UN kutumia dola mil.777 kwa miradi Tanzania

BabuK

JF-Expert Member
Jul 30, 2008
1,845
329
UMOJA wa Mataifa (UN) umetenga zaidi ya dola za Marekani milioni 777 kwa ajili ya kusaidia miradi 12 ya maendeleo nchini katika kipindi cha miaka minne.

Hayo yalisemwa jana na Mratibu Mkazi wa UN nchini, Dk. Alberic Kacou wakati wa mkutano na Jukwaa la Wahariri nchini uliofanyika jana Dar es Salaam.

Dk. Kacou alisema fedha hizo zimeshaanza kutumika ambapo katika kipindi cha miezi sita, wameshatumia asilimia nane ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 63,779,538 kwa ajili ya kuanza kusaidia miradi hiyo.

Alisema utekelezaji wa miradi hiyo umeanza Juni mwaka jana na utamalizika Julai 2015, na baadhi ya miradi itakayonufaika ni pamoja na elimu, utawala, kukua kwa uchumi, afya na lishe, majanga, wakimbizi, Ukimwi na Virusi Vya Ukimwi, ulinzi, mawasiliano, jinsia na haki za binadamu pamoja na maji.

Alisema lengo ni kuisaidia Tanzania katika kutoa elimu bora, kuwa na utawala bora, kutunza mazingira pamoja na matumizi ya ardhi, kutafuta njia ya kupunguza tatizo la wakimbizi, kuepukana na janga la umasikini na njaa pamoja na kuboresha huduma za afya.


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), Vibeke Jensen alisema licha ya Tanzania kupiga hatua katika sekta ya elimu, bado inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.

Jensen alisema changamoto nyingine ni kutokuwa na walimu wenye sifa, wanafunzi kukosa vifaa vya shule, jambo linalosababisha washindwe kufanya vizuri katika masomo na kutoendelea na masomo ya elimu ya juu.

“UN imetenga dola za Marekani milioni 103.6 kwa mradi elimu ambao umeanza Julai mwaka jana hadi Juni 2015 ili kuisaidia Serikali ya Tanzania kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula wakiwa mashuleni,” alisema Jensen.

Chanzo: HabariLeo

 
Back
Top Bottom