Uombaji mikopo kwa njia ya mtandao utamaliza migogoro elimu ya juu? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Uombaji mikopo kwa njia ya mtandao utamaliza migogoro elimu ya juu?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Apr 3, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Apr 3, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Uombaji mikopo kwa njia ya mtandao utamaliza migogoro elimu ya juu?

  Mojawapo ya eneo linalolalamikiwa na wanafunzi wa vyuo na taasisi za elimu ya juu kuhusu Bodi ya Mikopo ( HESLB), ni eneo la madaraja wanayopangiwa na bodi hiyo kwa ajili ya kupata mkopo wa masomo ya kozi wanazochukua.
  Kuna malalamiko kwamba, bodi ya mikopo imekuwa ikipanga madaraja kwa upendeleo kwa kuwa ile dhana ya kumkopesha mwanafunzi anayetoka katika familia maskini kwa kiwango cha asilimia 100,haionekani kufanya kazi kwa wanafunzi walio wengi.
  Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kwamba,katika upangaji wa madaraja unaofanywa na bodi,wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo mkubwa au wa kati, ndio wamekuwa wakipata asilimia 100 na wale wanaotoka katika familia maskini wakiishia kuambulia asilimia 60 mpaka 40.
  April Mosi mwaka huu, bodi ya mikopo nchini ilianzisha utaratibu mpya wa kuomba mikopo kwa wanafunzi wapya na wale wanaoendelea kwa njia ya mtandao.
  Mfumo huu unatarajiwa kuchukua nafasi ya ule wa zamani, ambapo mhusika alikuwa anatakiwa kujaza fomu kisha kuziwasilisha HESLB.
  Fomu hizo zilijazwa taarifa mbalimbali za muombaji zilizokuwa zinahitajika na bodi ili ziisaidie kumpangia muombaji daraja la fedha alizostahili kupewa kama mkopo kwa ajili ya kulipia gharama mbalimbali anazopaswa atika chuo au taasisi aliyokuwa anachukua kozi yake.
  Cosmas Mwaisoba, Mkurugenzi Msaidizi wa bodi ya mikopo, anasema kuwa mfumo huu unaweza kuwa na faida zaidi ukilinganishwa na ule wa awali.
  "Kwa nini tumeanzisha utaratibu huu,nasema kwamba tumeanzisha kwanza ili tuendane na ulimwengu huu wa kisasa wa utandawazi unaohitaji matumizi makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Teknohama) , " alisema.
  Vilevie alisema utaratibu huu unasaidia kuboresha uhifadhi wa kumbukumbu za wanafunzi wanaopewa mikopo na bodi,kwa kuwa matumizi haya ya teknohama katika eneo hili ni bora zaidi katika kurahisisha upatikanaji na utunzaji wa taarifa zote za wanafunzi zilizohifadhiwa.
  Kwani anasema mfumo huu mpya utaipunguzia bodi mlolongo mkubwa uliokuwepo katika utaratibu wa awali uliomtaka muombaji ajaze fomu,azipeleke bodi na bodi ikishazipokea, izichanganue taarifa hizo kielektroniki (scanning) na kisha ianze kuzipangia madaraja.
  Kwa utaratibu huu wa sasa la msingi analotakiwa kulifanya muombaji ni kuingia kwenye tovuti ya bodi ambayo ni Welcome to HESLB ambapo ndani yake atakuta kiungo kinachoitwa ‘Mfumo wa Maombi ya Mkopo kwa Njia ya Mtandao (Online Loan Application System)' ambapo atatakiwa kujaza taarifa zake.
  Mwaisobe alisema muombaji anaweza vile vile akaingia kwenye anwani ya bodi ambayo ni olas.heslb.go.tz ambapo pia anaweza kutuma maombi yake.Njia hizo mbili ndizo zitakazotumika kwa ajili ya kutuma maombi.
  " La msingi na ninaloomba kwa waombaji ni kuingiza taarifa zilizo sahihi kutokana na maswali yaliyoulizwa. Ieleweke daraja la muombaji litajipanga moja kwa moja kutokana na jinsi muombaji alivyoingiza taarifa zake,hivyo ninawaasa waingize taarifa zilizo sahihi ," anasema.
  Hata hivyo Mwaisobwa anapoulizwa iwapo uanzishwa utaratibu huu, ndiyo utahitimisha malalamiko ya wanafunzi dhidi ya bodi yaliyokuwa yanaituhumu kutoa madaraja kwa upendeleo, kwamba wale waliopaswa kupewa asilimia 100 walijikuta wakipata asilimia za chini na wale ambao hawakusitahili walijikuta wakipewa madaraja makubwa hatoi jibu la moja kwa moja .
  "Kwa suala hilo nitafute siku nyingine,lakini kwa leo tuzungumzie zaidi juu ya mfumo huu mpya ili tusipoteze utamu wenyewe, " anasema.
  Aidha anasema mfumo huu mpya unaambatana na kubadilisha kwa utaratibu wa malipo ya ada za maombi ya mkopo ambapo katika mfumo wa zamani,waombaji walilipia ada hizo kupitia benki ya CRDB.
  Maombi ya mkopo wa njia ya mtandao, ada zake zitalipwa kupitia kwenye mitandao ya makampuni ya simu za mikononi.Alisema waombaji watalipa ada ya shilingi 30,000 kupitia Tigo Pesa, M-pesa na Zap.
  Anaeleza kuwa wameamua kutumia mitandao ya makampuni haya ya simu za mkononi kwa ajili ya kurahisisha mlolongo wa utunzaji wa malipo yote ya ada za maombi kwa upande wa bodi na vilevile kurahisha malipo ya fedha wanazoomba wanafunzi.
  Baada ya muombaji kufanya malipo ya ada atapatiwa namba ya kitambulisho kutoka kwenye kampuni aliyolipia pesa, atakayoiingiza kwenye mtandao kwa ajili ya kuendelea na taratibu zingine za kujaza taarifa zake.
  Anasema bodi kwa sasa inaendesha elimu kupitia kwenye vyombo vya habari kwa nia ya kuutangaza mfumo huu mpya ili ueleweke kwa wanafunzi wote wapya wanaotarajia kuomba mikopo na wanaoendelea na masomo yao katika kipindi cha Mwaka wa masomo wa 2011/12.
  Aidha alisema kwamba wameandaa vipeperushi vinavyoelezea utaratibu mzima ulivyo,vipeperushi ambavyo watavisambaza katika vyuo na taasisis za elimu ya juu, kwa maofisa elimu wa wilaya na kwenye Ofisi za Posta nchini.

  Kwa lengo la kurahisisha mfumo huu Ai Mwaisobwa anasema , bodi yake itatembelea pia ‘intanet cafe' nchi nzima ili kutoa elimu maalumu (Technical support) kwa wahudumu kwa lengo la kuwasaidia waombaji watakaoenda kuzitumia cafĂ© hizo kutuma maombi ya mikopo.
  Malalamiko ya wanafunzi kuhusiana na upangaji wa madaraja na ucheleweshaji wa kuwapelekea fedha vyuoni, yamekuwa ni matatizo ambayo mara kwa mara yamekuwa chanzo cha migomo ya kutoingia darasani kwa vyuo vingi nchini.
  Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu nchini (TIA), Mdoe Alhaji Salum, akiongelea juu ya mfumo huu mpya wa uombaji mikopo anasema kwa upande wake hauungi mkono utaratibu huu mpya ulioanzishwa na bodi wa kutuma maombi ya mkopo kwa njia ya mtandao.
  "Mimi siungi mkono utaratibu huu mpya unaoanzishwa na bodi ya mikopo kwa msingi kwamba tatizo la upangaji wa madaraja litakuwa ni kubwa zaidi. Katika mfumo huu, maswali yanayoulizwa ni mafupi sana ambayo majibu yake hayatatoa taarifa za kutosha kumhusu mtu, " anasema.
  Alisema matokeo ya kutokuwa na taarifa za kutosha kumhusu muombaji ni kumfanya asipewe daraja linalomstahili, kwa kuwa anaweza akapewa asilimia 100 wakati hakustahili kabisa au akapewa asilimia 40 wakati alistahili kupata asilimia 100.
  Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Mathias Kipara, alikubaliana na utaratibu huo mpya unaoanzishwa na bodi kwa mantiki kuwa, wakati huu wa utandawazi ni wa matumizi ya teknohama katika shughuli mbalimbali.
  Kwani anasema nyakati za ujima zimeshapita na hivyo matumizi ya mtandao yanapoingia yanazitoa moja kwa moja nyakati hizo. Alisema ni bora kwa wanafunzi watakaohusika na utaratibu huo kuubali na kuutumia.
  "Pamoja na kwamba teknolojia inatakiwa itukute tukiwa tayari kuipokea na isitulazimishe kuipokea bado natoa angalizo kwa bodi ya mikopo kwamba wanapaswa watoe elimu ya kutosha kwanza kwa wadau wote na hasa wanafunzi juu ya namna utakavyofanya kazi, " alisema.
  Alifafanua kuwa wao kama Daruso walikutana na bodi na wakaieleza msimamo wao huo. Alipoulizwa na mwandishi, iwapo bodi itoe elimu ya mfumo huo kwa kipindi cha muda gani ndipo mfumo uanze, alisema elimu itolewe kwa muda ambao bodi itaridhika kwamba wadau wameufahamu kwa kina.
  Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha kilimo Cha Sokoine (SUA), Profesa Gerald Monela kwa upande wake anasema hana taarifa juu ya mfumo mpya wa kuomba mkopo wa fedha za masomo kwa njia ya mtandao unaoanzishwa na bodi ya mikopo.
  " Mimi sina taarifa ya kuwepo kwa mfumo mpya unaoanzishwa na bodi hiyo.Ninachojua mimi ni kwamba Rais Jakaya Kikwete ameunda tume ya kuangalia matatizo yaliyo katika bodi ya mkopo ambayo yamekuwa yakisababisha malalamiko na migomo toka kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, " anasema.
  Alifafanua kwamba ana taarifa na tume hiyo iliyoundwa na Rais na kwamba ana imani katika ushauri wake kwa Rais baada ya kukamilisha kazi iliyotumwa, itakuja na utaratibu muafaka wa namna ya kuomba mikopo kwa kuwa itakuwa imeshaainisha mapungufu yaliyoko katika mfumo huu wa sasa.
  Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ,Dk. Benson Bana, aliipongeza bodi kwa kuanza mchakato mapema hata kabla ya matokeo ya kidato cha sita hayatoka .
  "Wasiwasi wangu ni kuwa kuna tume ambayo imeundwa na Rais ili iangalie matatizo yaliyoko katika bodi ambayo yamepelekea malalamiko na migomo kwa wanafuzi wa vyuo vikuu, sasa endapo itatoa ushauri wa mfumo wa kuomba mkopo ulio tofauti na huu unaoanzishwa na bodi,itakuwaje, " alisema
  Dk. Bana alilitaja pia eneo linalotumika kupanga madaraja ambapo baadhi ya wanafunzi hunyimwa mikopo kwa kuwa tu walisoma shule za aina ya "Kifungilo" ambazo huelezwa ni za watu wenye uwezo.
  Hivyo anasema ni muhimu mikopo ikatolewa kwa wanafunzi wote waliofaulu vizuri zaidi ya wenzao bila ya kuangalia kuwa walisoma wapi kwa kuwa hadi wanafika ngazi ya kusoma vyuo vya elimu ya juu, waliokuwa wanawasomesha katika shule hizo wakati mwingine huenda wakawa hawana tena uwezo waliokuwa nao nyuma.
   
Loading...