Unapodaiwa au kumdai mtu uchukue hatua gani!!?

Salahan

JF-Expert Member
Sep 10, 2014
2,942
3,603
POLISI HAWARUHUSIWI KUCHUKUA KESI ZA KUDAIANA HELA.

Na Bashir Yakub.
+255784482959.

Yapo mambo tunatakiwa kuyazungumza mara kwa mara ili watu wayaelewe. Moja ya mambo hayo ni hili la watu kudaiana hela hadi kufikishana polisi. Mtu binafsi, Saccos au taasisi imekukopesha fedha, na hatimaye umeshindwa kulipa, wanachokifanya ni kukupeleka polisi.

Huko polisi ati unaandikishwa maelezo na wakati mwingine unatakiwa kusaini mkataba mpya wa lini na namna gani utalipa deni.

Au wakati mwingine unawekwa ndani kabisa, au huwekwi ndani ila siku ambayo umeambiwa kulipa ikifika hujalipa ati askari anakupigia simu kukuuliza kwa nini hujalipa deni , na vitisho vya kukukamata na kukuweka ndani, au wakati mwingine unakamatwa kabisa na kuwekwa ndani.

Kwa ufupi haya yote ni makosa makubwa. Ni makosa kwa askari yeyote ambaye ameamua kuchukua kesi ya aina hii, na ni makosa hata kwa yule anayedai ambaye amekwenda kuripoti .

1.KUDAIANA HELA.

Masuala ya kudaiana hela ni masuala ya madai(civil). Polisi hawahusiki kabisa na masuala ya madai. Polisi wanahusika na masuala ya jinai(criminal). Kudai hela si masuala ya jinai hata kidogo. Masuala ya jinai wanayohusika nayo polisi ni yale yote yaliyoorodheshwa katika Sheria ya Kanuni za adhabu, Sura ya 16 ambayo ni kama kubaka,kuiba, kutukana, kulawiti,kupigana, kuharibu mali , kujeruhi, rushwa, dawa za kulevya, uhaini, mauaji, kughushi, na mengine yaliyo katika sheria nyingine mtambuka yanayofanana na hayo.

2. HATA KUWEKWA CHINI YA ULINZI TU KWA MADAI YA HELA HAIRUHUSIWI.

Kutoruhusiwa kwa polisi kujihusisha na masuala haya ya madai ya kudaiana hela kumeelezwa kwa mapana. Si tu polisi hawaruhusiwi kukuweka ndani kwa makosa kama haya bali pia hawaruhusiwi hata kukuweka chini ya ulinzi. Kukuweka chini ya ulinzi ni kuzuia uhuru wako wa kutembea kwa namna yoyote ile, hata kwa kukwambia hapo ulipo usitoke.

Katika kesi ya Rudolf v Athumani (1982) TLR 100 mahakama ilisema kuwa ni kazi ya polisi pale wanapoletewa mashtaka kuchambua ikiwa mashtaka yaliyoletwa kwao ni madai au ni jinai ili ikiwa ni jinai wayachukue na ikiwa ni madai waachane nayo na wamshauri mleta mashtaka/malalamiko(informer) hatua sahihi za kuchukua.

Jaji Sammatta aliongeza kuwa polisi hawaruhusiwi kumweka mtu chini ya ulinzi kwa makosa ya madai.

3. NINI UFANYE UKIFIKISHWA POLISI KWA MAKOSA KAMA HAYA.

Ikiwa utafikishwa au kuitwa polisi kwa masuala ya kudaiana hela, waambie tu polisi kuwa haya ni mashauri ya madai na nyie hamhusiki na masuala ya madai kisheria. Lazima hili uwaambie wajue kuwa unalijua . Na usikubali kuingia makubaliano yoyote ya kulipa/au kusaini labda uamue kwa hiari yako.

Kama utaona hawaelewi waambie wakupeleke mahakamani kwa kosa hilo. Kwa uhakika hakuna wa kukupeleka mahakamani kwa kosa hilo. Labda wakutafutie kosa jingine la kubambikiwa(maliciously) lakini si hili la madai ya hela. Hakuna namna utafikishwa mahakamani na polisi kwa kosa hili, hakuna namna.

Pili, ikiwa umewekwa chini ya ulinzi kwa makosa kama haya basi unaruhusiwa kumfungulia shauri la madai ya fidia yule askari aliyekuweka chini ya ulinzi pamoja na huyo mleta taarifa polisi/aliyeshitaki. Katika kesi ya Simon Chatanda v Abdul Kisomi (1973),LRT,No 11mahakama ilisema kuwa kumweka mtu chini ya ulinzi kwa makosa ya madai ni makosa(wrongful confinement) na kuwa aliyewekwa chini ya ulinzi anaweza kudai fidia kutoka kwa yeyote aliyehusika akiwemo mtoa taarifa/aliyeshitaki.

Na tatu kwa wale mnaodai mnayo haki ya kufungua shauri la madai mahakamani na sio kwenda polisi. Ndio maana hujawahi kuona taasisi kubwa za fedha kama CRDB,NBC,NMB na nyingine zikifungua kesi polisi kwa mtu wanayemdai aliyeshindwa kurejesha mkopo. Hufungua madai mahakamani na sio polisi. Shida hii iko kwa watu binafsi wanaokopesha, na taasisi ndogo ndogo za mikopo.

Hawa wanatakiwa kuacha hii tabia kwakuwa yule unayemdai anaweza kukugeuzia kibao ukadaiwa fidia kubwa wewe na huyo askari wako unayemtumia.
 
Kweli dawa ya deni kulipa tu, vinginevyo mdai anaweza kutumia mbinu mbadala!
 
Asante kwa somo zuri, ustaarabu dawa ya deni ni kulipa ili kesho uaminike tena, cause shida haziishi. Tusifurahie tu kutokupelekwa police.
Hajamaanisha eti kwa kuwa hamna kupelekwa police eti ndo tuzurumu au kama unadaiwa usulipe bali ametuelimisha wote wanaokopa na wanaokopeshwqa na watu binafsi ila pia ameleekeza mahala sahihi pa kukwenda ikiwa unamdai mtu na hataki kukulipa kuwa ni mahakamani na sio police kama ambavo jamii ya watanzania wanavojua kila kitu na kupeleka police. Asante mleta huu uzi murua kabisa..
 
Sorry mkuu, mimi nikikopa Bayport na nikitakiwa kulipa deni ndani ya miaka 3, Sasa niliacha kazi serikalini.
Nikawapigia kuwauliza ni kwa namna gani nitawalipa pesa zao na wao walijibu kuwa mkopo una bima.
Baada ya mwaka wameanza kunipigia simu na kunitishia kuwa nisipowalipa watanipeleka mahakamani.
Niliwaomba nilipe kwa mkupuo zote lakini wanipunguzie kwakuwa Sina kazi walikataa.
Swali je nikiendelea kukaa kimya bila kulipa watachukua hatua gani?
Pia wamenipiga fine sijui kwa kosa lipi.
Pamoja na hilo mdhamini wa mkopo ilikuwa ajira yangu kama mtumishi na mkurugenzi na afisa utumishi ndio walio zamini Sasa mm nahusikaje?
 
Back
Top Bottom