Unahitaji Falsafa Ya Maisha, Jinsi Ya Kuwa Mstoa, Misingi Mitatu Ya Maisha Bora, Falsafa Ya Ustoa Na Utajiri Na Acha Dunia Ifanye Yake.

Konzo Ikweta

JF-Expert Member
Oct 3, 2013
735
1,464
Rafiki yangu ninayekupenda sana,

Nachukua nafasi hii kukukaribisha kwenye makala yetu ya TANO ZA JUMA ambapo nakukusanyia mambo matano muhimu ya kujifunza kwa kina na kuchukua hatua kupitia kitabu ninachokuwa nimesoma na kuchambua kwenye juma husika.

Kwenye juma hili la 33 la mwaka 2019 tunakwenda kujifunza kupitia kitabu kinachoitwa How to Be a Stoic: Using Ancient Philosophy to Live a Modern Life kilichoandikwa na mmoja wa wastoa wa zama zetu Massimo Pigliucci

Ustoa ni Falsafa ambayo imekuwepo kwa zaidi ya miaka elfu mbili sasa, ambayo lengo lake kubwa limekuwa kuwafanya watu kuwa na maisha bora, kwa kuishi kwa misingi sahihi. Hii ni falsafa ambayo kila mtu akiweza kuielewa na kuiishi basi lazima atakuwa na maisha bora.

Kwa kuwa mstoa, hakuna kitu chochote kinachokuwa na nguvu ya kukutikisa wewe, kwa sababu unajifunza msingi wa kutofautisha vitu vilivyo ndani ya uwezo wako na kuvichukulia hatua na vitu vilivyo nje ya uwezo wako na kuachana navyo.

Japo falsafa hii imeanzishwa miaka mingi iliyopita, na kuna kipindi ilipotea kabisa, lakini changamoto tunazopitia kwenye zama tunazoishi sasa, zinaweza kutatuliwa na misingi ya falsafa hii.

Karibu kwenye makala hii ya TANO ZA JUMA, ujifunze kwa kina kuhusu ustoa na uondoke ukiwa na hatua za kuchukua ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi.

#1 NENO LA JUMA; UNAHITAJI FALSAFA YA MAISHA

Zamani za kale, wakati binadamu wanajifunza kuwa na makazi ya kudumu, watu walijenga nyumba zao bila ya misingi. Lakini walijifunza somo moja kubwa sana, kwamba kipindi cha dhoruba mbalimbali kama mvua, kimbunga na tetemeko, nyumba hizo zilibomoka haraka sana. Hivyo wakajifunza kwamba ili nyumba iwe imara na idumu, basi inapaswa kuanza kujengwa kwa msingi imara. Na mpaka sasa wahandisi wote wanajua kwamba nyumba imara inaanza na msingi imara. Na kadiri nyumba inavyopaswa kuwa kubwa, ndivyo msingi unavyopaswa kuwa imara zaidi. Mfano, msingi wa nyumba ya kawaida hauwezi kufanana na msingi wa nyumba ya ghorofa.

Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu. Kwenye maisha tunakutana na dhoruba mbalimbali. Kuna kuugua, kuvunjika kwa mahusiano, kufukuzwa kazi, kufilisika kibiashara, kufa kwa watu wetu wa karibu na hata sisi wenyewe kufa. Dhoruba hizi huwa zina madhara tofauti kwa watu tofauti. Kuna watu wanapokutana na dhoruba za maisha zinawayumbisha sana na kuvuruga kabisa maisha yao. Lakini wapo wengine ambao wanakutana na dhoruba kali za maisha lakini maisha yao hayayumbi.

Kinachowatofautisha watu hao wa aina mbili ni msingi ambao wamejijengea. Kwenye nyumba tumeona msingi wa kuanza, kwenye maisha yetu, msingi muhimu sana ni falsafa ambayo mtu anakuwa nayo juu ya maisha. Falsafa unayokuwa nayo, ndiyo inapima kiasi gani dhoruba unazokutana nazo kwenye maisha. Kama huna falsafa unayoiishi na kuisimamia, dhoruba ndogo kama biashara kufilisika inatosha kukuvuruga kabisa. Lakini kama una falsafa unayoiishi, dhoruba kubwa kama kuhukumiwa kifo, inakufanya uwe imara na kuyafurahia maisha yako mpaka dakika ya mwisho.

Hii ni kukuambia wewe rafiki yangu kwamba unapaswa kuwa na falsafa ya maisha yako, falsafa ambayo unaitumia kama msingi wako wa kufanya maamuzi na kuendesha maisha yako. Falsafa ambayo itakuwezesha kukabiliana na dhoruba za maisha, ambazo kadiri siku zinavyokwenda zinazidi kuwa kali zaidi.

Dini zilipaswa kuwa msingi wetu kwenye changamoto hizi za maisha, lakini dini nyingi zimesahau jukumu hilo, na badala yake zimekuwa sehemu ya kuwapa watu hofu zaidi ya maisha kuliko matumaini. Dini zimekuwa zinaweka nguvu kubwa kwenye kuwaandaa watu kwa maisha yajayo (baada ya kifo) kuliko maisha waliyonayo sasa. Japokuwa unahitaji maandalizi ya maisha yajayo (kulingana na imani yako), lakini kitu muhimu sana unachohitaji ni maandalizi ya maisha unayoishi sasa, maana hayo ndiyo yanayokujenga au kukubomoa.

Kwa kuwa dini zimeshindwa kufanya kazi ambayo tulitegemea zifanye, kutujenga na kutuandaa kwa maisha ya sasa na kuweza kukabiliana na dhoruba tunazokutana nazo kwenye maisha yetu ya kila siku, basi linabaki kuwa jukumu la kila mmoja wetu kuwa na falsafa ya maisha, ambayo ataitumia kuendesha maisha yake.

Kukaa chini na kutengeneza falsafa yako mwenyewe ni kazi kubwa, inakuhitaji ujaribu na kukosea vitu vingi, kitu ambacho huna muda wala nguvu za kufanya, maana changamoto zinazokukabili ni nyingi.

Hivyo suluhisho ni wewe kujifunza falsafa zilizopo, na kisha kuchagua ile ambayo itakufaa wewe katika kuendesha maisha yako.

Zipo falsafa nyingi ambazo zinatokana na wanafalsafa mbalimbali kama Socrates, Plato, Aristotle, Epicurus, Zeno na wengineo.

Mimi rafiki yako, baada ya kujifunza falsafa nyingi nimechagua kuiishi falsafa ya Ustoa kwenye maisha yangu. Hii ni falsafa ambayo ilianzishwa na Zeno miaka 300 kabla ya Kristo na imeweza kukuzwa na wanafalsafa wengine. Ni falsafa ya matendo (practical) na siyo nadharia (theory) na ni falsafa inayokupa uhuru wa kuyaishi maisha yako na siyo kukupa hofu.

Karibu kwenye kitabu cha juma hapo chini, ujifunze kwa kina kuhusu falsafa hii ya USTOA na uweze kuifanya kuwa falsafa ya kuendesha maisha yako pia.

#2 KITABU CHA JUMA; JINSI YA KUWA MSTOA

Falsafa ya Ustoa ilianza miaka 300 kabla ya Kristo ambapo Zeno, mwanzilishi wa falsafa ambaye kwa wakati huo alikuwa mfanya biashara alikuwa safarini na chombo chake kikaharibika akiwa Athens Ugiriki. Akiwa hapo Athens, alitembelea maktaba na kuperuzi maandiko yaliyokuwepo, alikutana na mafunzo ya Socrates na yakamvutia sana. Akamuuliza mhusika wa maktaba ile, ni wapi anaweza kuwapata watu ambapo atajifunza zaidi kuhusu falsafa, na hapo akaoneshwa mwanafalsafa Crates na akamfuata, hapo ndipo safari yake ya kujifunza na kuwa mwanafalsafa ilipoanzia.

Zeno alijifunza kupitia Crates ambaye alikuwa kwenye shule ya falsafa inayoitwa Cynics, ambao ni watu ambao hawakujali kuhusu chochote, waliishi maisha kwa wakati waliokuwa nao na walihoji na kutilia mashaka kila kitu.

Baada ya kujifunza kwenye falsafa hii kwa muda, Zeno aliona falsafa ya Cynics ilikuwa na mapungufu, kwa sababu huwezi kupuuza kila kitu kuhusu maisha na ukawa na maisha bora. Hivyo alianzisha shule yake ya falsafa, ambapo alikuwa akifundisha chini ya mti ulioitwa stoa. Na hapo ndipo jina la Ustoa (Stoicism) lilipoanzia.

Tangu kipindi cha Zeno, pamekuwepo wanafalsafa ambao wameiendeleza na kuikuza zaidi falsafa hii ya zeno. Wanafalsafa kama Cato, Musonius Rufus, Seneca, Epictetus na Marcus Aurelius kwa nyakati tofauti waliishi na kufundisha falsafa hii.

Kwenye kitabu chetu cha juma, tunakwenda kujifunza kwa kina kuhusu falsafa ya ustoa na jinsi tunavyoweza kuiishi kwenye zama zetu kupitia kitabu kinachoitwa How to Be a Stoic: Using Ancient Philosophy to Live a Modern Life kilichoandikwa na mmoja wa wastoa wa zama zetu Massimo Pigliucci

Karibu tujifunze jinsi tunavyoweza kuwa wastoa na tukawa na maisha bora, yenye utulivu na mafanikio makubwa.

MATAWI MATATU YA FALSAFA YA USTOA

Falsafa ya ustoa inafananishwa na mti ambao una vitu vitatu ili uweze kuwa mti. Mti una mizizi ambayo inaupa uimara na virutubisho, shina ambalo linahifadhi chakula na kutoa umbo na matawi ambayo yanatengeneza chakula na kuvuta hewa.

Falsafa ya ustoa ina matawi matatu;

Moja ni fizikia (physics), hili ni tawi linalojihusisha na sayansi ya asili, jinsi dunia ilivyo na inavyojiendesha. Hii ndiyo mizizi ya falsafa hii.

Mbili ni maadili (ethics), hili ni tawi ambalo linaipa falsafa hii msimamo, jinsi ya kuishi na kujihusisha na wengine. Hili ndiyo shina la falsafa hii.

Tatu ni mantiki (logic), hili ni tawi ambalo linahusika na kufikiri pamoja na kufanya maamuzi sahihi. Haya ndiyo matawi ya falsafa hii.

Ili maisha yetu yakamilike, lazima tuwe vizuri kwenye maeneo hayo matatu, kuijua dunia na hapa tunapaswa kuwa na ujasiri na kiasi, kuwa na maadili tunayoyaishi ambapo tunapaswa kuwa watu wa haki na mwisho kutumia akili zetu kufikiri, ambapo tutaweza kuwa na hekima.

Ukiona hapo, matawi matatu ya ustoa ambayo ni FIZIKIA, MAADILI NA MANTIKI, ndiyo yanazalisha misingi mikuu minne ya ustoa ambayo ni HEKIMA, UJASIRI, HAKI NA KIASI. Kwa kifupi, falsafa nzima ya Ustoa imejumuishwa kwenye sentensi hiyo. Yote tunayokwenda kujifunza yanatokana na matawi hayo matatu na misingi hiyo minne.

UPACHA WA UDHIBITI

Kuna mambo mengi sana ambayo tunasumbuka nayo kwenye maisha yetu, ambayo hayapaswi kutusumbua kabisa. Katika kutusaidia kwenye hili, falsafa ya ustoa inatupa upacha wa udhibiti ambao tukiweza kuutumia hakuna kitu chochote kitakachotusumbua.

Upacha wa udhibiti unagawa mambo yanayotokea kwenye makundi mawili;

Kundi la kwanza ni vitu ambavyo vipo ndani ya uwezo wetu na tunaweza kuviathiri, hivi ni vile vitu ambavyo kuna hatua tunaweza kuchukua na kuvibadili.

Kundi la pili ni vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wetu na hatuwezi kuviathiri, hivi ni vile vitu ambavyo hakuna namna tunaweza kuvibadili.

Hivyo basi, unapokutana na kitu au hali yoyote kwenye maisha yako, jiulize je ipo ndani ya uwezo wako? Kama jibu ni ndiyo basi chukua hatua. Kama jibu ni hapana basi unaachana nacho na kuendelea na maisha yako. kwa namna hii hakuna kitakachokusumbua kamwe.

Kwa mfano unataka kuwahi kwenye mkutano muhimu sana, lakini njiani umekutana na foleni kali, na hivyo utachelewa. Ni rahisi kukasirika na kutamani foleni ile ingeenda haraka, lakini hilo halitasaidia chochote. Hivyo unapaswa kujiuliza je kuna hatua unaweza kuchukua, kama ndiyo basi ichukue (labda kushuka kwenye gari na kupanda pikipiki), kama jibu ni hapana basi tulia, tumia muda huo wa foleni kutafakari mambo mengine muhimu ya maisha yako na siyo kuupoteza kwa kutamani foleni ingeenda haraka zaidi.

Jua yaliyo ndani ya uwezo wako na chukua hatua, na yale yasiyokuwa ndani ya uwezo wako achana nayo.

KINACHOTUTOFAUTISHA SISI NA WANYAMA

Sisi binadamu tunafanana na wanyama kwenye vitu vingi, jinsi miili yetu ilivyo (anatomy) na jinsi inavyofanya kazi (physiology) hatutofautiani kabisa na wanyama wengine.

Lakini kuna kitu kimoja ambacho sisi binadamu tunacho ila wanyama wengine hawana, kitu hicho ni uwezo wa kufikiri. Wanyama wote wana ubongo kama tulionao sisi, ila wa kwetu umeendelea zaidi na tuna uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi. Wanyama wengine wanachukua hatua kwa hisia lakini sisi tuna uwezo wa kufikiri kabla ya kuchukua hatua.

Hivyo tunapaswa kutumia uwezo wetu vizuri, kuhakikisha tunafikiri kabla ya kuchukua hatua. Matatizo mengi tunayokutana nayo kwenye maisha ni kwa sababu tunakimbilia kuchukua hatua kabla ya kufikiri kwa kina. Ukijipa muda wa kufikiri kabla ya kufikia maamuzi, utaona hatua sahihi za kuchukua.

Hivyo ondoka hapa na funzo hili muhimu; kabla hujafanya maamuzi yoyote, kabla hujachukua hatua yoyote, fikiri kwanza. Usiendeshwe na hisia kwenye jambo lolote, hisia zinawapoteza wengi.

TABIA NJEMA NDIYO MSINGI MKUU

Msingi mkuu unaopaswa kuuishi na kuutumia kufanya maamuzi kwenye falsafa ya ustoa ni tabia njema (virtues). Kwenye ustoa kuna tabia njema nne; ambazo ni HEKIMA, UJASIRI, HAKI NA KIASI. Kwenye makala ya juma hapo chini utajifunza zaidi kuhusu tabia hizi nne na jinsi ya kuziishi kwenye maisha yako na yakaweza kuwa bora.

HAKUNA ANAYEKOSEA KWA MAKUSUDI

Upo msingi wa ustoa ambao utakuwezesha kuishi maisha yako kwa utulivu bila ya kujali wengine wanasema au kufanya nini. Moja ya vitu ambavyo vinatusumbua sana zama hizi ni mambo ambayo wengine wanasema au wanafanya. Huwa tunayaruhusu yatuumize, tukiamini kwamba watu hao wanafanya mambo hayo kwa makusudi ili kutuumiza.

Lakini wastoa wanatuambia kwamba, watu wanaofanya mambo ambayo yanatuumiza, hawafanyi hivyo kwa makusudi, bali wanafanya hivyo kwa sababu hawajui kulicho sahihi kufanya. Hivyo hupaswi kuumia kwa sababu yao, badala yake unapaswa kuwaonea huruma na kuona kama kuna namna unaweza kumsaidia ili asiendelee kukosea.

Mfano mzuri ni pale mtoto mdogo anapokupiga kofi, je utarejesha kwa kumpiga kofi pia? Je utakasirika? Je utamnunia? Je utasema amekudharau? Majibu hapo ni hapana. Lakini vipi mtu mzima mwenzako akikupiga kofi? Hapo mambo yanabadilika, unaona amekudharau, utataka kulipiza, utakasirika na hata kumnunia. Lakini kama utachukulia mtu huyo amekupiga kofi kwa kutokujua au kwa bahati mbaya, hutapata hisia hizo.

Hivyo cha kujifunza hapa, tusikimbilie kuhukumu pale watu wanapofanya vitu kwamba ni vibaya au wamedhamiria kutuumiza. Badala yake tuchukulie kwamba watu hao hawajui wanachofanya au wamefanya kwa bahati mbaya, na hilo litatuzuia sisi kuumia.

Mfano mzuri ni kwenye wizi au utapeli, mtu akikuibia, badala ya kuumia, unapaswa kumwonea huruma, kwa sababu kwanza hajui njia sahihi ya kutengeneza kipato ambayo itampa maisha ya utulivu na pili, kwa tabia yake hiyo, ataishia jela au kaburini, maana ataiba akamatwe na wananchi wenye hasira kali hadi kufa, au apelekwe polisi na baadaye kufungwa. Unaona jinsi ambavyo unaondoka kwenye upande wa lawama na kuwa upande wa utulivu!

CHAGUA SHUJAA WA MAISHA YAKO

Wastoa wamekuwa wanaelewa umuhimu wa kuwa na mashujaa, watu ambao tunayapima maisha yetu kupitia wao. Lakini hili ni eneo ambalo limekuwa na changamoto kubwa sana zama hizi, kwa sababu kumekuwa na mashujaa wengi feki. Siku hizi watu wanaoweza kutengeneza umaarufu rahisi kupitia mitandao ya kijamii, sanaa, michezo au siasa ndiyo wanaonekana mashujaa kwa wengi. Na wengi wanawafuata watu hao, lakini hakuna wanachojifunza kwa sababu mwisho wa siku umaarufu wa watu hao huanguka, kwa sababu haujajengwa kwenye misingi sahihi.

Ni muhimu uchague mashujaa sahihi wa maisha yako, kutokana na misingi wanayoiishi au waliyoiishi ambayo unaweza kujijengea kwenye maisha yako na ukaweza kupiga hatua pia. Kadiri unavyojifunza falsafa hii na kujifunza wengine walioiishi falsafa hii, utavutiwa na maisha ya baadhi ya wanafalsafa na kuwachagua kuwa mashujaa wako.

JINSI YA KUKABILIANA NA MABADILIKO MAKUBWA YA MAISHA KIAFYA

Kuna wakati tunakutana na mabadiliko makubwa kimaisha kwenye afya zetu. mabadiliko haya yanaweza kutuyumbisha sana kama hatuna msingi sahihi tunaouishi. Mfano ni pale mtu anapopata ulemavu wa mwili ambao unaathiri maisha na hata kazi za mtu. Wengi huvurugwa sana na mabadiliko ya aina hii, kitu ambacho hupelekea maisha yao kudorora na hata kufa mapema.

Wastoa wanatupa njia sahihi ya kukabiliana na mabadiliko ya aina hii, kwa kutuambia tunapaswa kufikiria na kutumia kile tulichonacho na siyo kuangalia tumekosa nini. Kama umepata ulemavu wa miguu, kumbuka bado una mikono, macho, masikio, na viungo vingine, ambavyo kama utaweza kuvitumia vizuri maisha yako yatakuwa bora.

Mmoja wa wanafalsafa wa Ustoa, Epictetus, ambaye alikuwa mwalimu bora sana wa falsafa hii, alikuwa mtumwa. Katika maisha yake ya utumwa, aliumizwa na kupata ulemavu wa miguu. Hili lilimpa ulemavu wa maisha, lakini hakuruhusu ulemavu huo uathiri maisha yake, aliangalia mambo gani mengine anayoweza kufanya, kama kujifunza na kufundisha falsafa na siyo kuangalia alichokosa.

Somo muhimu la kuondoka nalo hapa ni usiweke nguvu zako kwenye yale uliyokosa au kupoteza, badala yake weka nguvu zako kwenye yale uliyonayo na jinsi unavyoweza kuyatumia kwa ubora zaidi.

KUHUSU KIFO NA KUJIUA

Moja ya vitu ambavyo vimekuwa vinawasumbua watu wengi n kifo. Wote tunajua kuna siku tutakufa, lakini hatutaki kufikiria wala kupata picha ya kifo chetu. Kadhalika tunajua wale watu wa karibu kwetu, ambao tunawapenda sana kuna siku watakufa. Lakini huwa hatufikirii wala kupata picha ya vifo vyao. Kinachotokea ni tunakutana na vifo ghafla na vinatuumiza sana.

Wastoa wana maeneo matatu ya kuzingatia kuhusu kifo.

Kwanza ni kifo chako mwenyewe, ambapo wastoa wanasema hakuna sababu ya kukiogopa kifo, kwa sababu ni sehemu ya maisha yako na kinaweza kutokea muda wowote. Hivyo wakati wowote unapaswa kuwa tayari kukikabili kifo. Inapofanya jambo lolote, lifanye kama ndiyo mara ya mwisho kwako kulifanya, kama vile kifo kinakusubiri. Kwa njia hii hutaahirisha jambo lolote muhimu na utafanya mambo kwa usahihi. Wastoa wanasema kama unaogopa kifo, maana yake bado hujaanza kuishi. Lakini kama utachagua kuishi maisha yako, kifo hakitakusumbua, kwa sababu wakati wowote utakuwa tayari.

Mbili ni vifo vya watu wa karibu kwetu. Wazazi wetu, watoto wengu, wenzi wetu na ndugu wengine ni watu tunaowapenda na kuwajali sana. Inapotokea wamefariki dunia, huwa tunaumia, tunalia na kuhuzunika sana. Kwa wengine vifo vya watu wao wa karibu huwa vinawavuruga sana, vinaishia kuwapa magonjwa ya akili. Wastoa wanatuambia vifo vya watu wa karibu kwetu vinatuumiza kwa sababu vinatukuta hatujajiandaa. Wanatuambia kila unapoongea au kukutana na mtu wako wa karibu, jiambie kimoyomoyo kwamba hiyo ni mara ya mwisho kukutana naye. Epictetus anatuambia kila unapombusu mtoto wako, jiambie unambusu mtu ambaye anaweza kufa muda wowote. Kwa kuchukulia hivi, utajali sana, kwa sababu unajua mtu anaweza kupotea muda wowote, na hilo linapotokea utaumia, lakini halitakuvuruga, kwa sababu ni kitu ambacho ulijua kitatokea, a pia ulishatumia fursa ulizokuwa nazo kabla mtu huyo hajafariki.

Tatu ni kujiua. Wastoa wa zamani, wengi waliishia kujiua wenyewe au kupewa adhabu ya kifo. Hii ilitokana na tawala za kidhalimu zilizokuwepo enzi hizo na wastoa hawakuogopa kuzisema na kuzipinga. Hilo liliwafanya wawekwe vizuizini, kufukuzwa au kuhukumiwa kufa. Wastoa walikuwa wakipokea adhabu hizo bila ya kuruhusu ziharibu utulivu wao wa ndani. Mfano mstoa alipohukumiwa kifo, alikipokea kama sehemu ya maisha na kusimamia misingi yake. Lakini pia wapo wastoa ambao walipofika mwisho wa maisha yao, yaani uzee na kuona wameshakamilisha jukumu lao la maisha, basi walijiua. Hii ni dhana ambayo ilikuja kupotea, lakini zama hizi imeanza kurudi. Wapo watu ambao wanachagua kuyakatisha maisha yao kwa sababu mbalimbali. Hapa hatuzungumzii wale wanaojiua kukimbia majukumu au matatizo waliyosababisha, bali wale ambao wanaona imetosha sasa na wanataka kupumzika. Hilo pia ni zoezi la kistoa.

JINSI YA KUKABILIANA NA HASIRA

Zama tunazoishi sasa ni zama ambazo hasira za watu zimekuwa karibu sana. Siku hizi ni rahisi sana kukasirishwa na maneno au matendo ya wengine hata kama umelala kitandani kwako na watu hao wapo mbali kabisa. Kupitia mitandao ya kijamii imekuwa rahisi kufuatilia maisha ya wengine na yale wanayofanya.

Wastoa wanatuambia hasira tunazokuwa nazo ni kitu ambacho tumekizalisha wenyewe. Kinachokukasirisha siyo kile ambacho mtu amefanya au kusema, bali jinsi ambavyo umetafsiri kitu hicho.

Kwa mfano mtu akikutukana, utakasirika na kuumia, hiyo ni kwa sababu umetafsiri neno alilokuambia kama tusi linalokueleza wewe vibaya. Lakini kama mtu huyo angekutukana kwa lugha ambayo huielewi kabisa, je ungekasirika? Vipi kama mtu huyo alikutukana lakini hukusikia, je ungekasirika? Unaona jinsi ambavyo wewe mwenyewe unazalisha hasira kwa kutafsiri kwako mambo.

Kukabiliana na hasira, acha kuyapa mambo uzito ambao hayastahili, puuza mambo madogo madogo na jua hakuna kinachoweza kukuumiza wewe bali fikra zako mwenyewe. Jua hakuna mwenye nguvu ya kukuumiza au kukuteteresha wewe ila wewe mwenyewe. Hivyo usiruhusu mtu yeyote kuibua hasira ndani yako.

Hivi ndivyo unavyoweza kuitumia falsafa ya ustoa kuwa na maisha bora, yenye utulivu na mafanikio makubwa. Chagua kuwa mstoa leo, ishi misingi hii na mingine utakayoendelea kujifunza kwenye falsafa hii na maisha yako yatakuwa bora.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma, tutajifunza mazoezi 12 ya kiroho ya kistoa ambayo yatatuwezesha kuwa na maisha bora sana. Mazoezi hayo 12 ni hatua ndogo ndogo za kuchukua kila siku ambazo zitakufanya uwe imara na usiangushwe na changamoto yoyote. Mwisho wa makala hii kuna maelekezo ya jinsi ya kupata #MAKINIKIA, yasome na uchukue hatua.

#3 MAKALA YA JUMA; MISINGI MITATU YA MAISHA BORA

Ustoa ni falsafa ya matendo, ambayo inatufundisha njia sahihi ya kuendesha maisha yetu, kukabiliana na changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha yetu ya kila siku na kuwa na maisha bora na yenye furaha wakati wote, bila ya kujali tupo kwenye hali gani au tunapitia nini.

Ili kufikia aina hiyo ya maisha bora, ipo misingi mitatu muhimu ya falsafa ya ustoa ambayo tunapaswa kuijua na kuiishi kila siku. Kwenye makala ya juma hili nimekushirikisha misingi hiyo mitatu na jinsi ya kuiweka kwenye maisha yako.

Kwenye makala hiyo ya juma unajifunza misingi mitatu pamoja na tabia nne njema za kistoa za kujijengea, ambazo ukiwa nazo, hakuna kinachoweza kukuteteresha kamwe. Isome sasa makala hiyo, bonyeza hayo maandishi hapo juu.


#4 TUONGEE PESA; FALSAFA YA USTOA NA UTAJIRI

Kwenye Falsafa ya Ustoa, vitu vimegawanyika katika makundi matatu;

Kundi la kwanza ni vitu vizuri kufanya au kuwa navyo (virtues), ambavyo ni vinne; hekima, ujasiri, haki na kiasi.

Kundi la pili ni vitu vibaya kufanya au kuwa navyo (vices), ambavyo ni kinyume na hivyo vizuri, yaani, upumbavu, woga, udhalimu na tamaa.

Kundi la tatu ni vitu ambavyo siyo vizuri na wala siyo vibaya (indifferent), ambavyo hakuna ubaya kuwa navyo, lakini pia hupaswi kujitesa ili kuwa navyo. Hapa vitu vingine vyote kwenye maisha vinaingia hapo, kuanzia afya, kazi, biashara, fedha na kadhalika.

Sasa kwa misingi ya ustoa, wengi hufikiri inawataka wawe masikini, watu wasiojali fedha wala utajiri. Lakini katika historia, moja ya wanafalsafa waliokuwa na maisha mazuri basi ni wastoa. Seneca alikuwa tajiri mkubwa enzi zake na mwanasiasa, Marcus Aurelius alikuwa mtawala wa Roma. Kwa kifupi wastoa walijihusisha na maisha ya kila siku na ya kawaida, wakifanya yale ambayo kila mtu anafanya.

Na hii ni sababu nyingine nzuri kwa nini tunapaswa kuwa wastoa, kwa sababu ni falsafa ambayo haipingi mtu kuwa na fedha, au kujihusisha na mambo mengine, kama tu hayavunji msingi wa wema.

Zipo baadhi ya dini na falsafa ambazo zinawafundisha wafuasi wake kuachana kabisa na mambo ya dunia, kutoa maisha yao kwa ajili ya falsafa au Mungu pekee. Lakini wote tunajua maisha yana mahitaji yake, hutaenda kulipa ada za watoto kwa falsafa, na wala hutaenda dukani kupata chakula kwa kusema wewe ni mwanafalsafa.

Hivyo kwa kuishi kwa falsafa ya ustoa, unakuwa huru kufanya upendacho, ila tu kiwe sahihi kwako na kwa wengine, na pia unakuwa huru kujikusanyia fedha utakavyo, ila tu ufanye hivyo kwa usahihi na kwa manufaa ya wengine pia.

Na kikubwa nilichojifunza ni kwamba ukiishi misingi ya falsafa ya ustoa, una nafasi kubwa ya kuwa tajiri, lakini pia utakuwa huru na utajiri huo. Kwa sababu kwanza utakuwa unafanya kilicho sahihi na kuachana na yasiyo sahihi, pia utaepuka kufanya mambo ambayo yatakupotezea fedha, kwa kudhibiti vizuri hisia zako. Lakini kilicho muhimu zaidi ni kwamba hutafungwa na utajiri wako, hata kama utapoteza kila kitu, bado utabaki imara na maisha yako yataendelea.

Naweza kuhitimisha kwa kusema, Ustoa ni falsafa ya watu wakuu na matajiri, najua unapenda kuwa mkuu, unapenda kuwa tajiri na kuwa huru na maisha yako, hivyo basi, ijue na kuiishi misingi ya ustoa.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; ACHA DUNIA IFANYE YAKE

“One of the first lessons from Stoicism, then, is to focus our attention and efforts where we have the most power and then let the universe run as it will. This will save us both a lot of energy and a lot of worry.” ― Massimo Pigliucci

Tumekuwa tunajisumbua na mambo mengi kuhusu dunia, mambo ambayo hatuna nguvu ya kuyaathiri kwa namna yoyote ile. Hili limekuwa linatupotezea muda na nguvu zetu.

Mfano, una safari unataka kufanya, halafu kuna wingu limetanda, kiashiria kwamba mvua inaweza kunyesha. Halafu unakasirika kwa nini mvua inataka kunyesha wakati wewe una safari muhimu ambayo itaathiriwa sana na mvua hiyo. Je unafikiri hilo litakuwa na msaada wowote kwako?

Mvua itanyesha au haitanyesha kwa mipango yake yenyewe, na siyo kwa sababu wewe una furaha au hasira. Hivyo badala ya kupoteza muda na nguvu zako kuhusu mvua kunyesha au kutokunyesha, peleka nguvu hizo kwenye njia bora ya kuwa na safari yako hata kama mvua itanyesha. Hilo kidogo litakusaidia.

Hili ndiyo funzo kubwa sana ambalo falsafa ya Ustoa inatufundisha, ambalo tukiweza kulielewa na kulifanyia kazi, kamwe hatuwezi kuvurugwa na mambo yanayotokea au kuendelea duniani, kwa sababu yapo nje ya uwezo wetu wa kuyaathiri.

Muda wako na nguvu zako vina ukomo, tumia vizuri rasilimali hizo mbili katika kuwa na maisha bora.

Rafiki yangu mpendwa, hizo ndizo TANO ZA JUMA hili la 33 la mwaka 2019. Umejifunza kwa kina umuhimu wa kuwa na falsafa na pia falsafa ya ustoa na matumizi yake kwa zama tunazoishi sasa. Kilichobaki ni wewe kuchukua hatua, kuishi misingi ya ustoa ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi. Nenda kaishi misingi hii ya ustoa kwenye maisha yako, na kama bado hujawa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, basi fanya hivyo, maana ndani ya KISIMA ndiyo sehemu sahihi utakayoweza kuendelea kujifunza na kuiishi falsafa hii. Tuma ujumbe kwa wasap namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na utapewa maelekezo ya kujiunga.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili la 33 tunakwenda kujifunza mazoezi 12 ya kiroho kutoka kwenye falsafa ya Ustoa ambayo yatakuwezesha kuwa na maisha bora sana. Kwa kujua na kuweka kwenye matendo mazoezi haya 12, naweza kukuambia hakuna chochote kitakachokuteteresha. Mfano mzuri ni pale mtu anapokutukana, ni rahisi kukasirika na kujibu kwa matusi, lakini kwenye mazoezi hayo ya ustoa, utajifunza njia ya kujibu tusi ambalo mtu amekutukana, kwa njia ambayo aliyekutukana atajidharau sana yeye mwenyewe, na kukuheshimu mno, na hapo hujakasirika wala kujibu kwa tusi.

#MAKINIKIA yanapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA ambayo ipo kwenye mtandao wa telegram. Kama bado hujajiunga na channel hiyo, chukua hatua sasa ili usikose #MAKINIKIA hayo pamoja na chambuzi nyingine za vitabu. Utaratibu wa kujiunga na channel uko hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
 
Nice.

Ila kwenye kifo umepiga juu juu.

Kwa jinsi ulivyozungumzia kifo baasi izo zingine zooote hatuwez kuzikumbatia kwa kuwa tunakufa muda wowote


Nataka kutoka mvua inanyesha...unaniambia nitafute njia sahihi ya kukamilisha safari hata kama mvua inanyesha..

Sasa kwa nini nipoteze muda wa kutafuta njia sahihi wakati nakufaa muda wowote pengine hata iyo safari haijaanza.

Kaeni chini mzungumzie kifo kama hatua lakini haitakiw kuwa kikwazo kwa vitu vingine.
Hata yeye mtunzi wa kitaabu angewaza kifo asitamani kutengeneza hadhira wa kusoma kitaabu chake.
 
Nice.

Ila kwenye kifo umepiga juu juu.

Kwa jinsi ulivyozungumzia kifo baasi izo zingine zooote hatuwez kuzikumbatia kwa kuwa tunakufa muda wowote


Nataka kutoka mvua inanyesha...unaniambia nitafute njia sahihi ya kukamilisha safari hata kama mvua inanyesha..

Sasa kwa nini nipoteze muda wa kutafuta njia sahihi wakati nakufaa muda wowote pengine hata iyo safari haijaanza.

Kaeni chini mzungumzie kifo kama hatua lakini haitakiw kuwa kikwazo kwa vitu vingine...
Hata yeye mtunzi wa kitaabu angewaza kifo asitamani kutengeneza hadhira wa kusoma kitaabu chake.
Sawa mkuu
 
Shukrani kwa huu uzi, sababu uzi umejaa mengi yakujifunza katika harakati za kukomaza Akili na Hisia kuhusu mambo mbalimbali yanayomkabili mwanadamu.
 
Aliyeandika kitabu How to get rich alikuwa anazunguka mtaani kuomba pesa ya kuchapisha kitabu chake.
Njia za kujaribu kupata mafanikio hazina kanuni moja ya moja kwa moja ya kuyafikia mafanikio ila inahitaji uwe na Wazo, Mtaji (pesa na vifaa), Watu sahihi (connection), Maarifa, Ujuzi, Juhudi, Ubunifu, Kujitoa (self-motivation) na Strong Mentality ya Kutokukata tamaa.

Hivyo basi huyo mwandishi wa Kitabu "How to Get Rich" inawezekana yeye njia yake aliyoamua kuitumia kutoka kimaisha ni kupitia kuuza Vitabu vyake vinavyoelezea mambo yenye Mantiki na yanayosambaza Hamasa kwa watu ili wawe na Akili ya kutokukata tamaa katika utafutaji, na kuamini kila kitu kinawezekana.

Kadri nakala zake za vitabu vitakavyozidi kuuzwa, hapo ndugu mwandishi naye anakuwa akaunti yake ya Benki inazidi kuimarika kifedha.

Hivyo anakuwa amekuelekeza "How to Get Rich" huku naye aki-Get Rich pia vile vile kupitia Mauzo ya Nakala za Vitabu vyake.

Lakini shughuli zozote zile za mwanadamu ni "gamble" na zinahitaji ku-risk.
Kila shughuli inahitaji ku-gamble, iwe ni shughuli ya shule, ufundi, uhandisi (engineering), michezo, burudani, ulinzi, siasa, uvuvi, uchimbaji madini, ufugaji, kilimo, biashara etc.

You never know for sure, all you need to do is, try to get all the pieces of the puzzle together, get the skills and knowledge then calculate the risk and take a gamble. Just do it!!

Sometimes mambo yataenda, sometimes mambo hayataenda.
Ni mwendo wa ku-gamble tu. Maana hata hawa "richmen" nao huwa wanafeli pia katika "investment" zao zingine.
 
Back
Top Bottom