SoC01 Umuhimu wa kuwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa inayotekelezeka kwa wakati na kwa kuzingatia rasilimali zilizopo

Stories of Change - 2021 Competition

Abrianna

JF-Expert Member
Mar 30, 2021
4,697
15,374
Utangulizi
Dira kwa maana fupi ni muelekeo. Dira ya Maendeleo ya Tanzania (Tanzania Development Vision (TDV) 2025 ilianzishwa mwaka 1994 na kuzinduliwa rasmi mwaka 1999 ambapo utekelezaji wake ulianza mwaka 2000 lengo kuu likiwa kuongoza harakati za maendeleo ya uchumi na jamii zitakazoiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati na kuondokana na umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2025. 'www.tanzania.go.tz' (tovuti kuu ya serikali)

Melengo makuu matano yalioainishwa katika Dira ya Maendeleo 2025 ni pamoja na kuboresha hali ya maisha ya kila Mtanzania, kuwepo kwa mazingira ya amani usalama na umoja,kujenga utawala bora,kujenga jamii iliyoelimika na kujenga uchumi imara unaokabiliana na ushindani. (Nukuu kutoka Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025).

Katika andiko hili, nitaangazia malengo makuu matano kama yalivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo 2025. Andiko langu litaangazia pia utekelezaji wa malengo haya na uhalisia wa maisha ya Mtanzania.

Katika uhalisia, Maendeleo ya Nchi yetu kwa asilimia kubwa yamekua yakitegemea Ilani ya chama tawala pamoja vipaumbele vya Rais aliye madarakani. Mfano halisi ni ununuzi wa ndege na ujenzi wa madaraja ambao uliingiza nchi katika madeni makubwa na umaskini. Ni wazi kwamba Dira ya Maendeleo ni kijarida tu ambacho kimetengenezwa kutimiza wajibu lakini hakina nafasi kubwa katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Serikali imeunda mipango mingi kwa ajili ya utekelezaji wa maendeleo kama vile mpango wa maendeleo wa miaka mitanpo (Five Year Development Plan), MKUKUTA, Mpango wa Big Results Now (Matokeo Makubwa Sasa), Mpango wa maboresho ya utumishi wa Umma,pamoja na Maleongo ya Maendeleo ya Millenia chini ya nchi za Umoja wa Mataifa.

Katika mipango tajwa, yote ina malengo yanayolandana kwa maana ya kutokomeza umaskini kwa kuboresha huduma za afya, elimu, nishati, kilimo, maji, biashara, mahusiano ya kimataifa, ajira, kuboresha utumishi wa umma, kuweka usawa wa kijinsia pamoja na mengine mengi.

Hebu tuangazie miaka kumi nyuma tulinganishe na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na hali halisi ya Watanzania mpaka leo hii.

Hali ya maisha ya Mtanzania imezidi kuwa duni pamoja na kwamba nchi yetu ipo katika uchumi wa kati wa chini, Mtanzania wa kawaida anashindwa kumudu gharama ndogo za mlo wa siku ilhali tunatangaziwa uchumi wetu umekua kwa asilimia 7% ( NBS 2019/2020).

Katika kujenga utawala bora, hali imezidi kuwa tete, ni wazi kwamba utawala wa sheria umekua jambo gumu katika nchi yetu hali inayopelekea kutokuwajibika kwa pamoja na ubadhirifu wa mali za umma (Rejea ripoti ya CAG 2020).

Katika Dira ya Mendeleo 2025, serikali imeonyesha nia ya kujenga jamii iliyoelimika na inayojifunza kila siku kulingana na mazingira na nyakati tulizopo, tukirudi kwenye uhalisia, kiwango cha ubora wa elimu zetu hakikidhi viwango vitakavyowawezesha wasomi wetu kuingia katika ushindani ndani na nje ya Tanzania, shule zetu nyingi hazina waalimu wa kutosha wala vifaa vya kufundishia, matamko ya kisiasa kwa upande mwingine yamekua yakiathiri mifumo ya elimu.

Kwa mfano mnamo mwezi Desemba 2020, Rais JPM aliagiza somo la historia ya Tanzania lianze kufundishwa katika shue za msingi mpaka sekondari, Wizara ya elimu iliandaa machapisho kwa ajili ya somo husika lakini baada ya Rais Samia kuingia madarakani somo hilo lilisitishwa rasmi.

Kwa upande mwingine serikali ilichangia kupotosha jamii badala ya kuelimisha. Nitoe mfano mdogo wa janga la Covid 19. Serikali ilisimama kidete kuuaminisha umma kwamba janga hili ni vita ya mabeberu dhidi yetu badala ya kutumia wataalamu wa afya kutoa elimu kuhusu namna bora ya kujikinga ili kuepuka maambukizi. Serikali ilienda mbali zaidi na kuhamasisha tiba mbadala na njia za asili ambazo zilitumika katika vituo vya afya pia.

Kauli ya serikali pamoja na viongozi wakuu wa nchi imeleta mkanganyiko pamoja na hisia tofauti juu ya janga hili na kusababisha watu kuishi pasipo kuchukua tahadhari hata baada ya serikali kubadili msimamo na kuamua kufuata njia za kitaalamu. Ukijaribu kuongea na watanzania kumi, tisa kati yao wanaogopa chanjo na kuamini kwamba mabeberu wanataka kutumaliza.
1626861526209.png
1626861576665.png

(picha kutoka mtandaoni)

Katika uboreshaji wa utumishi wa umma, vilio vimekua vingi, utekelezaji wa dhima hii umesahaulika kwa miaka zaidi ya mitano iliyopita, vilio vingi vya wafanyakazi kuhusu nyongeza za mishahara pamoja na kupanda madaraja, makato makubwa, na mishahara duni ambayo haikidhi maisha ya kila siku.

Mambo ya muhimu yaliyotajwa katika utekelezaji wa malengo ya milenia ni pamoja na kukuza mahusiano ya kimataifa, kutokomeza umaskini wa kipato na njaa. Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania imepuuza kwa kiasi kikubwa sana mahusiano ya kimataifa kutokana na misimamo ya kiongozi aliyekua madarakani. Vipato vya wananchi vimeshuka kutokana na tozo kubwa katika bidhaa na huduma, mfumuko wa bei umeathiri pembejeo za kilimo na bidhaa mbalimbali, uonevu kwa wafanyabiashara,ubambikaji wa kesi na kodi uliosababisha biashara nyingi kufungwa. Tunao mfano halisi wa sasa katika tozo ya miamala ambayo imeleta taharuki kubwa kwa wananchi masikini ambao hata kula yao ni ya tabu.

Mapendekezo
• Serikali ianzishe taasisi maalumu kwaajili ya kuandaa na kusimamia Dira ya Maendeleo ya Taifa. Chombo hicho kiwe na kazi ya kuandaa, kusimamia pamoja na kuishauri serikali iliyopo madarakani bila kujali chama.Taasisi hii ihakikishe sera sera na mipango ya taasisi mbalimbali za serikali pamoja na wizara zina uelekeo mmoja na zinashirikiana ka ukaribu. Kwa mfano suala la kuzalisha wahitimu wenye weledi ni lazima liendane na uboreshaji mfumo wa elimu, kwa hiyo ni lazima wizara ya kazi na wizara ya elimu zishirikiane kubaini mapungufu yanayoonekana kwa wahitimu wanaoajiriwa ili waweze kubaini njia bora ya kuboresha.

Taasisi hii ipewe mamlaka ya kusimamia serikali kama ilivyo bunge na mahakama na kwamba ilani ya chama cha kiongozi aliyeko madarakani ilenge kutafuta au kuonyesha njia sahihi za kuipeleka nchi kule ambako dira inaonyesha, hii itasaidia kutekeleza miradi iliyoachwa au iliyoanzishwa na kiongozi aliemaliza muda wake, mfano wakati Rais JPM naingia madarakani alisitisha ujenzi wa bandari ya Bagamoyo kwa madai kwamba mikataba ilikua mibovu na iliyojaa unyonyaji, siku chache baada ya Rais Samia kuingia madarakani mapitio ya ujenzi wa bandari yameanza, hii ni kwa sababu hakuna mfumo wa kusimamia viapaumbele vya maendeleo ya Taifa badala yake kila kiongozi anajiamulia kile anachopenda.

• Ipatikane katiba imara ambayo itasaidia kudhibiti na kusimamia viongozi walioko madarakani na hata baada ya kustaafu kama ilivyo kwa nchi nyingine kama Marekani na Afrika ya Kusini. Hii itahakikisha viongozi wote wanafanya kazi kwa kuheshimu haki za binadamu na sheria na taratibu zilizopo bila kuathiri malengo ya Taifa kwa ujumla. Katiba imara pia itasaidia kuweka uwajibikaji na usawa kati ya watumishi/viongozi, kuondoa ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

• Serikali ijikite zaidi katika kuvumbua vyanzo vipya vya mapato badala ya kujikita katika kuongeza kodi katika huduma mbalimbali za kijamii ili kupunguza mzigo mkubwa wa kodi kwa wananchi na badala yake wananchi wapate unafuu wa maisha. Mfano sekta ya utalii na madini zinaweza kuwa vyanzo vizuri vya mapato kama tukiweka usimamizi mzuri na mifumo ya kuaminika ili kuepusha mianya ya ubadhirifu. Pia serikali ijikite katika kuboresha mfumo wa elimu ili kuruhusu vijana wengi kujiajiri katika nyanja mbalimbali badala ya kutegemea ajira kutoka serikalini.

• Bajeti za maendeleo zilizoidhinishwa na bunge zisitumike kinyume na lengo ili tuweze kutekeleza mipango iliyopangwa katika mwaka wa fedha wa serikali. Huko nyuma tulishuhudia pesa zikipelekwa katika matumizi ambayo hayakuidhinishwa na bunge hali iliyochangia kukwamishwa kwa miradi mingi ya maendeleo iliyoidhinishwa na bunge. Bajeti inayoidhinishwa pia iende sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa.

• Serikali iunde mfumo shirikishi utakaosaidia wananchi kushiriki katika kuonyesha vipaumbele vya maendeleo pamoja na utekelezaji. Hii itasaidia wananchi kuwa wasimamizi wa moja kwa moja wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

• Serikali iwatumie wataalamu wa masuala ya uchumi walioko nchini badala ya kutumia wanasiasa pekee katika kuandaa bajeti na matumizi ya serikali, pia serikali ijenge utamaduni wa kuwatumia wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali nchini katika kuandaa na kusimamia sera mbali mbali kwaajili ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya Taifa pamoja na kuheshimu mawazo na maelekezo ya wataalamu katika sekta mbalimbali hata pale yanapotokea majanga yanayohitaji ufumbuzi wa kitaalamu. Kwa kufanya hivi, tutapunguza au kudhibiti matamko ya kisiasa katika mambo nyeti yanayohitaji ufumbuzi wa kitaalamu kama vile Afya, Elimu na Uchumi.

Hitimisho
Natoa wito kwa viongozi/wenye mamlaka, na watunga sera wa nchi, maamuzi yoyote wanayofanya yanaathiri au kufaidisha jamii nzima, wao ni sehemu ya jamii na hivyo wataathirika au kufaidika na maamuzi hayo kwa namna moja au nyingine. Ni vyema kufanya uchambuzi yakinifu kabla ya kufanya maamuzi ili kuepuka athari zozote zitakazoisababishwa na maamuzi yao ikiwa ni pamoja na kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa.

Asanteni Sana​
 
Hiki chombo kinaweza kuwa
Economic Comitee..
Watu kama 12 hivi
Ambao kazi Yao kusimamia dira na muelekeo wa nchi..wao ndo washauri hadi hadi
Waziri gani akae wizara ya fedha.
Waipitishe bajeti
Na wawe washauri wakuu wa uchumi..
 
Hiki chombo kinaweza kuwa
Economic Comitee..
Watu kama 12 hivi
Ambao kazi Yao kusimamia dira na muelekeo wa nchi..wao ndo washauri hadi hadi
Waziri gani akae wizara ya fedha.
Waipitishe bajeti
Na wawe washauri wakuu wa uchumi..
Asante sana, ikiwezekana mawaziri wasichaguliwe kwa sababu ya uchama bali taaluma na perfomance
 
Hiki chombo kinaweza kuwa
Economic Comitee..
Watu kama 12 hivi
Ambao kazi Yao kusimamia dira na muelekeo wa nchi..wao ndo washauri hadi hadi
Waziri gani akae wizara ya fedha.
Waipitishe bajeti
Na wawe washauri wakuu wa uchumi..

Nilitaka niku tag utoe maoni yako kuhusu hili jambo mkuu.

Nakubaliana na wewe kuhusu uundwaji wa hichi chombo, usiingiliwe na Rais, kiwe ni chombo kinachojitegemea.
Kinachoweza kufanya kazi bila kuegemea upande wowote zaidi ya kusimamia mpango/ dira ya taifa.
 
Hutaki kuelewa kwamba wewe ni binti yangu! Tulia basi...

On a serious note, nchi yetu ina ombwe kubwa sana la kuiongozi na kuizalendo. Tunakosa uzalendo kuanzia ngaI ya chini hadi viongozi wetu, ona Bunge limejaa mambo ya hovyo tu, wanakaa kupitisha tozo na kodi zinazotuumiza lakini wao hawakatwi kodi yoyote.

Huenda tukawa ni taifa la hovyo tu yani!
Viongozi wetu ni wabinafsi sana
 
Kwa kweli hichi chombo kinahitajika,tena kama wabunge wale wazembe wawe wanawajibishwa mapema, chombo kiwe na framework ya ku measure perfomance ya wabunge,wale wabunge wazembe wanatolewa kila baada ya miaka miwili, 🤣 🤣 🤣 🤣 🤣 sio sasa hivi unaona kabisa mbunge hana mchango wowote bungeni wala katika jimbo lake then unasubiri mpaka muda wake wa miaka mitano uishe, tena akitoka hapo anahonga tena arudi bungeni..hapana this is problematic...you have my vote Abrianna,is a brilliant thread!
 
Serikali ianzishe taasisi maalumu kwaajili ya kuandaa na kusimamia Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Nakubaliana na pendekezo lako.
Gvt imekuwa inapewa ushari mzuri sana shida ni ukosefu wa viongozi wasio wabunifu wasio na maono ya maendeleo kwataifa.
Kufanya kazi kwa mihemuko na mazoea kunalifanya Taifa hili kuwa masikini.

Umasikini wa watanzania ni watanzania wenyewe hasa wale tunaowapa jukumu la kusimamia, kuongoza, kutawala na hata kutekeleza majuku yao.
 
Kwa kweli hichi chombo kinahitajika,tena kama wabunge wale wazembe wawe wanawajibishwa, chombo kiwe na framework ya ku measure perfomance ya wabunge,wale wabunge wazembe wanatolewa kila baada ya miaka miwili, 🤣 🤣 🤣 🤣 🤣 sio sasa hivi unaona kabisa mbunge hana mchango wowote bungeni wala katika jimbo lake then unasubiri mpaka muda wake wa miaka mitano uishe, tena akitoka hapo anahonga tena arudi bungeni..hapana this is problematic...you have my vote Abrianna,is a brilliant thread!
Thank you Rebeca 83, kweli tuna umuhimu wa kangalia hili suala la wabunge wanaokaa bungeni na kuliowa marupurupu makubwa mabayo hayaendani na elimu zao wala perfomance zao, tunahitaji wabunge wapimwe kwa perfomance na taaluma, kujua kusoma na kuandika haitoshi kabisa
 
Nakubaliana na pendekezo lako.
Gvt imekuwa inapewa ushari mzuri sana shida ni ukosefu wa viongozi wasio wabunifu wasio na maono ya maendeleo kwataifa.
Kufanya kazi kwa mihemuko na mazoea kunalifanya Taifa hili kuwa masikini.

Umasikini wa watanzania ni watanzania wenyewe hasa wale tunaowapa jukumu la kusimamia, kuongoza, kutawala na hata kutekeleza majuku yao.
Hali inazidi kuwa ngumu kila siku, viongozi tunaowaamini hawapo tena upande wa wananchi bali upande wa watawala, ifike mahali wananchi tupewe ngucu ya kuwasimamia hawa viongozi maana naona katiba haina maana tena
 
Pia serikali kwa namna ya pekee haina budi kuziangalia kwa jicho la tatu sekta ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la taifa mfano sekta ya kilimo, Ujenzi na Utalii.

Sekta ya kilimo inachangia pakubwa kwenye pato la Taifa lakini bado imekua na changamoto nyingi, vile vile sekta ya Utalii na Ujenzi licha kuchangia pakubwa lakini ukweli ni kwamba ni watanzania wachache sana walioajiriwa kwenye sekta hizi (utalii na ujenzi) na ndio maana licha kuonekana zinakua na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi hadi kufikia 7% kwenye kipindi miaka tatu hadi minne iliyopita. Laikini ukuaji huu wa uchumi umekua hauna tija kwenye maendeleo ya mtu mmoja mmoja kwa sababu sekta zinazochangia kwa kiasi kukubwa kwenye pato la taifa mfano Kilimo, Utalii na ujenzi bado zimekua na changamoto lukuki.

Ili tufikie kikamilifu malengo ya kwenye Dira ya taifa 2025 (National Vision 2025) haina budi tuachane na masuala ya Economic Growth na badala yake tujikite zaidi kwenye Economic Development (uchumi wa maendeleo) tukitumia zaidi Expansionary Fiscal Policy. Hii itasaidia kuwa na uchumi ambao ukuaje wake utakua na mahusiano ya moja kwa moja na maendeleo ya watu.

NB:
Naunga mkono hoja.
 
Pia serikali kwa namna ya pekee haina budi kuziangalia kwa jicho la tatu sekta ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la taifa mfano sekta ya kilimo, Ujenzi na Utalii.

Sekta ya kilimo inachangia pakubwa kwenye pato la Taifa lakini bado imekua na changamoto nyingi, vile vile sekta ya Utalii na Ujenzi licha kuchangia pakubwa lakini ukweli ni kwamba ni watanzania wachache sana walioajiriwa kwenye sekta hizi (utalii na ujenzi) na ndio maana licha kuonekana zinakua na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi hadi kufikia 7% kwenye kipindi miaka tatu hadi minne iliyopita. Laikini ukuaji huu wa uchumi umekua hauna tija kwenye maendeleo ya mtu mmoja mmoja kwa sababu sekta zinazochangia kwa kiasi kukubwa kwenye pato la taifa mfano Kilimo, Utalii na ujenzi bado zimekua na changamoto lukuki.

Ili tufikie kikamilifu malengo ya kwenye Dira ya taifa 2025 (National Vision 2025) haina budi tuachane na masuala ya Economic Growth na badala yake tujikite zaidi kwenye Economic Development (uchumi wa maendeleo) tukitumia zaidi Expansionary Fiscal Policy. Hii itasaidia kuwa na uchumi ambao ukuaje wake utakua na mahusiano ya moja kwa moja na maendeleo ya watu.

NB:
Naunga mkono hoja.
Bila kusahau sekta ya madini, tena serikali ikiweka mkazo kwenye sekta hii hatutakua na haja ya kulipa hata tozo za miamala
 
Back
Top Bottom