Undani wa ugonjwa wa pumu, dalili na namna ya kukabiliana nao

Status
Not open for further replies.

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Aug 7, 2018
529
1,000
20210216_110854_0000.png


Pumu au ‘asthma’ ni moja kati ya magonjwa hatari sana yanayoathiri mfumo wa upumuaji ambao huathiri takriban watu million 130 duniani kote. Ingawa hakuna sababu ya moja kwa moja ya kupelekea kupata ugonjwa huu, utafiti umethibitisha ya kuwa ugonjwa huu hutokea kutokana na sababu kuu mbili, yaani vinasaba na mazingira.

Nadharia ya vinasaba inatueleza kua ugonjwa huu huwapata zaidi watu ambao wana undugu wa damu na watu wenye ugonjwa huu, yaani ugonjwa unaweza kurithiwa kizazi na kizazi katika familia moja. Mbali na vinasaba, ugonjwa huu huweza kutokea kwa sababu za kimazingira kama vile hali ya baridi, moshi, vumbi na vitu vyote ambavyo vinaweza kuvutwa na kuingia ndani ya mfumo wa upumuaji.

Mfumo wa upumuaji na kutokea kwa pumu

Kabla ya kuendelea ni vyema sana tukatambua kwa kifupi mfumo wa upumuaji. Katika mwili wa binaadamu mfumo wa upumuaji umegawanyika katika makundi makuu mawili, yaani mfumo wa upumuaji wa juu na mfumo wa upumuaji wa chini.

Mfumo wa juu unahusisha pua, koo pamoja na mrija unaounganisha koo mpaka kwenye mapafu wakati mfumo wa chini unahusisha mapafu na kila kilichomo ndani yake. Ili kupata hewa safi, mfumo wa upumuaji [hasa wa juu] umelindwa na vinyweleo pamoja na ute ambao hunasa na kuchuja uchafu wowote ambao umeingia pamoja na hewa.

Ndugu msomaji, elewa ya kuwa, kitendo cha mfumo wa upumuaji kutoa ute ni kawaida kabisa kwa watu wote na ute huu hutolewa kulingana na uhitaji lakini hali huwa tofauti kwa wagonjwa wa pumu kwani ute huu hutolewa kwa wingi na kusinyaza mrija wa kusafirishia hewa hivyo kumpeleka mgonjwa kukosa hewa ya kutosha na kitendo hiki ndicho kinachoitwa shambulio la pumu.

Pumu kwa watoto

Ingawa dalili za pumu kwa watoto zinaweza kufanana na zile wanazopata wagonjwa watu wazima, wakati mwingine inaweza kuwa si kazi rahisi kuthibitisha dalili hizo kuwa zinaashiria pumu.

Kutokana na kuzaliwa na maumbile madogo, njia ya kupitishia hewa pia huwa ndogo na kuwasababishia watoto kupata dalili za pumu. Hali hii hushamiri zaidi endapo njia hizi zitaathirika na ugonjwa wowote mwengine usiokua pumu.

Watu walio hatarini

Kama tulivyojionea, ugonjwa huu una uhusiano wa moja kwa moja wa vinasaba na mazingira hivyo ugonjwa huu unaweza kuwapata watu ambao ndugu zao wa damu wana ugonjwa huu. Pia ugonjwa huu unaweza kuwapata watu wenye matatizo ya mzio [allergy], wenye uzito mkubwa pamoja na wavutaji wa sigara.

Dalili zake

Dalili za pumu zinaweza kuwa tofauti baina ya mtu na mtu, yaani wapo wanaopata dalili za mara kwa mara na wengine wanaweza kupata dalili mara chache sana.

Kwa ujumla dalili za pumu zinaweza kuwa kukosa pumzi, kifua kubana na kuuma, kukosa usingizi, kikohozi pamoja na kutoa sauti kama ya filimbi wakati wa kupumua.

Namna ya kuzuia shambulio la pumu

Kama tunavyojua, mpaka sasa hakuna matibabu ya moja kwa moja [dawa za viwandani] ya kuondoa tatizo hili, hivyo njia nzuri zaidi ya kuepuka pumu ni kuvitambua visababishi na kuviepuka.

Visababishi hivi vinaweza kuwa vumbi, manyoya ya wanyama, baadhi ya kemikali [pafyumu n.k], moshi, hali ya hewa ya baridi, mazoezi makali, hasira na msongo wa mawazo pamoja na baadhi ya madawa. Hivyo basi, jambo la muhimu wagonjwa kutambua kisababishi kipi hasa kinachochea kupata mashambulio na kukiepuka.
 
Upvote 0
Status
Not open for further replies.

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom