Uchaguzi 2020 Unamfahamu mgombea atakayekuja kuwa kiongozi bora?

Amalrik TZ

JF-Expert Member
Aug 9, 2020
341
301
Demokrasia ni mfumo wa siasa ambao wananchi wana mamlaka ya kuwachagua viongozi wao wenyewe kupitia sanduku la kura.Mataifa mengi hasa ya magharibi yanaamini demokrasia ndiyo mfumo bora zaidi wa kisiasa.

Baadhi ya nguzo kuu za demokrasia ni pamoja na utawala wa sheria na uchaguzi wa uhuru na haki.Moja kati ya faida inayopata nchi ya kidemokrasia ikiwa misingi yake yote ya demokrasia ikifuatwa ni mabadilishano ya madaraka kwa njia ya amani bila ya umwagikaji wa damu.

Uchaguzi ni moja kati ya nguzo inayofanya demokrasia iwe hai katika nchi ya kidemokrsia.Nchini Tanzania uchaguzi hufanyika baada ya miaka mitano.Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi na utafanyika tarehe 28 Oktoba kuchagua viongozi wa ngazi ya Udiwani,Ubunge pamoja na Rais.

Viongozi watakaochaguliwa tarehe 28 Oktoba wataunda serikali na wataongoza nchi yetu kwa miaka mitano ijayo 2020-2025.Kitu kimoja ambacho tuna uhakika nacho tarehe 28 Oktoba ikifika ni kupata viongozi wapya lakini hatuna uhakika na ubora wa viongozi watakao chaguliwa.

Mfumo wa demokrasia unampa nafasi mwananchi kuchagua viongozi,lakini mfumo huu haumpi uhakika mwananchi kuwa viongozi atakayewachagua watakuwa viongozi bora.Kupitia Demokrasia mshindi hupatikana kwa idadi kubwa ya kura.

Oktoba 28 kura yako utakayopiga ndiyo itakayoamua mshindi kati ya wagombea waliopo katika nafasi ya Udiwani, Ubunge na Urais.Mgombea hupata kura nyingi kutokana na ushawishi alionao dhidi ya wagombea wenzake.

Umaarufu wa baadhi ya wagombea unatokana na shughuli ambazo walizifanya nje ya ulingo wa siasa.Wengi hutumia hiyo kete kupata ushawishi kirahisi kwa wananchi.Baadhi yao hao wagombea hawana uwezo wa kisiasa hasa kujenga hoja ila wanaushawishi mkubwa kuliko wapinzani wao.

Kwenye uchaguzi huu tumeshuhudia watu maarufu kutoka kwenye sekta mbalimbali wakiomba ridhaa za kuwa wagombea wa ubunge na udiwani kwenye vyama vyao vya siasa.Baadhi ya watu maarufu ni pamoja na msanii Hamisi Mwinjuma(MwanaFA) aliyepitishwa na chama chake cha CCM kugombea ubunge jimbo la Muheza.

Kwangu mimi kiongozi bora ni yule mwenye nia,dhamira na mipango ya kweli ya kutatua matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi. Naomba niweke mambo sawa kuwa maarufu kwangu siyo tatizo ikiwa una nia,sera,mipango halisi na uchungu mkubwa moyoni mwako kuwaletea watanzania maendeleo.

Tatizo lipo pale ambapo watanzania wanamchagua kiongozi kwa umaarufu wake bila ya kuangalia sera na hoja alizonazo.Tunafahamu kwamba demokrasia inampa ushindi aliyepata idadi nyingi ya kura.Hii husababisha mara nyingi mgombea maarufu kupata ushindi japo hawezi kuwa kiongozi bora.

Nilipata nafasi ya kuhudhuria kampezi za takrabani vyama vyote kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Uzoefu nilioupata kwenye kampeni za mwaka 2015 ni wagombea kutumia muda mchache sana kujinadi na kueleza sera zao.

Kampeni zile zilitawaliwa na wapambe ambao walikuwa wanamsifia mgombea, vijembe, matusi pamoja na burudani za muziki.Mara nyingi nilirudi nyumbani bila ya kuelewa mgombea yule atafanya jambo gani na ni kwa namna gani atazitatua changamoto zinazotukabili.

Naamini sikuwa peke yangu ambao hatukupata nafasi ya kuwaelewa vyema wagombea wa nafasi mbalimbali. Hii tabia ipo kwa vyama vyote na wengi walisema tunataka mgombea X wa chama flani atoke madarakani bila ya kueleza wananchi watavyoshughulikia matatizo yanayowakabili.

Mambo kama haya yakiendelea kwenye kampeni za mwaka huu ninaamini watu wengi watachagua viongozi wasio na sifa za kuwa viongozi bora.

Rai yangu kwa wagombea wananchi tunahitaji suluhu za matatizo na changamoto tunazozikabili na siyo tuu umshinde mshindani wako.
Suluhu ya changamoto tulizonazo zitakuja tuu pale ambapo watapatikana viongozi bora.

Bahati mbaya bado baadhi ya Watanzania wanauelewa mdogo katika masuala ya siasa. Watanzania wengi bado hawaelewi namna gani siasa zinaathiri maisha yao ya kila siku.Bado kuna wanaoamini kwamba tunaweza kutenganisha maisha ya kila siku na siasa.

Watu wenye mtazamo wa aina hii ndio ambao imekuwa rahisi sana kwao kuchagua viongozi kutokana na umaarufu wao bila ya kuangalia sera. Mbaya zaidi ni kwamba watu wengi wana mtazamo wa aina hii na watashiriki kupiga kura Oktoba 28.

Matokeo yake wataenda kupiga kura bila ya kujua kiongozi aliye bora kwao ni wa aina gani kulingana na changamoto wanazopitia, wataishia kupiga kura kutokana na umaarufu wa mgombea.Hatma ya hili ni kupatikana kwa viongozi wengi wabovu.

Tunaelekea kuanza kampeni tarehe 26 Agosti katika kipindi hiki wagombea wataanza kunadi sera zao.

Moja ya njia ya kujua kiongozi aliye bora ni katika kipindi cha kampeni ambapo tutazijua sera na mipango waliyonayo kwa miaka mitano ijayo.

Jukumu lipo kwetu wapiga kura je, tunazifahamu vyema changamoto na matatizo tunayopitia katika kata, jimbo na nchi tunayoishi?
Ombi langu ni tutumie muda wa kampeni kusikiliza sera za wagombea wote na kuwachagua wale wanaoifaa Tanzania kwa miaka mitano ijayo.

Binafsi mimi nitamchagua kiongozi wa chama chochote kile mwenye sera na mipango halisi zenye kuleta suluhu ya ajira kwa vijana.Hii ndiyo changamoto kubwa kwangu kwa sasa na huyo ndiye kiongozi bora kwangu mimi.

Je, wewe Mtanzania mwenzangu kiongozi bora kwako ni mwenye sera gani katika uchaguzi huu?
 
Back
Top Bottom