SoC01 Umuhimu wa kuwa na mfumo wa ufuatiliaji na tathmini matokeo katika kujenga Uwajibikaji na Utawala Bora (Result-based monitoring and evaluation system)

Stories of Change - 2021 Competition

hafidhia

Member
Jan 30, 2016
15
13
Mataifa mengi duniani yamekumbwa na msukumo wa nje na hata wa ndani wa kuleta mabadiriko katika uongozi wa uma. Na madai ya kuataka mabadiriko yanatoka katika vyanzo mbalimbali ikihusisha Wananchi , Asasi za kiraia , vyombo vya habari na vyama vya upinzani.M ara nyingi madai yao yamejikita katika uwajibikaji,uwazi wa kupata taarifa au kuchagiza maendeleo ya haraka yanayotokana na miradi ya kimaendeleo ili kuleta matokeo yanayoonekana. Utawala bora sio ufahari au starehe bali ni nguzo muhimu inayohitajika kuleta maendeleo ( Benki ya dunia, 1997, uk.15)

Hili si jambo dogo hata kidogo,viongozi wengi wa serikali wamekuwa wagumu kufanya mabadiriko juu ya uendeshaji wa serikari kutokana na umaaufu wao kisiasa na nafasi waliyonayo katika jamii. Uwazi wa kupata taarifa umekuwa mgumu kwa wananchi,sera zilizotungwa zimekosa utekelezaji wa yalioainishwa na miradi ya kimaendeleo imekuwa haitekelezeki na hakuna kiongozi yeyote anawajibika , matokeo yake ni kujenga mifumo ya uongozi mbaya mpaka kupelekea kuzorota kwa hali ya uchumi na kijamii.Kwa kipindi kirefu mataifa mengi yaliyoendelea yamejitahidi kutafuta mbinu za kujikwamua kuleta maendeleo katika nchi zao lakini yamebakia palepale.

Si kwamba hakuna anaejua mifumo inayotumika dunia nzima kufuatilia na kutathmini matokeo yanayopatikana kutokana na miradi ya kimaendeleo ambayo imepitishwa na bunge na kusaidiwa na sera ndani ya wizara husika. Tatizo kubwa ni utayari wa kuweza kupokea hii mifumo iweze kutumika katika nchi zilizoendelea. Utayari wa kuweza kupokea hii mifumo ya uwazi katika kujenga uwajibikaji na utawala bora,umekumbwa na pingamizi kubwa za kisiasa na kushindikana kuwepo kwa watu ambao wangejitolea kupiga kelele ili mifumo hii iweze kutumika katika nchi zetu.

Mfumo wa ufatiliaji na kutathmini matokeo, ni mfumo ulioundwa kuwezesha watunga sera na watoa maamuzi kufanya ufatiliaji juu ya miradi ya kimaendeleo au sera. Nchi nyingi duniani zimekuwa zikitumia mfumo huu kusimamia matokeo ya sera na miradi ya kimaendeleo, na dhumuni lake ni kuongeza uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali ili kujenga utawala mzuri wa kusimamia miradi ili kupata uungwaji mkono kutoka makundi mbali mbali na wananchi wanao waongoza.

Tangia mfumo huu uanzishwe umeleta tija sana katika nchi tofauti ambao wamesifika kuleta matokeo katika nchi zao.Benki ya dunia imeitaja nchi ya uganda kuwa imeweza kufanikiwa kupata unafuu wa kulipa mkopo kutokana na matumizi ya mfumo wa ufatiliaji na tathmini juu ya miradi ya kimaendeo lakini pia wanasema nchi nyingi masikini wameshindwa kufuzu kupata nafuu hiyo kutokana na kutotumia mfumo huo, ambapo chapisho hilo linataja sababu kuu ni kutokuwepo kwa wataalamu wa kutosha wa kuendesha mfumo huo. (Chapisho la hatua kumi za kuunda mfumo wa ufatiliaji na kutathmini matokeo ulioandikwa na Jody Zall Kusek na wengineo)

Bila kupoteza muda, tuangalie umuhimu wa huu mfumo katika kuchochea uwajibikaji na utawala bora kwa ngazi mbalimbali za serikali katika kuleta mabadiriko makubwa kwa wananchi. Serikali imekuwa ikitumia mifumo tofauti katika kufanikisha matumizi ya rasilimali zake kwa ngazi tofauti za uongozi, Lakini mfumo wa kufanya tathmini na ufatiliaji juu ya rasilimali zake hautumiki kikamirifu kwa sehemu kubwa ndani ya serikali.

Kwanza mfumo huu utatoa tathmini au mrejesho wa mabadiriko (outcome) yaliyotokea katika miradi ya kimaendeleo ambayo imeanzishwa au sera ambayo imetungwa. Serikali imekuwa ikifanya tathmini juu ya matokeo ya muda mfupi tu (output) na viongozi wengi wamekuwa wakitoa matokeo hayo bila kuangalia ni kwa namna gani miradi hiyo ya kimaendeleo imechochea mabadiriko na vipi wananchi imeawasaidia , mfano unaweza kuta kiongozi akitoa mrejesho wa mradi kuwa “ fedha tuliyoileta tumefanikiwa kujenga vituo 120 vya afya kwa miaka mitano.

Yapo maswali ya kujiuliza, je ujenzi wa vituo hivyo vimeweza kutoa huduma iliyohitajika kwa watu? watu wangapi wamekuwa wakitibiwa katika vituo hivyo? vipi kuhusu watoa huduma , kama daktari na manesi wanatosha au bado mtoa huduma mmoja lakini wagonjwa 300 kwa siku. Mfumo huu wa ufatiliaji na tathmini ni muhimu ili kujibu maswali yote ambayo yanaweza kutokea katika miradi ya maendeleo ili kuboresha miradi hiyo kwa wananchi.

Kupima na kuchunguza matumizi ya rasilimali kwa muda wote wa uendeshwaji wa miradi ya kimaendeleo,mfumo huu unatoa fursa kwa viongozi na wanachi kushiriki na kuweza kupima matumizi ya rasilimali juu ya miradi ya kimaendeleo ambayo inaendelea kwenye sehemu zao.

Kiongozi ataweza kufahamu rasilimali zilizotumika kuanzia mradi unaandaliwa mpaka unafanyiwa kazi na hapa ataweza kupima matokeo ya mradi na rasilimali zilizotumika kama vinaendana.Lakini cha kushangaza taarifa hizi anakuwa nazo mtu mmoja na hata linapokuja suala la ufatiliaji linakuwa gumu, ndio taarifa za uongo hutengenezwa na kusambazwa kwa wananchi na wanufaika wengine wa miradi ya maendeleo.Lakini kuwepo kwa mfumo huu utaleta tija mana utakuwa na wafatiliaji kwa kila hatua ambapo mradi umefikia na matumizi ya rasilimali, hii itamwezesha kiongozi au mwananchi kuwaajibisha viongozi wao pale matumizi ya uma yanapotumika vibaya.

Pia mfumo huu wa ufatiliaji na tathmini wa matokeo, utasaidia serikali kupanga na kubana matumizi ya fedha iliyopangwa. Bado kuna shida kubwa ya kuoanisha matumizi ya fedha ndani ya serikali na matokeo(outcome or impact) yaliyopatikana kutokana na fedha hizo .Taarifa ama mrejesho unaotokana na mfumo huu utawezesha serikari kujua kiasi gani cha fedha kitumike katika miradi husika na kubana matumizi ya sio kuwa ya lazima. Hivyo mfumo huu utawezesha kupata taarifa za mapema kama kuna umuhimu wa kuendelea na mradi ama kusitisha ili kutoruhusu matumizi mabaya ya fedha za wananchi.

Mfumo pia utawezesha serikali kugundua mapema mapungufu au changamoto zinazoikumba miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kuchukua hatua stahiki za kuinusuru. Mfumo huu ukitumiwa vizuri utaweza kuondoa uwoga wa viongozi ndani ya serikali na kufungua nafasi ya watu kujifunza kutokana na makosa waliyofanya na kufanya maboresho yatakayochagiza kuleta mabadiriko kwa wananchi.

Kuwezesha upatikanaji wa taarifa katika ngazi tofauti za uongozi ndani ya serikali kwenda kwa wananchi, ni muhimu sana katika kuleta maendeleo ya kiuchumi hasa ndani na nje ya nchi. Serikali imekuwa ikificha taarifa juu ya utendaji wake pamoja na matokeo ya miradi mbalimbali ambayo wanaiendesha, Upatikanaji wa taarifa ni kitu muhimu sana katika mipango ya kimaendeleo, na kama tupo makini na uhitaji wa kupunguza umasikini kwa watu wetu basi ni lazima tuanzishe tabia ya kuwashirikisha na kuwapa taarifa muhimu zenye uhakika na ubora.(Stiglits na Islam 2003,uk.10). Hii itajenga uaminifu kwa wananchi juu ya viongozi wao na kuhimiza utawala bora na uwajibikaji kwa muda wote.

Kuongezeka kwa uwazi na uwajibikaji serikalini, matumizi ya huu mfumo utachagiza kwa nafasi kubwa kuleta uwazi na uwajibikaji ndani ya serikali. Mfano ushirikishwaji wa watu wote kuanzia hatua za mwanzo kabisa mpaka jinsi mradi unavyoendelea utawezesha wanufaika kufahamu hali ya mradi na kuwapa msukumo mkubwa viongozi wa serikali kuweza kuwajibika .Japo kufanya hivi kuna gharama nyingi ambazo viongozi wengi hawazitaki, mfano wa gharama hizo ni kama kupoteza mvuto wa kisiasa na umaarufu, pindi watakapo wajibishwa na wananchi kwa kushindwa kuleta mabadiriko ya miradi ambayo wameianzisha. Lakini kwa uhakika kuna gharama kubwa Zaidi za kisiasa na umaarufu kama kiongozi hakuweza kuusimamia huu mfumo kutumika katika sehemu yake ya uongozi.

Mfumo pia utaonyesha mchango wa shughuri zingine tofauti na mradi husika katika kuleta mabadiriko yanayoonekana kwa wananchi. Mara nyingi tumekuwa tukipata taarifa kutoka kwa viongozi wetu kuwa mradi waliouanzisha ndio umeleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi. Lakini kwa kutumia mfumo huu utaweza kuonesha michango mingine ambayo yamechangia mabadiriko yanayoonekana, viongozi wengi wamekuwa wakijificha katika matokeo ili kupata sifa ya kisiasa juu ya miradi mbalimbali lakini mara nyingi miradi hiyo imekuwa sio chanzo sahihi cha mabadiriko kwa wananchi.

Mfano unaweza kuta mradi wa ujenzi wa shule za kata haujachangia kuongezeka kwa matokeo makubwa ya wanafunzi katika shule hizo. Kumbe sababu kuu inaweza kuwa ni kutokana na jitihada za wanafunzi husika na uwepo wa walimu wa ziada( tusheni) za mitaani wanafunzi wengi wa shule hizo wameweza kufanya vizuri katika mitihani yao.Mfumo huu utawezesha kuonyesha uhalisia na visababishi vingine vilivyochochea mabadiriko katika eneo husika mbali na mradi. Hii itakuza uwajibikaji wa viongozi kufanya ufuatiliaji wa miradi ya kimaendeleo.

Mfumo utawezesha kuunganisha ngazi mabalimbali za uongozi ndani ya serikali. Mfumo huu utawezesha usambazaji wa taarifa kutoka ngazi moja ya uongozi kwenda ngazi nyingine. Miradi ya kimaendeleo itaweza kuendeshwa bila uwepo wa moja kwa moja wa kiongozi wa juu.

Kwa sasa ni tofauti lazima kiongozi aje kwanza kufanya ziara ndio agundue changamoto au mapungufu yaliyopo katika miradi husika, hivi karibuni miradi mingi ya maji imekuwa ikizinduliwa na waziri baada ya kuwa imekwisha telekezwa. Lakini kupitia mfumo huu, kiongozi atagundua mapema changamoto na kila mtu atawajibika kulingana na malengo ya serikali yaliyowekwa. Ni vema kuwepo na mfumo huu ili kuunganisha ngazi za serikali hii italeta uwazi ndani ya serikali na kuacha mtindo wa kukusanya taarifa za miradi na kufanyiwa maamuzi sehemu moja bila kushirikisha ngazi nyingine .

Mfano taarifa juu ya maaendeleo ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya maji katika wilaya husika inapaswa kuwasilishwa katika ngazi mbalimbali za serikali na sio kubakia kwa meneja wa maji wa wilaya husika afanye maamuzi. Na hii mara nyingi imekuwa ikisababisha ufanyajikazi wa mazoea na viongozi kushindwa kuwajibika.

Matumizi sahihi ya mfumo huu kwa kiasi kikubwa utaongeza uwajibikaji ndani ya serikali kuanzia ngazi ya wizara mpaka mashirika ya uma. Hii itasaidia kubana matumizi ya fedha, kufunga au kusimamisha miradi ya kimaendeleo ambayo haina tija kwa wananchi, pia kutokana na kupatikana kwa taarifa za kimaendeleo tena kwa uwazi kutaruhusu ukosoaji ama uungwaji mkono juu ya utendaji wa serikali kutoka makundi mbalimbali yaliyomo ndani na hata nje ya nchi.
 
Back
Top Bottom