Unataka kufanya transfer (kubadili jina) la kiwanja/nyumba, utaratibu wa haraka ni huu

Gasy wa Ukweli

JF-Expert Member
Nov 7, 2010
387
187
Watu wengi wamenunua viwanja/nyumba lakini mali hizo zimeendelea kubaki katika majina ya waliowauzia. Wapo ambao imepita hata miaka kumi tangu wanunue maeneo lakini bado hawajabadili jina kuingia jina lake. Zipo sababu nyingi zinazosababisha hali hiyo lakini moja ni watu kutokujua umuhimu wa kubadili jina kwa haraka. Hapa sizungumzii tu kubadili jina isipokuwa nazungumzia kubadili jina kwa haraka. Kupitia makala haya napenda kuwaamsha watu kuhusu umuhimu mkubwa wa kubadili jina kwa haraka iwapo umenunua nyumba/kiwanja kwa mtu. Ni muhimu sana kufanya hivyo na itakuepusha na mambo mengi.

1. KAMA HUJABADILI JINA ALIYEKUUZIA BADO NDIYE MMILIKI.

Ikiwa kutatokea mgogoro wa umiliki wakati ambao umenunua nyumba/kiwanja na hujabadili jina kwenda kwenye jina lako kuna hatari kubwa zaidi ya kupoteza ulichonunua. Hii ni kutokana na ukweli kuwa utapokuwa unatatuliwa mgogoro wa nani mmiliki swali la kwanza huwa ni nani ambaye nyaraka ya umiliki ina jina lake.

Yule ambaye jina lake linaonekana kwenye hati au leseni ya makazi ndiye hupewa kipaumbele na kwa mujibu wa sheria mwenye jina kwenye hati au leseni ya makazi ndiye mmiliki. Wewe uliyenunua utakuwa na mkataba na jina lako litakuwa kwenye mkataba lakini pamoja na kuwa na jina kwenye mkataba bado huwezi kulinganisha mkataba na hati au leseni ya makazi. Jina linalotokea kwenye hati au leseni ya makazi huwa na nguvu zaidi kuliko lile la kwenye mkataba.

2. UMUHIMU WA KUBADILISHA JINA KWA HARAKA.

Upo umuhimu mkubwa mara tu baada ya manunuzi ya kiwanja/nyumba kukimbilia hatua za kubadili jina. Ni vyema wakati unajipanga kununua nyumba/kiwanja ukajipanga moja kwa moja na hatua za kuanza kubadili jina mara baada ya kukamilika kwa mkataba wa manunuzi.
Mara nyingi tumekuwa tukiwashauri watu kuwa mkataba wa manunuzi unapokuwa umekamilika leo basi hakikisha kesho unaanza taratibu za kubadili jina( transfer).

Ni utaratibu huu pekee utakaokufanya kujiamini na ulichonunua. Pia unapotokea mgogoro kabla ya kubadili jina kuanzia hapo unakuwa na nafasi ndogo ya kuweza kubadili jina kwakuwa kama mgogoro utaenda mahakamani inaweza kutokea kuzuiwa kufanya hivyo mpaka kesi itakapokwisha. Kesi yenyewe itaisha lini haijulikani . Kama ikiisha baada ya miaka kumi, kumi na tano ina maana muda wote huo utakuwa una mali ambayo ni kama si ya kwako.

3. UTARATIBU WA KUBADILI JINA( TRANSFER) BILA USUMBUFU.

( a )
Kwanza hakikisha una mkataba wako wa kununulia ambao una muhuri wa wakili uliondaliwa kitaalam huku ukiwa na picha za wote mnunuzi na muuzaji ikiwa ni pamoja na sahihi zenu wote. Kwa ufupi hakikisha mkataba wako ni mzuri ambao una viwango vya kisheria ili kuepuka kurudishwa rudishwa kwa ajili ya marekebisho au kukataliwa kabisa uwapo mamlaka za ardhi.

( b ) Pili hakikisha una fomu namba 29 ambayo ni taarifa ya kutoa umiliki .Fomu hii ni taarifa maalum ambayo aliyekuuzia anatoa taarifa kwa kamishna wa ardhi kuwa anataka kutoa umiliki wake kwa wewe mnunuzi. Atakuwa akizungumza kwa mtindo wa kiapo kuwa mimi fulani wa sehemu fulani ninatarajia kutoa umiliki wangu wa ardhi wa eneo fulani kwa fulani fulani.
Mwisho muuzaji ataweka sahihi yake na atakuwa ameichambua plot anayotoa umiliki na anuani zake za makazi zitakuwa zimeoneshwa vyema. Fomu hii hupatikana mamlaka za ardhi na kwenye ofisi za wanasheria.

( c ) Tatu ni kujaza fomu Namba 30 ambayo ni kudhibitisha nia ya kutoa umiliki. Ile ya juu namba 29 inatoa umiliki wakati hii inathibitisha nia ya kutoa au kuachia umiliki kwenda kwa mnunuzi. Hivyo hii namba 30 ni msisitizo wa namba 29. Hii ni kutokana unyeti wa masuala ya ardhi. Aidha taarifa nyingine katika fomu hii ni zilezile zilizo katika fomu namba 29. Fomu hii nayo hujazwa na muuzaji tu na hupatikana mamlaka za ardhi au ofisi za wanasheria.

( d )Nne baada ya fomu hizo hapo juu sasa inakuja fomu namba 35 ambayo ni fomu rasmi ya kuhamisha umiliki ( transfer of right of occupancy). Katika fomu hii ndimo muuzaji anapotamka rasmi kuachia umiliki na kuutoa kwa mnunuzi ikiwa ni pamoja na kuainisha bei ya mauzo.

Fomu hii itachambua nyumba/kiwanja ambacho kimetolewa umiliki na hii itakuwa na majina yote mawili yaani muuzaji na mnunuzi. Pia itakuwa na sahihi zao wote ikiwa ni pamoja na picha. Pia itakuwa na muhuri wa wakili akiwa kama shahidi wa wote wawili muuzaji na mnunuzi. Fomu hii nayo hupatikana mamlaka za ardhi na ofisi za wanasheria.

4. LAZIMA UWE NA RISITI ZA KODI.

Hiki ni kiambatanisho kingine kinachohitajika. Utatakiwa kupeleka taarifa ya uthamini wa ardhi mamlaka ya mapato ambapo kupitia taarifa hiyo watakupa hesabu za kodi utalipa na utapewa risiti na risiti hiyo ndiyo utakayoambatanisha kwenye maombi yako.

5. USHAURI WA KITAALAM.

Hakikisha siku ya kununua nyumba/kiwanja inakuwa ndio siku ya kuanza hatua za kufanya transfer. Kuchelewa kunapunguza hadhi yako ya umiliki na kunakuweka karibu zaidi na mgogoro. Ni vigumu kumaliza mgogoro kwa usalama pindi utakapotokea ukiwa haujafanya transfer. Zingatia sana haya.

MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO.

Source: Sheria Yakub Blog
 
Msaada sheria ya manunuzi je mhasibu anaruhusiwa kushika tenda na kujilipa?

Ndiyo, ilimradi mchakato uwe wazi na shindanishi. But pia azingatie dhana ya mgongano wa kimaslahi( conflict of interest)
 
Back
Top Bottom