kuwa wote wanaoshindana ni Watanzania wanaolazimika kuishi katika nchi yenye amani.

  Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, anasema mwaka 2008 unakwisha wakati hali ya maisha kwa Watanzania wengi ikiwa ngumu. Mtazamo wake unawiana na kwa sehemu fulani na wa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi anaposema pengo kati ya masikini na matajiri nchini limetanuka mno.

  Lakini Mrema kwa upande wake anasisitiza kuwa pengo katika masikini na matajiri limepanuka sababu kuu ni kushamiri kwa ufisadi.

  Kwa upande mwingine Mrema anautazama mwaka 2008 kama mwaka usio mwiba mkali kwa watuhumiwa wa ufisadi kwa kuwa wengi bado hawajafikishwa mahakamani.


  "Hivi mwaka mzima unapeleka mahakamani watuhumiwa watatu tu …nchi hii wezi ni wengi sana bado hawajafikishwa mahakamani. Namshauri Rais Jakaya Kikwete aongeze speed..aachane na mambo ya haki za binadamu katika kuwashughulikia mafisadi...mbona wao walipokuwa wakiiba hawakukumbuka hizo haki za binadamu," anasema Mrema na kuongeza: "Kikwete akaze buti, barabara ina kokoto nyingi asiogope."

  Lakini kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utawala Bora, Sophia Simba anasema katika mwaka 2008 mambo ya Serikali katika kipengele cha Utawala Bora yamekwenda vizuri.

  Alipoulizwa uzuri anaoutambua upo katika vigezo gani, hakuwa tayari kuzungumza zaidi na badala yake akasisitiza kuwa utawala bora umedorora zaidi mwaka 2008 katika vyombo vya habari bila kufafanua.

  [/SIZE]
   
 2. J

  JokaKuu Platinum Member

  #2
  Jan 1, 2009
  Joined: Jul 31, 2006
  Messages: 12,769
  Likes Received: 4,982
  Trophy Points: 280
  ..hii ni hoja ya msingi sana na ninashangaa haina mvuto kwa vyama vya upinzani na hata wananchi.

  ..tunaweza kuishambulia CCM ktk masuala ya ufisadi. matokeo yake CCM watawa-disown mafisadi na kudai mbele ya wananchi kwamba CCM ni chama kizuri.

  ..CCM hawawezi kukwepa kuwajibika kutokana na mfumo mbovu wa elimu nchini. wanafunzi wanamaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma na kuandika.

  ..wapinzani wakijenga hoja zinazowagusa wananchi moja kwa moja ndipo watakapoweza kuwatoa CCM madarakani.

  ..hoja za mafisadi is fine, lakini hizo zinasaidia kuwaondoa Mramba,Yona,Karamagi, na badala yake you end up with Mkulo,Masha,Sofia Simba,....
   
Loading...