Unayo pumzi ya kugandamiza mpira? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Unayo pumzi ya kugandamiza mpira?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Paparazi Muwazi, Jan 15, 2009.

 1. P

  Paparazi Muwazi JF-Expert Member

  #1
  Jan 15, 2009
  Joined: Dec 23, 2007
  Messages: 310
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Na Muhingo Rweyemamu

  GAZETI la Raia Mwema wiki iliyopita lilikuwa na makala ya Ayoub Rioba yenye kichwa cha habari: ‘CCM kitavunjika ili kipate nguvu’.

  Tulijadili naye sana kuhusu maudhui ya makala yake na hasa niliyokuwa nayatafakari tofauti na tafakuri yake. Ingawa hoja zake zilitosha ukurasa na nusu, ziligusa mambo mengi. Migogoro ndani ya chama tawala, ufisadi nchini, nani fisadi na nani mzalendo. Baada ya mazungumzo na Rioba, tulikubaliana nitanue mjadala huo ili kuwavuta ambao wangependa kuchangia. Na hivi ndivyo ninavyofanya.

  Yapo maeneo mawili au matatu ambayo tunatofautiana kimaono. Amejaribu kueleza jinsi CCM ya awali ilivyokuwa ikiwapa wanachama wake nafasi ya kutoa maoni yao na kwamba chama hicho kingeendeleza tabia hiyo, kingefanikiwa sana.

  Ukweli ninaoufahamu mimi ni kwamba CCM ya awali, haikuwa na sifa hiyo. Kimsingi, CCM tangu TANU, ilikuwa na msemaji mmoja aliyetungiwa misemo kama Zidumu Fikra za Mwenyekiti wa CCM. Yeye alikuwa akifikiri, wengine wakisikiliza na kupiga makofi. Hali hiyo ndiyo inakisumbua chama hicho kwa sasa. Wanachama wake wengi wana shauku ya kuongea lakini chama hakina utamaduni huo; ni kama jini kafunguliwa kutoka kwenye chupa.

  Sera ya habari ya chama na serikali yake, ilivitaka vyombo vya habari kutangaza uamuzi wa vikao vya chama na serikali na si kujadili kinyume chake.

  Orodha ya waliowahi kuathirika na kilichoitwa kimbelembele chao ni ndefu. Wapo akina Kasanga Tumbo, Zuberi Mtemvu, Oscar Kambona, Eli Anangisye, Kasella Bantu, Aboud Jumbe, Horace Kolimba, Shaaban Mloo, Seif Sharif Hamad, Hamad Rashid na Ramadhani Haji kwa kutaja wachache.

  Kimsingi, Chama Cha Wananchi (CUF) ni matokeo ya tabia ya CCM ya kugandamiza mawazo ya wanachama wake. Jumla ya viongozi 19; wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, walitimuliwa kwenye chama hicho baada ya kuhoji mambo, tena ya msingi kabisa. Baada ya kutimuliwa, wanasiasa hao wakaanza vuguvugu la kutaka watu waruhusiwe kusema na kusikilizwa. Vuguvugu hilo lilianzishwa chini ya mwavuli wa Kamahuru ambayo baadaye ilijigeuza sura na kuwa CUF.

  Kwa ujumla, si CCM wala mtangulizi wake TANU, kilichokuwa na sera ya kuwaruhusu watu kutoa maoni yao. Chama kiliheshimu sana vikao, ndiyo! Lakini ajenda ziliandaliwa Dar es Salaam, wazungumzaji walitoka Dar es Salaam na aliyetaka kuzungumza asiyetoka Dar es Salaam, alilazimika kupata ruhusa kutoka kwa watu wa Dar es Salaam. Mfano halisi ni Munasa Sabi Munasa aliyetaka kuzungumza kutokea Mara. Kilichompata ni kuitwa mwendawazimu. Na aliambiwa yeye ni mwendawazimu baada ya kuwatuhumu wenzake kuwa ni wajumbe wa kutimiza akidi (quorum).

  Rioba alizungumzia pia suala la CCM kuwa na makundi mengi yanayopingana.

  Munasa alipata kusema hivi: “Ukiangalia aina ya wanachama wa CCM unakuta mchanyato wa ajabu. Kuanzia waliberali, wahafidhina, wajamaa damu, wakomunist wastaafu, mabepari, wafanyakazi, wachuuzi, wasomi, waganga wa kienyeji, wakulima na wote wanakubaliana kila kitu. Kuna ishara za dhahiri kuwa CCM sasa wanaanza kutofautiana. Kwamba zile tofauti nilizozitaja hapo juu, zinafikia mahala zinaanza kufanya kazi. Wengi tuliziona zikifanya kazi kwa namna fulani katika Bunge kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.”

  Hapa ndipo kuna hoja ya msingi. Nikianza na wana CCM kueleza ukweli wazi wazi, nadhani ni kwa bahati mbaya Rioba amewaona Membe na Anna Makinda kwa leo. Wapo wana CCM walianza kuonya muda mrefu.

  Septemba 11, 2001, nikiwa Naibu Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi na Dany Mwakiteleko akiwa Mhariri wa Habari, tulitoa habari kuu iliyokuwa na kichwa cha habari: ‘MKAPA CCM INAKUANGUKIA MKONONI’. Habari hiyo ilikuwa ni mahojiano maalum na mwanachama mmoja Aloo Sagamba. Yeye hakuishia kusema, alijiuzulu wadhifa wake kama kiongozi wa Umoja wa Vijana kwa kutoridhika jinsi CCM ilivyokuwa ikiendesha mambo wakati huo. Nasikitika kwamba imepita miaka minane sasa tangu tukio au kauli hiyo itoke, waandishi wa historia ya migogoro ya CCM wanataka kuisahau kauli hiyo.

  Pili, katika hoja ya mchanyato wa CCM kukubaliana kila kitu, Rioba ni mwanataaluma na naomba nimrejeshe katika taaluma. Nawapeleka katika kitabu cha Social Psychology cha 1995 cha magwiji Irwin Horowizt wa Chuo Kikuu cha Oregon na Kenneth Bordens wa Chuo Kikuu cha Indiana. Katika sura ya 10, Group Processes, wanazuoni hawa walijadili tabia za makundi na wakaangalia kwa kina mtafaruku uliotokea katika vita maarufu ya Bay of Pigs. Kwa taarifa, Bay of Pigs ni vita iliyopiganwa na Wacuba waishio Miami nchini Marekani. Katika vita hiyo, askari wa Cuba waishio Miami waliomba msaada kwa Serikali ya Marekani kwenda kumpindua Fidel Castro.

  Jeshi la Marekani likakubali kuwasaidia kwa makubaliano kwamba wao (Wacuba) watangulie na vita ikianza, Jeshi la Marekani litafuata. Sasa hawa magwiji wanahoji ni kwa vipi hawa askari maarufu wa Cuba walikubali mipango nusu nusu wakijua wanaweza kuhatarisha maisha yao?

  Wanasema askari hao walichaguliwa kutokana na uwezo wao lakini walikubali kuingia vitani wakiwa na taarifa nusu nusu. Katika maelezo yao baada ya kushindwa vibaya vita, wengi wao walisema kuwa walikuwa na wasiwasi na mipango hiyo tangu mwanzo ingawa hawakusema chochote. Lakini pia ilikuja kujulikana kuwa askari hawa, hawakuulizwa chochote mmoja mmoja bali kama kundi.

  Na wanasema kushiriki katika kundi, kuliwabadilisha mawazo na misimamo yao. Wasomi hawa wanahitimisha kwa kusema kuwa mara nyingi, mawazo ya mtu mmoja, hubadilishwa na uwepo wa watu wengine. Kwa maneno yao wenyewe wanasema: “In social setting, people may doubt their own perceptions, suppress their reservations, withhold their opinions, be swayed by social pressures. These effects can be even stronger in true groups.” (uk. 399).

  Kuhusu hoja ya kuwa na makundi katika chama tawala, labda nianze kwa kusema kuwa hakuna chama hata kimoja duniani ambacho wanachama wake hukubaliana kwa kila kitu. Vyama vyote vikubwa na vidogo duniani vyenye demokrasia ya ndani, huwa na tofauti za kimtazamo na kimrengo. Vyama vyote vikuu vya Uingereza, vinatofautiana vyenyewe kwa vyenyewe ndani kwa ndani. Kinachompata Gordon Brown wa Uingereza ndani ya chama chake kinashuhudiwa na dunia nzima.

  Kule Marekani nako ndani ya vyama vikuu viwili kuna kachumbari ya hali ya juu. Kwa mfano, kwa mujibu wa Kituo cha Utafiti cha Pew, Chama cha Democrat kina watu wenye itikadi za aina tatu tofauti. Chama hicho chenye wanachama milioni 72, kina wahafidhina (conservatives) wanaofanya asilimia 33.2, liberals (waliberali) wanaofanya asilimia 45.6 na disadvantaged (wanyonge) asilimia 21.2. Hiki chama bado kina mshikamano wa hali ya juu na safari hii ndicho kimemtoa Rais wa Marekani atakayeanza kazi mwezi ujao. Tangu kilipoanzishwa 1792, chama hiki kimepitia katika vipindi vingi vigumu vinavyotokana na mawazo yanayopingana ya wanachama wake. Lakini ugumu wa vipindi hivyo, ndiyo unakifanya kuwa imara zaidi.

  Mbali ya kuwa na wanachama wanaotofautiana kiitikadi, chama chenyewe kina itikadi tofauti kwa mambo tofauti. Kwa mfano, katika suala la uchumi, kina mrengo wa ujamaa (leftist). Pamoja na kwamba chama hicho kinakubaliana na maisha ya nchi hiyo ya kibepari, bado kinaamini kuwa kila binadamu anastahili kumjali mwingine. Kwamba mali zitumike kwa faida ya wote. Lakini chama hicho hicho katika masuala ya kijamii wao hujiita free will au libertarians (uhuru wa kiuamuzi). Unataka kutoa mimba? Toa! Unataka kutumia kondomu? tumia! Hutaki kutumia? Shauri yako! Na kwao, mambo yote haya ni ya msingi na huleta changamoto kubwa kwa wagombea wakati wa uchaguzi.

  Pamoja na kwamba Hillary Clinton na Barack Obama walikuwa wa mrengo mmoja katika eneo la uchumi, wanaendelea kuwa na tofauti kubwa katika eneo la kijamii. Hata hivyo, tofauti zao hazijamzuia Obama kumchagua Clinton kushika moja ya nafasi kubwa serikalini.

  Republican ni chama cha kibepari. Democrat ni chama cha kijamaa. Lakini hiyo haijamzuia Obama kuwateua Republicans kuingia katika serikali na kuunda serikali moja yenye nguvu. Kwa hiyo makundi ya wajamaa na mabepari katika CCM si jambo la ajabu.

  Na si la ajabu kwa sasa kwa sababu Tanzania tunaishi katika dunia nyingi. Ipo dunia ya Mwalimu haijafa, ingawa hata akifufuka hawezi kuiishi kwa sababu imebaki katika fikra tu; ipo dunia ya kibepari ambayo imesukumwa kwetu na mfumo wa uchumi wa dunia nzima. Kwa hiyo kutofautina kwa misingi inayokubalika, ndiyo uhai wa chama chochote cha kisiasa duniani. Siasa ni kukubaliana kutokukubaliana. Na mkiondoka hapo, mnafanana na watu wanaokubaliana kumbe mmekubaliana kutokukubaliana.

  Lakini pia hatuhitaji kwenda nje ya nchi ili kujifunza juu ya kuhitilafiana katika vyama na kuendelea kufanya kazi pamoja. Vyama vikuu vya upinzani humu nchini navyo vina makundi ndani mwake. Tena makundi yaliyomo katika vyama hivi ni mabaya kuliko yaliyomo ndani ya CCM kwa sababu makundi ya vyama vya upinzani ni ya kiitikadi.

  Kwa mfano, CUF ina makundi makubwa mawili. Kundi moja linaongozwa na Juma Duni Haji likiwa na watu kama Profesa Ibrahim Lipumba na Rwakatare; ni kundi la jino kwa jino. Ni ‘militants’ linalotaka kila kitu kifanyike sasa na wala siyo kesho.

  Kundi hili linatofautiana kimsimamo na kundi linaloongozwa na Maalim Seif Shariff Hamad likiwa nao akina Hamad Rashid Mohammed, Ismail Jussa na Mbarala Maharagande. Hili ni la moderation, linaloamini kutatua mambo katika meza ya mazungumzo. Kwa misimamo yake ni wahafidhina. Kwa upande mwingine, CHADEMA ina makundi yenye kutofautiana sana. Freeman Mbowe anakubaliana sana na Mzee Ndesamburo kuliko anavyokubaliana na Zitto Kabwe na John Mnyika ambao ni wajamaa (centrists). Kwa kiwango fulani, mambo wanayoyaamini yanafanana sana na ya Dk. Wilbroad Slaa ingawa tofauti yake na akina Zitto ni kwamba yeye ni ethicist zaidi. Kwa upande wake, Mbowe, na Mzee Ndesamburo msimamo wao ni wa CHADEMA asilia ya Mzee Edwin Mtei ambao ni waumini wa ubepari.

  Zitto Kabwe na Mnyika wanaweza kukaa wakazungumza, wakaelewana na sera za CCM kuliko wanavyoweza kukubaliana na sera za CHADEMA kwa imani ya kundi la akina Mbowe na mwasisi wake, Mzee Mtei. Hawa CHADEMA wanahitaji kuwa waangalifu mno kwa sababu tofauti yao imejikita katika itikadi. Na wakiingia kwenye madaraka, inaweza kuwa mbaya zaidi kwao kuliko ilivyo mbaya kwa CCM.

  Tatizo la CCM si itikadi. Wote walio katika usukani wa chama, ni ma leftists. Jakaya Kikwete ni leftist anayeamini katika ujamaa. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ni mjamaa, Pius Msekwa ni mjamaa, Kingunge Ngombale – Mwiru ni mjamaa pia. Tofauti kubwa inayotokea ndani ya CCM ni mgawanyiko wa ugomvi wa madaraka na kila mtu anataka kuwa juu ya mwenzake.

  Mgawanyiko mkubwa uliotokea katika siku za hivi karibuni, ni kundi moja la wana CCM kuonekana kuwa katika vita ya ufisadi kuliko wanachama wenzao. Hawa ndio anawasema Rioba kwamba wameanza kujitokeza na wanakemea hali hii ya viongozi kujitakia manufaa binafisi. Mimi nasema sawa, lakini kama vyombo vya habari, tulitakiwa kwenda mbali zaidi ya hapo. Kwa kiasi fulani tunawafahamu wanasiasa wetu na hasa waliomo kwenye chama tawala na hasa hawa wanaoitwa mafisadi, na wale wanaowaita wenzao mafisadi.

  Na tunafahamu kwamba kwa muda wa miaka zaidi ya 20 wengi wa hawa wanaoitana mafisadi walikuwa marafiki, tena marafiki wakubwa. Kundi lililoingia madarakani 2005 limeanza rasmi harakati hizo zaidi ya miaka 10 iliyopita. Mwaka 1995, ndiyo kundi lililochukizwa na hatua ya Mwalimu Nyerere kumbeba Benjamin Mkapa.

  Wasio na kumbukumbu nzuri, wakasome magazeti jinsi kundi hili lilivyomchafua Nyerere. Mmoja ndiye alikuwa akitengeneza vichwa vya habari vya magazeti. Wengi, na hasa waandishi wa habari ni mashahidi. Mwanasiasa mmoja katika harakati hizi hajasahau kichwa cha habari alichokiasisi kilichosema: ‘Nyerere apaka chokaa makaburi’.

  Hawa wanaoita na wanaoitwa mafisadi walikuwa pamoja, walipanga pamoja, walikusanya pamoja, walikula na kunywa pamoja, na lugha yao ilikuwa moja. Ilikuwa ndege wa mbawa zinazofanana wanaruka pamoja.

  Kundi kubwa linalojulikana zaidi katika harakati hizi lilikuwa na watu wengi. Lakini vinara wake walikuwa Edward Lowassa, Samuel Sitta na Rostam Aziz.

  Hili kundi liliendelea kuwa pamoja hadi uchaguzi wa 2005. Lilikuwa pamoja hadi kwenye kampeni ya Sitta kuwania ubunge.

  Chai pamoja na maandazi ya wajumbe wa timu ya kampeni ya Sitta ilichemshwa/yalichomwa na mke wa Rostam Aziz nyumbani kwake hapa Dar es Salaam na Dodoma. Lowassa ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Sitta. Nusu ya hotuba ya Sitta ya kuomba kura iliandaliwa na Rostam. Sehemu ya utafiti kuhusu Bunge la Kenya ilifanywa na Rostam. Marehemu Juma Jamaldin Akukweti ndiye alikuwa kizingiti kwa Sitta kuwania ubunge, lakini ni marafiki zake hawa waliopewa jukumu kuachia nafasi hiyo. Hawa hivi sasa wamefarakana, lakini hawatuelezi wamefarakana lini na ni jambo gani limewafarakanisha baada ya kuwa marafiki. Je, ni fedha, ni vyeo au ni uzalendo? Kundi hili limetengana sasa. Wapo wazalendo na wapo mafisadi.

  Nionyeshe rafiki zako nitakueleza wewe ni nani. Tungependa kujua, uzalendo wa wazalendo hawa ulianza lini na ufisadi wa mafisadi hawa ulianza lini.

  Hawa waliogharimiana kila kitu, wamekorofishana lini na kwa sababu zipi? Waandishi wa habari tunatakiwa kuchunguza kwa kuwauliza maswali pande zote zinazohusika. Na tuache ushabiki kwa sababu ushabiki wetu kwa kiasi fulani umetuzuia kupata habari za pande mbili. Wapo watu hawataki kuwauliza wengine maswali eti wanasema hawa ni mafisadi. Huo si uandishi wa habari.

  Na mwandishi anayejizuia kuandika habari za mtu, analo lake jambo. Inawezekana hataki habari za huyo zisikike kwa kuwa zikisikika zitaua ukweli alio nao. Lakini pia, inawezekana wapo watu, hawataki habari za huyo zisikike kwa sababu zikisikika zinaweza kuwa na mnyororo na habari zake yeye mwenyewe. Huyu atafanya kila mbinu habari za hawa wanaoitwa mafisadi zisisikike kabisa. Atahakikisha zimegandamizwa. Lakini tutagandamiza ukweli hadi lini?

  Tuwape nafasi hawa ‘mafisadi’ wa ndani ya CCM watueleze, walikosana lini na hawa ‘wazalendo’. Na tuwape nafasi hawa ‘wazalendo’ watueleze walikosana lini na wenzao. Watueleze ufisadi huu umeanza lini? Ni hivi karibuni? Miaka 10 iliyopita au 20? Na hawa wazalendo watueleze wamejua lini kwamba hawa ni mafisadi? Tukiamua kuwauliza, tuwaulize swali la msingi kabisa. Kila mbunge wa CCM atueleze alikopata fedha zake za kampeni. Najua wapo watu wasiotaka kusikia swali hili likiulizwa. Lakini swali hili tu moja limebeba majibu ya maswali mengi.

  Tusipokuwa waangalifu, tunaweza kukuta tunatumiwa na kundi la watu, lenye lengo la kutaka kunyamazisha habari kutoka upande wa pili wa marafiki zao waliokorofishana. Na uandishi wa habari, haujakamilika kama hatujapata taarifa kutoka pande mbili.

  Wale viongozi wana CCM wanaowaita marafiki zao mafisadi, bila kutueleza urafiki wao umekoma lini, wana lao jambo. Kuna ukweli wanataka kuuficha. Wana kitu wanakijua, na wanatumia nguvu zao zote kuhakikisha hakitoki hadharani. Nawafananisha na nadharia ya ‘Beach Ball Effect’ ya mwanamama Debby Ford aliyoifafanua vizuri sana katika kitabu chake ‘Why Good People Do Bad Things’. Huyu mama pia ni mtunzi wa kitabu cha ‘The Dark Side of the Light Chasers’.

  Katika falsafa yake hiyo, anasema ukichukua mpira na kuujaza pumzi, kisha ukaugandamiza kwenye pipa la maji au ufukweni baharini, unaweza kudhani mpira huo umezama. Na anasema, ipo dakika au sekunde utakapojisahau na kulegeza mkono wako uliogandamiza mpira huo, ndipo mpira utakapokufyatukia usoni mwako na kukujeruhi.

  Wapo watu ambao maisha yao yote yamekuwa ni ya Beach Ball Effect. Fikiria muda ambao watu wameutumia ‘kuugandamiza mpira kwenye maji’. Wametumia fedha nyingi, wametumia nguvu, nyingi, wamewajeruhi watu wengi, ili kuficha mipira yao kwenye pipa la maji. Lakini kati ya hao hakuna hata mmoja anayefanikiwa kuificha mipira hiyo maishani.

  Katika filamu ya Doughtfire, baba mmoja aliyeamua kuwa mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya mke wake waliyeachana huku akijifanya kuwa mwanamke, aliumbuka siku alipokwenda kwenye choo cha wanaume na kukojoa akiwa amesimama badala ya kuchuchumaa kama wafanyavyo wanawake. Watoto wake wakaenda chooni kwao na kumkuta ‘mama’ akikojoa kama mwanaume. Wakamshikia fagio na kutaka kumfukuza nyumbani mwao, mpaka alipovua vinyago, wakamtambua kuwa ndiye baba yao mzazi. Sekunde moja tu, mpira ulifyatuka!

  Mel Gibson, yule mtunzi wa picha maarufu ‘Passion of Christ’, aliendelea kuheshimika kama mmoja wa watu wanaotunza maadili. Alipotunga Passion of Christ, wapo waliomlaumu kwamba ana upinzani na dini, mpaka waliipeleka kwa Baba Mtakatifu ili atoe uamuzi wake kama ionyeshwe au ipigwe marufuku. Gibson akaonana na Papa na kupewa baraka akisifika kwa maadili yake. Lakini siku aliposhikwa akiendesha gari amelewa, matusi aliyoporomosha, hakuna mtu aliyependa kuamini kama yalitolewa na Gibson. Alijisahau akauondoa mkono kwenye mpira aliougandamiza kwa muda mrefu kwenye pipa la maji.

  Zipo njia nyingi za Beach Ball kujitokeza. Unaweza kumwita mkeo kwa jina la hawara yako ambaye mara nyingi umekana kuwa na uhusiano naye.

  Hapo ndipo utakapofurumua mambo yote. Unaweza kuugandamiza ukweli kwa njia yoyote ile kwa kutumia fedha, vitisho, waandishi wa habari na hata cheo chako. Lakini siku moja ukajikuta umejiingiza katika anga za mwandishi jasiri anayejua ukweli wako uliouficha na akalipulia mambo yako yote na kuyaweka hadharani. Huko ndiko tunakoelekea

  Naomba nimalizie kwa kuwapa angalizo. Wakati wa uchaguzi wa Marekani 2000, Al Gore alifanya kosa kubwa lililomkosesha urais. Alidhani skandali juu ya Monica Lewinsky imemmaliza kweli kweli Rais Bill Clinton. Na ili kudhihirisha kwamba anajitenga na Clinton aliyetumika naye kwa muda wote kama makamu wake wa rais, akamteua Joe Lieberman kuwa mgombea mwenza. Lieberman alikuwa mpinzani mkubwa wa Clinton ndani ya Democrat.

  Badala ya kuendeleza katika yale mazuri yaliyofanywa na Clinton, Al Gore akaanzisha sera ya ajabu ya ‘Clinton fatigue’. Wamarekani wakamwona mpumbavu wakamnyima kura. Makosa hayo hayo hayo yamefanywa na John McCain ambaye amekuwa kikaragosi cha George W. Bush katika kipindi chake chote cha miaka minane ya utawala wa kimabavu.

  Lakini ilipofika wakati wa uchaguzi akatangaza: “I am not George Bush.” Mwaka 2000 watu wakasema Al Gore wewe ni Democrat. Kujitenga na Clinton ni unafiki. Mwaka 2008 watu wakasema wewe McCain ni Republican, kujitenga na George Bush ni uzandiki. Wakawanyima wote kura. CCM wanaoitwa mafisadi na wanaowaita wenzao mafisadi mna la kujifunza hapa kwa sababu nyote ni wa kijani na njano.
   
 2. Mpita Njia

  Mpita Njia JF-Expert Member

  #2
  Jan 15, 2009
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 7,012
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Paparazi, ningependa kupata gazeti lililoandika hii, ni lipi hilo?
   
 3. I

  Ilongo JF-Expert Member

  #3
  Jan 15, 2009
  Joined: Feb 25, 2007
  Messages: 292
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  Mpita Njia,


  Linaitwa Rai. Ebu gonga hapa
   
 4. Ochu

  Ochu JF-Expert Member

  #4
  Jan 15, 2009
  Joined: May 13, 2008
  Messages: 972
  Likes Received: 7
  Trophy Points: 35
  unatuchanganya; Rai au Raia Mwema?
   
 5. Baba_Enock

  Baba_Enock JF-Expert Member

  #5
  Jan 15, 2009
  Joined: Aug 21, 2008
  Messages: 6,802
  Likes Received: 163
  Trophy Points: 160
  RAI -> Muhingo Rweyemamu

  Rai Mwema -> Ryoba
   
 6. I

  Ilongo JF-Expert Member

  #6
  Jan 15, 2009
  Joined: Feb 25, 2007
  Messages: 292
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0

  Ubishi hauisaidii!!!!! teh teh teh teh teh


  Gonga hapa
   
 7. BabaDesi

  BabaDesi JF-Expert Member

  #7
  Jan 15, 2009
  Joined: Jun 30, 2007
  Messages: 2,793
  Likes Received: 33
  Trophy Points: 145
  ...Makala nzuri. PR nzuri kwa Mafisadi. Swali, Yeye Muhingo ameishachukua hatua za kwenda kwa Mafisadi kupata upande wao wa habari ama anawashutumu tu wenzake kwa kutofanya hivyo? Na kama aliishakwenda, what is their story? Ninachoona ni Muhingo
  ku-preach ambacho yeye mwenyewe ameshindwa ku-practise...!
   
 8. Mpita Njia

  Mpita Njia JF-Expert Member

  #8
  Jan 15, 2009
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 7,012
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Nadhani ni la wiki iliyopita maana ninalo la leo na halina hiyo makala
   
 9. I

  Ilongo JF-Expert Member

  #9
  Jan 15, 2009
  Joined: Feb 25, 2007
  Messages: 292
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0


  Well, pakikosekana cha kujadili, wataalamu wanaingia kwenye stoo na kuibua yaliyopita ama yale ambayo hayakupata kujadiliwa. Umeshahau ile kuhusu Mangula??

  Hii habari iliandikwa mwaka jana (18 Disemba 2008).
   
 10. Nemesis

  Nemesis JF-Expert Member

  #10
  Jan 15, 2009
  Joined: Feb 13, 2008
  Messages: 3,833
  Likes Received: 1,089
  Trophy Points: 280
  huyu Muhingo Rweyemamu ni mchambuzi mzuri, tatizo lipo pale anapojitoa mhanga kuwatetea mafisadi. LOL! hivi anataka wanaCCM wasipigie kelele ufisadi? ebaneee elimu zetu hizi zinatupeleka pabaya. Muhingo anatakakusema Mccain angemsifia Bush angepata Urais!
   
Loading...