Unaishi katika ndoto zako, ndoto za wazazi wako au maisha yalipo kupeleka?

marcoveratti

JF-Expert Member
Sep 21, 2017
964
1,689
Inawezekana kabisa asilimia zaidi ya 90 ya Watanzania tunaishi kutokana na wazazi wetu walivyotaka tuwe, yaani mzazi amehusika sana kukufanya uishi hivyo unavyoishi.

Yamkini wazazi walitaka uwe Daktari lakini wewe unapenda kuwa msanii au mwanasoka, sasa wakazima ndoto zako na walipopachika ndoto zao bado zikafeli na ukajikuta unaishia kupoteza vyote, yaani unapoteza ndoto zako na unapoteza ndoto za wazazi wako na unajikuta unaishi kulingana na maisha yanavyotaka.

Inakuwa ngumu kueleweka eti? Basi fuatana nami katika makala hii.

Mama yake mzazi alizaliwa katika taifa la Burundi, akakua akasomea hapo mpaka akawa mhandisi wa kampuni ya mafuta ya petroli ndani ya taifa la Burundi.

Baadaye akatimkia zake katika taifa la Ivory Coast huko ndiko akaenda kukutana na kijana anayeitwa Herwig, wakaanzisha uhusiano uliokolea mpaka wakafunga ndoa na baada ya kufunga ndoa wakahamia barani Ulaya na wakalichagua taifa la Ubelgiji kama makao yao mapya.

Miezi sita baada ya kuhamia Ubelgiji wakapata mtoto waliyemuita Kevin, inamaanisha kwamba hata mimba ya huyu mtoto ilitunga wakiwa hapa hapa Afrika.

Ukoo wao ni wasomi, mambo ya mpira hawana uhusiano nao kivile labda kuutazama tu wachezaji wakiwa wanacheza.

Ndoto za wazazi zilikuwa ni kumsomesha mtoto wao avuke kiwango cha elimu walichokuwa nacho wazazi wake lakini mtoto ndoto zake zinatofautiana na wazazi.

Wazazi wakasema isiwe nongwa, ilihali una kipaji acha tukupeleke kwenye academy ili ukajifunze zaidi,

Sisi Waafrika haswa watanzania tunataka watoto watimize ndoto tulizowapangia, yaani unamlazimisha mtoto akomae na kusoma kisa tu unataka mwanao aje kuwa mwanasheria au daktari, mtoto akikwambia anataka kuwa mwanasoka unamwambia nionyeshe kwenye ukoo wetu nani mchezaji wa mpira

Ukifuatilia hizo ndoto za wazazi kwa mtoto wao unagundua kumbe hata kwenye ukoo wao hakuna cha mwanasheria wala daktari lakini wanalazimisha tu bila kusikiliza mtoto wao ana ndoto zipi au ana kipaji gani

- Anyway, tuendelee na makala yetu, akiwa na umri wa miaka 7 tu akawa ameshajiunga na academy ya KVV Drongen, kumbuka hii ni academy ya mtaani kwao alipozaliwa Kevin,

Miaka miwili baadaye academy kubwa ikamuona kuwa ana kipaji, hivyo mipango ikafanyika na hatimaye akajiunga na academy ya Gent

Alipohudumu hapo kwa miaka sita, mahasimu wao wakubwa wakamsainisha katika academy yao, nawazungumzia KRC Genk, wakati huo ulikuwa mwaka 2005 wakati Kevin alikuwa na miaka 14, alikaa kwenye academy hiyo kwa miaka mitatu na hatimaye akapandishwa kwenye timu ya wakubwa wakati huo alikuwa na miaka 17 tu,

Akakinukisha sana, akicheza kama kiungo wa katikati na wakati mwingine akicheza kama kiungo mshambuliaji,

Miaka minne akiwa na klabu ya KRC Genk ikatosha kuwashawishi wana blues kumsajili,

Mwaka 2012 klabu ya Chelsea ikatangaza kumsajili, akacheza kwa msimu mmoja, tena muda mwingi akikaa benchi, msimu ulipomalizika wakaona kwamba hatoshi, wakamtoa kwa mkopo kwenda Ujerumani kwa msimu mmoja katika klabu ya Werder Bremen

Hapo ndipo akaenda kukinukisha, akapiga soka dunia ya 7, msimu ulipomalizika klabu ya VfL Wolfsburg wakambakisha Ujerumani baada ya kufikia makubaliano na klabu ya Chelsea kumuuza,

Ebwana eeh, kama kuna kosa lilifanyika hapa ni klabu ya Chelsea kumuuza Kevin, wao walimuona hawafai, tena Mourinho akasema Kevin De Bruyne ni mchezaji nyanya nyanya sana, haiwezi mikiki mikiki ya ligi kuu ya Uingereza,

Hayawi hayawi, si yakawa, Kevin De Bruyne alipojiunga na klabu ya VfL Wolfsburg pale alipokuwa ameishia katika msimu wake uliopita ndipo alipoanzia, msimu mmoja tu akatangazwa kuwa mchezaji bora wa ligi kuu ya Ujerumani

Ukumbuke kuwa msimu wa kwanza akiwa kwa mkopo katika klabu ya Werder Bremen alitwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi, na msimu uliofuata akachukua tuzo ya mchezaji bora wa ligi kuu,

Msimu ulipoisha tu, Shekhe Mansour akasema hii dhahabu inarudishwa Uingereza lakini safari hii inabadilishiwa makao, safari hii itaenda kung'ara pale Etihad

Mwaka 2015 akajiunga na klabu ya Manchester City na tangu hapo amekuwa mchezaji muhimu sana katika kikosi cha Manchester City, ni aibu kubwa sana kama utaambiwa utaje top 3 ya viungo bora kwa sasa balani Ulaya, halafu kwenye hiyo list jina la Kevin De Bruyne likakosekana, nakwambia tena ni aibu kubwa sana

Hilo jina linaanzaje kukosekana kwa mfano .??? Yaani umetumia sababu zipi mpaka jina la Kevin De Bruyne ukaliweka pending.???

Ujue nini.??? Kuna aina ya wachezaji hata wakiwa timu pinzani lazima ujikute wanakuvutia, muda wote wanang'arisha mboni za macho yako, yaani huwezi kujutia kuwatazama maana wanakupa vyote, yaani matokeo na burudani bila kusahau fundisho

Namna Kevin De Bruyne anavyocheza anatufanya tuuone kama mpira ni kitu rahisi sana, anauagiza mpira na unafuatisha maelekezo yake, mpira unamtii, unashawishika kusema mpira ni kazi rahisi kuliko hata kuwa mhasibu wa benki

Lakini namna anavyojituma, anavyojitolea na kutokukata tamaa huwa anatufundisha mengi sana kwenye harakati za maisha yetu ya kawaida huku kitaa,

Kevin De Bruyne muda wote awapo uwanjani anacheza akimaanisha, yupo Sirius, mpambanaji asiyechoka, yaani hata kama timu yake itapoteza lazima ataonyesha kuwa amefanya jambo au alitaka kufanya jambo lakini muda au bahati havikuwa upande wake

Namna anavyokokota mpira, anavyopiga chenga, kasi yake, akili kubwa ya kuwatawanya wapinzani, namna anavyopiga zile pasi zake za kuzungungusha, mtaalamu wa kupiga pasi mpenyezo, mashuti yake makali, na uwepesi wa kufanya maamuzi, aisee anafurahisha na anaburudisha sana kumtazama

Msimu wa kwanza wa Pep Gurdiola aliulizwa ataje list ya wachezaji wataounda kikosi cha kwanza tangu aanze kuwa kocha, kwenye hicho kikosi Pep Gurdiola aliwataja wachezaji wengi lakini eneo la katikati akamtaja Sergio Bosquete, Andreas Iniesta pamoja na Kevin De Bruyne yaani wachezaji kama Bastian Shwanstaiger, Xavi Hernandez, Thomas Muller hawakumshawishi Pep Gurdiola, uzingatie hapo alikuwa amemaliza msimu mmoja akiwa na Kevin De Bruyne

Sitaki kusema kwamba Kevin De Bruyne ni bora kuliko Xavi Hernandez maana hawa ni wachezaji wanaotofautiana aina ya soka lao lakini ukweli usemwe, Kevin De Bruyne amekamilika yaani katika umri wake sina nachoweza kumdai tena

Kwa level yake na uwezo wake amelifanyia soka kila kitu lakini soka linaweza lisimfanyie kila kitu, si mnaona hata waandishi wa habari wameshafanya ukanjanja kwenye tuzo ya mchezaji bora wa msimu katika ligi kuu ya Uingereza, hapa tunangoja chama cha soka kama kitaemdeleza hii dhuluma iliyoanzishwa na waandishi wa habari za michezo,

Kwa sasa anapokea mshahara wa £320833 na baada ya makato pamoja na kodi anaingiziwa cash money £300,000 kwenye account yake kila wiki,

Hebu tujikumbushe darasani kidogo, katika hesabu za fedha

£1 ni sawa na Tshs 2693 za kitanzania, hii inamaanisha kwamba Kevin De Bruyne anapokea mshahara usiopungua Tshs 807,900,000/= za kitanzania kwa kila wiki,

Pesa ambayo itabidi waungane takribani waalimu 80-90 waliofanya kazi kwa miaka 30+ wakapokea mafao wayaunganishe kwa pamoja ndipo wamkaribie au waufikie mshahara anaoupokea Kevin De Bruyne kwa wiki moja tu,

Wapwa zangu umejifunza nini leo.????
----------------------------------

Wapwa hivi ulishwahi kumsaidia mtu kisha ukasikia anakwambia "Hakika nimeamini sura sio roho" wewe huwa unamuelewaje..?? Hebu fikiria kiundani hiyo sentensi kisha niambie kama nimekosea kumkata mtu pua zake
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom