Upawa una umuhimu wa kipekee jikoni

Donatila

JF-Expert Member
Oct 23, 2014
7,557
21,495
Usiukimbize , bado una nafasi ya kipekee jikoni kwako. Haipendezi kukoroga juisi na vijiko vya bati au platisiki tumia miti, upawa na mwiko ndiyo marafiki zako hapa.

Si jambo la kufurahia upawa ukitoweka kwa vile ni kupoteza ajira, kwani mabingwa wa sanaa za kuchonga wanakosa kazi , wanabakia kuchonga miko na pengine vibao vya kukunia nazi kwa kuwa kibao cha chapati nacho kinatoka ng’ambo.

Licha ya sanaa na mambo ya kale kama uchongaji wa vijiko, miko na pawa kuwa utambulisho wa taifa, pia ni sehemu ya kujenga na kukuza vipaji kwa vijana na kuongeza ajira.

Upawa ni kama mwiko kila jiko utaukuta, matumizi yake yanaanzia kwenye kupakua, kukoroga, kuchota uwe unga au mafuta, chumvi na sukari jikoni lakini si hapo pekee hata kwenye biashara upawa ni kipimo.

Pawa ni mahususi kukoregea na kuchotea mchuzi, uji, dawa na vyakula mbalimbali vya maji maji na hupendeza zaidi . Upawa hutengenezwa kwa kifuu hasa ukanda wa pwani, kuna mianzi na mbao kadhalika huwekewa kijiti ambacho ndicho mpini au kikamatio.

Huku Zanzibar na Pemba uchongaji pawa ni maarufu na sehemu nyingine za mwambao wa pwani hususan Tanga, Bagamoyo na hata Lindi ambako kila kwenye wazee utakuta upawa unachongwa ama unatumiwa.

Ukweli ulipo sasa ni kwamba upawa wa asili unaotengenezwa kwa kifuu umeanza kupoteza umaarufu na hautumiki na watu wengi .

Lakini pia hata nazi zimetoweka kutokana na kuadimika kwa kiungo hicho cha mafuta hasa hapa Zanzibar kulikosababishwa na uharibifu wa mazingira na kukata minazi ovyo ama kuitumia zaidi kwenye madafu na kwingineko kukigemwa kuzalisha pombe ya mnazi.

Upawa wa kifuu au mti muhimu kiafya kwani hauna kemikali wala madhara kutokana na malighafi yake kuwa asilia.

Upawa hutengenezwa zaidi vjijini visiwani Unguja na Pemba na wahusika wakubwa ni wazee wa rika za kati, ambao wanaifanya kazi hii kama sehemu ya kujipatia riziki.

Utengenezaji wake ni wa kiasili kuna kuchonga kwa kutumia zana za asili kama panga kukata miti , patasi kuchimba na kipande cha chupa kuulainisha.
Kwa upande wa upawa wa kifuu kazi si ngumu, kinachojiri ni kuulanisha zaidi kwa kuwa kifuu kipo tayari kutumika.

Kijiko hiki ni muhimu hivyo ili kuweza kuuenzi utamaduni wa kutumia upawa na kuhakikisha unabakia, kuna haja kwa watengenezaji ambao wengi ni wenye kipato cha chini kuongeza ujasiriamali, kurembesha na kuboresha pawa hizo ikiwa ni pamoja na kutengeneza vijiko vya miti vinavyoweza kutumiwa na watalii.

Lakini pia kuna haja kwa serikali kusaidia wananchi kuimarisha kilimo cha miti ya minazi kwa sababu inaweza kutumiwa kwenye uzalishaji wa vijiko hivi kwa kuwa minazi inatoweka.

Chanzo: Nipashe
 
images.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom