Upanga kuliwahi kuwa sehemu muhimu katika Muziki wa vijana miaka ya 60, 70 na 80

John Kitime

Member
May 25, 2020
7
30
KATIKA miaka ya 1960 na 1970 mpaka 1980, karibu kila eneo la jiji la Dar es Salaam kulikuwa na makundi ya muziki. Wakati huo muziki ulifanywa kwa vikundi tofauti na sasa ambapo msanii anaweza kuwa peke yake katika kutunga, kurekodi na hata kufanya kazi yake jukwaani. Muziki wa dansi uligawanyika katika makundi makubwa mawili, makundi yaliyopiga muziki wa rhumba na yale yaliyopiga muziki wa magharibi.

Kulikuwa na ushindani mkubwa sana kati ya makundi haya kila mtaa ukijitahidi kupiga muziki bora Zaidi ya mwingine. Hata wazazi nao walijihusisha kuchangia ufanisi wa vikundi vya watoto wao, kwa kuwanunulia vyombo vya muziki na kuwapa maeneo ya kufanyia mazoezi. Kulikuwa na ushindani mkubwa sana kati ya vikundi vya muziki kutoka Kurasini na Chang’ombe, na vikundi ambavyo vilitoka Upanga. Hii ilitokana na kuwa maeneo haya yalikuwa ya Waafrika wa kwanza waliokuwa na nyadhifa katika serikali na mashirika ya umma, hivyo watoto wao walikuwa na malezi yaliyofanana.

jeff.gif


Ukiliangalia eneo la Upanga leo huwezi kudhani kuwa lilikuwa eneo muhimu sana katika shughuli za muziki wa vijana, lakini hakika eneo hili lilikuwa na vikundi kadhaa vilivyokuwa na wanamuziki ambao wengi walikuwa ni watoto wa Upanga na wenzao ambao walijiunga nao wakitoka mitaa mingine jirani kama Kariakoo na Magomeni. Upanga ni eneo muhimu sana katika historia ya muziki wa Tanzania.

Enzi hizo vijana walipagawa na muziki wa soul, muziki ambao asili yake ilikuwa Marekani, muziki ambao uliporomoshwa na wanamuziki kama Otis Redding, Percy Sledge, Sam Cooke, James Brown, Clarence Carter, Wilson Pickett, Aretha Franklin na wengi wengine. Vikundi vingi vya muziki vya vijana wa Upanga, waliiga na kupiga muziki huu, na hata kuamua kupaita upanga, Soulville.

Kwenye kona ya barabara ya Mindu na United Nations, palikuwa nyumbani kwa familia ya Mzee Jengo, hapo ndipo palikuwa mahala pa mazoezi pa kundi moja maarufu lililoitwa Groove Makers. Baadhi ya wanamuziki wa kundi hili walikuwa Mohamed Maharage, Joseph Jengo na nduguye Emmanuel Jengo, Herbert Lukindo, Willy Makame, na mpiga Drums ambae mpaka leo yupo katika anga za muziki nae ni Habib Jeff mwanamuziki ambaye toka amejiunga na Mlimani Park miaka ya 70 hajawahi kuhama kundi hilo. Kundi jingine maarufu pale Upanga lilikuwa The Strokers, hili lilikuwa na awamu mbili, awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Donald Max, David Max, Harry Chopeta, Vincet Chopeta, Pino Makame na Ochiwa na Freddy Lukindo.

Awamu ya pili ya kundi hili walikuweko akina Sajula Lukindo,Onesmo Kibira,Innocent Galinoma,Ben Galinoma, Denis Pad, Francis Kasambala, Vicent na Harry Chopeta, Ally Mwarabu, Sabri Mmanga na wengineo. The Barlocks ni bendi nyingine iliyochipukia Upanga, jina la Barlocks lilitokana na kuweko kwa kundi jingine lililojiita The Barkeys, kundi ambalo lipo hai mpaka leo, kwa sasa linajulikana kwa jina la The Tanzanites, lililo chini ya mkongwe Abraham Kapinga. The Barlocks walikuwa wakitumia vyombo vya Barkeys kwani kwa wakati huo bendi hizi zilikuwa kama mkubwa na mdogo. Zamani lilikuwa jambo la kawaida kabisa bendi kuwa na makundi mawili A na B.

Kwa mfano Dar es Salaam Jazz Band enzi za Michael Enoch, iliwahi kuwa na Dar es Salaam Jazz Band B, bendi ambayo ilikuwa na mwanamuziki maarufu Patrick Balisdya. Na bendi hii ikawa bora kiasi cha kuwa tishio kwa Dar es Salaam Jazz Band A, ikalazimika Michael Enoch amshauri mwenye bendi kulivunja kundi hilo la pili na kuwaunganisha wanamuziki pamoja, jambo lililomuudhi Patrick na kuwa sababu moja ya kuanzishwa kwa Afro 70.

Barlocks hiyo ya awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Jimmy Jumba, Pimbi Sokoine, huyu alipewa jina la utani Pimbi kutokana na kuwa mrefu sana (ukikumbuka kuwa Pimbi halisi wa gazeti la Sani alikuwa mfupi sana), Said Mbonde, kaka yake Amina Mbonde binti aliyekuja kuwa muimbaji wa kike mzuri sana enzi zake, pia walikuweko Sajula Lukindo na Abraham.

Kulikuweko na makundi mengine mengi hapo Upanga, kama White Horse, Aquarius ambako ndiko alikotoka producer maarufu Hendrico Figueredo, ambaye pamoja na wenzie walikuja kuanzisha kundi ambalo liko hai mpaka leo linaoitwa InAfrika. Wanamuziki wengine wa Upanga walikuwa akina Joe Ball, Joel De Souza, Mark De Souza,Roy Figueredo, Yustus Pereira, Mike De Souza.

Na kama unavyoona majina yao hawa walikuwa wengi ni Magoa. Kulikuwa na bendi nyingi za Magoa katika miaka hiyo kwani hawa walikuwa ni Waasia wa asili ya kisiwa cha Goa, na lugha waliyotumia ilikuwa Kiingereza, hivyo muziki waliokuwa wakipiga ulikuwa wa lugha hiyo. Bendi ya Kilimanjaro, wananjenje, asili yake ni bendi iliyokuwa ya Magoa wa Tanga iliyoitwa The Love Bugs Baadhi ya wanamuziki niliowataja walienda na kuungana na wanamuziki wengine Arusha na kuvuma sana na kundi lililoitwa Crimson Rage, baadae wakarudi Dar na kujiita The Strange. Leo ukijidai kupiga gitaa Upanga kuna hatari ukaitiwa polisi kwa kupigia watu kelele. Kila zaman a vitabu vyake.
 
Madini tupu, vitu kama hivi vinafaa documentary ama kipindi fulani cha kukumbushia enzi hizo katika music nchini either kwenye radio or TV!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom